Friday, June 9, 2017

Wizara ya Mambo ya Nje yafanya uzinduzi wa shindano la kubuni nembo mpya ya EAC

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi akizungumza katika halfa ya uzinduzi wa shindano ya kubuni nembo mpya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Taasisi zake kwa vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 wa Jumuiya hiyo, uliofanyika katika Ukumbi wa Nkurumah, chuo kikuu cha Dar es Salaam tarehe 09 Juni, 2017. Pembeni ni Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam, Profesa Curthbert Kimambo.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakifuatilia maelekezo ya vigezo vya shindano pamoja na zawadi zitakazotolewa kwa mshindi wa kwanza ambaye atapata dola za Kimarekani 25,000, wa pili dola  5,000 na wa tatu dola 2,500.

Sehemu nyingine ya Wanafunzi wakifuatilia maelekezo.

Picha ya pamoja uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje, Chuo kikuu cha Dar es Salaam na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Picha ya pamoja Viongozi na wanafunzi.

Siku ya Kongamano la Biashara ya Kilimo na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uholanzi yafana



 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Siku ya Kongamano la Biashara ya Kilimo na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uholanzi yafana

Katika kutekeleza Sera ya Diplomasia ya Uchumi, Ubalozi wa Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uholanzi uliopo Tanzania, Wizara ya Masuala ya Uchumi na Wizara ya Mambo ya Nje za Uholanzi na Taasisi ya Netherlands–African Business Council (NABC)kwa pamoja ziliandaa Kongamano la Biashara na Uwekezaji lililofanyika hapa The Hague, Uholanzi tarehe 31 Mei 2017. Lengo kuu la Kongamamo hilo, pamoja na kuendeleza na kukuza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uholanzi, nikutangaza fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania hususan katika Sekta za Kilimo, Ufugaji, Uvuvi na Miundombinu ya Kilimo. Aidha, Kongamano hilo lililohudhuriwa na Wawakilishi wa Makampuni takriban mia moja (100) ni mwendelezo wa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye Mkataba kati ya Tanzania na Uholanzi kuhusu Uingizwaji wa Mbegu za Viazi kutoka Uholanzi uliosainiwa kwenye ziara ya Mhe. Martijn Van Dam, Waziri wa Kilimo wa Uholanzi nchini Tanzania tarehe 16 Juni 2016. Aidha, Kongamano hii lilitanguliwa na ziara ya ujumbe kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo mashamba yanayomilikiwa na wakulima na wafugaji binafsi nchini Tanzania pamoja na kupata fursa za kusikiliza mada mbalimbali zilizotolewa na wakulima/wafugaji na wakufunzi wa Chuo Kikuu cha Wageningen kinachohusika na kufanya tafiti za Kilimo na Ufugaji.
Ujumbe kutoka Tanzania uliongozwa na Mhe.Eng. Mathew Mtigumwe, Katibu Mkuu anayeshughulikia Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, akimwakilisha Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Wajumbe wengine ni:
ü  Mhe. Yohana Budeba, Katibu Mkuu anayeshughulikia Uvuvi, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi,
ü  Mhe. Irene F.M. Kasyanju, Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi,
ü  Bw. Twahir Nzallawahe, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi,
ü  Bibi Anuciata Njombe, Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Mifugo na Masoko, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi,
