Monday, December 7, 2020

TANZANIA, NAMIBIA ZAKUBALIANA KUIMARISHA SEKTA ZA UVUVI NA MIFUGO

Katika jitihada za kuendeleza Diplomasia ya Uchumi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekubaliana na Jamhuri ya Namibia kuimarisha sekta za uvuvi na mifugo.

Makubaliano hayo yamefanyika leo jijini Dar es Salaam ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) amekubaliana na Naibu Waziri Mkuu Wa Jamhuri ya Namibia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Ndaitwah kuimarisha ushirikiano katika sekta ya Uvuvi pamoja na Sekta ya Mifugo.

"Tumekubalina kuimarisha ushirikiano katika enao la uvuvi wa bahari kuu lakini pia kuwahamasisha wadau wa sekta binafsi kutoka Tanzania na Namibia kuwekeza katika eneo hilo. Kwa upande wa mifugo na uuzaji wa nyama nchi za nje Namibia wamepiga hatua kubwa sana na sasa wanauza nyama Ulaya na Asia," Amesema Prof. Kabudi

Aidha, Prof. Kabudi ameongeza kuwa wamekubaliana pia kuhamasisha sekta binafsi kutoka Namibia kuja kuwekeza katika machinjio na viwanda vya kusindika nyama hapa nchini (Tanzania) kwa ajili ya kuuza nyama hiyo nje ya Tanzania na kuendeleza sekta za uvuvi na mifugo.

Pamoja na mambo mengine, kikao cha leo kimepitia makubaliano ya miaka miwili iliyopita ambapo Tanzania na Namibia zimekubaliana kutumia fursa zilizopo kati yao kuendeleza sekta za uwekezaji, uvuvi, kilimo na mifugo kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu Wa Jamhuri Ya Namibia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Ndaitwah amesema kuwa wamekubaliana kuimarisha sekta mbili ambazo ni Uvuvi na mifugo pamoja na kilimo kwa ujumla kwa kuzingatia mazingira bora ya uwekezaji na biashara ndani ya Umoja wa Afrika (AU).

"Kuna maeneo mbalimbali ambayo kwa pamoja tumekubaliana kuyaimarisha ikiwemo uvuvi, mifugo na kilimo kwa ujumla, kupitia kikao cha leo tunaamini kuwa wawekezaji kutoka Namibia watakuja kuwekeza Tanzania na vilevile wawekezaji kutoka Tanzania watawekeza Namibia," Amesema

Ameeleza kuwa Namibia itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania katika kuhakikisha kuwa wanakuza uchumi wa nchi zetu zote mbili na Afrika kwa ujumla kwa kuzingatia misingi ya biashara na uwekezaji iliyopo ndani ya Umoja wa Afrika (AU).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) akimuelezea jambo Naibu Waziri Mkuu Wa Jamhuri ya Namibia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Ndaitwah walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri Mkuu Wa Jamhuri ya Namibia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Ndaitwah akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) wakati walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri Mkuu Wa Jamhuri ya Namibia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Ndaitwah na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi katika picha ya pamoja. Kushoto mwa Mhe. Ndaitwah ni Balozi wa Namibia hapa nchini, Mhe. Theresia Samaria ambaye amamaliza muda wake wa utumishi, na Kulia mwa Prof. Kabudi ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Bw. Frank Mwega. 


Naibu Waziri Mkuu Wa Jamhuri ya Namibia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Ndaitwah akimkabidhi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi zawadi za vitabu 



TANZANIA YAUNGA MKONO AZIMIO LA AU KUONGEZA MIAKA 10 YA KUONDOA NA KUTOKOMEZA SILAHA HARAMU

Umoja wa Afrika (AU) umezitaka nchi wanachama wa umoja huo kutilia mkazo azimio la kuondoa na kutokomeza silaha haramu ili kuliondoka na migogoro inayolifanya bara hilo kushindwa kusonga mbele kiuchumi.

