Wednesday, September 2, 2020

KATIBU MKUU WA MAMBO YA NJE AFANYA MAZUNGUMZO NA MRATIBU MKAZI WA UMOJA WA MATAIFA NCHINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Generali Wilbert A. Ibuge akizungumza na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini,
Bw. Zlatan Milišić
 alipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 2 Septemba 2020.

Katika mazungumzo yao walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa ambapo Balozi Ibuge alitoa shukrani kwa Shirika hilo kwa ushirikiano uliopo kati yake na Serikali hususan kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kwa upande wake, Bw. 
Milišić aliipongeza Tanzania kwa kudumisha amani na utulivu ambao ni chanzo cha uchumi wa nchi kustawi. Pia aliipongeza kwa kuendelea kuchangia vikosi vya ulinzi wa amani kwenye mataifa mbalimbali  yenye  migogoro duniani na kuitakia Tanzania uchaguzi wa amani na utulivu hapo mwezi Oktoba 2020.

Ujumbe wa Wizara ukimjumuisha Bw. Hangi Mgaka, Katibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Bi. Prisca Mwanjesa, Afisa Mambo ya Nje wakifuatilia mazungumzo kati ya Balozi Ibuge na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Milišić (hawapo pichani)

Mazungumzo yakiendelea
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ibuge akiwa katika picha ya pamoja na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Milišić mara baada ya kukamilisha mazungumzo yao.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ibuge akiagana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini, Bw. Milišić mara baada ya mazungumzo kati yao.

 

Monday, August 31, 2020

KATIBU MKUU WA MAMBO YA NJE AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA KENYA NCHINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Generali Wilbert A. Ibuge akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dan Kazungu alipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 31 Agosti 2020 kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao walizungumzia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kwenye nyanja za diplomasia, biashara na uwekezaji. Pia Balozi Kazungu alitumia fursa hiyo kuipongeza Tanzania kwa kuwa nchi ya uchumi wa kati pamoja na kuongoza kwa mafanikio Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kipindi cha mwaka mmoja. Kadhalika aliitakia Tanzania uchaguzi wa amani na mafanikio hapo mwezi Oktoba 2020. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Generali Wilbert A. Ibuge akifafanua jambo wakati wa mazungumzo kati yake na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dan Kazungu

Sehemu ya ujumbe uliofuatana na Balozi Ibuge ukifuatilia mazungumzo. Kushoto ni Bw. Hangi Mgaka, Katibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Bw. Isaac Isanzu, Afisa Mambo ya Nje.

Balozi Dan Kazungu akimkabidhi Balozi Ibuge zawadi ya picha zinazowaonesha waasisi wa mataifa ya Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Kenya, Hayati Mzee Jomo Kenyatta na Uganda, Hayati Mzee Milton Obote. Balozi Ibuge alizipokea picha hizo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ambaye aliahidiwa picha hizo na Serikali ya Kenya wakati wa ziara yake nchini humo mwezi Novemba 2019.

Mhe. Balozi Kazungu akimkabidhi Balozi Ibuge zawadi ya picha inayowaonesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta. Picha hiyo ilipigwa wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Rais Kenyatta aliyoifanya hapa nchini mwezi Julai 2019.








 

Friday, August 28, 2020

KATIBU MKUU WA MAMBO YA NJE AZUNGUMZA NA BALOZI WA UBELGIJI NCHINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Generali Wilbert A. Ibuge akizungumza na Balozi wa Ubelgiji hapa nchini, Mhe. Peter van Acker. Mazungumzo hayo ambayo yalifanyika kwa njia ya mtandao yalijikita kwenye kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ubelgiji. Katika mazungumzo hayo, Balozi Ibuge aliishukuru Serikali ya Ubelgiji kupitia kwa Balozi huyo kwa ushirikiano mkubwa iliyoonesha kwa Tanzania katika mapambano dhidi ya janga la ugonjwa wa COVID-19 na ushirikiano katika miradi mbalimbali ikiwemo ya sekta ya maji kwenye baadhi ya mikoa hapa nchini. Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 28 Agosti 2020 huku Balozi Ibuge akiwa jijini Dodoma na Balozi Peter van Acker akiwa jijini Dar es Salaam

Balozi Ibuge akimsikiliza Balozi Peter van Acker wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika kwa njia ya mtandao.

