Wednesday, March 28, 2018

UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UHOLANZI WASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA MAJI DUNIANI


Wanafunzi wa Shule za Msingi mbalimbali mjini Gouda,

 wakishiriki matembezi huku kila mmoja akiwa amebeba

mgongoni lita 6 za maji kila mmoja.

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe.Irene Kasyanju

 akikaribishwa Gouda na Bibi Rola

Hulsbergen, Mwenyekiti wa Rotary Club ya nchini Uholanzi

 Meya wa Wanafunzi wa Gouda,

 Bi. Romaissa Magou (kulia) akimkabidhi Balozi Kasyanju 

mfano wa Hundi ya kiasi cha fedha kilichokusanywa baada

 ya matembezi hayo.

Balozi Kasyanju na Bibi Hulsbergen wakisikiliza kwa makini

 shairi kuhusu Tanzania lililoandaliwa na wanafunzi wa 

Gouda.

=====================================================

UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UHOLANZI WASHIRIKI KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA MAJI DUNIANI YALIYOFANYIKA MJINI GOUDA, UHOLANZI TAREHE 21 MACHI 2018

Katika kuadhimisha Siku ya Maji Duniani, Manispaa ya mji wa Gouda nchini Uholanzi, kwa kushirikiana na Taasisi za Rotary na shule za msingi za mji huo zilimwalika Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju kushiriki katika matembezi ya hisani maarufu kama Walking for Water yaliyoandaliwa kwa lengo la kuisaidia Tanzania katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa maji safi inayowakabili watoto katika nchi zinazoendelea.

Matembezi hayo yalishirikisha walimu, wazazi na wanafunzi wa shule za msingi za mjini Gouda ambao walitembea umbali wa kilometa 6 huku kila mmoja akiwa amebeba lita sita (6) za maji kuashiria kutambua changamoto kubwa ya ukosefu wa maji safi inayowakabili watoto, hususan katika Nchi Zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Maadhimisho ya Siku hii kwa mwaka huu, yalilenga kuisaidia Tanzania ambapo sambamba na matembezi hayo, kiasi cha Euro 24,021.29 kutoka mji wa Gouda kilichangwa kwa ajili ya kusaidia miradi ya afya na ujenzi wa vyoo inayoendeshwa katika Mikoa ya Tabora na Dodoma. Mhe. Balozi Irene Kasyanju alikabidhiwa mfano wa Hundi ya kiasi hicho cha fedha kilichokusanywa kutokana na michango ya Taasisi husika, wazazi wa wanafunzi na wadau mbalimbali.

Akipokea mfano wa Hundi hiyo Mhe. Balozi Irene Kasyanju, kwa niaba ya wananchi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa shukrani za dhati kwa waandaaji, wadhamini na hususan wanafunzi kwa matembezi pamoja na mchango huo mkubwa na kueleza kuwa utasaidia kubadilisha maisha ya watoto na wananchi wa maeneo husika kwa ujumla. Aidha, Mhe. Balozi Kasyanju alisisitiza umuhimu wa matumizi makini ya maji kwani maji ni muhimu kwa viumbe pamoja na mimea.

Jumla ya kiasi cha Euro 360,000.00 kinatarajiwa kukusanywa kutokana na michango iliyotolewa kutokana na matembezi kama hayo katika miji mingine ya Uholanzi siku hiyo pamoja na Serikali ya Uholanzi kuisaidia Tanzania hususan kwenye mikoa tajwa. 







Monday, March 26, 2018

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA YA UFAFANUZI KUHUSU RAIA WA TANZANIA NCHINI OMAN


Kuna kipande cha video kinasambaa mitandaoni kikiwa na maelezo kuwa raia wa Tanzania wanaoishi nchini Oman wamekusanyika ofisi ya Ubalozi kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana na mateso na adhabu kali wanazopata kutoka kwa mabosi wao.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, baada ya kutazama kipande hicho cha video iliwasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini Oman kwa madhumuni ya kujua usahihi wa jambo hilo.

Ubalozi ulitoa ufafanuzi kuwa uliandaa mkutano wa Watanzania wote wanaoishi Oman na ulipangwa kufanyika katika hoteli ya Golden Tulip jijini Muscat tarehe 23 Machi 2018. Matangazo ya mkutano huo yalitaka Watanzania watakaopenda kushiriki wajisajili kabla ya siku ya mkutano. Watanzania takriban 200 walijisajili na ubalozi ulifanya maandalizi ya ukumbi, vyakula na vinywaji kwa ajili ya watu 300 kwenye hoteli ya Golden Tulip.