Akifungua Mkutano wa 14 wa dharura wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia ya mtandao (virtual Conference) Mwenyekiti wa Umoja huo ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa amesema ni vigumu Bara la Afrika kupiga hatua za kimaendeleo kiuchumi endapo suala la usalama halitapewa kipaumbele na kuruhusu migogoro kuendelea.

Rais, Ramaphosa ameongeza kuwa wakati umefika kwa nchi za afrika hususani zilizopo katika migogoro na vita kuhakikisha kuwa zinatatua vyanzo vya machafuko hayo na kuboresha hali ya kiuchumi kwa wananchi, utawala wa sheria, na kuzingatia misingi ya haki na utawala bora.

Akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Meh. John Pombe Joseph Magufuli katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi amesema mkutano huo ulikuwa unajadili mpango na mkakati wa miaka 10 iliyopita wa kuondoa na kutokomeza silaha haramu na kujenga amani katika bara la Afrika.

"Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeunga mkono azimio la nchi za AU kuongeza miaka mingine 10 ya kutokomeza silaha haramu na kusisitiza tena ushiriki wake kikamilifu katika kuhakikisha kuwa Afrika inatatua migogoro yake yote yenyewe bila kuingiliwa na nchi za nje, lakini pia kuzitaka nchi za Afrika kuzuia mitafaruku na migogoro yote ambayo kwa miaka mingi imeigharimu sana bara la Afrika," Amesema Prof. Kabudi

Prof. Kabudi ameongeza kuwa, toka hatua ya kuondoa na kutokomeza silaha haramu ilipoanza mwaka 2017 hadi 2019, silaha zaidi ya 1,233 zimerejeshwa na Serikali itaendelea na jitihada ya kuhakikisha kuwa inazitambua silaha zote.

Aidha, Prof. Kabudi ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi zote ili kuwa na amani endelevu na utulivu endelevu katika eneo lote la Maziwa Makuu, pia Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa mchango wake katika nchi mbalimbali zenye mapigano ikiwemo DRC halikadhalika katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na sehemu nyingine ambapo vikosi vyake vya kijeshi vitatumwa kulinda amani.     

Nae Rais wa Ghana, Mhe. Nana Akufo-Addo amesema kuwa Ghana inaungana na Umoja wa Afrika (AU) na itaendelea kuhakikisha inaondoa na kutokomeza silaha haramu kwa lengo la kuimarisha masuala ya Amani, umoja na ushirikiano wa nchi za AU.

"Ghana tangu mwaka 2014 tulishaanza mkakati wa kuzuia na kutokomeza matumizi holela silaha haramu kwa kuzihakiki na kuandikisha wamiliki wote wanaomiliki silaha,….….pia mwaka jana 2019 kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) tumeweza kuendelea kudhibiti silaha matumizi ya silaha holela," Amesema Rais Akufo-Addo

Nae Rais wa Somalia, Mhe. Mohamed Farmajo amesema kuwa suala la Amani na usalama ni suala muhimu sana kwenye jamii hivyo Somalia inaungana na Umoja wa Afrika katika kuhakikisha kuwa wanaondoa na kutokomeza silaha haramu na kujenga amani katika bara la Afrika.

Rais Mohammed ameongeza kuwa amani na usalama vitakumbukwa kuwa ni msingi wa maendeleo kwenye katika jamii. Aidha, Rais huyo ameuomba umoja wa Afrika kushirikiana kwa karibu na Somalia katika kuhakikisha kuwa wanatokomeza vikundi vya kigaidi (Alshabab) kwa maendeleo ya ukanda wa Afrika.

