Thursday, November 24, 2016

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.  Dkt. Augustine Mahiga amefanya mazungumzo na waandishi wa  habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam. Katika mazungumzo hayo. Mhe. Waziri aliwahabarisha kuhusu ziara ya Rais wa Zambia, Mhe Edgar Lungu anayetarajiwa kuifanya nchini kuanzia tarehe 27 - 29 Novemba 2016.
Waziri Mahiga akiendelea kuzungumza na waandishi wa habari 


Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Grace Mujuma  akielezea jambo kwa waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo (hawapo pichani), wa kwanza kutoka kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samuel Shelukindo naye akielezea faida zitakazo tokana na ziara nzima ya Rais wa Zambia
Sehemu ya waandishi wa habari wakiwa katika kikao na Waziri Mahiga.

1.Rais wa Zambia, Mhe. Edgar Lungu kuzuru Tanzania Novemba 27 - 29, 2016

UTANGULIZI

1.1        Ndugu waandishi, nimewaita leo ili kuwaeleza kuhusu Ziara Rasmi hapa nchini ya Mhe. Edgar Chagwa Lungu, Rais wa Jamhuri ya Zambiainayotarajiwa kufanyika hapa nchini. Najua baadhi yenu mtakuwa mmekwishasikia taarifa za Rais huyokufika nchini hivi karibuni.

1.2        Sasa niwatangazie rasmi kuwa taarifa hiyo ni sahihi na ziara hiyo itafanyika kuanzia tarehe 27 hadi 29 Novemba 2016. Hii ni ziara Rasmi ya kwanza kwa Mhe. Rais Lungu kuifanya nchini tangu alipochaguliwa katika nafasi hiyo ya Urais mwezi Septamba, 2016.

1.3        Ndugu Waandishi, mnafahamu kwamba, mbali na kuwa nchi majirani, mahusiano  kati ya nchi za  Tanzania na Zambia yana historia ndefu, tangu enzi ya waanzilishi wa mataifa haya mawili, yaani Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Mzee Kenneth Kaunda wa Zambia.

1.4        Ifahamike kuwa, kutokana na mahusiano haya ya karibu ndipo nchi za Tanzania na Zambia kwa pamoja zilifanya uamuzi wa kihistoria wa kutekeleza mradi mkubwa wa ushirikiano wa ujenzi wa Reli ya TAZARA. Licha ya kwamba mradi huo ni wa kimaendeleo, lakini pia Reli hiyo ya TAZARA ilitoa mchango mkubwa katika ukombozi wa bara la Afrika, wakati ambapo Tanzania na Zambia zikiwa miongoni mwa nchi ziizokuwa mstari wa mbele katika harakati za ukombozi (Frontline States).

1.5        Mradi mwingine mkubwa ambao nchi zetu mbili zimeufanya kwa ushirikiano ni mradi wa Bomba la Mafuta la TAZAMA.

Ndugu waandishi, haya, pamoja na mengineyo mengi ambayo nitayaeleza baadaye, yanaufanya ugeni huu kuwa wa muhimu na wa heshima kubwa sana kwetu.

1.6        Mhe. Rais Lungu anafika nchini kufutia mwaliko rasmi kutoka kwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na akiwa nchini, pamoja na mambo mengine, atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Magufuli. Mhe. Rais Lungu ataambatana na Maafisa wengine Waandamizi wa Serikali ya Zambia.

2.0       RATIBA YA MGENI KWA KIFUPI

Ndugu Waandishi, sasa niwaeleze kwa kifupi ratiba ya ziara hiyo.

2.1        Mhe. Rais Lungu anatarajiwa kuwasili nchini siku ya jumapili tarehe 27Novemba 2016saa 10 kamili jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ndege maalumu ambapo atalakiwa na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa wakiongozwa na mwenyeji wake Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ambapo atapigiwa mizinga 21 ya kijeshi kwa heshima yake kumkaribisha nchini.

2.2        Siku inayofuata ya tarehe 28 Novemba 2016 asubuhi, Mhe. Rais Lungu atatembelea Makao Makuu ya Mamlaka ya TAZARA ili kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika hilo la ubia baina ya nchi zetu mbili. Baada ya kutoka TAZARA, Mhe. Lungu atazuru pia Shirika la Bomba la Mafuta la TAZAMA, ambapo atatembelea mitambo ya kupampu mafuta, pamoja na matenki ya kuhifadhi mafuta ya TAZAMA vyote vilivyopo eneo la Kigamboni.

2.3        Baada ya ziara hizo za asubuhi, Mhe. Rais Lungu pamoja na ujumbe wake watafanya mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Magufuli, pamoja na Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mazungumzo hayo yatafanyikia Ikulu kuanzia saa 5 kamili? mchana.

2.4        Baada ya mazungumzo rasmi, Mhe. Rais Lungu pamoja na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli watashuhudia utiaji saini wa Makubaliano na Mikataba mbalimbali minne(4) ya ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniakwa upande mmoja na Serikali ya Jamhuri ya Zambia kwa upande mwingine. Kwa kifupi mikataba hiyo inahusu kuimarisha na kukuza zaidi mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi zetu mbili.

2.5        Jioni ya siku hiyo, Mhe. Rais Lunguatahudhuriadhifa ya kitaifa(State Banquet) itakayoandaliwa  kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli. Dhifa hiyo itafanyika Ikulu kuanzia saa 12 na nusu jioni. Hilo ndilo litakuwa tukio la mwisho kwa siku ya kwanza hiyo.

