|
Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akipokea taarifa ya kazi kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Norway mwenye makazi yake Stockholm Sweden, Mhe. Dkt. Wilbroad Slaa, katika Hoteli ya Grand Oslo iliyopo kwenye mji wa Oslo, Norway. |
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
ZIARA YA WAZIRI
MAHIGA NCHINI NORWAY
Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania imeihakikishia Serikali ya Norway kuwa inaendelea
kuelekeza nguvu zake kwenye kuweka mikakati sahihi ya kuvutia uwekezaji kutoka
nje ya nchi, ikiwemo nchi ya Norway, ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa
Tanzania.
Hayo yamesemwa na
Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki wa Tanzania alipokutana na Bw. Jon Lamoy, Mkurugenzi wa Shirika la
Maendeleo la Norway lijulikanalo kwa kifupi kama NORAD mwanzoni mwa ziara yake
ya kikazi ya siku tatu Mjini Oslo, makao makuu ya Norway.
Katika mazungumzo
yao, Mkurugenzi Lamoy alimueleza Waziri Mahiga kuwa shirika hilo limekuwa na
uhusiano wa karibu na wa kindugu kwa zaidi ya miongo mitano na nchi ya
Tanzania. Yeye binafsi na washirika wengi wa Tanzania nchini humo wanasifu
utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli hususan kwenye mapambano dhidi ya rushwa. Rushwa
inarudisha nyuma maendeleo kwa kuikosesha nchi mapato, hivyo jitihada za
Tanzania za kupambana na rushwa, hususan kwenye ukusanyaji kodi, zitawawezesha
wananchi wa Tanzania kunufaika na huduma za kijamii na hatimaye kupata
maendeleo kwa haraka.
Hata hivyo
mkurugenzi huyo alitoa angalizo kuwa nia nzuri ya Serikali ya Tanzania ya
kuweka mifumo thabiti ya uwekezaji wenye faida ukiwemo ule wa sekta
ya madini, ni muhimu ikakamilika mapema ili kutoa fursa kwa wawekezaji wapya
kuwekeza kwenye sekta hiyo kwa wakati.
Kwa upande wake,
Mheshimiwa Mahiga alielezea kuwa suala hilo tayari linafanyiwa kazi ambapo
pamoja na Serikali kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji, uwekezaji huo
ni lazima uwe na faida kwa Watanzania na kwa maendeleo ya nchi.
“Serikali ya Rais
Magufuli imedhamiria kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati unaoongozwa na
sekta ya viwanda. Katika kutekeleza hilo, Serikali imepitia na kurekebisha
baadhi ya sheria na mikataba ambayo ilikua inanufaisha upande mmoja.
Marekebisho yanayofanyika sasa yanalenga kwenye kuleta faida kwa pande zote
mbili yaani win win situation”alisisitiza Dkt. Mahiga.
Kwenye mkutano huo
ambao pia ulihudhuriwa na Prof. Adolf Mkenda, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Balozi wa Tanzania nchini Norway,
Dkt. Wilbroad Slaa mwenye makazi yake nchini Sweden kwa pamoja walielezea kuwa
marekebisho hayo, yatakapokamilika, yatarutubisha mazingira ya uwekezaji
Tanzania ikiwemo mikataba itakayoridhiwa na Bunge ambayo italeta manufaa kwa
pande zote mbili kama zifanyavyo nchi nyingi duniani, ikiwemo Norway.
Awali kabla ya
mkutano huo, Mheshimiwa Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa
Kampuni ya STATOIL yenye makao yake makuu Mjini Oslo, ambayo kwa sasa nchini
humo inajulikana kama Equinor. Kampuni ya STATOIL Tanzania ni mshirika mkubwa
nchini Tanzania kwenye shughuli za utafutaji na upatikanaji wa gesi.
Makamu wa Rais
Mtendaji wa kampuni ya Statoil Bw. Lars Christian Bacher alielezea shughuli za
kampuni hiyo Tanzania ikiwemo kujenga uwezo wa ndani ya nchi kwa Watanzania
kuijua na kuendesha sekta hiyo muhimu kwa ukuaji wa uchumi. Kwa sasa kampuni
hiyo inatoa ufadhili wa masomo ya shahada ya uzamili kwa Watanzania kumi kila
mwaka kwenye eneo la mafuta na gesi.
Bw. Bacher pia
alieleza kuwa uwekezaji wa kampuni hiyo kwenye masuala ya gesi ni wa muda
mrefu, na matunda yake yanachukua muda kuonekana. Lakini yakishatoka yataongeza
mara mbili upatikanaji wa nishati ya umeme nchini Tanzania, ambapo itaongeza
uzalishaji wa viwanda pamoja na faida nyingine nyingi za kiuchumi.
Ujumbe wa Waziri
Mahiga ulisifu jitihada za kujenga uwezo kwa Watanzania na kuelezea kuwa hatua
hiyo itasadia sana kwenye kutoa elimu kwa Watanzania ili wawe na matarajio
sahihi ya matokeo ya shuguli za uwekezaji wa kampuni hiyo nchini Tanzania.
Waziri Mahiga aliwasihi kuendelea kujenga uwezo wa kada ya kati ya wataalam wa
gesi kwa kushirikiana pia na vyuo vya ndani ya nchi ili utaalamu huo uendelezwe
nchi nzima.
Waziri Mahiga yupo
nchini Norway kwa ziara ya kikazi kuanzia tarehe 18 hadi 20 Juni 2018, kufuatia
mualiko wa mwenyeji wake Mhe. Ine Eriksen Soreide, Waziri wa Mambo ya Nje wa
Norway. Ziara hiyo imekuja baada ya Tanzania na Norway kusaini makubaliano ya
ushirikiano mwaka 2017.
Mbali na kufanya
mazungumzo na mwenyeji wake, Mheshimiwa Mahiga na ujumbe wake wanatarajiwa
kukutana na makampuni ya Norway yanayowekeza Tanzania pamoja na kuzungumza
kwenye Jukwaa la Oslo kuhusu uthabiti wa amani kwenye Eneo la Maziwa Makuu na
mchango wa nchi jirani.
Jukwaa la Oslo
linakutanisha watu mashuhuri duniani wanaoshughulika na utatuzi wa migogoro
duniani akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Mkutano huu hufanyika mara moja
kila mwaka kujadili masuala ya utatuzi wa migogoro duniani.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 19 Juni, 2018