Friday, February 21, 2020

Rais wa Zanzibar afungua Kikao cha Mawaziri wa SADC

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema “Kufanyika kwa Mkutano wa SADC ni hatua muhimu katika kujenga matumaini mapya ya wananchi kuhusiana na maafa, tukizingatia kwamba katika miaka ya hivi karibuni  kumekuwa na ongezeko kubwa la  maafa pamoja na viashiria  vyake  katika nchi wanachama wa SADC.”Ameyasema hayo wakati akifungua  Mkutano wa Mawaziri wenye Dhamana ya Menejimenti ya Maafa kwa Nchi za SADC, leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu  Mhe. Jenista Mhagama amesisitiza “Ushiriki wa kisekta katika kukabiliana na maafa ni njia pekee ya kupunguza madhara ya  maafa kwa Nchi wanachama wa SADC”, leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar, wakati wa Mkutano wa Mawaziri wenye Dhamana ya Menejimenti ya Maafa kwa Nchi za SADC.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Stergomena Tax akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa kwanza wa Mawaziri wenye dhamana ya kusimamia maafa na kusisitiza kuwa  “Majanga hayana urasimu kitu muhimu kushirikiana kwa pamoja katika kukabiliana nayo pindi yanapotokea nchini”, leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar.  
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi  wanachama wa SADC wakiwemo Mawaziri, Washauri wa Rais na Makamanda wa Vikosi vya ulinzi na Usalama wakisikiliza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na Maafa Zanzibar, leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar.
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi  wanachama wa SADC, wakifuatilia  mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar. 
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi  wanachama wa SADC, wakifuatilia  mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar. 
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi  wanachama wa SADC, wakifuatilia  mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wenye dhamana ya Menejementi ya maafa kwa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika SADC baada ya kufungua Mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar.


Na. OWM, ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein amesema maeneo ya visiwa yapo katika hatari  kubwa  zaidi ya kukumbwa na maafa ukilinginisha na maeneo mengine duniani, hivyo alitoa wito kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuja na mikakati imara itakayoainisha mbinu za kutambua na kuwahi viashiria vya maafa kabla madhara hayajatokea.

“Tuna jukumu la kuendelea kushirikiana kati ya Serikali zetu, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Kimataifa, Taasisi za Utafiti, Sekta Binafsi, Taasisi za Kidini, Taasisi za Fedha na  Mashirika yasiyo ya Serikali, Asasi za Kiraia na Vyombo vya Habari katika suala hili. Tukifanya hivyo, itakuwa tumeitekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya mkutano huu isemayo:  “Ushiriki wa kisekta kwenye kupunguza madhara ya maafa ni njia bora ya kujenga uhimili katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.” 

Rais Shein amesema hayo leo tarehe 21, Februari, 2020 Zanzibar alipokuwa anafungua kikao cha Mawaziri wa nchi za SADC wenye Dhamana ya Menejimenti ya Maafa.

Rais Shein ameeleza kuwa maafa yana madhara makubwa katika nchi, endapo hakutakuwa na mipango thabiti ya kukabiliana nayo na kutolea mfano namna vimbunga vya Idai, Kenneth na vinginevyo vilivyosababisha vifo, uharibifu wa mali na miundombinu katika nchi za Malawi, Zambia, Zimbawe, Msumbiji na Comoro.

Rais Shein amefafanua kuwa maafa yanabadilisha agenda za maendeleo ya nchi mbali mbali duniani kwa sababu fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinabadilishwa matumizi kukidhi dharura za maafa kwa gharama kubwa zaidi.

Akitoa mfano wa mpango wa Sendai wa kukabiliana na maafa ambao unaonesha kati ya mwaka 2015 hadi 2018 nchi za Afrika zimekubwa na matukio 160 ya maafa ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu. Ameeleza kuwa mpango huo unaonesha kuwa zinahitajika Dola za Marekani bilioni 3700 ili nchi zilizoathirika ziweze kurejesha hali yake ya kawaida. “Kiasi kikubwa hiki cha fedha kinatumika kujenga upya miundombinu iliyoharibika badala ya kujenga miundombinu mipya”, Rais Shein alisema.