Pamoja na mambo mengine, Umoja wa Afrika umekubaliana kuongeza muda wa kuondoa na kutokomeza silaha haramu na kujenga amani katika bara la Afrika kwa kipindi cha miaka 10 ijayo kuanzia mwaka 2021 hadi 2030.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akichangia moja ya agenda katika mkutano wa 14 wa dharua Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandao (virtual Conference) jijini Dar es Salaam 



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akiwa pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe pamoja na washiriki wengine wakifuatilia mkutano wa 14 wa dharua Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandao (virtual Conference) 



Sunday, December 6, 2020

MAWAZIRI SADC - TROIKA WAJADILI UPIGAJI KURA KWA WAGOMBEA WA KAMISHENI YA AU

Mawaziri wa SADC Double Troika wamejadili na kutolea maamuzi mapendekezo ya namna ya kupigia kura kwa wagombea kutoka Kundi la Kusini wanaowania nafasi mbalimbali kwenye Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika katika Mkutano Mkuu wa 34 mwezi Februari, 2021.

Majadiliano hayo yamefanyika katika mkutano wa Mawaziri ulifanyika mwishoni mwa wiki (Ijumaa) kwa njia ya mtandao (Video Conference) chini ya Uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano kutoka Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Verónica Nataniel Macamo Dlhovo.

Aidha, Mkutano wa Mawaziri ulitanguliwa na Kikao cha Makatibu Wakuu siku hiyo hiyo ambapo kikako hicho kilichoratibiwa chini ya Uenyekiti wa Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda na Kibara na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa SADC kutoka Jamhuri ya Msumbiji, Balozi Alfredo Fabiao Nuvunga.

Katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) aliwakilishwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.

Itakumbukwa kuwa, mnamo mwezi Juni, 2020 Umoja wa Afrika (UA) ulitangaza nafasi za kazi za ngazi za juu ikiwa ni pamoja na nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni (1), Naibu Mwenyekiti wa Kamisheni (1) na Makamishna (6). Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zilialikwa kushiriki katika mchakato huo kwa kutangaza na kuhamasisha umma kuomba nafasi hizo.  

Tanzania pia ni nchi mojawapo inayogombea nafasi mbalimbali kwenye Kamisheni ya Umoja wa Afrika. Nchi zilozoshiriki katika mkutano huo ni pamoja Msumbiji, Malawi, Tanzania, Botswana Afrika Kusini na Zimbabwe. 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiwasilisha mada katika Mkutano wa Mawaziri wa SADC Double Troika kwa njia ya mtandao (Video Conference) jijini Dar es Salaam  

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiwasilisha mada katika Mkutano wa Mawaziri wa SADC Double Troika kwa njia ya mtandao (Video Conference) jijini Dar es Salaam 

 




MKUTANO WA DHARURA WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA UMOJA WA AFRIKA WAFANYIKA KWA NJIA YA MTANDAO (VIRTUAL MEETING)

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika Mkutano wa dharura wa 13 wa Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandano            (Virtual Meeting) mkutano uliohusu umuhimu wa mkataba wa eneo huru la biashara la Bara la Afrika. Prof. Palamagamba amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mabilionea kutoka nchini Japan wavutiwa na fursa za uwekezaji nchini


Mabilionea kutoka nchini Japan wavutiwa na fursa za uwekezaji nchini 

Tarehe 3 Disemba 2020 kundi la Watalii 37 kutoka nchini Japan liliwasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kutalii sambamba na kufanya mikutano 

ya mafunzo. Watalii hawa wanaofahamika kama Klabu ya Mabilionea (Billionaires Club) watakuwepo nchini kuanzia tarehe 3 hadi 10 Disemba 2020. Watalii hawa ambao watatembelea vituo mbalimbali vya utalii nchini ni viongozi na wamiliki wa makampuni kutoka katika sekta mbalimbali nchini Japan. 

Watalii hao mara baada ya kuwasili nchini walipata fursa ya kusikiliza mawasilisho (presentation) kutoka taasisi mbalimbali kama vile Mamlaka ya Hifadhi Tanzania, Kituo cha Uwekezaji Tanzani na Bodi ya Utalii ya Tanzania ambapo, sambamba kufahamishwa zaidi kuhusu Tanzania, vilevile walielezwa kuhusu fursa na taratibu za kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini.

