HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH
MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE HAFLA ALIYOINDAA KWA AJILI
YA MABALOZI NA VIONGOZI WA TAASISI
ZA KIMATAIFA KUKARIBISHA MWAKA MPYA 2018
IKULU, DAR ES SALAAM, 9 FEBRUARI, 2018
Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki;
Mheshimiwa Brahin Salem Buseif, Balozi wa Saharawi na Kaimu Kiongozi wa Mabalozi nchini;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi na Mashirika ya Kimataifa;
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana:
Habarini
za Jioni. Karibuni sana hapa Ikulu. Nawashukuru, Waheshimiwa Mabalozi, kwa
kukubali mwaliko wangu wa kuhudhuria hafla hii, ambayo kwenye utamaduni wa kidiplomasia,
imezoeleka duniani kote. Tanzania na sisi tumekuwa tukifanya hafla hii kila
mwaka; na bila shaka, tutaendelea kuifanya. Hata hivyo, napenda kuwaarifu kwamba,
mwaka huu, huenda ukawa wa mwisho kwa hafla hii kufanyika hapa Dar es Salaam. Tunatarajia,
kuanzia mwakani, kufanyia Dodoma, Makao Makuu ya nchi yetu.
Hivyo
basi, niwaombe, Waheshimiwa Mabalozi, mwakani, mjiandae kuja Dodoma, ambako viongozi
wengi wa Serikali tayari wamehamia, ikiwa ni pamoja na Mawaziri, Waziri Mkuu na
Makamu wa Rais. Mimi pia natarajia kuhamia mwaka huu. Dodoma ni pazuri na ni
katikati mwa nchi yetu. Napongeza Umoja
wa Mataifa na mashirika yake kwa kuanza mchakato wa kuhamia Dodoma, ambapo mwezi
Desemba 2017, walifungua Ofisi zao za Muda. Hongereni sana. Nawasihi Mabalozi
wengine ninyi muige mfano huu wa Umoja wa Mataifa; na napenda kuwaarifu kuwa
Serikali itagawa bure viwanja mjini Dodoma, ambapo kila Ofisi ya Kibalozi
itapata Ekari 5.5.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za
Kamataifa;
Hivi sasa ni takriban
mwezi mmoja na siku kadhaa umepita tangu kuanza kwa Mwaka Mpya 2018. Kwa utamaduni
wetu sisi Watanzania, mwaka ukianza, hadi mwezi Machi, huwa tunaendelea kupeana
heri ya mwaka mpya. Hivyo basi, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya
Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kutumia fursa
hii, kuwawatakia heri ya Mwaka Mpya wa 2018, ninyi Waheshimiwa Mabalozi na
Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa, familia pamoja na watumishi wenu. Aidha, naomba mnifikishie salamu zangu za Heri
ya Mwaka Mpya 2018 kwa Wakuu wa Nchi pamoja na Taasisi na Mashirika, ambayo mnayawakilisha
vizuri hapa nchini.
Nafahamu kuwa,
kwa baadhi yenu, hii ni mara ya kwanza kushiriki katika hafla hii hapa Tanzania.
Napenda nirudie tena kuwakaribisha sana nchini kwetu. Tanzania ni nchi nzuri;
watu wake ni wakarimu na ina vivutio vingi vya utalii. Nina uhakika, mmeshasikia
kuhusu Visiwa vya Zanzibar, Mlima Kilimanjaro, pamoja na Mbuga za Serengeti na
Ngorongoro. Lakini, mbali na vivutio hivyo, vinavyotambulika ulimwenguni kote,
tunavyo vivutio vingine vingi vizuri. Mti mrefu zaidi Barani Afrika upo hapa
nchini, tena karibu kabisa na Mlima Kilimanjaro. Aidha, tuna Hifadhi ya Taifa
ya Ruaha ambayo ni kubwa zaidi nchini na inasifika kwa kuwa na tembo wengi.