Rais wa Zanzibar amewambia wajumbe wa mkutano huo hatua zilizo fanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha uhimili wa kukabiliana na maafa, kwa kuzingatia kuwa Zanzibar ni miongoni mwa visiwa ambavyo hupata madhara ya maafa.

Hatua hizo ni pamoja na kuandaa Sera ya kukabiliana na maafa ya mwaka 2011 na sheria yake ya mwaka 2015, kuanzisha Kamisheni inayoshughulikia masuala ya maafa na mpango wa mawasiliano wakati wa maafa. 

Aidha, amebainisha hatua nyingine kuwa ni pamoja na mpango wa elimu ya kujikinga na maafa kwa wanianchi, kuimarisha vyombo vya usafiri wa baharini ikiwemo ununuzi wa meli mbili kubwa za MV. Mapinduzi II ya abiria na MV. Ukombozi II kwa ajili ya kubeba mafuta, ujenzi wa vituo vitatu vya uokozi, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kufuatilia usafiri wa majini ikwemo ndege zisizokuwa na rubani na boat za uokoaji na kuzimia moto.

Dkt. Shein amesema ili kukabiliana na maafa ya mafuriko ambayo huwa yanakikumba kisiwa hicho kutokana na mvua za mwezi Oktoba hadi Desemba na mwezi Machi hadi Juni, nchi hiyo kwa msaada wa Serikali ya Falme za Kiarabu (UAE) imejenga kituo cha kuhifadhi watu wanaoathirika na mafuriko ambacho kina nyumba 30 zenye miundombinu yote kwa ajili ya maisha ya mwanadamu.

Aidha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua mkopo wa Dola za Marekani milioni 93 kwa ajili ya ujenzi wa mitaro inayopeleka maji baharini wakati wa mafuriko. Ujenzi huo ambao upo katika hatua za mwisho utakapokamilika, Dkt. Shein aliwahakikishia wajumbe wa mkutano huo kuwa, Zanzibar itaweza kuepuka mafuriko au Kupunguza kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Jenista Muhagama (Mb)ameeleza kuwa malengo ya kuanzishwa kwa Kamati ya Mawaziri wenye Dhamana ya Maafa likiwemo lengo la kulishauri Baraza la Mawaziri wa nchi za SADC namna ya kupunguza madhara ya maafa. Alisema maafa yaliyosababishwa na majanga ya vimbunga vya Idai na Kenneth katika nchi za SADC, ukame na mafuriko ambayo hayana mipaka yamedhihirisha umuhimu wa nchi hizo kuwa na mpango wa ushirikiano wa kukabiliana na maafa.

Alieleza ili kwenda sambamba na juhudi za kikanda na kimataifa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli itaendelea kuimarisha uwezo wake wa usimamizi wa maafa katika Nyanja zote. 

Amebainisha hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ni pamoja na kuandaa Mkakati wa Taifa wa Kupunguza Madhara ya Maafa; kuandaa Wasifu wa Janga la Mafuriko na Ukame; kuandaa Mpango wa Dhamira ya Taifa wa Utekelezaji wa Makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi; kuandaa Mfumo wa Taifa wa Ufuatiliaji wa Taarifa za Gesi Joto;  Kuandaa Mipango ya Kukabiliana na Dharura za Afya ya Binadamu, Mifugo na Wanyama; kuandaa Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mazao baada ya Kuvuna.

Naye Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena Tax aliwambia wajumbe wa mkutano huo kuwa majanga hayataki urasimu yanapotokea, yanahitaji hatua za haraka na zinazoeleweka ili kuyakabili ipasavyo kabla hayajasababisha madhara makubwa.