Watalii hao wengi walionesha kuvutiwa na fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kuridhishwa na namna Serikali ilivyoandaa mazingira rafiki kwa wawekezaji. Akizungumza baada ya kusikiliza mawasilisho Bi. Nanako Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya kutengeneza viungo bandia vya binadamu, alisema amevutiwa na fursa zilizopo katika sekta ya afya na namna Serikali ilivyojiandaa kutoa motisha kwa wawekezaji wa eneo hilo hapa nchini. Maeneo mengine ya uwekezaji yaliyowavutia watalii hao ni sekta ya utalii, usafirishaji, kilimo na viwanda. 

Watalii hawa wametembelea hapa nchini kwa juhudi kubwa za utangazaji na uhamasishaji utalii zinazoendelea kufanywa na Bodi ya Utalii Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Japan ambao unafanya juhudi kubwa ya kufungua soko la utalii la Japan kwa vivutio vya utalii vinavyopatikana hapa nchini hasa baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona. 

Vilevile watalii hao wametaja mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika kupambana na mlipiko wa ugonjwa wa CORONA, amani iliyopo nchini, ukarimu wa watanzania na uwepo wa vivutio hadhimu vya utalii nchini ni miongoni mwa sababu nyingi zilizowafanya kuja kutalii Tanzania.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya Watali hao Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania Haji Thomas Mihayo  alisema Ilani ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2020-2025 inazungumzia kukuza utalii wa mikutano ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hapa nchini Pamoja na kuongeza mapato kufikia Dola Billioni 9. "Sisi Bodi ya Utalii Tanzania Pamoja na Balozi zetu utekelezaji wa ilani umeshaanza mara moja, kwani katika kipindi hiki cha miaka mitano ya pili ya awamu hii ya tano ya muheshimiwa Rais Dr. John Pombe Magufuli tunalengo la kufikia watalii million 5 na utalii wa mikutano ni moja ya aina za utalii zitakazosaidia kufikia lengo hilo.

Baadhi ya Watalii kutoka nchini Japan wakijanza taarifa kwenye fomu maalumu mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) 

Watalii kutoka nchini Japan  wakiwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA)
Watalii kutoka nchini Japan  wakisikiliza mwasilisho (presentation) kutoka kwa Wataalamu wa Taasisi za Serikali zilizolenga kuwaelezea kuhusu fursa na taratibu za kuwekeza nchini Tanzani. Mawasilisho hayo yalifanyika katika eneo la Hoteli ya Serena iliyopo mbugani Serengeti.
Watalii kutoka nchini Japan  wakiendelea kufutalia mwasilisho (presentation) kutoka kwa Wataalamu wa Taasisi za Serikali zilizolenga kuwaelezea kuhusu fursa na taratibu za kuwekeza nchini Tanzani. 

Saturday, December 5, 2020

Tanzania yafungua ofisi ya Mwakilishi wa Heshima jijini Mumbai

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda kwa pamoja na Mwakilishi wa Heshima Mteule wa Tanzania jijini Mumbai Bwana Nayan Patel wakisaini Mkataba wa Kazi wa kumwezesha Bwana Patel kuwa Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika mji huo. Mkataba huo ulisainiwa jijini Mumbai, India tarehe 04 Desemba 2020.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda na Bwana Nayan Patel wakibadilishana Mkataba wa Kazi wa kumwezesha Bwana Patel kuwa Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika mji wa Mumbai.

Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania Jijini Mumbai Bwana Nayan Patel akihutubia katika hafla ya ufunguzi rasmi wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania Jijini humo iliyofanyika tarehe 04 Desemba 2020.

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akitoa hotuba kumpongeza Bwana Patel kwa kukubali kuiwakilisha Tanzania jijini Mumbai na kumtaka kuiwakilisha vema nchi.


Balozi wa Tamzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania Jijini Mumbai Bwana Nayan Patel wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wageni walioshriki halfla ya uwekaji saini wa Mkataba wa Kazi wa Mwakilishi wa Heshima.