Balozi Ibuge akiwa na ujumbe aliofutana nao wakati wa mazungumzo kati yake na Balozi wa Ubelgiji hapa nchini, Mhe. Peter van Acker (hayupo pichani). Kulia ni Bw. Hangi Mgaka, Katibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Bw. Anthony Mtafya, Afisa Mambo ya Nje

Kikao kikiendelea

FURSA YA AJIRA KWA WATANZANIA - WHO, AUDA-NEPAD PAMOJA NA UN - HABITAT




 

Thursday, August 27, 2020

KATIBU MKUU BALOZI BRIGEDIA JENERALI WILBERT IBUGE AFANYA MAZUNGUMZO NA ENG. STEVEN MLOTE


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Eng. Steven Mlote walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi za Wizara zilizopo Mtumba, jijini Dodoma.

Katika mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine Eng. Mlote alitoa taarifa fupi ya maendeleo ya miradi mbalimbali ya Jumuiya ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara zinazoiunganisha nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, nishati na Vituo vya Kutoa Huduma Pamoja Mipakani (OSBPs)

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Eng. Steven Mlote wakiwa katika mazungumzo. Wengine kutoka kulia ni Balozi Stephen P. Mbundi  Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama na Hangi Mgaka, Afisa Mambo ya Nje

Mazungumzo yakiendelea


Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Miundombinu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Kamugisha Kazaura, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Eng. Steven Mlote,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama Balozi Stephen P. Mbundi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo.

Thursday, August 13, 2020

TANZANIA YAJIVUNIA MAFANIKIO WAKATI WA UENYEKITI WA SADC

 Tanzania imejivunia mafanikio yaliyopatikana wakati ikiwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mafanikio hayo yameelezewa katika Mkutano wa 40 wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ulifanyika kwa njia ya mtandao jijini Dar es Salaam.

Kupitia mkutano huo, Prof. Kabudi  amekabidhi uenyekiti wa Baraza la Mawaziri kwa Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Monica P. Clemente kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji Mhe. Verónica Nataniel Macamo Dlhovo   

Prof. Kabudi amesema pamoja na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID 19) jumuiya ya SADC imeendelea kufanya kazi zake, mikutano yake chini ya uongozi wa Tanzania kwa ufanisi wa hali ya juu kwa kupitia njia ya mtandao (video conference)

"Nasema ni mafanikio makubwa kwa sababu Jumuiya nyingine za kikanda zimeshindwa kufanya hivyo, sisi ndiyo jumuiya pekee iliyoanza utaratibu huu wa aina hii ya mikutano kwa sababu kwetu tuliona COVID 19 ni changamoto ambayo haiwezi kutuzuia kufanya shughuli zetu,". Amesema Prof. Kabudi

Prof. Kabudi ameongeza kuwa mbali na kupambana a janga la COVID 19, mafanikio mengine ni kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne katika jumuiya ya SADC, lugha nyingine ni Kiingereza, Kireno na Kifaransa.   

"Lugha ya Kiswahili kwa Tanzania ni lugha ya ukombozi wa Afrika, ndiyo lugha iliyotumika wakati wa kuwafundisha wapigania uhuru mbinu za kuwasiliana wakati wa ukombozi kwa mataifa ya Afrika," Amesema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi ameyataja mafanikio mengine yaliyopatikana wakati Tanzania ikiwa mwenyekiti wa SADC ni kusimamia na kukamilika kwa Mwongozo wa kusafirisha bidhaa na huduma kwa nchi wanachama katika kipindi cha (COVID-19). Mwongozo huo umelenga kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma mbambali baina ya nchi wanachama.

Tanzania imewezesha agenda ya viwanda kutekelezwa ambapo wakati wa COVID 19 tumeweza kuongeza uwezo wetu wa kutengeneza dawa kwa kuwa mataifa makubwa duniani mara baada ya kuibuka kwa covid 19 walisitisha kuuza dawa katika nchi nyingine ili wazitumie dawa hizo ndani ya nchi zao.

"Tunaimani kuwa msingi uliowekwa wakati wa COVID 19 utaimarisha jitiada zetu za kuwa na uchumi wa viwanda, uchumi wa kati na uchumi wa juu. Na sisi imekuwa jambo la faraja kubwa kuingia katika uchumi wa kati kabla ya miaka mitano iliyokuwa imepangwa hapo awali," Amesema Prof. Kabudi.