Vilevile, tunayo Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ambayo inasifika kwa kuwa na aina
nyingi za maua ya ndwele ya asili ambayo hayapatikani sehemu nyingine yoyote
duniani; na pia Maporomoko ya Mto Kalambo, kule Rukwa, ambayo ni ya pili kwa
kuwa na kina kirefu Barani Afrika, baada ya yale ya Tugale yaliyopo nchini
Afrika Kusini. Hivyo basi, nawahimiza, mkipata muda, tembeleeni vivutio hivyo
ili mjionee uzuri wa Tanzania. Tunawaomba pia muwahamasishe wananchi wenu kuja
kutembelea vivutio vyetu.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za
Kamataifa;
Bila
shaka, mtakubaliana nami kuwa, duniani kote, katika kipindi cha mwanzo wa mwaka
kama hiki; ni jambo la kawaida kufanya tafakari ya masuala ya mwaka uliopita na
kupanga mikakati ya mwaka mpya. Kwetu sisi Tanzania, Mwaka 2017, ulikuwa wenye
mafanikio makubwa katika ngazi ya kitaifa na kimataifa; japo changamoto nazo
zilikuwepo.
Mathalan,
katika ngazi ya kitaifa, mwaka jana, tuliendelea kutekeleza Mpango wetu wa
Maendeleo wa Miaka mitano wa 2016/17 – 2020/2021, unaolenga kuifanya nchi yetu
kuwa ya uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025, kama ambavyo
Dira ya Taifa ya Maendeleo inavyoelekeza. Na katika kutekeleza Mpango wetu,
tuliweka pia mkazo katika kushughulikia matatizo yaliyokuwa yakitukwamisha katika
kupiga hatua za kimaendeleo. Kama mjuavyo “Ukitaka
kupata maendeleo, badala ya kuongeza tu bidii, jambo la kwanza unatakiwa kushughulikia
au kurekebisha mambo yanayokukwamisha kupata maendeleo”. Mathalan, ukitaka
kujitosheleza kifedha, njia nzuri sio kuongeza bidii ya kutafuta fedha, bali
unatakiwa kwanza kudhibiti matumizi ya kile kidogo unachokipata. Na vilevile, ukitaka
kupungua unene, njia nzuri sio kuanza kufanya mazoezi, bali ni kuacha kufanya mambo
yanayosababisha uwe mnene.
Kwa
kuzingatia hilo, mwaka 2017, tuliendelea kushughulikia matatizo yenye kuikwamisha
nchi yetu kupata maendeleo. Tulizidisha mapambano dhidi ya rushwa, wizi na
uporaji wa rasilimali zetu. Kama mnavyofahamu, miongoni mwa mambo yanayozikwamisha
nchi za Afrika kupata maendeleo ya haraka kiuchumi, Tanzania ikiwemo, ni
vitendo vya rushwa, ukwepaji kodi na uporaji wa rasilimali. Ripoti ya Jopo la
Umoja wa Afrika, ambalo liliongozwa na Rais wa Zamani wa Afrika Kusini, Thabo
Mbeki, iliyotolewa mwaka 2015, ilibainisha kuwa katika kipindi cha miongo
mitatu iliyopita nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo, zimepoteza takriban Dola za Marekani trilioni 1.8, wastani
wa Dola za Marekani bilioni 50 – 80
kwa mwaka. Aidha, Ripoti hiyo iliendelea kueleza kuwa, hivi sasa, nchi za
Afrika, kila mwaka, zinapoteza wastani wa Dola
za Marekani bilioni 150 kutokana na rushwa, wizi, ukwepaji kodi na uporaji
wa rasilimali.
Hivyo
basi, katika mwaka 2017, tumeendelea kuchukua hatua za kudhibiti vitendo hivyo.
Tumepitisha sheria ya kulinda na kusimamia rasilimali zetu ili ziweze
kuinufaisha nchi yetu. Ni wazi kuwa hatua hii huenda haikuwafurahisha baadhi ya
watu, lakini ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi kwa nchi yetu. Hivyo, ilikuwa
ni lazima tuichukue. Sambamba na hilo, tumeendelea kuziba mianya ya ukwepaji
kodi, na hivyo kuweza kuongeza ukusanyaji mapato. Mathalan, katika kipindi cha
mwezi Julai hadi Desemba 2017, tulifanikiwa kukusanya kodi kiasi cha shilingi trilioni 7.87, sawa ongezeko
la asilimia 8.45 ukilinganisha na
mapato ya kipindi kama hicho mwaka 2016. Lakini, kubwa zaidi ni kwamba, mwezi
Desemba 2017, mapato ya kodi yaliyokusanywa ni shilingi trilioni 1.66. Kiwango hiki ni kikubwa zaidi kuwahi kukusanywa
hapa nchini.