-------------------------------------------------------------------------------
Na. Mwandishi Maalum, India

Tanzania yafungua ofisi ya Mwakilishi wa Heshima jijini Mumbai

Serikali ya Tanzania imefungua rasmi ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika Jiji la Mumbai katika hafla iliyofanyika jijini humo tarehe 04 Desemba 2020.

Mumbai ni jiji kuu la biashara na viwanda nchini India (commercial and industrial hub) ambapo linachangia zaidi ya asilimia 6 la pato la India na pia linachangia zaidi ya asilimia 25 ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani nchini India (25% of industrial output).

Aidha, Mumbai ni jiji mojawapo kati ya majiji kumi duniani, yanayoongoza kwa biashara, hususan katika mzunguko wa fedha duniani (global financial flow). Vilevile, Mumbai ni Jiji linaloongoza kuwa na mabilionea wengi nchini India, ambapo linashika nafasi ya 9 kuwa na mabilionea wengi duniani.

Kadhalika, shughuli za biashara na huduma za kifedha katika Jiji hilo lenye watu zaidi ya milioni 20 zinachangia mzunguko wa fedha katika uchumi wa India kwa zaidi ya asilimia 70.

 

Ni kutokana na umuhimu wa Jiji hilo, Serikali iliamua kusogeza karibu huduma za kikonseli, biashara, uwekezaji, utalii na mengineyo kwa kuwa na Mwakilishi wa Heshima atakayeratibu shughuli hizo kwa karibu. Ikumbukwe India ni nchi kubwa yenye uchumi mkubwa na idadi kubwa ya watu duniani wanaofikia bilioni 1.2. Hivyo, si rahisi kwa nchi zenye uwakilishi mjini New Delhi kuweza kuhudumia kwa ukamilifu nchini India bila kuwa na ofisi za aina hii.

 

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda alielezea juu ya umuhimu wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima jijini Mumbai kuwa itasaidia kutoa huduma za Kikonseli kwa karibu zaidi na pia itasaidia zaidi kuvutia na kutangaza fursa mbalimbali za biashara, uwekezaji zilizopo nchini, kutafuta masoko ya bidhaa za kilimo na viwanda vya Tanzania pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii wa Tanzania ili kukuza sekta ya utalii nchini.

Aidha, Balozi Luvanda alieleza kuwa ofisi hiyo itachangia katika kukuza biashara zaidi kati ya Jiji la Dar es Salaam na Mumbai kufuatia kuimarishwa kwa huduma za usafiri wa anga baada ya Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) kuanza safari zake za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Mumbai tangu mwezi Julai 2019. Vilevile, majiji haya yanaunganishwa na bandari kuu muhimu ambazo ni Bandari ya Dar es Salaam, kwa upande wa Tanzania, na Bandari ya Mumbai, kwa upande wa India.

 

Bwana Nayan Patel, ni raia wa India na mfanyabiashara mwenye mtaji mkubwa jijini Mumbai na amekwishaanza rasmi kazi ya Uwakilishi wa Heshima baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kidiplomasia. 

 

Bwana Patel aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa heshima kubwa ya kuiwakilisha Tanzania jijini Mumbai na maeneo mengine ya jirani na akaahidi kuitendea haki nafasi hiyo kadri atakavyoweza.


Friday, December 4, 2020

WIZARA YA MAMBO YA NJE YAJIPANGA KUWAJENGEA UWEZO WA KAZI WATUMISHI WAKE

Mkurugenzi wa Kitengo cha Dispora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Anisa Mbega akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert Ibuge wakati wa ufunguzi rasmi wa Awamu ya Kwanza ya  Mafunzo Maalum kwa Maafisa Waandamizi wa Wizara kuhusu Utaalamu katika Uchambuzi wa masuala mbalimbali (Analytical Skills). Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Maafisa hao ili kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku. Kadhalika, Mafunzo hayo ambayo yalifanyika jijini Dodoma hivi karibuni, yaliandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya UONGOZI na Shirika la UNDP.

Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Peter Pinda akizungumza na mmoja wa Washiriki wa Mafunzo hayo alipotembelea eneo hilo akiwa kwenye shughuli zake za ujenzi wa Taifa na kuwasalimia Washiriki 

Sehemu ya Washiriki wa Mafunzo ya Utaalam katika Uchambuzi wakifurahia jambo

Washiriki wengine wakiwa tayari kuanza kujifunza mbinu mbalimbali za kufanya uchambuzi

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo akiwasilisha Mada kwa Washiriki kuhusu "Umuhimu wa Uchambuzi katika Kufanya Maamuzi".

Sehemu ya Washiriki wakimsikiliza Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Singo (hayupo pichani) 

Sehemu nyingine ya Washiriki wakifuatilia mafunzo

Mwezeshaji kutoka Taasisi ya UONGOZI, Bibi Zuhura Muro akiwasilisha Mada kwa Washiriki kuhusu "Umuhimu wa Kutumia Akili Hisia (Emotional Intelligence) katika Uongozi". 

Mmoja wa Washiriki, Bw. Suleiman Magoma akichangia jambo wakati wa mafunzo hayo

Mwezeshaji kutoka Taasisi ya UONGOZI, Prof. Joseph  akiwasilisha Mada kwa Washiriki kuhusu "Umuhimu wa Uchambuzi katika Kutafuta Suluhisho la Matatizo mbalimbali".

Mmoja wa Washiriki, Bw. Ismail akieleza jambo kwa Washiriki wenzake ikiwa ni sehemu ya Washiriki kufanyia kazi yale waliyojifunza 

Washirki wakiwa kwenye mjadala

Sehemu nyingine ya Washiriki wa Mafunzo hayo.

 

TANZANIA, INDONESIA ZAAHIDI KUENDELEA KUKUZA BIASHARA

 Tanzania na Indonesia zimeahidi kushirikiana na kuendeleza kukuza biashara kwa kuanzisha kwa manufaa ya nchi zote mbili.  

Akihutubia katika usiku wa shukrani kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania na Indonesia kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili, Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Prof. Ratlan Pardede amesema kuwa maendeleo yaliyopatika kwenye sekta ya biashara nzuri inayofanywa na wafanyabiashara kutoka nchi zote mbili.

"Sisi Indonesia na Tanzania tumekuwa tukifanya biashara yenye manufaa kwa mataifa yetu mawili, bidhaa tunazouza ni imara na zimekuwa na ubora mzuri ambapo kwa sasa biashara imeongeza mapato zaidi ya asilimia 10," Amesema Balozi Pardede  

Ameongeza kuwa mwaka 2017 aliahidi kuwaleta wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Indonesia kuja Tanzania kwa ajili ya kuwekeza, ambapo hadi sasa tayari wameanzisha kiwanda cha Sabuni na Losheni Mkuranga

Kwa upande wake Mgeni Rasmi, ambaye ni Waziri wa Biashara na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga amempongeza Balozi kwa hatua na mipango mizuri ya kuinua uchumi wa mataifa yote mawili na kumuahidi ushirikiano katika kuhakikisha kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuwaboreshea mazingira wawekezaji na wafanyabiashara ili kuwawezesha kufanya biashara vizuri katika mazingira salama.

Nataka nikuhakikishie kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara kati ya Indonesia na Tanzania kwa kiwango cha juu." Amesema Soraga. Pia Mhe. Waziri alielekeza wakati mwingine Baraza la kuundwe Biashara la Tanzania na Indonesia (TIBC) ili mpango huo uweze kujumuisha zaidi na kuwafikia wadau wengi nchini Tanzania.

Kulingana na rekodi za Ubalozi wa Indonesia, bidhaa takribani 54 za Kiindonesia zipo kwenye soko la Tanzania kama vile mafuta ya Mawese, nguo, karatasi pamoja na sabuni. Kwa upande mwingine, Indonesia imekuwa ikiagiza bidhaa kadhaa kutoka Tanzania, ambazo ni karanga, pamba, kakao, kahawa, chai, viungo na tumbaku.

Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Prof. Ratlan Pardede akiongea na wafanyabiashara (hawapo pichani) katika hafla ya usiku wa shukrani kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania na Indonesia iliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Biashara na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga akihutubia hadhara ya wafanyabiashara (hawapo pichani) katika hafla ya usiku wa shukrani kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania na Indonesia iliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Biashara na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Soraga akipokea zawadi kutoka kwa Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Pardede jijini Dar es Salaam   


Waziri wa Biashara na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Soraga (katikati) akiwa pamoja na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Pardede katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Bw. Caesar Waitara (kushoto) na Afisa Mkuu Mambo ya Nje, Bw. Francis Luangisa jijini Dar es Salaam   


Washiriki (wafanyabiashara) wakifuatilia mkutano  


Baadhi ya Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Waziri Bw. Soraga pamoja na Mhe. Balozi, Pardede



Ubalozi wa Tanzania, Qatar Washiriki Tamasha la Kumi la Kiasili la Majahazi

Ubalozi wa Tanzania Qatar ukishirikiana na Wanadiaspora kutoka Tanzania unashiriki kwenye Tamasha la Kumi la Kiasili la Majahazi lijulikanalo kama 10th Katara Traditional Dhow Festival.Tamasha hilo  linafanyika Doha kuanzia tarehe 1-5 Disemba 2020 ambapo Tanzania inaelezea utamaduni wa kiasili wa jahazi wa mwambao wa Afrika Mashariki na Zanzibar ambapo ndio kitovu cha utamaduni huo. 

Utamaduni huo ulipelekea kuibuka muingiliano wa utamaduni wa lugha, mavazi, chakula na dini pamoja na matumizi ya Majahazi. Ubalozi umepata fursa pia ya kutangaza bidhaa za kitanzania kama viungo(spices) asali, korosho na kahawa pamoja na kutangaza utalii wetu. 

Mgeni Rasmi, Mhe. Hamad bin Abdulaziz Al Kawari, Waziri wa Nchi na Mkurugenzi wa Maktaba ya Taifa pamoja na Meneja Mkuu wa kijiji hicho cha Katara, Dr. Khalid bin Ibrahim Al Sulaiti  wakipata maelezo kwenye banda la Tanzania walipotembelea wakati wa uzinduzi wa Tamasha hilo.

Mabalozi wa Nchi za Afrika Mashariki waliopo Qatar wakiwa katika picha ya pamoja kwenye Banda la Maonesho la Tanzania

 

Thursday, December 3, 2020

HABARI KATIKA PICHA MATUKIO MBALIMBALI ALIYOFANYA PROF. KABUDI

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akipokea barua ya pongezi kutoka kwa Balozi wa Ufaransa hapa Nchini Mhe. Frederic Clavier  iliyoandikwa na  Rais wa Ufaransa Mhe. Emmanuel Macron kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kumpongeza kwa Tanzania kuingia katika uchumi wa kati


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiteta jambo na Balozi wa Ufaransa hapa Nchini Mhe. Frederic Clavier katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (International Residual Mechanism for Criminal Tribunals -IRMCT) Bw. Abubacar Tambadou akimsikiliza Prof. Palamagamba John Kabudi wakati walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (International Residual Mechanism for Criminal Tribunals -IRMCT) Bw. Abubacar Tambadou mara baada ya mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro Balozi wa Italia hapa nchini, Mhe. Roberto Mengoni ambaye amamaliza muda wake wa utumishi hapa nchini


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akimkabidhi zawadi ya picha Balozi wa Namibia hapa nchini, Mhe. Theresia Samaria ambaye amamaliza muda wake wa utumishi hapa nchini

 

 










RAIS WA UFARANSA AMTUMIA BARUA YA PONGEZI RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT JOHN POMBE MAGUFULI KWA KUIWEZESHA TANZANIA KUINGIA KATIKA ORODHA YA NCHI ZA UCHUMI WA KATI