Wednesday, April 21, 2021

MKUTANO WA KAWAIDA WA 20 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA KISEKTA LA AFYA UNAENDELEA KUFANYIKA JIJINI ARUSHA, TANZANIA.

Mkutano wa Kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya umeendelea kufanyika kwa siku ya tatu leo, katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania. 

Mkutano huu ambao utafanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 19 hadi 23 Aprili 2021,una lenga kufanya mapitio ya hatua ya maendeleo iliyofikiwa katika utekelezaji wa maamuzi na maagizo yaliyotolewa na Mkutano uliopita wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na la Kisekta. Vilevile mkutano huu ataangazia masuala mengine muhimu katika Sekta ya Afya ndani ya Jumuiya. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huu katika ngazi ya wataalamu Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo amewashukuru wataalamu wa Sekta ya Afya kwa juhudi zao za kutatua changamoto mbalimbali na kutoa mapendekezo na ushauri wa kitaalamu kwa ngazi za maamuzi ambayo yamepelekea utekelezaji wa mipango ya ubunifu katika sekta ya Afya na kuunganisha vipaumbele vya uwekezaji kwenye sekta hiyo katika Jumuiya. 

Katika ngazi ya Wataalamu mkutano huu unafuatilia na kutathimini maendeleo ya utekelezaji wa masuala mbalimbali katika sekta ya afya kama ilivyoelekezwa na Mkutano uliopita wa Baraza la Mawaziri na la Kisekta, ikiwemo; maendeleo ya utekelezaji wa mikakati ya pamoja ya kukabiliana na Ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu unaosababishwa na Virusi vya Korona (UVIKO-19), usalama wa dawa na chakula, masuala ya afya ya uzazi, Watoto na Lishe na hali ya utekelezaji wa miongozo na taratibu za taaluma na huduma za afya katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano katika ngazi ya wataalamu Dkt. Leonard Subi Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto ameeleza kuwa; Tanzania imeendelea kuongeza mikakati ya kuzuia na kudhibiti janga la UVIKO-19 tangu lilipozuka katikati ya Machi 2020. Ameongeza kusema kuwa UVIKO-19 ni ugonjwa mpya wa aina yake kwani tumeshuhudia tishio la ukuaji wa uchumi wa ulimwengu na umegharimu maisha ya watu wengi sehemu mbalimbali duniani, hivyo mshikamano ni muhimu ili kuukabili. “Tanzania tunadhamini juhudi zinazofanywa na Wanasayansi mbalimbali ulimwenguni katika kupata suluhisho la kudhibiti ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na mshikamano ulioonyeshwa na WHO, GAVI na Taasisi zingine zinazounga mkono jitihada hizo. Tanzania haikatai chanjo ya UVIKO-19, isopokuwa tunafanya tathmini thabiti kabla ya kukubali matumizi ya chanjo nchini. Mathalani, Tanzania nyakati zote imekuwa na rekodi za juu kwenye matumizi ya chanjo kwa watoto wachanga walio chini ya miaka 5 hivyo tutaendelea kutoa ushirikiano mzuri kwa wadau wa ndani na Wakimataifa katika mapambano dhidi ya janga la COVID-19.” Ameeleza Dkt.Subi

Mkutano huu unaofanyika kwa njia mbili ya ana kwa ana na video, umehudhuriwa na nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Aprili 22, 2021 watakutana Makatibu Wakuu na Aprili 23, 2021 watakutana Mawaziri wanaosimamia masuala ya Afya kutoka nchi Wanachama.

Kaimu Mkurugezi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Bw. Eliabi Chodota akichangia jambo kwenye Mkutano wa kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya unaoendelea kufanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Dkt.Leonard Subi akifuatilia mkutano wa kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya unaofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Dkt.Leonard Subi akifafanua jambo kwenye Mkutano wa Kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya unaoendelea kufanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania

 

Ujumbe kutoka Tanzania wakifuatilia Mkutano
Mkutano wa kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania.

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JAMHURI YA AFRIKA KUSINI

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Grace Naledi Pandor kujadili mambo ya kuendeleza mashirikiano baina ya Jamhuri ya Afrika Kusini na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Balozi Mulamula amefanya mazungumzo hayo Pretoria nchini Afrika Kusini ambapo pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula alieleza kuwa mahusiano kati ya Afrika Kusini na Tanzania ni ya kihistoria na yameendelea kuimarika tangu enzi a kupigania uhuru kwa nchi za kusini mwa Afrika.