Kutokana
na hatua tunazozichukua, uchumi wetu umeendelea kuimarika. Katika nusu ya
kwanza ya mwaka 2017, uchumi ulikua kwa asilimia
6.8, na hivyo kuifanya nchi yetu kuongoza katika Ukanda wetu wa Afrika
Mashariki, lakini pia kuwa miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakua kwa
kasi kubwa Barani Afrika. Tulifanikiwa pia kudhibiti mfumko wa bei, ambapo
mwezi Desemba 2017 ulifikia asilimia 4.
Kwa ujumla, wastani wa mfumko wa bei nchini mwaka jana ulikuwa chini ya asilimia 5.5, kiwango ambacho ni cha chini ukilinganisha na nchi nyingi
za Afrika. Akiba ya fedha za kigeni nayo imeongezeka; na tumeweza kutekeleza
miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuboresha huduma za jamii, hususan zile
zenye kuwagusa wananchi wengi kama vile afya, elimu na maji. Na hii, bila
shaka, ndio moja ya sababu iliyoifanya nchi yetu itajwe kuongoza kwa uchumi
shirikishi kwa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za
Kamataifa;
Mbali
na kushughulikia matatizo ya rushwa, wizi, ukwepaji kodi, n.k.; tumeendelea kushughulikia
changamoto nyingine zilizokuwa zikikwamisha maendeleo ya nchi yetu. Kama
mnavyofahamu, ukiachilia mbali vitendo vya rushwa pamoja na wizi na ubadhirifu
wa rasilimali, changamoto nyingine kubwa inayokabili Bara la Afrika, ni tatizo
la kukosekana kwa miundombinu imara ya usafiri na nishati ya umeme. Mathalan,
kwa mujibu wa Ripoti ya Maendeleo ya Afrika (Africa Progress Report) ya mwaka 2015, watu zaidi ya milioni 600, ambao ni takriban nusu ya watu wote wa Bara la Afrika, hawatumii
umeme. Takwimu pia zinaonesha kuwa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika, zote kwa
pamoja, ukiondoa Afrika Kusini, zinatumia umeme kidogo ukilinganisha na nchi ya
Hispania. Aidha, matatizo haya ya umeme yanachangia kushusha kwa asilimia 2.4 Pato la Afrika. Lakini, ukiachilia
mbali umeme, gharama za usafirishaji Barani Afrika ni kubwa ukilinganisha na
Mabara mengine kutokana na ama kukosekana au udhaifu wa miundombinu ya usafiri.
Mambo haya yote kwa pamoja, ndio yanasababisha
mchango wa Bara la Afrika kibiashara na uwekezaji duniani kuwa mdogo sana.
Kwa
kutambua hilo, tumeendelea kuchukua hatua za kuimarisha miundombinu ya usafiri pamoja
na upatikanaji wa umeme. Sehemu kubwa ya nchi hivi sasa imeunganishwa kwa
barabara; na nyingine zinaendelea kujengwa. Aidha, mwaka 2017 tumeanza ujenzi
wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) kutoka hapa Dar es
Salaam kwenda Mikoa ya Mwanza na Kigoma. Reli hii baadaye itaungana na reli za
kwenda nchi za Burundi na Rwanda. Ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam hadi
Dodoma chenye urefu wa kilometa 712
tayari umeanza na utagharimu kiasi cha shilingi
trilioni 7.062, zote zitatolewa na Serikali yetu. Aidha, hivi karibuni,
wakati wa ziara ya Rais Kagame wa Rwanda, tumekubaliana kuanza ujenzi wa
kipande cha kutoka Isaka kwenda Kigali nchini Rwanda. Sambamba na hayo, tunaendelea na upanuzi wa viwanja vya ndege
vikubwa vya Dar es Salaam, Zanzibar, Kilimanjaro pamoja na vingine takriban 11 katika mikoa mbalimbali lengo likiwa
kukuza sekta yetu ya utalii. Vilevile, tunafanya upanuzi mkubwa na kuboresha
utendaji wa bandari zetu kuu za Dar es Salaam na Mtwara kwa gharama ya takriban
shilingi trilioni 1.1. Tunatekeleza
miradi hii kwa vile takriban asilimia 90
ya shehena ya mizigo inayokuja hapa nchini upitia kwenye bandari hizi. Bandari
hizi, hususan ya Dar es Salaam, inategemewa pia na nchi nyingine jirani. Sambamba
na bandari hizo, tunaiboresha Bandari ya Tanga, hususan baada ya nchi yetu pamoja
na Uganda kuingia makubaliano ya kutekeleza mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta
kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga. Ujenzi wa Bomba hilo lenye
urefu wa kilometa 1,415 utaanza
mwaka huu, ambapo, kama mtakavyokumbuka, mwaka jana, mimi na Rais Museveni wa
Uganda tuliuwekea jiwe la msingi.
