Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kushoto) akimsikiliza mdau kutoka sekta binafsi, Bw. Mustapha Hassanal ambaye alishiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uganda. =================================================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TANZANIA NA UGANDA ZAKUBALIANA KUIMARISHA
SEKTA YA BIASHARA
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
amesema Serikali ya Tanzania na Uganda zimedhamiria kuimarisha sekta ya
biashara kwa kushughulikia changamoto zote zilinazoikabili sekta hiyo.
Kauli
hiyo imetolewa na Mhe. Rais Magufuli leo tarehe 6 Septemba 2019 wakati wa ufunguzi
rasmi wa Kongamano la Kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Uganda
lililofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amesema kwamba wakati sasa umefika wa kutumia makongamano na mahusiano ya kihistoria, kidiplomasia na kindugu yaliyopo kati ya Tanzania na Uganda ili kusukuma mbele agenda ya maendeleo ya kiuchumi kwa maslahi ya nchi hizo mbili. Aliongeza kwamba nchi hizi mbili zina rasilimali za kutosha kujiletea maendeleo ikiwemo utalii, madini, mifugo, uvuvi, kilimo na gesi na mafuta.
Akionesha kusikitishwa na kiwango kidogo cha ufanyaji biashara kati ya Tanzanai na Uganda, Mhe. Rais Magufuli alieleza kuwa kwa miaka mingi kiwango hicho bado kipo chini sana ukilinganisha na nchi nyingine zinazoshirikiana kibiashara na Tanzania. Alisema hadi sasa ni Kampuni 22 pekee za Uganda zimewekeza nchini huku tani 167,000 pekee za mizigo zikipita Tanzania kwa mwaka 2017/2018 tofauti na tani milioni 7.1 za bidhaa zilizoingizwa nchini humo.
Akielezea
sababu zilizoshusha kiwango cha biashara kati ya nchi hizi mbili, Mhe. Rais Magufuli
alisema kuwa ni pamoja na urasimu kutoka kwa watendaji wa Serikali hizi mbili,
kuwepo kwa vikwazo vya kodi na visivyo vya kodi; miundombinu hafifu ya usafiri
na usafirishaji na ufanisi mdogo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania.
Hata
hivyo, Mhe. Rais Magufuli alifafanua kuwa, Serikali ya Tanzania iliitambua changamoto
hiyo mapema na kuanza kuchukua jitihada za makusudi za kukabiliana nayo ili
kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kati ya Tanzania na Uganda. Alisema jitihada
hizo ni pamoja na kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirshaji kwa kuanza
ukarabati wa reli ya kati na ununuzi wa vichwa vya treni; upanuzi wa Bandari ya
Dar es Salaam kwa gharama ya takribani Shilingi Trilioni moja na ujenzi wa Reli
ya Kiwango cha Kimataifa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Aidha,
Mhe. Dkt. Magufuli aliongeza kuwa, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na
Uganda zimefufua vivuko kwa ajili ya kusafirisha mizigo kutokea Bandari ya
Mwanza kupitia Bandari ya Portbell nchini Uganda pamoja na kufufua shirika la
ndege la Tanzania na Uganda ambapo Ndege za Shirika la Tanzania zilianza safari
nchini Uganda mwezi Agosti 2018 huku ndege za Shirika la Uganda zikizindua
safari zake nchini mwezi Agosti 2019.
Jitihada
zingine ni kudhibitiwa kwa vitendo vya uhalifu kwenye Bandari pamoja na kuimarishwa
kwa vituo vya kutoa huduma za pamoja mipakani na kuendelea kubuni mipango
mahsusi ya kitaifa yenye lengo la kuboresha biashara na uwekezaji.
“Nawakaribisha
sana Uganda tufanye biashara yenye tija kwani kimsingi tumechelewa. Hivyo ni imani
yangu kuwa Mkutano huu utakuwa mwanzo wa biashara kubwa kwa watu wetu”
alisisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais
alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa pande zote
kuheshimu sharia na kanuni zilizowekwa na nchi husika na zile za Jumuiya ya
Afrika Mashariki ili kujenga uchumi wa nchi hizi mbili. Vilevile, alitoa wito
kwa washiriki wa Kongamano hilo kuchangamkia fursa za kibiashara zilizopo kati
ya nchi hizi mbili na kutumia kongamano hilo kuainisha changamoto zote za
kibiashara na kutoa mapendekezo ya namna ya kuzitatua.
Akizungumzia
Mradi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi
Chongoleani, Tanga ambao unarajiwa kutengeneza zaidi ya ajira 20,000, Mhe. Rais
Magufuli alitoa rai kwa Serikali ya Uganda kuongeza kasi ya kukamilisha masuala
yaliyosalia ili mradi huo uanze mapema.
Kwa
upande wake, Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni aliwataka watendaji wa
Serikali zote kutambua umuhimu wa sekta ya biashara na mchango wake katika
maendeleo ya nchi zao badala ya kuendelea kuweka vikwazo na urasimu.
Aidha,
Mhe. Rais Museveni alimshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuupa kipaumbele Mradi wa
Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka nchini kwake hadi Tanzania na kuahidi
kutekeleza yale yote waliyokubaliana ili mradi huo uanze kutekelezwa haraka
iwezekanavyo.
Awali
akizungumza kwenye Kongamano hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi alisema kuwa, Tanzania na Uganda
zimefanya mkutano wa tatu wa Tume ya pamoja ya Ushirikiano ambapo masuala ya kuimarisha
ushirikiano katika sekta mbalimbali yalijadiliwa. Alisema kuwa, Mkutano huo
pamoja na mambo mengine pia uliteua Maafisa
kutoka pande hizo mbili kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano
yaliyofikiwa.
Naye Mwenyekiti
wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, Bw. Salum Shamte ambaye
alizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara na sekta binafsi nchini alisema kuwa,
ana imani kubwa kuwa Kongamano hilo la biashara litakuwa mwanzo mzuri wa kukuza
biashara kati ya Tanzania na Uganda, kwani litatoa nafasi kwa wafanyabiashara
na wawekezaji wa Uganda na Tanzania kuelewa kwa undani fursa zilizopo kati ya
nchi hizi mbili. Pia alisisitiza umuhimu wa kampuni za Uganda kufanya biashara
kwa ubia na kampuni za Tanzania na vivyo hivyo kwa kwa Tanzania ili kurahisisha
biashara miongoni mwao.
Wakati
wa Kongamano hilo ambalo limewashirikisha zaidi ya wafanyabiashara na
wawekezaji 1,000 kutoka Tanzania na Uganda, Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais
Museveni walishuhudia kusainiwa kwa Hati za Makubaliano ya ushirikiano katika masuala
ya Uhamiaji, Magerereza, Kilimo na Tume ya Pamoja ya Ushirikiano.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar
es Salaam.
6 Septemba 2019
|