Siku ya mkutano ilipowadia, Watanzania zaidi ya elfu moja walijitokeza na kusababisha ugumu wa kuendelea na mkutano kutokana na maandalizi yaliyofanywa yalilenga watu 300.

Kamati ya maandalizi ilipoona ukumbi umejaa na watu walio nje ni weng mara mbili zaidi ya watu waliokuwemo ndani ya ukumbi iliamua kufunga milango na kuwaomba waliochelewa warejee nyumbani.

Uamuzi huo haukuwafurahisha watu waliochelewa, hivyo walishinikiza waingizwe kwenye ukumbi wa mkutano, kitendo ambacho kiliashiria uwezekano wa kutokea vurugu kubwa.

Kutokana na uhalisia huo, Kamati ya maandalizi ambayo ilijumuisha pia viongozi wa Watanzania wanaoishi nchini humo ilishauriana na kuamua kuwa mkutano huo uahirishwe na maandalizi yaanze upya kwa madhumuni ya kupata ukumbi na huduma nyingine zitakazokidhi idadi kubwa ya watu.

Kutokana na ufafanuzi huo, Wizara inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa kipande hicho cha video kimechukuliwa wakati Watanzania wanashinikiza kuingia kwenye ukumbi wa mkutano na sio kwamba wamekusanyika kwenye ofisi ya ubalozi wa Tanzania kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana na mateso wanayoyapata.


-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 26 Machi, 2018

Thursday, March 22, 2018

Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Israeli


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Israeli

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Taifa la Israeli Mhe. Avigdor Liberman. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa kupokelea wageni maalum(VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere,Jijini Dar es Salaam, tarehe 22 Machi,2018.

Mazungumzo haya yalijikita zaidi katika kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Israeli. Akiongea katika mazungumzo hayo Waziri Mahiga alisema ziara hii ina maana kubwa sana kwa Tanzania na itazidi kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizi mbili. Kama inavyofahamika nchi ya Israeli ina Utaalam wa hali ya juu  katika maeneo mbalimbali hasa katika masuala ya Ulinzi na Usalama, Kilimo cha Umwagiliaji, mbinu za kisasa za kupambana na Ugaidi, Uhalifu wa Kimtandao na Teknolojia ya tiba na vifaa tiba.

"Tunatarajia Tanzania kunufaika zaidi  na Utaalam huu hasa katika maeneo ya mbinu za Kilimo bora cha umwagiliaji, Teknolojia ya tiba na vifaa tiba, mbinu za kupambana na Ugaidi, Ulinzi wa Mipaka na Uharamia, Biashara na Ushirikiano wa Teknologia na mafunzo mbalimbali ya kujenga uwezo wa Wataalam wa Tanzania hasa katika Sekta ya Viwanda, Afya na Kilimo" alisema Waziri Mahiga.

Naye Mhe. Liberman amesema Israeli inaishukuru Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia kulinda Amani ya Dunia hasa kwa kushiriki katika Ulinzi wa amani nchini Lebanon na nchi nyingine za afrika zenye migogoro, na ameahidi nchi yake  itaendelea kuongeza maeneo ya Mashirikiano zaidi na Tanzania. 

Katika Ziara hii Mhe. Liberman alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu na Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Mhe. Liberman ameondoka tarehe 22 Machi, 2018, kurejea nchini Israeli baada ya Ziara ya siku tatu(3) hapa nchini.




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akifafanua jambo kwa Waziri wa Ulinzi wa Taifa la Israeli ambaye pia ni Naibu Waziri wa Taifa hilo Mhe. Avigdor Liberman walipokutana kwa mazungumzo tarehe 22 Machi,2018, mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa kupokelea wageni Maalum(VIP) Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.



Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mashariki ya Kati Bw. Ayoub Mdeme na Bi. KisaDoris Mwaseba wakifuatilia mazungumzo hayo
Balozi wa Israeli nchini, ambaye Makazi yake yapo Jijini Nairobi Mhe. Balozi Noah Gal Gendler na Msaidizi wa Viongozi wakiwa katika mazungumzo hayo.
Waziri Mahiga akiagana na Mhe. Liberman baada ya kumaliza mazungumzo, 

Wednesday, March 21, 2018

Waziri wa Ulinzi wa Israeli afanya Ziara Nchini.