Kuhusu
umeme, tunaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kuzalisha, kusafirisha
na kusambaza umeme. Mwaka 2017, tumeanza Awamu ya Tatu ya kupeleka Umeme Vijiji,
ambapo tunatarajia kufikisha umeme kwenye vijiji 7,873. Lengo letu ni kwamba,
ifikapo Mwaka wa Fedha 2020/2021, vijiji vyote nchini viwe vimefikiwa na
miudombinu ya umeme. Tunatekeleza pia miradi mikubwa ya kuzalisha umeme,
hususan kwa kutumia gesi yetu asilia. Aidha, mwaka huu, tunatarajia kuanza
utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa kutumia maji wa Stiglier’s Gorge, ambao utazalisha Megawati 2,100. Tunataka ikifika mwaka
2020, nchi yetu angalau iwe Megawati
5,000 kutoka Megawati 1,460 za
sasa. Nafahamu kumekuwa na maneno maneno kuhusu mradi wetu wa Stiglier’s Gorge; ukihusishwa na
uharibifu wa mazingira katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Ukweli ni kwamba,
hakutakuwa na uharibifu wowote. Tumefanya
tathmini ya kina ya mazingira, na tumeweka mikakati ya kudhibiti uharibifu. Zaidi
ya hapo, mradi huu, utatekelezwa katika eneo dogo sana. Ni chini ya asilimia 4 ya eneo zima la Hifadhi ya Ruaha.
Hivyo, hakuna uwezekano wowote wa kuathiri mazingira ya eneo hilo.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za
Kamataifa;
Kuhusu
azma yetu ya kujenga viwanda, kwa ujumla, tunaendelea vizuri. Kama mjuavyo,
duniani kote, hakuna nchi imewahi kupata maendeleo ya kiuchumi bila kutegemea
viwanda. Na mnafahamu pia kuwa, sekta ya viwanda ni muhimu katika kupiga vita
umaskini na tatizo la ajira. Hivyo basi, mwaka 2017 tumeendelea na jitihada za
kujenga uchumi wa viwanda nchini. Na napenda niwaarifu kuwa, katika kipindi cha
miaka miwili iliyopita, takriban viwanda
3,500 vimejengwa. Na vingine vingi
vinaendelea kujengwa. Nitumie fursa hii, kuishukuru sekta binafsi ya hapa
nchini na kutoka nje kwa namna ilivyoitikia vizuri wito wa Serikali yetu wa kujenga
viwanda. Nafahamu kuwa kuna baadhi ya watu wanaeneza uzushi kuwa sisi
hatuipendi sekta binafsi. Hiyo sio kweli hata kidogo. Tunaipenda sekta binafsi
na tunathamini na kutambua mchango wao. Na tunafahamu kuwa katika dunia ya sasa
sekta binafsi ni mhimili muhimu katika kujenga uchumi.