Dkt. Tax alifafanua kuwa mkutano huo kufanyika Zanzibar ni fursa nzuri kwa nchi za SADC kujua vizuri muungano wa Tanzania na Zanzibar ambao umedumu kwa miaka mingi sasa. Aidha, alisema itakuwa fursa nzuri kwa nchi hizo kujionea vivutio vya kipekee vya kisiwa cha Zanzibar ambacho kina umaarufu mkubwa duniani kote.

Serikali ya Tanzania imekuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kwanza wa Kamati ya Mawaziri wanaohusika na Menejimenti ya Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika baada ya Tanzania kuchukua rasmi nafasi ya Mwenyekiti wa jumuiya kuanzia mwezi Agosti, 2019 kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi mwezi Agosti, mwaka huu (2020).  Hatua hii inatokana na utaratibu wa kawaida wa mzunguko wa kushika nafasi hiyo kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.
MWISHO.


BALOZI IBUGE AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA KUWAIT NCHINI TANZANIA


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mhe. Balozi Mubarak Mohammed Alsehaijan katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Pamoja na mambo mengine, mazungumzo hayo yalijadili mambo mbalimbali ikiwemo kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Kuwait kupitia Nyanja mbalimbali ikiwemo uwekezaji wa miradi na biashara pamoja na uundwaji wa tume ya kudumu ya pamoja ya ushirikiano.

Aidha, Mhe. Balozi Alsehaijan alitumia fursa hiyo kumkabidhi Katibu Mkuu, Balozi Ibuge salamu za rambirambi kufuatia ajali zilizotokea hapa nchini hivi karibuni.

Kwa upande wake Balozi Ibuge, alimweleza Mhe. Balozi Alsehaijan umuhimu wa kuendeleza jiji la Dodoma na kumkaribisha jijini Dodoma.

Mazungumzo hayo yamefanyika siku moja baada ya Ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania kusheherejea 59 ya Uhuru wake na miaka 29 ya ukombozi wa taifa hilo yaliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge, akimkaribisha Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mhe. Balozi Mubarak Mohammed Alsehaijan leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mhe. Balozi Mubarak Mohammed Alsehaijan akimuelezea jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge walipokutana katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge, akimulezea jambo Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mhe. Balozi Mubarak Mohammed Alsehaijan leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge, akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mhe. Balozi Mubarak Mohammed Alsehaijan leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



VACANCY ANNOUNCEMENT



PRESS RELEASE

VACANCY ANNOUNCEMENT AT THE COMMONWEALTH SECRETARIAT

The Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation has received vacancy notification from the Commonwealth Secretariat inviting qualified Tanzanians to apply for the post of Economic Adviser-Trade Policy Analysis.

Application details can be found through the Secretariat’s website, http://thecommonwealth.org/jobs. Closing date for application is Friday 28th February, 2020.

“The Ministry encourages qualified Tanzanians to apply”.



Issued by:
Government Communication Unit,
Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation,
Dodoma.
21ST February, 2020.