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi(Kulia) na Waziri wa Ulinzi wa Taifa la Israeli Mhe. Avigdor Liberman (kushoto) wakizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani), baada ya Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Makao Mkuu ya Jeshi (Ngome), Dar es Salaam, tarehe 21 Machi,2018. 


Lengo la mazungumzo hayo ni kuboresha mashirikiano hasa katika eneo la Ulinzi na Usalama, Israeli imekuwa na Ushirikiano na Tanzania wa muda mrefu na imekuwa ikisaidia katika eneo la Ulinzi na Usalama kwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa Wanajeshi wa Tanzania kama vile kupambana na ugaidi, Uharamia na Ulinzi wa Mipaka. Pia, kama itakavyokumbukwa katika Miaka ya 60 Israeli ilishiriki kikamilifu katika uanzishwaji wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Katika kuendelea kuboresha Mahusiano kati ya nchi hizi mbili, Tanzania  Mwaka 2017 ilifungua Ubalozi wake katika Mji wa Tel Aviv

Mhe. Avigdor Liberman yuko nchini kwa ziara ya Siku tatu(3), ambapo aliwasili tarehe 20 Machi,2018 na anatarajiwa kuondoka   tarehe 22 Machi,2018 


                  Mkutano ukiendelea
Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi,Mhe. Avigdor Liberman, Balozi wa Israeli nchini mwenye Makazi yake Jijini Nairobi Mhe. Noah Gal Gendler wakiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania pamoja na Ujumbe wa Israeli.

Thursday, March 15, 2018

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje atembelea Ofisi za Kamisheni ya Kiswahili ya EAC Zanzibar

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (katikati upande wa kulia), akizungumza na Prof. Kenneth Simala (kushoto), Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.  Pamoja na mambo mengine Prof. Simala alimkabidhi Prof. Mkenda Mpango Mkakati wa Kamisheni hiyo wa mwaka 2017/2022. Kamisheni hiyo ina lengo la kukuza na kutangaza Lugha ya Kiswahili kwa nchi za Afrika Mashariki. Prof. Mkenda alitembelea Ofisi za Kamisheni hiyo zilizopo Zanzibar wakati wa ziara yake ya kujitambulisha kwenye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo ni Wizara ya Muungano. Wakati wa ziara


Prof. Mkenda (katikati) akiwa ameshikilia  Mpango Mkakati wa Kamisheni hiyo huku akisikiliza maelezo kutoka kwa Prof. Simala (kulia). Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Mohammed Hamza
Prof. Mkenda (kushoto) akiwa ameongozana na Prof. Simala (wa pili kushoto), Balozi Hamza (mwenye suti) na Maafisa wengine mara baada ya kutembelea Ofisi za Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.

Wednesday, March 14, 2018

Prof. Mkenda afanya ziara ya kujitambulisha Zanzibar

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (kulia) akiagana na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ofisini kwa Dkt. Mzee, Zanzibar.  Prof. Mkenda alifanya ziara Zanzibar kwa lengo la  kujitambulisha kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo ni Wizara ya Muungano.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Balozi Amina Salum Ali wakati wa ziara ya Prof. Mkenda ya kujitambulisha.
Balozi Amina Salum Ali akimkabidhi Prof. Mkenda bidhaa za viungo mbalimbali vya chakula vinavyozalishwa Zanzibar
Bidhaa za viungo vya chakula zinazozalishwa Zanzibar.
Katibu Mkuu wa WIzara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na  Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Salum Maulid Salum alipo kwenda kujitambulisha Ofisini kwake Zanzibar hivi karibuni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (wanne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Idara ya  Mambo ya Nje Zanzibar alipofika kuwatembelea wakati wa ziara yake ya kujitambulisha aliyoifanya Visiwani humo hivi karibuni.



Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa akutana na Katibu Mkuu wa WTO


Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Samwel Shelukindo akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), Bw. Zurab Pololikashvili. Balozi Shelukindo alikutana na kufanya mazungumzo na Bw. Pololikashvili ambapo pamoja na mambo mengine walizungumzia uwezekano wa Shirika hilo kusaidia miradi mbalimbali hapa nchini.
Balozi Shelukindo na wajumbe wengine