Kwa
sababu hiyo, tutaendelea kushirikiana na sekta binafsi ya hapa nchini na ile ya
nje. Tutaendelea pia kushughulikia vikwazo mbalimbali vinavyoikabili sekta hii,
ikiwa ni pamoja na kurekebisha sera na sheria zetu pale inapobidi; kuongeza
vivutio vya uwekezaji na biashara; kushughulikia matatizo ya urasimu, rushwa,
utitiri wa kodi, n.k. Hivyo basi, nahimiza sekta binafsi kuendelea kuwekeza
hapa nchini. Na niwaombe Waheshimiwa Mabalozi, nanyi wahimizeni wafanyabishara
kutoka nchi zenu kuja kuwekeza hapa nchini. Nchi yetu ina fursa nyingi za
uwekezaji. Ukiachilia mbali sekta ya viwanda, tuna fursa kwenye sekta za
kilimo, mifugo, uvuvi, utalii, ujenzi wa miundombinu, huduma, n.k. Aidha, nchi
yetu ina soko kubwa. Tunapakana na nchi takriban 8, lakini pia sisi ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na
halikadhalika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, ambazo kwa pamoja zina
idadi ya watu wapatao milioni 500.
Hili ni soko kubwa kwa mwekezaji yeyote.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za
Kamataifa;
Kimataifa, mwaka 2017, nchi yetu
imeendelea kushiriki kikamilifu kwenye masuala mbalimbali katika ngazi ya Kikanda,
Bara na duniani kwa ujumla. Kama mnavyofahamu, msingi mkuu wa Sera yetu ya
Mambo ya Nje ni kuimarisha ujirani mwema, ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Hivyo, tumeendelea kutekeleza Sera hiyo. Mimi pamoja na viongozi wenzangu,
tumefanya ziara na kushiriki kwenye mikutano mbalimbali ya kimataifa. Binafsi, mwaka
jana, nilihudhuria Mkutano wa Umoja wa Afrika na kutembelea nchi ya Uganda. Aidha,
tulipata bahati ya kutembelewa na viongozi kadhaa wa nchi na taasisi za
kimataifa, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn;
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma; Rais wa Uganda, Yoweri Museveni; Makamu wa
Rais wa Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika, Dkt. Makhtar Diop;
Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Yong Kim; na Naibu Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Mhe. Tao Zang; pamoja na
viongozi wengine wengi. Wakati wa ziara hizo, tuliweza kufikia makubaliano
mbalimbali yenye lengo la kuimarisha ushirikiano, hususan kwenye nyanja za
kiuchumi.
Mwaka
jana pia, tumeendelea kushirikiana na nchi pamoja na taasisi nyingine za
kimataifa katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokabili Kanda, Bara
na dunia yetu kwa ujumla. Na moja ya changamoto hizo ni suala la migogoro. Kama
mnavyofahamu, tangu imepata uhuru, mwaka 1961, nchi yetu imekuwa mstari wa
mbele katika kutafuta amani Barani Afrika na duniani. Tumeshiriki na
tunaendelea kushiriki katika harakati za usuluhishi wa migogoro ya Burundi, DRC, n.k. Tunafarijika kuona kuwa
amani nchini Burundi inaendelea kuimarika; na tunaendelea kuwahimiza wahusika
kwenye migogoro nchini DRC, Sudan Kusini, n.k., kumaliza tofauti walizonazo ili
kuweza kurejesha amani kwenye nchi zao.
Mbali
na ushiriki wetu katika usuluhishi wa migogoro, nchi yetu, hivi sasa, ina
vikosi kwenye misheni za kulinda amani nchini DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati,
Lebanon, Sudan na Sudan Kusini. Nitumie fursa hii, kuzishukuru nchi na taasisi
za kimataifa zilizotutumia salamu za rambirambi na pole kufuatia tukio lililotokea
tarehe 8 Desemba 2017 la kuuawa kwa askari wetu 15 na wengine 43
kujeruhiwa, wakati wakiwa katika jukumu la kulinda amani nchini DRC. Tukio
hili, kwa hakika, liliacha majonzi na simanzi kubwa kwa Watanzania. Hata hivyo,
napenda niseme kuwa, pamoja na majonzi makubwa tuliyopata, halijatukatisha tamaa
wala kutuyumbisha kama nchi yetu. Tutaendelea kushiriki katika harakati za
kutafuta amani mahali popote duniani, na tutaendelea kushiriki kwenye misheni
za kulinda amani. Tunaushukuru Umoja wa Mataifa kwa kuunda Timu kuchunguza
chanzo cha tukio la tarehe 8 Desemba, 2017. Tunaihimiza Timu iliyoundwa kukamilisha
mapema uchunguzi wake, ili chanzo kijulikane, wahusika wafahamike na hatimaye
sheria ifuate mkondo wake.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za
Kamataifa;
Katika
mwaka huu wa 2018, Tanzania itaendelea kutekeleza Mpango wake wa Maendeleo wa
Miaka Mitano. Tutazidisha mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu. Tutaendelea
kuimarisha miundombinu ya kiuchumi, hususan ya usafiri na nishati ya umeme. Tutaboresha huduma mbalimbali za kijamii,
hususan elimu, afya a maji.