"Chaguzi katika nchi za Malawi, Mauritius, Namibia zimefanyika kwa amani na utulivu. Ii imedhihirisha wazi kuwa demokrasia katika ukanda wetu inazidi kukua………haya yote ni mafanikio makubwa kwetu tukiwa mwenyekiti wa SADC," ameongeza Prof. Kabudi.

Nae Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Monica Clemente aliyemuwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje Msumbiji, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa aliyofanya wakati wa Uenyekiti wake wa SADC.

Amefanya mambo makubwa kabisa kwa nchi wanachama wa SADC na amekuwa kama Mwalimu kwa nchi nyingine kutokana na maendeleo yaliyopatikana wakati wa uongozi wake akiwa mwenyekiti wa SADC.

"Sisi Msumbiji tunashukuru kwa kupokea Uenyekiti wa SADC na tunaahidi kujitahidi kadri ya uwezo wetu kuendeleza yale yote yaliyofanywa na Tanzania wakati akiwa Mwenyekiti, kwani Tanzania amekuwa mwalimu kwetu na nchi nyingine za SADC," amesema Balozi Monica.

Mkutano wa 40 wa baraza la mawaziri umehudhuriwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Afya , Maendeleoya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa wakifuatilia mkutano kwa njia ya Mtandao (Video Comnference) 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akifungua mkutano wa 40 wa Baraza la Mawaziri uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia Mtandao (Video Comnference)

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akikabidhi uenyekiti wa SADC ngazi ya mawaziri kwa Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Monica P. Clemente ambaye amemwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje Msumbiji Mhe.Verónica Nataniel Macamo Dlhovo   

Baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali wakifuatilia Mkutano wa 40 wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao  jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa wakifuatilia mkutano kwa njia ya Mtandao (Video Conference) 
Baadhi ya maafisa waandamizi/Makatibu Wakuu wakifuatilia mkutano wa 40 wa Baraza la Mawaziri uliofanyika leo kwa nnjia mtandao jijini Dar es Salaam 

Sunday, August 9, 2020

MKUTANO WA 40 WA SADC KUFANYIKA JIJINI DODOMA

Mkutano wa 40 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaotarajiwa kufanyika tarehe 17 Agosti, 2020 kwa njia ya mtandao (video conference) Ikulu Chamwino Jijini Dodoma.

 

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge amesema mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utatanguliwa na vikao vya Kamati ya kudumu ya Maafisa Waandamizi/Makatibu Wakuu na Mkutano wa Baraza la Mawaziri itakayoanza kufanyika tarehe 10 -13 Agosti, 2020 jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao (video conference).

 

"Kulingana na taratibu na miongozo ya uendeshaji wa SADC, nafasi ya uenyekiti hushikiliwa na nchi wanachama kwa kupokezana kwa kipindi cha mwaka mmoja mmoja. Tanzania imekuwa Mwenyekiti tangu Mwezi Agosti, 2019 na inatarajwa kukabidhi Uenyekiti kwa Jamhuri ya Msumbiji katika Mkutano huo. Aidha, itakumbukwa kuwa mara ya mwisho Tanzania ilishika nafasi hii mwaka 2003," Amesema Balozi Ibuge.


Ameongeza kuwa, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa sasa wa SADC,  atakabidhi Uenyekiti kwa Mheshimiwa Philipe Jacinto Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji tarehe 17 Agosti 2020 jijini Dodoma kwa njia ya Video Conference. 

 

Balozi Ibuge ameongeza kuwa, kwa kuwa kwa sasa Kiswahili ni moja kati ya lugha rasmi za mikutano ya SADC, lugha hiyo itatumika katika ngazi ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri na ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali.

 

Aidha, Katibu Mkuu, Balozi Ibuge amesema kuwa, kutokana na janga la COVID-19 na  mwongozo uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) juu ya kufanya mikutano ya ana kwa ana, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania italazimika kukabidhi uenyekiti kwa njia ya mtandao ambapo Balozi wa Msumbiji hapa nchini atakabidhiwa uenyekiti kwa niaba ya nchi yake. Hali kadhalika, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji atakabidhi Uenyekiti kwa Serikali ya Jamhuri ya Msumbiji kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Katika hatua nyingine, Balozi Ibuge amesema kuwa mkutano huo utaongozwa na kauli mbiu ambayo ni “Miaka 40 ya Kuimarisha Amani na Usalama, Kukuza Maendeleo na kuhimili Changamoto zinazoikabili Dunia” ambapo kauli mbiu hiyo inatakiwa kutekelezwa na nchi zote Wanachama.

