Saturday, October 5, 2019

RAIS MAGUFULI AZINDUA KITUO CHA HUDUMA PAMOJA (OSBP) MPAKANI TUNDUMA/NAKONDE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John  Pombe Magufuli, akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), alipowasili katika Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja (OSBP) Mpakani Tunduma/Nakonde.

Kituo hicho kimefunguliwa leo tarehe 5 Oktoba 2019, na 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John  Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Changwa Lungu.

Wakizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza katika zoezi la uzinduzi wa kituo hicho, kwa nyakati tofauti Mhe. Dkt. Magufuli na Mhe. Lungu walieleza kuwa wataendelea kudumisha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliodumu kwa muda mrefu baina ya nchi hizo mbili (Tanzania na Zambia) kwa maendeleo ya wananchi.

Aidha, Rais Magufuli alizungumzia umuhimu wa kuiongezea ufanisi Reli ya TAZARA ili kuchagiza kasi ya biashara baina ya Tanzania na Zambia.

Kadhalika, Mhe. Rais Magufuli amewahimiza Wananchi wa mji wa Tunduma kuulinda mpaka kwa kuepuka kujenga katika eneo la mpaka huo.

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amewapongeza Wananchi wa Mji wa Tunduma kwa kuendelea kulinda na kudumisha amani mpakani hapo. Vilevile ametumia fursa hiyo kuwasihi kuendelea na juhudi za kukuza biashara baina yao na Zambia ili kuboresha maisha yao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John  Pombe Magufuli akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, alipowasili katika Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja (OSBP) Mpakani Tunduma/Nakonde kwa ajili ya ufunguzi.
Taswira ya Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja (OSBP) Mpakani Tunduma/Nakonde.
Taswira ya Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja (OSBP) Mpakani Tunduma/Nakonde.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John  Pombe Magufuli, akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) alipowasili katika Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) Tunduma/Nakonde
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John  Pombe Magufuli  akifuatilia maelezo kutoka  kwa Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) kabla ya kuanza kwa zoezi la ufunguzi wa Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) Tunduma/Nakonde. 
Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb)  akizungumza na wananchi (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) Tunduma/Nakonde.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John  Pombe Magufuli, na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Changwa Lungu ,wakiangalia jiwe la msingi wakati wa zoezi la ufunguzi wa Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja (OSBP) mpakani Tunduma/Nakonde tarehe 5 Oktoba, 2019 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John  Pombe Magufuli, na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Changwa Lungu, pamoja na Wafadhili wa Ujenzi wa Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja (OSBP) mpakani Tunduma/Nakonde wakipanda mti katika zoezi la uzinduzi wa Kituo hicho 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John  Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Changwa Lungu wakikata utepe kuashiria kufunguliwa rasmi kwa Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja (OSBP) mpakani Tunduma/Nakonde tarehe 05 Oktoba, 2019.

Thursday, October 3, 2019

MAANDALIZI KUELEKEA UFUNGUZI WA KITUO CHA PAMOJA (OSBP) MPAKANI TUNDUMA/NAKONDE


UBALOZI WA TANZANIA, UHOLANZI WASHIRIKI KWA MAFANIKIO TAMASHA LA EMBASSY FESTIVAL

Balozi wa Tanzania, The Hague, Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju akitoa maelezo kwa mgeni aliyetembelea Banda la Tanzania wakati wa Tamasha maarufu kama Embassy Festival lililofanyika hivi karibuni. Tamasha hilo huandaliwa na Manispaa ya The Hague kwa kushirikiana na Balozi za nchi mbalimbali zenye Ofisi zake The Hague kwa lengo la kutangaza tamaduni za nchi hizo.
Balozi Irene Kasyanju (mwenye fulana kulia) pamoja na Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Bibi Naomi Zegezege Mpemba (wa pili kushoto) wakitoa maelezo kuhusu Tanzania kwa wageni
waliotembelea Banda la Tanzania, huku Bw. Denis Baraka (wa kwanza kushoto)  ambaye ni Mtanzania na mdau wa shughuli za utalii ambaye kwa sasa anasoma nchini Ujerumani na ambaye kutokana na kupenda kutangaza utalii wa Nchi yake alisafiri kutoka Kiel, Ujerumani kuja Uholanzi kuungana na Ubalozi pamoja na Watanzania wengine kwenye Embassy Festival.
Mwonekano wa Banda la Tanzania na wageni waliotembelea.
Balozi Irene Kasyanju (wa tatu kushoto) akiwa na walishiriki wa maonesho ya mavazi pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Ubalozi wakiwa wamevaa fulana za kuitangaza Tanzania ambao ni Bw. Issa Lupatu, Mwambata Fedha wa Ubalozi (wa pili kulia aliyevaa miwani) na Bw. John Appolo Kilasara,Katibu wa Chama cha Watanzania wanaoishi Uholanzi (Tanzanians in the Netherlands – TANE) ambaye pia ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha ISS nchini Uholanzi
Balozi Irene Kasyanju akiwa na Bi. Bahia Kihondo, Mtanzania aliyeandaa maonesho ya mavazi
pamoja na watoto ambao walifungua maonyesho hayo kwa kusoma shairi fupi kwa lugha ya Kidachi na Kiswahili. 
Watazamaji wa maonesho ya mavazi yaliyotangaza utamaduni wa Mtanzania walikusanyika kwa
wingi kutazama maonesho hayo