Sambamba
na hayo, tutaendelea kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya kimataifa. Tutakuwa
wanachama waaminifu wa taasisi za Kikanda, katika Bara na kimataifa, ambazo
sisi ni wanachama. Tutaendelea kushiriki kwenye usuluhishi wa migogoro; na
vikosi vyetu vitandelea kushiriki kwenye misheni za kulinda amani. Vilevile, tutaendelea
kutekeleza mipango na malengo mbalimbali ya kikanda, kibara na kidunia, ikiwemo
Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063 na Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya Malengo
Endelevu ya 2030. Na moja ya malengo ya dunia tuliyopanga kutekeleza, ni kuhakikisha
kuwa ifikapo mwaka 2030 ni kuzuia maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU). Katika
kufikia azma hii, tumeanzisha Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi, ambapo tumelenga
kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 6
katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Hivyo basi, tunawaomba mtuunge
mkono.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za
Kamataifa;
Nafahamu,
katika hafla kama hii, hotuba huwa haziwi ndefu. Lakini leo, nimeeleza mengi. Nimefanya
hivyo, kwa kuwa, kama nilivyosema awali, hii huenda itakuwa mara ya mwisho kwa
sherehe hizi kufanyika hapa Dar es Salaam. Mwakani ni Dodoma. Na kwa sababu
hiyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba mniruhusu nieleze masuala matatu
ya mwisho.
Suala
la kwanza; muda mfupi uliopita, nimeeleza kuwa Tanzania itaendelea kushiriki
kwenye misheni za kulinda amani. Na napenda kusisitiza tena kuwa tutaendelea
kushiriki kwenye misheni hizo. Hata hivyo, wakati nikisisitiza hilo, napenda
kueleza masikitiko yetu kuhusu uamuzi wa Umoja wa Mataifa kuanza kutekeleza
sera ya kupunguza gharama kwenye misheni za kulinda amani. Ni kweli, uendeshaji
wa misheni za kulinda amani ni gharama kubwa. Lakini, ni ukweli pia usiopingika
kuwa, hakuna gharama inayozidi maisha ya watu na umuhimu wa amani. Tanzania
tunauona uamuzi huu utadhoofisha jitihada za kutafuta amani kwenye maeneo yenye
migogoro; na kuhatarisha maisha ya walinda amani pamoja na raia wasio na hatia
wanaoishi kwenye maeneo yenye migogoro. Hivyo basi, tunauomba Umoja wa Mataifa
pamoja na Nchi Tano Wanachama wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa kutafakari upya
uamuzi huo.