Mkutano huo unatarajiwa kushirikisha Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi 16 wanachama wa SADC wakiwa katika nchi zao. Nchi hizo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Angola, Jamhuri ya Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Muungano wa Visiwa vya Comoro, Ufalme wa Eswatini, Ufalme wa Lesotho, Jamhuri ya Namibia, Jamhuri ya Visiwa vya Shelisheli, Jamhuri ya Afrika Kusini, Jamhuri ya Malawi, Jamhuri ya Msumbiji, Jamhuri ya Mauritius, Jamhuri ya Madagascar na Jamhuri ya Zambia, Jamhuri ya Zimbabwe.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Briedia Jenerali, Wilbert Ibuge akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Briedia Jenerali, Wilbert Ibuge akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam

 Mkutano ukiendelea jijini Dar es Salaam


Friday, August 7, 2020

SADC NGAZI YA MAKATIBU WAKUU WAJADILI, KUBORESHA RASIMU ZA NYARAKA ZA KISERA NA KIMKAKATI

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ngazi ya Makatibu Wakuu wamekutana na kujadili rasimu ya mpango mkakati elekezi mpya wa maendeleo wa kanda (2020 - 2030) pamoja na rasimu ya dira ya SADC (2020 - 2050) kwa njia ya mtandao (Video Conference) jijini Dar es Salaam.

Akiongea mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Mwenyekiti wa mkutano ambae ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali, Balozi Wilbert Ibuge amesema kuwa lengo la mkutano huo lilikuwa ni kuangalia mambo mawili makubwa ambayo ni dhima ya SADC kuanzia sasa 2020 hadi 2050 pamoja na mpango mkakati wa SADC kuanzia mwaka 2020 - 2030 kwa sababu mpango mkakati wa SADC uliokuwa unatumika tangu mwaka 1992 umeisha muda wake. 

Nyaraka hizi mbili ni za muhimu sana kwa sababu hadi sasa hivi toka SADC ilipoanzishwa 1992 imefanya mambo makubwa lakini sasa ule mpango mkakati wake uliokuwa unatumika tangu mwaka 2010 na ambao ulihuishwa mwaka 2015 ukafika hadi 2020 umeisha muda wake hivyo ilikuwa ni muhimu kuandaa rasimu ya nyaraka hizi muhimu.

Ameongeza kuwa, rasimu za nyaraka hizo mbili zitawasilishwa kwenye mkutano wa 40 wa Wakuu wa nchi wanachama wa SADC na Serikali unaotegemewa kufanyika tarehe 17 Mwezi Agosti 2020 kwa njia ya mtandao.

Mpango Mkakati wa SADC ni mpango wa maendeleo wa kanda uliopitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika mwaka 2003 jijini Dar es Salaam na ulianza kutekelezwa rasmi mwaka 2005 kwa kipindi cha miaka 15 (2005 - 2020). Aidha, mpango huo una vipaombele vinne ambavyo ni maendeleo ya viwanda na mtangamano wa soko, miundombinu bora, amani na usalama, pamoja na programu maalum.

Dira ya SADC 2020 - 2050 inatoa taswira ya Jumuiya kwa miaka 30 ijayo ambapo msingi wake ni amani, ulinzi, utulivu na utawala bora, uchumi wa kati unaoendeshwa na sekta ya viwanda na wanajumuiya wenye hali bora ya maisha. 

Hivyo dira ya SADC 2050 ni muhimu kwa maendeleo ya Ukanda wa Kusini mwa Afrika hususan katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia 2030 na ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063.