Wednesday, February 19, 2020

UBELGIJI NA TANZANIA  ZAPANIA KUDUMISHA URAFIKI NA KUONGEZA USHIRIKIANO.
 Ubelgiji na Tanzania zimedhamiria kudumisha urafiki na kuongeza zaidi ushirikiano katika ubia wa maendeleo, uwekezaji, biashara, utalii na masuala mengine ya Kikanda na kimataifa. Hayo yalielezwa wakati wa mazungumzo baina ya Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mheshimiwa Jestas Abuok Nyamanga na  Mfalme wa Ubelgiji, Mtukufu Philippe  wakati Balozi Nyamanga akiwasilisha Hati zake za utambulisho kwa Mfalme huyo katika kasri yake jijini Brussels  tarehe 6 Februari 2020.
Wakati wa utambulisho huo, Balozi Nyamanga aliwasilisha salaam za Mheshimiwa Dkt John Pombe Joesph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Mfalme huyo na kueleza jinsi Tanzania inavyoridhika na urafiki na ushirikiano mzuri uliodumu kwa miaka mingi baina ya nchi mbili na imedhamiria kuueleza ushirikiano huo na kupanua wigo wake.
Balozi Nyamanga katika mazungumzo hayo  amemweleza  Mfalme Philippe, juhudi za pekee zinazofanywa na serikali inayoongozwa na Rais Magufuli katika kuweka msingi wa uchumi wa viwanda;  kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu; kuboresha mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji; na kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mipango mbalimbali  ya kitaifa, kikanda na kimataifa. 
Aidha, Balozi Nyamanga amemweleza Mfalme Philippe kuwa Tanzania imedhamiria kushirikiana na Ubelgiji hususan katika ubia wa maendeleo, biashara na uwekezaji wenye kuleta faida kwa pande zote.
 Kwa upande wake,   Mfalme huyo wa Ubelgiji ambaye kwa kuipenda Tanzania miaka ya nyuma  amewahi kuja Tanzania kwa mapumziko binafsi Zanzibar na kueleza kuwa Tanzania ni nchi muhimu kwa Ubelgiji na hivyo nchi yake itaendeleza ushirikiano zaidi na Tanzania katika kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo nchini pamoja na kushirikiana katika masuala ya amani na usalama hususan kwa wa nchi za Maziwa Makuu na ajenda zingine zinazogusa maslahi ya nchi zetu mbili kimataifa. 
Ubelgiji ni miongoni mua Nchi zinazoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania ikiwa inashika nafasi ya kumi kati ya nchi zaikai ya 90 zilizowekeza nchini Tanzania. Aidha kutokana na ushirikiano mzuri uliopo Tanzania ni kati ya nchi 14 zinazoendelea duniani ambazo Ubelgiji imeingia nazo makubaliano maalum ya ushirikiano wa ubia wa maendeleo (Developmet Coop[eration Framework)


Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mheshimiwa Jestas Abuok Nyamanga akiwa na  Mfalme wa Ubelgiji, Mtukufu Philippe mara baada ya kuwasilisha Hati zake za utambulisho kwa Mfalme huyo katika kasri yake Jijini Brussels - Ubelgiji Februari 06,2020.

Tuesday, February 18, 2020

Katibu Mkuu Mwaluko azitaka sekta zishirikiane kukabili maafa


Na. OWM, ZANZIBAR

“Tatizo la athari za maafa yanayotokana na majanga ya asili linahitaji ushiriki wa sekta zote ili kukabiliana nalo ipasavyo, katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)” Mwaluko.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Zanzibar na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko wakati alipokuwa anafungua kikao cha SADC cha Makatibu Wakuu wenye dhamana ya maafa katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambaye yeye ni mwenyekiti.

 Mwaluko amesema nchi zote za SADC zina uzoefu wa masuala ya maafa, hivyo ni matarajio yake kuwa kazi waliyopewa ya kuandaa nyaraka kwa ajili ya mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya maafa utakaofanyika siku ya Ijumaa tarehe 21 Februari 2020,  uweze kufikia malengo yake.

Katika kikao hicho, Makatibu Wakuu wataandaa nyaraka itakayo ainisha mikakati na programu za kukabiliana na maafa na mpango unaobainisha namna nchi za SADC zilivyojipanga kukabiliana na maafa yanapotokea katika ukanda huo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mtendaji wa SADC wa Masuala ya Ushirikiano wa Kikanda, Dkt. Thembinkosi Mhlongo  alieleza kuwa athari za maafa zikiwemo vifo, uharibifu wa mali na miundombinu zimezikumba takribani nchi zote za SADC. Hivyo amesisitiza umuhimu wa nchi hizo kushirikiana kwa pamoja kuandaa mikakati ya menejimenti ya maafa.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar, Bw. Abdallah Hassan Mitawi amewaeleza  wajumbe wa kikao hicho kuwa nchi za SADC zimelipa umuhimu mkubwa suala la kukabiliana na athari za maafa na hilo linadhihirishwa na ushiriki wa nchi 15 kati ya 16 wanachama wa SADC katika mkutano huo.