Mwonekano wa Banda la Tanzania kwa sehemu ya ndani, likiwa limefurika Diaspora waliofika
kulitembelea na kupata fursa ya kuzungumza na mmoja wa wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania Uholanzi, Bi Linda Mkony (aliyevaa koti katikati) na Bw. Denis Baraka, wakiwa pia wamevaa
na fulana maalum za kuitangaza Tanzania
Washiriki wakionesha vazi lenye michoro ya wanyama “animal prints” wanaopatikana kwenye mbuga za Tanzania
kwa mtindo wa kisasa
Maonesho ya mavazi yakiendelea– vazi la khanga.

 Washiriki wa maonyesho ya mavazi wakiwa katika vazi la Kimasaai.
====================================================================================================

UBALOZI WA TANZANIA, UHOLANZI WASHIRIKI KWA MAFANIKIO
TAMASHA LIJULIKANALO KAMA “EMBASSY FESTIVALTHE HAGUE”

Ubalozi wa Tanzania The Hague, Uholanzi umeshiriki katika Tamasha maarufu la Embassy Festival lililofanyika mwezi Septemba, 2019. Tamasha hili huandaliwa na Manispaa ya The Hague kwa kushirikiana na Balozi za nchi mbalimbali zenye Ofisi zake nchini humo kwa lengo la kutangaza utamaduni wa nchi hizo.

Kama ilivyokuwa kwa balozi nyingine, Ubalozi wa Tanzania ulikuwa na banda lake kwa ajili ya kuonesha utamaduni wa Tanzania. Kwa kushirikiana na Watanzania wanaoishi Uholanzi (Diaspora), Ubalozi ulitumia fursa hiyo kutangaza utamaduni pamoja na vivutio vya utalii zikiwemo mbuga za wanyama.

Ubalozi uliandaa maonesho ya mavazi (fashion show) kwa kuonesha vazi la Kimasai (shuka na shanga, n.k.), pamoja na khanga. Aidha, Ubalozi uliandaa maonesho ya mavazi na vitambaa vyenye animal prints za Simba, Chui (The big five), Twiga na Pundamilia na kuvionesha kwa mtindo wa kisasa na hivyo kuvutia watu wengi.

Diaspora wajasiriamali walipata fursa ya kuuza bidhaa zao mbali mbali za asili kama vile khanga, chai, kahawa ya Tanzania, shanga, hereni, viatu na bangili. Watu wengi waliotembelea Banda la Tanzania walifurahia korosho, chai na kahawa vyote kutoka Tanzania vilivyokuwa vimeandaliwa mahsusi kwa ajili yao.

Ubalozi umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuitangazaTanzania kupitia tamasha hilo ambapo idadi kubwa ya watu walishiriki na kuchukua vipeperushi vya kutangaza utalii wa nchi.

PROF. KABUDI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA NAIBU KATIBU KATIBU MKUU UMOJA WA MATAIFA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamgamba John Kabudi (Mb) akislimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dkt. Amina Mohammed katika ofisi za Umoja huo zilizopo New York Marekani.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dkt. Amina Mohammed akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) hayupo pichani,wakati akimkaribisha kwa mazungumzo katika ofisi za Umoja huo zilizopo New York Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiteta jambo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dkt. Amina Mohammed (Hayupo pichani) wakati alipokwenda katika ofisi za Umoja wa Mataifa zilizopo New York Marekani.

Naibu katibu mkuu wa Umija wa Mataifa Dkt. Amina Mohammed na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi na ujumbe wake (hawapo pichani) katika ofisi za Umoja wa Mataifa zilizopo New York Marekani.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dkt. Amina Mohammed na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) na ujumbe wake. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizopo New York,Marekani.


Sunday, September 29, 2019

DKT. SALIM ATUNUKIWA NISHANI YA JUU YA URAFIKI YA JAMHURI YA WATU WA CHINA

Dodoma, 29 Septemba 2019

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

DKT. SALIM ATUNUKIWA NISHANI YA JUU YA URAFIKI YA JAMHURI YA WATU WA CHINA

Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Xi Jinping, leo asubuhi tarehe 29 Septemba 2019 amemtunukia Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa. Dk. Salim Ahmed Salim, Nishani ya Juu ya Urafiki ya Jamhuri ya Watu wa China ikiwa ni sehemu ya matukio ya maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China iliyofanyika jijini Beijing.  Mheshimiwa Dkt. Salim anakuwa mwafrika wa kwanza kupewa heshima na tuzo hiyo ya juu katika historia ya China.