Katika tukio jingine, Brigedia Jenerali, Balozi Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania, Bw. Antonio Canhandula katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Balozi Wilbert Ibuge amesema kuwa UNHCR imekuwa na mchango mkubwa sana unaohusisha kulinda haki za wakimbizi lakini pia kuwarejesha wakimbizi nchini mwao. Pamoja na mambo mengine, mazungumzo yao yalilenga kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) kwa ujumla. 
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi  Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akifuatilia mkutano wa SADC ngazi ya Makatibu Wakuu wakati wakujadili rasimu ya mpango mkakati maendeleo wa kanda pamoja na rasimu ya dira ya SADC jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali, Balozi Wilbert Ibuge pamoja na baadhi ya Maafisa Waandamizi wakifuatilia mkutano
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali, Balozi Wilbert Ibuge akimuelezea jambo Mwakilishi UNHCR nchini Tanzania, Bw. Antonio Canhandula 
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania, Bw. Antonio Canhandula akiongea na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki,Brigedia Jenerali, Balozi Wilbert Ibuge katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

TANZANIA YASAINI MKATABA WA MAPITIO WA GEORGETOWN WA JUMUIYA YA NCHI ZA AFRIKA, CARIBBEAN NA PACIFIC

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TANZANIA  YASAINI MKATABA WA MAPITIO WA GEORGETOWN WA JUMUIYA YA NCHI ZA AFRIKA, CARIBBEAN NA PACIFIC

 

Dodoma, 06 Agosti 2020

Tanzania imesaini Mkataba wa mapitio wa Georgetown unaosimamia mahusiano na uendeshaji wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pacific ambayo zamani ilikuwa ikiitwa  ACP na sasa Organisation of African, Carribean and Pacific States (OACPS) iliyo na nchi wanachama 79.


Mkataba huo ulisainiwa na balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji,  Mhe. Jestas Abuok Nyamanga kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Brussels, Ubelgiji tarehe 31 Julai 2020. Hivyo Tanzania inakuwa nchi ya 42 kati ya nchi 79 kusaini Mkataba wa mapitio wa Georgetown.

Mkataba wa Georgetown umefanyiwa mapitio ili uweze kuendana na wakati kwa kuzingatia mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea duniani katika nyanja za  kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimazingira tangu kuanzishwa kwa ACP mwaka 1975. Mchakato wa kufanya mapitio ya mkataba huu ulianza mwezi Machi 2013 kupitia timu maalum iliyoanzishwa kukusanya maoni na kuleta mapendekezo chini ya Uenyekiti wa Rais Mstaafu wa Nigeria, Mhe. Olusegun Obasanjo.

Aidha, Mwaka 2019 mchakato wa mapitio hayo ulihitimishwa kwa  kuridhiwa na Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi za OACPS katika mkutano wao uliofanyika mwezi Desemba 2019 jijini Nairobi, Kenya.

Mkataba wa Georgetown ndiyo ulianzisha ACP mwaka 1975 katika mji wa Georgetown nchini Guyana.  Tanzania ilisaini Mkataba huo wa awali tarehe 11 Desemba 1975 na imedumu ikiwa mwanachama wa ACP tangu wakati huo.

Pamoja na kuwa mwanachama Tanzania imekuwa ikinufaika katika masuala ya kiuchumi, kijamii, biashara, na uwekezaji kupitia ushirikiano maalum baina ya nchi za ACP na Umoja wa Ulaya unaosimamiwa na mikataba ya Lome na Cotonou. Vilevile miradi ya ubia wa maendeleo na ile ya mtangamano wa nchi za ACP chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya. Pia ushirikiano katika masuala ya kubadilishana ujuzi na uzoefu na nchi za ACP, mshikamano wa kisiasa na kidiplomasia katika kutetea maslahi ya Tanzania kimataifa kupitia jukwaa la ACP.

 

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali

==============================================

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga akisaini Mkataba wa Mapitio wa Georgetown mjini Brussels, Ubelgiji tarehe 31 Julai, 2020


Mhe. Nyamanga, Maafisa wa Ubalozi na Mwanasheria wa Jumuiya ya OACPS, Dkt. Emmanuel Opoku wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilisha zoezi la kusaini Mkataba.


Thursday, August 6, 2020

TANZANIA YACHAGULIWA KUWA RAIS WA BARAZA LA MAWAZIRI WA JUMUIYA YA NCHI ZA AFRIKA, CARRIBEAN NA PACIFIC

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 


TANZANIA YACHAGULIWA KUWA RAIS WA BARAZA LA MAWAZIRI WA JUMUIYA YA NCHI ZA AFRIKA, CARRIBEAN NA PACIFIC

 

Dodoma, 6 Agosti 2020

Serikali ya Tanzania imechaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Carribean na Pacific (Organisation of African, Carribean and Pacific States-OACPS)  kwa kipindi cha miezi sita kuanzia tarehe 1 Agosti 2020 hadi tarehe 31 Januari 2021.