ü  Bw. Geoffrey Kirenga, Mtendaji Mkuu wa Kituo cha kuendeleleza Kilimo Ukanda wa Kusini (SAGCOT),
ü  Bibi Jennifer Baarn, Naibu Mtendaji Mkuuwa Kituo cha kuendeleleza Kilimo Ukanda wa Kusini (SAGCOT),
ü  Professa Andrew Temu, Mkurugenzi wa Diligent Consulting Ltd na Mwanachama wa Bodi ya SAGCOT,
ü  Bibi Jacqueline Mkindi, Mtendaji Mkuu wa Tanzania Horticulture Association (TAHA),
ü  Bw. Hussein Sufiani Ally, Mkurugenzi wa AZAM Bakhresa Group,
ü  Bibi Mona Mahecha, Afisa Mambo ya Nje Mwandamizi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
ü  Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania Uholanzi Bw. Matiku Kimenya (MC), Bibi Naomi Z. Mpemba (CO) na Bibi Agnes K. Tengia (FS).
Kwa upande wa Serikali ya Uholanzi, ujumbe uliongozwa na Mhe. Bibi Marjolijn Sonnema, Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kilimo, Wizara ya Masuala ya Uchumi ya Uholanzi ambaye pia anakaimu kama Naibu Waziri wa Kilimo. Wengine ni;
ü  Mhe. Jaap Fredericks, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania,
ü  Bw. Bert Rikken, Afisa anayeshughulikia Masuala ya Kilimo, Ubalozi wa Uholanzi nchini Tanzania/Kenya,
ü  Bibi Ingrid Korving, Afisa Sera Mwandamizi, Wizara ya Masuala ya Uchumi ya Uholanzi,
ü  Bibi Hennie Wellen, Mratibu Wageni wa Kimataifa, Wizara ya Masuala ya Uchumi ya Uholanzi,
ü  Bibi Theresia Mcha, Afisa Kilimo, Ubalozi wa Uholanzi nchini Tanzania.
Katika Kongamano hili, Viongozi wa Ujumbe wa Serikali ya Tanzania na Uholanzi walionesha dhamira ya kuendelea kushirikiana kwa pamoja kwa kusaini Barua (Letter of Intent) ya kuanzishwa kwa Kituo cha Kuendeleza Zao la Viazi nchini Tanzania (Centre for Development of the Potato Industry in Tanzania- CD PIT). Aidha, Makampuni takriban kumi (10) yanayojishughulisha na kilimo cha viazi, yalionesha utayari wa kuwa wanachama kwa kushirikiana na Serikali za nchi hizi mbili katika uanzishwaji wa Kituo hicho. Tukio hilo lilikamilishwa kwa Wawakilishi wa Makampuni hayo kuweka saini kwenye Kadi/Bango kuonesha utayari wao.
Kituo cha CD PIT kinatarajiwa kuanzishwa Mkoani Mbeya ambapo pamoja na kukuza maendeleo ya sekta binafsi na kutoa ajira, kitatoa mafunzo ya kujenga uwezo hususan katika uzalishaji na utafutaji masoko, kitaendesha tafiti mbalimbali za kilimo ikiwemo pia kukuza uhusiano wa kibiashara kati ya  Tanzania na Uholanzi. 
Ubalozi kwa upande wake umeridhishwa na mwitikio mkubwa uliooneshwa na wadau mbalimbali waliojitokeza kushiriki katika Kongamano hilo. Hii inadhihirisha kuzidi kuimarika kwa mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi hizi mbili.
Pamoja na kubadilishana uzoefu, kujifunza na kufahamiana, Kongamano hilo liliwezesha wadau kupata fursa ya kujadili pia changamoto wanazokabiliana nazo katika shughuli mbalimbali za biashara na uwekezaji wanazoziendesha nchini Tanzania.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
The Hague, Uholanzi, 09 Juni 2017
Mhe. Mathew Mtigumwe, Katibu Mkuu wa Wizara Kilimo, Mifugo na Uvuvi akisoma hotuba.
Mhe. Irene Kasyanju, Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi akisoma hotuba ya ufunguzi.

Mhe. Marjolijn Sonnema, Katibu Mkuu na Kaimu Naibu Waziri wa Kilimo wa Uholanzi  akisoma hotuba
Picha ya Pamoja ya Waheshimiwa Mabalozi wa Tanzania na Uhoalnzi na Makatibu Wakuu wa Kilimo na Uvuvi na Mkurugenzi wa TAHA.