Mkutano huo unaofanyika kwenye Hoteli ya Madinat AL Bahir iliyopo Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar unatarajiwa kuhitimishwa kwa kikao cha ngazi ya Mawaziri tarehe 21 Februari 2020 ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.

“Ushiriki wa kisekta kwenye Kupunguza madhara  ya maafa ni njia  bora ya kujenga Uhimili  katika ukanda wa nchi wanachama wa  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)”
MWISHO.


Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko akifafanua umuhimu wa ushiriki wa kisekta kwenye Kupunguza madhara ya maafa, wakati akifungua kikao cha SADC cha Makatibu Wakuu wenye dhamana ya maafa katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambapo yeye ni mwenyekiti wa kikao hicho, leo tarehe 18 Februari 2020, Zanzibar.

Naibu Katibu Mtendaji wa SADC wa Masuala ya Ushirikiano wa Kikanda, Dkt. Thembinkosi Mhlongo akifafanua umuhimu wa Nchi  za SADC kuwa na mikakati ya kukabili maafa yanayo zikabili, wakati wa kikao cha SADC cha Makatibu Wakuu wenye dhamana ya maafa katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC, leo tarehe 18 Februari, 2020, Zanzibar
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar, Bw. Abdallah Hassan Mitawi akifafanua namna ya nchi za SADC zinavyoathirika na maafa ya asili, wakati wa kikao cha SADC cha Makatibu Wakuu wenye dhamana ya maafa katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC, leo tarehe 18 Februari, Zanzibar


Baadhi ya makatibu wakuu kutoka Tanzania, wakifuatilia kikao cha SADC cha Makatibu Wakuu wenye dhamana ya maafa katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC, leo tarehe 18, Februari, 2020, Zanzibar, (katikati), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi,anayeshughulikia Mifugo,  Profesa Olesante Ole Gabriel (kulia kwake), Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Dkt. Faraij Mnyepe,  na Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya Ndani ya Nchi, Christopher Kadio.

Baadhi ya maafisa waandamizi kutoka ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wakifuatilia kikao cha SADC cha Makatibu Wakuu wenye dhamana ya maafa, leo tarehe 18 Februari, 2020, Zanzibar.


Baadhi ya maafisa waandamizi kutoka ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wakifuatilia kikao cha SADC cha Makatibu Wakuu wenye dhamana ya maafa, leo tarehe 18 Februari, Zanzibar, Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali, Jimmy Matamwe,(kulia), Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Zanzibar , Makame Khatibu Makame na Naibu Mkurugenzi wa Kamisheni hiyo, Muhidin Ali Muhidin
Makatibu Wakuu wenye dhamana ya maafa katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC,wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo, leo tarehe 18, 2020, ambapo kauli mbiu ya mkutano huo ni “Ushiriki wa kisekta kwenye Kupunguza madhara  ya maafa ni njia  bora ya kujenga Uhimili  katika ukanda wa nchi wanachama wa  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)”
Makatibu Wakuu na maafisa waandamizi wenye dhamana ya maafa katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC,wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo, leo tarehe 18, Februari, 2020, ambapo kauli mbiu ya mkutano huo ni “Ushiriki wa kisekta kwenye Kupunguza madhara  ya maafa ni njia  bora ya kujenga Uhimili  katika ukanda wa nchi wanachama wa  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)”


NAIBU WAZIRI DKT.NDUMBARO AHITIMISHA ZIARA YAKE KATIKA ENEO LA USHOROBA WA MTWARA


Sunday, February 16, 2020

WAZIRI KABUDI: WATUMISHI FANYENI KAZI KWA BIDII NA USHIRIKIANO


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amewataka Watumishi wa Wizara hiyo kuchapa kazi kwa bidii na kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Katibu Mkuu mpya, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge.