Suala
la pili, ni kuhusu uamuzi wetu wa hivi karibuni wa kujitoa kwenye Mpango wa
Majaribio wa Kutafuta Suluhu ya Kudumu ya Tatizo la Wakimbizi (Comprehensive Refugee Response Framework –
CRRF). Kwanza kabisa, napenda kueleza kuwa, nchi yetu, tangu imepata Uhuru
mwaka 1961, imekuwa ni miongoni mwa nchi zenye kupokea wakimbizi wengi. Mpaka
sasa tunaendelea kuwapokea; na bila shaka, tutaendelea kuwapokea, lakini ni wale
tu wenye kustahili; na kwa kuzingatia sheria za kimataifa. Nchi yetu pia
imeweka historia duniani kwa kuwa ya kwanza kutoa uraia kwa wakimbizi wapatao 150,000 kwa wakati mmoja. Hakuna nchi
imewahi kufanya hivyo. Hata hivyo, kutokana na sababu za usalama, tumelazimika
kujitoa kwenye Mpango wa CRRF, ambao pamoja na masuala mengine, unaelekeza
kutolewa kwa ardhi kwa ajili ya wakimbizi, kuwaruhusu kutembea mahali popote na
kutoa vibali vya ajira. Tumejitoa kwa sababu tunadhani kuwa, katika kipindi
hiki cha sasa ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za usalama, ikiwemo ugaidi,
kushamiri kwa biashara ya binadamu na makosa mengine ya kimataifa, utekelezaji
wa Mpango huu unaweza kuleta madhara makubwa ya kiusalama kwa nchi yetu.
Lakini, mbali na hilo, tumesita kuendelea na Mpango huu kutokana na uzoefu
tulioupata wakati tulipotoa uraia kwa wakimbizi 150,000. Wakati tunatoa uraia,
jumuiya ya kimataifa iliahidi ingetoa fedha za kuwapatia makazi na masuala
mengine muhimu. Lakini, mpaka sasa, hakuna fedha iliyotolewa; na badala yake
tumeanza kushawishiwa tukope fedha za kuwahudumia wakimbizi. Hali hii
imetukatisha tamaa; na bila shaka mtakubaliana nasi kuwa, kukopa fedha kwa
ajili ya kuhudumia wakimbizi kutaibebesha Serikali yetu mzigo mkubwa. Hivyo, tunaiomba jumuiya ya kimataifa ielewe
uamuzi wetu wa kujitoa.
Suala
la tatu na la mwisho ni kuhusu taarifa za kukamatwa kwa meli zenye kupeperusha bendera
ya Tanzania, ambazo zimejihusisha kwenye matukio ya uhalifu. Taarifa hizi kwa
hakika zimetusikitisha sana sisi kama Taifa, kwa sababu zinachafua jina na sifa
nzuri ya nchi yetu. Hata hivyo, ningependa kufafanua kuwa, kimsingi, meli hizo si
za kwetu; zimesajiliwa tu hapa Tanzania. Kama mnavyofahamu, usajili wa meli za
nje ni jambo la kawaida na linafanywa na nchi mbalimbali duniani. Hata hivyo,
kutokana na matatizo yaliyojitokeza, Serikali imeamua kuchukua hatua. Tumesitisha
usajili wa meli zote 470 zilizosajiliwa
hapa nchini zenye kupeperusha bendera yetu, na tumeanza kufanya uchunguzi wa
kina kuthibitisha uhalali wa shughuli zao. Zile zitakazobainika kukiuka sheria
na taratibu, tutazifutia usajili. Sambamba na hilo, tumesitisha usajili wa meli
mpya kutoka nje mpaka pale itakapotangazwa tena. Tumechukua hatua hizo, ili
nchi yetu isiwe kichaka cha kujificha wahalifu.
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za
Kamataifa;
Napenda
kuhitimisha hotuba yangu, kwa kurudia tena kuwashukuru kwa kuhudhuria hafla
hii. Aidha, nawashukuru kwa namna ambavyo nchi zenu na mashirika mnayowakilisha
yanashirikiana na nchi yetu katika nyanja mbalimbali: kiuchumi, kisiasa,
kijamii, kiulinzi na usalama, n.k. Mchango wenu ni mkubwa sana. Bila ninyi,
huenda mambo mengi tuliyotekeleza mwaka jana, yasingewezekana. Hivyo basi,
tunawashukuru sana; na kupitia kwenu, tunaendelea kuziomba nchi na taasisi
mnazoziwakilisha ziendelee kutuunga mkono. Kwa upande wetu, tutazidi kuimarisha
uhusiano wetu na nchi, mashirika na taasisi zenu.
Baada
ya kusema hayo, napenda kurudia tena kuwatakia Heri ya Mwaka Mpya 2018. Uwe
mwaka wa Amani na Mafanikio.
“Ahsanteni
kwa kunisikiliza”