Nishani hiyo ilipokelewa na Bi. Maryam Salim, Binti ya Dk. Salim Ahmed Salim ambaye pia ni Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Albania kwa niaba ya Baba yake kutokana na kushindwa kuhudhuria kwa sababu za kiafya. Katika tukio hilo, Serikali ya Tanzania iliwakilisha na Balozi wa Tanzania nchini China Mheshimiwa Mbelwa Kairuki.

Hafla hiyo kubwa ya kitaifa ya kukabidhi nishani ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Chama na Serikali ya China akiwemo Makamu wa Rais Mheshimiwa Wang Qishan, Waziri Mkuu Mheshimiwa Li Keqiang, Spika wa Bunge Mheshimiwa Li Zhanshu na Wajumbe wote wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Baraza la Taifa.

Mbali na Dk.Salim,  wengine waliotunukiwa Nishani ya Urafiki ni pamoja na Kiongozi wa Chama cha Kikoministi cha Cuba Jenerali Raul Castro, Dada wa Mfalme wa Thailand Maha Chakri Sirindhorn, Kiongozi wa Jumuiya ya Urafiki ya China na Urusi Ndugu Galina Kulikova, Waziri Mkuu Mstaafu wa Ufaransa Jean-Pierre Raffarin na Bi  Isabel Crook  kutoka Canada.

Vilevile  Rais Xi alitoa Nishani  ya Jamhuri na Nishani ya Heshima ya Taifa kwa raia 36 wa China kwa kutambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa la China kupitia kazi zao katika fani mbalimbali.

Nishani ya Juu ya Urafiki ya Taifa la China imetolewa kwa Dkt. Salim  kutokana na mchango wake wa kuiwezesha Jamhuri ya Watu wa China kuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 1971 alipokuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.  Aidha, mchango wa Dk. Salim katika kuimarisha mahusiano kati ya China na Tanzania wakati aliposhikilia nyadhifa mbalimbali umetajwa kama sababu ya kutunukiwa Nishani hiyo. Vilevile, mchango wa Dk.Salim katika kujenga mahusiano kati ya China na Afrika akiwa na nafasi ya Katibu Mkuu wa OAU umetajwa kuwa sababu nyingine ya kutunukiwa Nishani.

Tukio la Kutoa Nishani limetangazwa moja kwa moja na Televisheni zote za Jamhuri ya Watu wa China na kushuhudiwa na watu zaidi ya Milioni 500.

Kwa mujibu wa maelezo ya Balozi wa Tanzania nchini China Ndugu Mbelwa Kairuki Kupitia tukio la leo, mamilioni ya Wachina hususan vijana wamepata fursa ya kufahamu nafasi na mchango wa Tanzania na Bara la Afrika katika historia ya taifa lao. Aidha, tukio la leo limeifanya Tanzania kufahamika kwa watu wengi zaidi nchini China kupitia tukio mara moja. Hatua hiyo itaamsha udadisi na hamasa miongoni mwa Wachina wengi wa kizazi kipya kutaka kuifahamu zaidi Tanzania. Hali hii yaweza kujitafsiri katika fursa kubwa ya kukua kwa utalii, biashara na wawekezaji ikizingatiwa kuwa  wananchi wa China hutoa mwitikio mkubwa kwa nchi ambazo husemwa vizuri na kuthaminiwa na Serikali yao.

Aidha Balozi Kairuki ameeleza kwamba maadhimisho ya miaka 70 ya Jamhuri ya Watu wa China mwaka huu yanaambatana na maadhimisho ya miaka 55 ya urafiki na udugu kati ya China na Tanzania kufuatia kuanzishwa kwa mahusiano rasmi ya kidiplomasia mwaka 1964. Uhusiano wa China na Tanzania uliotokana na uhusiano mzuri wa waasisi wa mataifa haya mawili, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mao Tsetung. Uhusiano huo umeendelezwa na viongozi wa pande zote mbili ambao umekuwa ukiimarika siku hadi siku. Uhusiano huu umekwenda mbali zaidi ya uhusiano kati ya Serikali na Serikali na kushamiri kwa uhusiano wa watu kwa watu.

Ni kwasababu hiyo, katika maadhimisho ya miaka 70 ya Taifa la China, Jumuiya ya Urafiki wa watu wa China na Tanzania ni miongoni mwa Jumuiya za mataifa 17 yenye urafiki wa majira yote na China walioalikwa  kushiriki kwenye maadhimisho hayo na tarehe 1 Oktoba 2019 watakuwa na gwaride lao maalum. Katika jumuiya hizo 17, Kutoka Barani Afrika ni Tanzania na Zambia ndio watahudhuria.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Bi. Maryam Salim mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim akiwa na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping mara baada ya kupokea tuzo kwa nimba ya Baba yake.


 Bi. Maryam Salim mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salimakiwa na Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Mbelwa Kairuki mara baada ya kupokea nishani kwa nimba ya baba yake.