Mhe. Prof. Kabudi ametoa rai hiyo jana jijini Dodoma wakati wa kikao na Watumishi wa Wizara ambapo pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilitoa fursa ya kutakiana heri ya mwaka mpya 2020 na kumkaribisha Wizarani Katibu Mkuu Mpya, Balozi Kanali Ibuge.

Aidha, Mhe. Prof. Kabudi aliwaeleza watumishi hao kuwa, mwanzo wa mwaka ni kipindi kizuri cha kujipanga na kuweka mikakati ya namna bora ya kutekeleza majukumu  kwa ajili ya maendeleo ya Taifa ikiwa ni pamoja na kufahamu vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Joseph Pombe Magufuli.

Kadhalika amewataka kufanya kazi kwa bidii, kujitambua na kujenga umoja  na ushirikiano katika kutekeleza majukumu hayo kikamilifu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge ameahidi ushirikiano kwa watumishi wa Wizara na kuwakumbusha kuwa kila mmoja ana wajibu mkubwa wa kuchangia maslahi mapana ya Taifa ilimradi kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa kuendelea kujituma, kuwa tayari kurekebishwa, kuwa watiifu na kuwa tayari kupokea maelekezo.

"Watumishi wenzangu, kila mmoja hapa ana mchango mkubwa kwa maslahi ya Taifa letu. Ninasisitiza kuwa mwendelee kujituma, kufanya kazi kwa weledi, kuwa watiifu, kuwa tayari kurekebishwa na kuwa tayari kupokea maelekezo. Binafsi nitaendelea kutoa usikivu kwenu kama ilivyokuwa kwa watangulizi wangu" alisema Balozi Ibuge.

Kuhusu changamoto mbalimbali zinazoikabili Wizara, Balozi Kanali Ibuge amewataka Watumishi wote kushirikiana kuzitatua kwani hakuna changamoto ya kudumu endapo Watumishi wote watakuwa kitu kimoja.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na Watumishi wa Wizara wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge akiongea na watumishi wa wizara wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dodoma

 Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia kikao kilichofanyika jijini Dodoma 




NAIBU WAZIRI DKT.NDUMBARO AHITIMISHA ZIARA YAKE KATIKA ENEO LA USHOROBA WA MTWARA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amehitimisha ziara yake katika Mikoa  inayopitiwa na mradi wa maendeleo wa kuboresha miundombinu ya Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (Mtwara Corridor). Mradi huu unahusisha ujenzi wa bandari ya Mtwara (ambao unaendelea kwa kasi), ujenzi wa barabara katika kiwango cha lami kuanzia Bandari ya Mtwara hadi bandari ya Mbamba Bay iliyopo Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma sambamba na ujenzi wa bandari hiyo.

Lengo la ziara hii ilikuwa ni kuangalia hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu ya bandari na barabara katika ushoroba huo, kufanya mazunguzmzo na viongozi wa Serikali za Mikoa na Wilaya, ambapo Mheshimiwa Ndumbaro alitumia nafasi hiyo kuhimiza Mamlaka za Mikoa na Wilaya, kulinda na kuboresha uhusinao wa kidipolomasia na nchi tunazopakana nazo katika ukanda huo ili kujenga mazingira rafiki ya kibiashara, wakati huu ambao Serikali ya Awamu ya Tano imeboresha miundombinu inayowezesha kuzifikia nchi hizo kiurahisi zaidi.

Ujenzi wa miundombinu katika Ukanda wa Kusini mwa Nchi unachochea ukuaji wa biashara katika ukanda huo kwa kurahishisha usafirishaji na mawasiliano na kuzifikia kiurahisi Nchi jirani za Malawi, Kaskazini mwa Msumbiji na Zambia.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri wa Mambo Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Ndumbaro aliambatana na Balozi wa Malawi nchini Mhe.Glad Chembe Munthali, ambaye amefurahishwa na kuridhishwa na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga mazingira rafiki ya kibiashara na nchi jirani kwa kuboresha miundombinu inayoziwezesha nchi hizo kunufaika na huduma za bandari nchini kiurahisi na kwa gharama nafuu. 

