TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la
Ujenzi wa Bomba la Mafuta
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameitaja
tarehe ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi
kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania kuwa ni siku
ya maendeleo ya kweli kwa Tanzania na Uganda na nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa ujumla.
Uwekaji
wa jiwe la msingi la ujenzi wa bomba hilo litakalokuwa na urefu wa kilomita
1445 litakalogharimu takribani Shilingi trilioni 8 za Tanzania ulifanywa na
Rais Magufuli na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika eneo la
Chongoleani mkoani Tanga siku ya Jumamosi tarehe 05 Agosti 2017 na kushuhudiwa
na umati mkubwa wa watu wakiwemo viongozi wakuu wa Serikali na vyama vya siasa
kutoka pande zote mbili.
Rais
Magufuli alieleza kuwa hadi kufikia hatua ya uwekaji wa jiwe la msingi wa
ujenzi wa bomba hilo, vikwazo vingi vilijitokeza, hivyo anamshukuru Rais
Museveni kwa kuipa kipaumbele Tanzania kwa kuwa bomba hilo lingeweza kupita
mahali pengine ambako umbali ungekuwa mfupi kwa zaidi ya kilomita 500.
Aliendelea
kueleza kuwa licha ya Tanzania kutoa vivutio vingi kwa Uganda ikwemo kusamehe
baadhi ya kodi kama za ongezeko la thamani lakini ujenzi wa bomba hilo utakuwa
na manufaa makubwa kwaTanzania katika kipindi cha ujenzi unaotarajiwa kuanza
mwezi Januari 2018 na kukamilika mwaka 2020 na baada ya kukamilika kwa ujenzi
huo.
"Tutapata
mamilioni ya Dola yatakayotokana na ada ya usafirishaji ambayo ni Dola 12.5 kwa
pipa moja na inakadiriwa kwa siku yatasafirishwa mapipa 216,000". Rais
Magufuli alisema.
Manufaa
mengine ni pamoja na ajira ambapo inakadiriwa watu kati ya elf 10 hadi 15
watapata ajira za kudumu bomba litakapokamilika na ajira za muda mfupi za watu
zaidi ya elf 30 katika kipindi cha ujenzi.
Aidha,
bomba litakuza biashara ya bidhaa mbalimbali ikiwemo saruji na vifaa vingine
vitakavyotumika katika ujenzi wa bomba, ujenzi wa nyumba za kupangisha na
kuchochea ujenzi wa viwanda ambavyo malighafi zake zinatokana na mabaki
yanayotokana na usafishaji wa mafuta kama vile viwanda vya mbolea.
Vile
vile, bomba linatarajiwa kupunguza gharama za uendeshaji katika sekta ya anga
kutokana na unafuu wa mafuta na linakuja wakati mwafaka kwa kuwa Tanzania
imeshaanza kulifufua shirika lake la ndege na Uganda ipo mbioni pia kulifufua
shirika lake. Imeelezwa kuwa moja ya sababu ya Mashirika ya ndege ya nchi za
Mashariki ya Kati kufanya vizuri kibiashara inatokana na unafuu wa mafuta ya
ndege.
Mhe.
Rais alitoa wito kwa wakandarasi watakaojenga bomba hilo kuharakisha
ujenzi ili uweze kukamilika kabla ya muda uliopangwa wa miaka mitatu.
"Kuna
sababu gani ya kutumia muda wote huo wakati fedha zipo na wakandarasi wote
mnatoka nchi kubwa zilizopiga hatua ya maendeleo, Tuoeni zabuni kwa wakandarasi
wengini (sub contractors) ili ujenzi ukamilike kwa muda mfupi". Rais
Magufuli alishauri.
Wakandarasi
watatu, wawili kutoka Ufaransa, Total na Cnooc na mwingine kutoka Uingereza,
Tullow Oil kwa pamoja watajenga bomba hilo.
Mhe.
Magufuli alibainisha kuwa Tanzania na Uganda zipo katika mazungumzo ili
wataalamu wa Kiganda waliogundua mafuta hayo mwaka 2006 waje Tanzania kufanya
utafiti kwenye maziwa ya Tanganyika na Eyasi ambayo yana viashiria vya kuwepo
kwa mafuta.
Rais
Magufuli alihitimisha hotuba yake kwa kumuhakikishia Mhe. Museveni kuwa
Tanzania ni nchi iliyokamilika kiulinzi, hivyo Waganda wasiwe na wasi wasi
kuhusu usalama wa bomba hilo ambalo litapita katika mikoa 8 ya Tanzania ,
wilaya 24 na vijiji 124.
Kwa
upande wake, Rais Museveni aliishukuru Tanzania kwa kutoa vivutio vingi ili
ujenzi wa bomba hilo uendelee kwani bila ya hivyo mafuta hayo hayatakuwa na
faida ukizingatia bei ya mafuta katika soko la dunia imeshuka.
Alisema
sababu kubwa ya bara la Afrika kuwa masikini hadi leo ni kutumia bidhaa
isiyozalisha na kuzalisha bidhaa isiyotumia.
Kwa
mujibu ya takwimu alizotoa, nchi za Afrika Mashariki zinaagiza bidhaa zenye
thamani ya Dola za Marekani milioni 33 na inauza bidhaa zenye thamani ya Dola
milioni 13.8 tu kwa mwaka. Fedha hizo zinafaidisha nchi zilioendelea kuimarisha
uchumi wao na kuziacha nchi za Afrika kubaki masikini.
Kutokana
na hali hiyo, Rais Museveni alizisihi nchi za Afrika zibadilishe mfumo wa
uchumi kwa kujenga viwanda na kuuziana bidhaa. Hivyo, ana matumaini
makubwa kuwa ujenzi wa bomba hilo litaongeza kipato kitakachotumika
kuchochea mabadiliko ya kiuchumi ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkuu wa
Mkoa wa Tanga, Mhe. Martine Shigella aliwahakikishia Marais wawili kuwa mkoa
umejipanga kutoa huduma stahiki kwa wageni wote watakaoingia mkoani humo kwa
ajili ya ujenzi wa bomba hilo.
"Tumejipanga
kuzalisha chakula cha kutosha na tumetenga maeneo ya kujenga nyumba za makazi,
hivyo wawekezaji jitokezeni kuchukua maeneo hayo". Mkuu wa Mkoa alihimiza.
Aliwasihi watu wa Tanga wasomeshe watoto wao ili waweze kuwa na vigezo vya kupata
ajira zitakazotokana na ujenzi wa bomba hilo.
Alihitimisha
kwa kumuomba Rais Magufuli asaidie kuimarisha bandari ya Tanga angalau iwe na
kina cha mita 12 ili iweze kuhudumia meli zote zitakazotumika kubeba shehena za
vifaa vya kujengea bomba la mafuta.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Tanga, 05 Agosti, 2017.
|