 

Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alikabidhiwa rasmi nafasi hiyo iliyopokelewa kwa niaba yake na Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro,  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati wa Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 28 Julai 2020.

 

Tanzania inakuwa Rais wa Baraza hilo kutokana na Balozi  wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga kuchaguliwa kwa kauli moja kuwa Mwenyekiti wa Mabalozi wa Nchi za OACPS waliopo Brussels. Kwa mujibu wa Jumuiya ya OACPS,  nchi inayotoa Mwenyekiti wa Mabalozi wa Jumuiya hiyo, Waziri wake anayesimamia masuala ya OACPS ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje moja kwa moja anakuwa Rais wa Baraza la Mawaziri. Uamuzi wa kuichagua Tanzania ulifanywa na Mabalozi kutoka nchi 15 za Ukanda wa Mashariki mwa Afrika kwenye kikao kilichofanyika tarehe 2 Julai 2020 na kuthibitishwa kwa kauli moja na mabalozi wote wa nchi 79 wa OACPS kupitia kikao chao kilichofanyika Brussels tarehe 14 Julai 2020.

 

Tanzania ambayo inachukua nafasi hiyo kutoka kwa Gambia, imejipanga kutekeleza masuala mbalimbali yenye maslahi kwa Nchi za OACPS ikiwa ni pamoja na kusimamia ukamilishwaji wa majadiliano kuhusu Mkataba mpya wa ushirikiano wa Nchi za OACPS na Umoja wa Ulaya (EU) unaotarajiwa kuanza kutumika mwezi Januari 2021 baada ya mkataba wa sasa wa Cotonou (Cotonou Partnership Agreement) kufikia ukomo mwezi Desemba 2020, pamoja na kuhakikisha  maslahi ya nchi za OACPS yanaingizwa kwenye mkataba huo mpya. Aidha, Tanzania imejipanga kusimamia utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya Jumuiya ya OACPS katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa COVID-19 na madhara yake kiuchumi kwa nchi wanachama.

 

Kadhalika, maeneo mengine ya kipaumbele yatakayosimamiwa na Tanzania katika kipindi cha Urais wa Baraza hilo ni kusimamia  mikakati ya kuongeza mtangamano na ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya; kusimamia mabadiliko ya kiutendaji na mifumo ili kuendana na wakati pamoja na kudumisha mshikamano na umoja miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya.

 

Vilevile miongoni mwa manufaa ya Tanzania kuwa Rais wa Baraza hilo  ni pamoja na kuongeza ushawishi wa nchi yetu katika kupanga na kutekeleza mikakati, miradi na programu mbalimbali za Jumuiya ya OACPS ambazo ni pamoja na zile zinazotekelezwa kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya na wabia wengine wa maendeleo kama vile kilimo, uwekezaji, biashara na ujasiriamali, mazingira, miundombinu, vijana na utamaduni.

 

Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kuwa Rais wa Baraza la Mawaziri na Mwenyekiti wa Mabalozi  wa nchi za OACPS tangu ilipojiunga mwaka 1975. Miongoni mwa sababu zilizopelekea Tanzania kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo ni kutokana na kuongozeka kwa ushawishi wake kwenye Jumuiya ya OACPS, Sera na hatua thabiti zinazochukuliwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusimamia masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa pamoja na utendaji madhubuti wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kusimamia Sera ya Mambo ya Nje  ikiwemo ushiriki mahiri wa Tanzania katika masuala yanayogusa maslahi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya OACPS.

 

 

 

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali.

Wednesday, August 5, 2020

TROIKA YAJADILI NAMNA YA KUIMARISHA HALI YA USALAMA NCHINI DRC

Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama (OrganTroika) ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imekutana na kujadili namna ya kurejesha hali ya amani, ulinzi na usalama nchini DRC ili nchi hiyo iweze kupiga hatua katika maendeleo.