2.6        Siku itakayofuata ya tarehe 29 Novemba 2016, Mhe. Rais Lungu atatembelea Bandari ya Dar es Salaam ambapo atajionea shughuli mbalimbali za upokeaji na upitishwaji wa mizigo bandarini hapo. Baada ya tukio hilo, Mhe. Rais Lungu atafanya ziara fupi kwenye Kampuni ya kusafirisha mizigo inayomilikiwa na Zambia inayojulikana kama Zamcargo.

2.7        Baada ya hapo Mhe. Rais Lungu ataelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K. Nyerere ambapo ataagwa rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli kurejea nchini Zambia.

3.0       MANUFAA YA ZIARA HIYO

3.1        Ndugu Waandishi, kama nilivyoeleza awali, mahusiano yetu na Zambia ni ya kidugu na yana historia ndefu. Kupitia uhusiano huo, Tanzania na Zambiazimeendelea kufanya kazi kwa kuaminiana na kushirikiana katika nyanja mbalimbali za kitaifa, kikanda na kimataifa. Hivyo, ziara hii ya Mhe. Rais Lungu, itatoa fursa ya kuimarisha zaidi mahusiano hayo kwa manufaa ya Serikali na wananchi wa Tanzania na Zambia.

3.2         Kwa upande wa ushirikiano wa kiuchumi, ziara hiyo inatarajiwa kuzidisha zaidi uhusiano katika maeneo bayana kama ifuatavyo:

a).  Kukuza ushirikiano ili kuongeza ufanisi wa Reli ya TAZARA:
·        Kama nilivyoeleza hapo awali, Reli ya TAZARAni mhimili na kiungo muhimu sana katika ukuzaji wa uchumi wa Tanzania na Zambia, lakini pia na kwa nchi nyingine majirani za ukanda wa kusini na kati mwa Afrika za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zimbabwe, Malawi n.k. Reli hiyo inatoa huduma ya usafirishaji wa mizigo, rasilimali ghafi pamoja na abiria katika nchi hizo.

·        Hata hivyo, kama ambavyo wengi wenu mtakuwa mnafahamu, ufanisi wa Reli ya TAZARA umekuwa chini ya matarajio ya wadau wa sekta hiyo ya usafiri. Serikali za Tanzania na Zambia kama wamiliki wa Reli hiyo kwa ubia sawa wa 50% kwa 50% zimeendeleakuchukua hatua mbalimbali kuisaidia TAZARA, hususan kwa kushirikiana na marafiki zetu Serikali ya China.

·        Napenda kuwataarifu kuwa, katika ziara hii ya Mhe. Rais Lungu, suala hili la TAZARA litajadiliwa kwa kina baina ya viongozi hao wawili ili Shirika hilo liweze kuongeza ufanisi na kujiendesha kwa tija kibiashara.

b). Kukuza Ushirikiano katika Matumizi ya Bomba la TAZAMA.
·        Ndugu waandishi, bomba la TAZAMA lilijengwa mwaka 1968 kwa lengo la kutoa njia nafuu ya Kusafirisha mafuta ghafi kwenda nchini Zambia na hivyo kuiepusha nchi hiyo na athari za kupanda kwa bei ya mafuta. Hata sasa umuhimu wa bomba hilo bado upo.

·        Nchi zetu mbili zinamiliki bomba hilo kwa ubia ambapo Zambia ina mtaji wa mbili ya tatu na Tanzania inamiliki bomba hilo kwa mtaji wa moja ya tatu. Bomba hilo limekuwa likijiendesha kibiashara kwa faida na limeendelea kuziingizia kipato nchi zetu mbili.

·        Wakati wa ziara hii ya Mhe. Rais Lungu, suala la TAZAMA linatarajiwa pia kujadiliwa, hususan namna ya kulifanya bomba hilo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa manufaa ya nchi zetu mbili.

c).  Ushirikiano katika Matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam:
·        Ndugu Waandishi, kama mnavyofahamu kuwa nchi ya Zambia haina bahari (land locked country), na kwa muda mrefu imekuwa ikitumia Bandari ya Dar es Salaam kupitisha mizigo yake. Kwa sababu za kiuchumi na za kihistoria, nchi hiyo imeendelea kuwa mdau mkubwa katika matumizi ya bandari hiyo.
·        Tunatarajia pia wakati wa ziara hiyo, Viongozi wetu wawili watapata fursa ya kujadiliana kuhusu suala hilo.

3.3         Ndugu waandishi, yapo masuala mengine ya ushirikiano baina ya nchi zetu mbili yatakayojadiliwa wakati wa ziara hiyo na taarifa kamili itatolewa baada ya kukamilika kwa ziara hiyo.

4.0       HITIMISHO

5.1    Ndugu waandishi, kwa mara nyingine tena tunatarajia kumpokea kiongozi wa kitaifa kutoka nje ya nchi. Huu ni mwendeleze wa utekelezaji mzuri wa Sera ya Mambo ya Nje inayosimamiwa vizuri na Serikali ya Awamu ya Tano ambapo tunanuia kuimarisha mahusiano yetu, hususan ya kiuchumi, na nchi zote majirani na nyinginezo barani Afrika na  kote duniani. 

5.2    Hivyo basi, kupitia kwenu, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba Watanzania wote kwa ujumla tujitokeze kwa wingi kumlaki Mhe. Rais Lungu atakapokuwa anawasili kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K. Nyerere mpaka Hoteli ya Hyatt Regency/Kilimanjaro atakapofikia kwa kupitia Barabara ya Julius K. Nyerere/Pugu.

Asanteni!



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.