Kadhalika, nia ya Mhe. Munthali Balozi wa Malawi nchini, katika ziara hiyo ilikuwa ni kuangalia kwa namna gani wafanyabiashara kutoka nchini kwake watanufaika na uboreshwaji wa miundombinu ya ushoroba wa Mtwara katika kusafirisha bidhaa zao kwa muda mfupi na gharama nafuu. 

Aidha, kwa nyakati tofauti Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius G. Byakanwa, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina Mndeme na Mkuu wa Wilaya Nyasa Mhe. Isabela Chilluba wameelezea utayari wao wa kuratibu na kusimamia shughuli na fursa za biashara zinazotokana na maboresho ya miundombinu katika ukanda huo.

Ziara hii ni mwendelezo wa jitihada zinazofanywa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa  kushirikiana na Mamlaka mbalimbali za ndani katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kukuza biashara na kuvutia uwekezaji nchini.   

Ujenzi wa barabara ya Mtwara hadi bandari ya Mbamba Bay kwa kiwango cha lami unafikia ukingoni, mkandarasi anaendelea na ujenzi wa sehemu iliyosalia (Mbinga hadi Mbamba bay) ambapo anataraijia kukabidhi barabara hiyo Septemba, 2020.

Ujenzi wa miundombinu katika ushoroba wa Mtwara umeleta mapinduzi makubwa ya maendeleo ya uchumi na kijamii katika Mikoa ya Kusini mwa Tanzania sambamba na kuliongezea Taifa mapato.  
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius G. Byakanwa (kulia) wakiwa kwenye mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius G. Byakanwa akielezea jambo kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro kwa kutumia kielelezo cha ramani, walipokuna kwa mazungunzumzo wakati wa ziara ya Dkt.Ndumbaro katika ushoroba wa Matwara. 
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius G. Byakanwa (kulia) na Balozi wa Malawi nchini Mhe.Glad Chembe Munthali (kushoto) wakiwa katika mazungumzo walipokutana wakati wa ziara ya Mhe. Dkt. Ndumbaro katika Mkoa huo
Kutoka kulia ni Mhe.Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Balozi wa Malawi nchini Mhe.Glad Chembe Munthali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius G. Byakanwa, Bw. Alfayo Kidata Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, na Mhe. Evod Mmanda Mkuu wa Wilaya ya Mtwara wakiwa katika picha ya pamoja.
Mhe.Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  akisalimiana na Wafanyakazi wa Bandari ya Mtwara alipotembelea Ofisi za Bandari hiyo wakati wa ziara yake mkoani humo.
Mhe.Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akizungumza na wafanyakazi wa Bandari ya Mtwara (hawapo pichani). Aliwahimiza kujituma na kuongeza ubunifu ili kuongeza  ufanisi na tija wa bandari hiyo ambayo ukarabati wa kuiboresha unaendelea.
Mhe.Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na Watendaji wa Bandari ya Mtwara na Viongozi wa Mkoa alipotembelea eneo la bandari ya Mtwara
Kutoka kushoto; Mhe.Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Christina Mndeme Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, na Mhe.Glad Munthali Chembe Balozi wa Malawi nchini wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma. 
Mhe.Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisalimiana na Mhe. Isabela Chilluba Mkuu wa Wilaya ya Nyasa alipowasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja
 Mkuu wa Wilaya Nyasa Mhe. Isabela Chilluba akitoka maelezo kwa Mhe.Dkt. Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  na Ujumbe wake katika moja ya fukwe na eneo la bandari ya Mbamba Bay iliyopo katika Ziwa Nyasa. 
Picha ya pamoja