 Akiongea katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao (Video Conferencing) na kujadili masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama nchini Kongo DRC, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amesema kuwa mkutano huo ulizihusisha nchi za utatu wa siasa ulinzi na usalama pamoja na nchi tatu ambazo zinazotoa askari wa kikosi maalumu kinachoshughulikia masuala ya ulinzi na usalama katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (Force Intervention Brigade). 

 “Tangu mwaka jana SADC na Umoja wa Mataifa tumekuwa katika mazungumzo ya jinsi ya kuimarisha kikosi hicho pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama nchini DRC hasa upande wa Mashariki mbapo umekuwa ukipambana na vikundi vyenye misimamo mikali na kuifanya DRC kukosa utulivu na amani,” Amesema Prof. Kabudi 

Waziri ameongeza kuwa Tanzania kwa muda mrefu ikiwa ni sehemu ya SADC imepeleka askari wake upande wa mashariki mwa DRC, ambapo pamoja na mambo mengine mkutano wa leo ulikuwa ni nwebdelezo wa mazungumzo kati ya Tanzania na nchi nyingine za SADC ili kuwa na msimamo wa pamoja katika mazungumzo yake yanayoendelea na Umoja wa Mataifa (UN) kwa lengo moja la kusisitiza suala la kurejesha hali ya amani nchini Kongo hasa Mashariki mwa Kongo.

 “Tunashukuru kusema kwamba DRC ambayo ni sehemu ya SADC msimamo wake umekuwa ni ule ule unaofanana na wa nchi za SADC, pili Nchi za SADC na umoja wa Mataifa tumeazimia jambo linalofanana kuhakikisha kwamba Kongo inamaliza migogoro yake, Kongo inarejea kuwa na Amani na utulivu na Kongo inakuwa na mshikamano ili wananchi wa Kongo waweze kupiga hatua kubwa katika maendeleo,” Amesema Waziri Kabudi.

Kongo imekuwa ni muhanga wa machafuko na vita kwa muda mrefu ni imani ya Tanzania na nchi za SADC kwamba wakati umefika sasa kwa Kongo na hasa kwa Mashariki ya Kongo kupewa nafasi yake ya utulivu na mshikamano ili iweze kupiga hatua kubwa ya maendeleo. 

Mkutano umehudhuriwa na Jamhuri ya Afrika Kusini, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Malawi, Zimbabwe, Botswana, Zambia, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati) akiwa na Waziri wa Ulinzi Mhe.Dkt. Husseni Mwinyi (kushoto) pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Brigadia Generali, Balozi Wilbert Ibuge (kulia kwa Prof. Kabudi).  Wengine ni Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi Dkt. Faraji Mnyepe (wa kwanza kushoto) pamoja na Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika Mkutano wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama (Organ Troika) ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao (Video Conference). 

Mkutano ukiendelea 


                                   Mkutano ukiendelea 

BALOZI WA TANZANIA NCHINI UBELGIJI NA MWAKILISHI KATIKA UMOJA WA ULAYA AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO


Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Mwakilishi katika Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Mhe. Ursula von der Leyen katika hafla iliyofanyika kwenye ofisi za Makao Makuu ya Umoja huo jijini Brussels, Ubelgiji tarehe 30 Julai 2020.

Wakizungumza baada ya kukamilika kwa makabidhiano hayo viongozi hao waliazimia kudumisha na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano mzuri uliodumu kwa zaidi ya miaka 50 baina ya Serikali ya Tanzania na Umoja wa Ulaya.

Kadhalika, Mhe. Nyamanga alieleza Tanzania na Umoja wa Ulaya zimekuwa na ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote mbili hususan katika eneo la ubia wa maendeleo kwenye sekta za kilimo, miundombinu, elimu, nishati, afya na mazingira. Hivyo, ushirikiano huo pia umehamasisha uwekezaji, biashara na kutembeleana baina ya watu wa pande zote na kuzidi kuongeza fursa kwa wananchi wake.

Tanzania na Umoja wa Ulaya pia zinashirikiana katika mikakati mbalimbali ya kutafuta na kudumisha amani, usalama na utulivu katika ukanda wa nchi za Maziwa Makuu, barani Afrika na duniani kwa ujumla.


Balozi Nyamanga akitoa maelezo mafupi kwa Mhe. Ursula von der Leyen kabla ya kuwasilisha rasmi Hati za Utambulisho.


Picha ya pamoja baada ya kukamilika kwa zoezi la kuwasilisha Hati za Utambulisho.