Uwekaji saini wa makubaliano (letter of intent) ya kuanzishwa kwa kituo cha kuendeleza zao la viazi Tanzania


Thursday, June 8, 2017

Vijana wahamisishwa kushiriki mashindano ya kubuni nembo ya EAC

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika MasharikI, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi akimsikiliza Afisa  Mkuu wa Uhusiano wa Sekrearieti ya Jumuiya ya Afrika Mshariki, Bw. Otrhieno Richard Owora (kushoto). Katika mazungumzo hayo, wawili hao walizungumzia maandalizi ya uzinduzi wa mashindano ya kubuni nembo mpya ya EAC yatakayowahusisha wanafunzi wa Vyuo Vikuu vilivyopo kwenye nchi wanachama wa Jumuiya hiyo. Uzinduzi huo utafanyika kwenye Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam tarehe 09 Juni 2017. 
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga (wa kwanza kushoto), pamoja na Maafisa Habari wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, wa kwanza kulia ni Bw. Ally Kondo pamoja na Robi Bwiru wakinukuu mambo yaliyokuwa yakizungumzwa na Balozi Mwinyi pamoja na Bw. Owora.
Mazungumzo yakiendelea.
Balozi Mwinyi akipokea kitabu chenye mwongozo wa namna ya kushiriki mashindano hayo.
Picha ya pamoja.

Wednesday, June 7, 2017

Tanzania yashiriki Mkutano wa kujadili matumizi ya Bahari na rasilimali zake

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu Na. 14 (Sustainable Development Goals-SDGs14)  maarufu kama Oceans Conference unaojadili matumizi endelevu ya bahari na rasilimali zilizomo baharini.

Waziri wa Kilimo, Nifugo na Uvuvi, Mhe. Charles Tzeba akiwasilisha hotuba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania kwenye Mkutano wa Kimataifa wa kuweka mikakati ya utekelezaji wa SDG14 unaoendelea Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York, Marekan. Mkutano huo ni maalum kwa ajili ya kujadili kuhusu matumizi endelevu ya bahari na rasilimali zilizomo baharini kama sehemu ya utekelezaji wa lengo la 14 la malengo ya maendeleo endelevu






Monday, June 5, 2017

Wizara ya Mambo ya Nje yafanya usafi kwenye ufukwe wa Feri



Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki waadhimisha siku ya mazingira duniani kwa kufanya usafi kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Feri jijini Dar es Salaam.  Wanaoenekana wakifanya usafi wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Bw. James Lugaganya akiwa pamoja na wafanya kazi wengine wa Wizara.
Mkurugenzi msaidizi Idara ya Utawala na Rasilimali watu Bw. Hamid Mbegu (kushoto) naye akifanya usafi
Sehemu nyingine ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakijumuika kwa pamoja katika kufanya usafi kwenye ufukwe wa bahari eneo la Feri.
wakisomba taka
Sehemu nyingine ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiendelea kufanya usafi
Usafi ukiendelea

Kaimu Mkurugenzi wa idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Jestas Nyamanga  akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza zoezi la kufanya usafi kwenye ufukwe eneo la ferri



HOTUBA YA BALOZI DKT. AZIZ P. MLIMA, KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI KATIKA SHUGHULI YA KUFANYA USAFI KWENYE UFUKWE WA BAHARI YA HINDI, ENEO LA KIVUKONI (FERRY), DAR ES SALAAM
TAREHE 05 JUNI 2017

Waheshimiwa Mabalozi, Wakurugenzi na Makaimu Wakurugenzi kutoka Wizarani,
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Umoja wa Mataifa kwenye tukio hili;
Uongozi wa Kata ya Kivukoni ukiongozwa na Mhe. Henry Massaba, Diwani wa Kata ya Kivukoni;
Uongozi wa Mtaa wa Kivukoni ukiongozwa na Ndugu Gasper Makame, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivukoni;
Wafanyakazi wa Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara;
Wananchi wote mlioshiriki;
Waandishi wa Habari;
Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote, napenda kuwasilisha salamu kutoka kwa Mhe. Waziri, Dkt. Augustine P. Mahiga (Mb.), pamoja na Mhe. Naibu Waziri, Dkt. Susan A. Kolimba (Mb.). Wanawasalimu sana na walitamani wajumuike nasi kwenye zoezi hili, ila kutokana na kubanwa na majukumu mengine ya kitaifa wameshindwa. Lakini wamefurahishwa na hiki tulichokifanya na wanatupongeza sana.

Wizara inawashukuru sana wote mliojumuika nasi kwenye tukio hili muhimu la kusafisha mazingira ya ufukwe huu tunapoadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.
Maadhimisho haya kidunia yanafanyika nchini Canada, na kwa hapa Tanzania, yanafanyika kitaifa huko Butiama, Mkoani Mara, chini ya kaulimbiu: “Hifadhi ya Mazingira: Muhimili kwa Tanzania ya Viwanda”.
Kaulimbiu hii inatukumbusha kuwa tunapoelekea kwenye Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa Kati, hatuna budi kutunza mazingira, kwani rasilimali tunazozihitaji kutimiza azma yetu hii adhimu zinapatikana kwenye mazingira na mazingira ndiyo maisha yetu. Hivyo utajiri wetu wa kwanza ni mazingira.

Mabibi na Mabwana,
Tumechagua kufanya zoezi hili la usafi kwenye ufukwe wa bahari kwa sababu tunapozungumzia utunzaji wa mazingira, suala la utunzaji wa bahari linasahaulika. Hivyo, sisi tunaikumbusha jamii kuwa bahari nayo ni sehemu ya mazingira, ni urithi wetu, ni lazima tuitunze.

Kwa bahati, wakati sisi tunafanya zoezi hili, leo hii pia kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, huko New York, dunia inakutana kujadili namna ya kuhakikisha uhifadhi wa bahari na matumizi endelevu ya rasilimali zake, ukiwa ni Mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala hili.
Hivyo, ndugu wananchi wenzangu, naomba tuone umuhimu wa kutunza bahari, tunaitegemea sana kwenye uchumi wetu na maisha yetu ya kila siku, tuache kuichafua kwani ikipoteza uhai ni hasara kwetu sote.

Mabibi na Mabwana,
Mtakubaliana nami kuwa, bila kufanya zoezi hili kwa ushirikiano, tusingefanya chochote cha msingi hapa. Basi, na hili liwe funzo wakati huu tunapotekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Makubaliano ya Paris ambayo yote yanasisisiza uhifadhi wa mazingira. Bila ushirikiano, itakuwa vigumu kutimiza azma hiyo ya Makuibaliano ya Paris na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Dunia ni yetu sote, inatutunza sote, inatukirimia sote sawa sawa, basi sote tuna jukumu la kuitunza, tena kwa ushirikiano.

Mabibi na Mabwana, Wananchi Wote Mliopo Hapa,
Kabla sijamaliza kuzungumza, napenda kutumia nafasi hii kuishukuru Ofisi ya Umoja wa Mataifa hapa nchini; Uongozi wa Manispaa ya Ilala na Kata ya Kivukoni kwa misaada yao ya hali na mali katika kufanikisha zoezi hili. Tunawashukuru sana.

Asanteni sana kwa kunisikiliza!

Serikali Mpya ya Lesotho yashauriwa kutekeleza Mageuzi - SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Mkuu wa Timu ya waangalizi ya SADC ya uchaguzi wa Lesotho akiwasilisha taarifa ya awali kuhusu uchaguzi huo

Waziri Mahiga akiendelea kuwasilisha taarifa ya awali ya uchaguzi wa Lesotho jijini Maseru

Waziri Mahiga bado anasoma taarifa ya awali ya uchaguzi wa Lesotho kwa wajumbe.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali Mpya ya Lesotho yashauriwa kutekeleza Mageuzi - SADC



Serikali itakayoingia madarakani  baada ya Uchaguzi wa Wabunge uliofanyika nchini Lesotho Julai 3, imeshauriwa kutekeleza kikamilifu na kwa nia ya dhati maazimio yote ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC yanayohusu mageuzi kwenye sekta muhimu za katiba, sheria na mahakama, ulinzi na usalama, utumishi na sekta ya umma na vyombo vya habari kwa muda muafaka ili kuimarisha utawala bora na wa kidemokrasia nchini humo. 

Mnamo mwezi Machi mwaka 2017, baada ya Mfalme Letsie wa III wa Lesotho kutangaza tarehe ya uchaguzi mkuu, kikao cha juu cha maamuzi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC Summit), kilielekeza Serikali mpya itakayoshinda uchaguzi na kuingia madarakani, itekeleze maazimio hayo kwa kuweka muda maalum na vigezo vya utekelezaji ili kuepuka chaguzi za mara kwa mara. 

Msimamo huo wa Jumuiya ya SADC umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Mheshimiwa Augustine P. Mahiga, Mwenyekiti wa Kamati ya Asasi ya Ushirikiano ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC alipokuwa akitoa taarifa ya awali ya timu ya uangalizi siku mbili baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika. 

Mheshimiwa Mahiga alisema, japokuwa zoezi la kuhesabu kura bado linaendelea, ni dhahiri kuwa wapiga kura nchini Lesotho wanatarajia mageuzi makubwa kutoka kwenye Serikali mpya yatakayoandika historia mpya nchini Lesotho, ambayo imafanya chaguzi tatu kuu ndani ya miaka mitano. 

Mapendekezo mengine yaliyotolewa kwenye taarifa hiyo ya awali ya SADC yanaitaka Serikali mpya kupitia na kufanyia mageuzi mfumo mzima wa uchaguzi ambao kwa sasa unatoa fursa kwa wabunge kuhama chama bila kupoteza ubunge wao (Floor Crossing). Alisema mfumo huo unayumbisha mfumo wa siasa na wa kibunge kwenye Falme ya Lesotho.

Kwenye upande wa ulinzi na usalama wa raia wakati wa uchaguzi, taarifa hiyo ilisifu Tume Huru ya Uchaguzi ya Lesotho kwa kuendesha kwa weledi mkubwa zoezi la upigaji kura na kushirikiana na Jeshi la Polisi kuimarisha usalama vituoni kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. 

Hata hivyo taarifa za awali za waangalizi wa kimataifa zimeeleza kuwa Jeshi la Lesotho pia lilionekana kwenye baadhi ya maeneo,  nje ya vituo wakiimarisha ulinzi kwa mujibu wa sheria ya jeshi hilo.  Balozi Mahiga alieleza kuwa japokuwa uwepo wa jeshi  hakuathiri mwenendo mzima wa upigaji kura, bado kuna umuhimu wa kufanya mageuzi ndani ya vyombo hivyo ili kuainisha majukumu ya kila taasisi na kuondoa muingiliano wa kimajukumu kama ilivyo sasa. 

Mapendekezo mengine yaliyotolewa na Jumuiya ya SADC kwa Serikali mpya nchini humo ni kuweka mazingira bora yatakayowezesha wanawake na watu wanaoishi na ulemavu kushiriki kikamilifu kwenye shuguli za kisiasa bila ubaguzi. Vilevile kuifanyia mageuzi sekta ya habari nchini na kuwawezesha wananchi kupata habari za uhakika na kwa wakati.

Matokeo ya uchaguzi wa Wabunge yanaendelea kutangazwa ambapo na yanatarajiwa kukamilika ndani ya siku mbili ambapo upinzani mkali unaonekana baina ya Chama cha Democratic Congress kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa sasa Mhe. Pakalitha Mosisili na Chama cha All Basotho Convention kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Mhe. Thomas Motsoahae Thabane.

 -Mwisho-



Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Maseru, Lesotho, 05 Juni 2017



Rais Magufuli atoa pole kufuatia kifo cha Balozi Mtiro


Friday, June 2, 2017

Waziri Mahiga awasiliha Ujumbe Maalum nchini Kenya


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta katika mji wa Nyeri tarehe 01 Juni 2017. Waziri Mahiga alikwenda nchini Kenya kuwasilisha Ujumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Waziri Mahiga akiwa na Rais wa Kenya Mhe. Kenyatta walipoonana Nyeri, Kenya.