Kwa upande wake Waziri Pandor ameishukuru kwa ujio wa Balozi Mulamula na kwa kufika nchini Afrika Kusini na pia alieleza kuwa Jamhuri ya Afrika Kusini inathamini mashirikiano ya kihistoria kati ya nchi zetu mbili na hivyo kinachohitajika ni kuendeleza na kuimarisha mashirikiano ya kiuchumi na kisiasa tuliyonayo sasa hivi. Jamhuri ya Afrika Kusini inayo azma ya kushiriki kikamilifu kujenga makumbusho ya urithi (heritage museum) ya harakati za kupigania uhuru kusini mwa Afrika zenye chimbuko lake nchini Tanzania na vilevile kuonyesha juhudi za Tanzania katika harakati za kupigania uhuru na kwa nchi za kusini mwa Afrika.

Mawaziri hao wamejadili pia mchakato wa tathimini ya utekelezaji wa Bi-National Commission (BNC) ambapo kwa mwaka huu Afrika Kusini ndiyo itakuwa mwenyeji wa tathimini hiyo ambayo hujumuisha ngazi ya watedaji wakuu wa sekta mbalimbali wan chi hizi mbili, Mawaziri na huitimishwa na Waheshimiwa Marais wa nchi zote mbili. 

Aidha, Balozi Mulamula kabla ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, alikutana na watumishi wa ubalozi wa Tanzania Pretoria katika mkutano ulifanyika Ubalozini, Mhe. Waziri alipokea taarifa ya eneo la uwakilishi la Ubalozi ambalo linajumuisha Afrika Kusini, Botswana, Falme ya Lesotho na SADC. Taarifa hiyo ilieleza juhudi za Ubalozi katika kukuza mahusiano na nchi za eneo la uwakilishi, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, diplomasia ya siasa, wanadiaspora wa eneo la uwakilishi.

Balozi Mulamula ameutaka Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kuendela kufanya kazi kwa malengo, watumishi kujiwekea malengo ili kufanikisha malengo ya Ubalozi na hatimaye Ubalozi kuchangia malengo ya Wizara kwa ujumla.

“Nawasihi kuendeleza mahusiano na nchi za uwakilishi na Balozi nyingine zilizopo katika nchi za uwakilishi na suala hili la kujenga mahusiano na watumishi wote na siyo Balozi pekee yake,” amesema Balozi Mulamula.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Pretoria nchini Afrika Kusini. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Grace Naledi Pandor  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Grace Naledi Pandor


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo

Monday, April 19, 2021

VACANCY


 

KONGOLE BALOZI YUSUPH TINDI MNDOLWA


 

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHE. SAMIA SULUHU HASSAN AKIMUAPISHA YUSUPH TINDI MNDOLWA KUWA BALOZI

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mkuu wa Itifaki (Chief of Protocol) Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Yusuph Tindi Mndolwa kuwa Balozi katika hafla fupi iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma  


Mkuu wa Itifaki (Chief of Protocol) Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Yusuph Tindi Mndolwa akiapa kuwa Balozi Ikulu, Chamwino - Dodoma  




Friday, April 16, 2021

KATIBU MKUU BALOZI BRIGEDIA JENERALI IBUGE ARIDHISHWA NA UENDESHWAJI WA MIRADI MWANZA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge ameeleza kuridhishwa kwake na ubunifu na uendeshwaji wa miradi mbalimbali ya maji na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi katika Bonde la Ziwa Victoria. Miradi hiyo inatekelezwa chini ya usimamizi wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC). 

Balozi Ibuge kwenye ziara hiyo akiwa ameambatana na wataalamu kutoka Sekta ya Maji, Uchukuzi, Wizara ya Fedha na Wataalumu kutoka LVBC, amebainisha kuwa lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kutambua maendeleo ya Miradi inayotekelezwa katika ukanda wa Ziwa Victoria ambayo inawagusa wananchi zaidi ya milioni 40 kutoka Nchi Tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kubaini changamoto zilizopo ili kutoa suluhisho linalofaa. 

Akizungumza wakati akihitimisha ziara hiyo Katibu Mkuu Balozi Brigedia Jenerali Ibuge ameongeza kueleza kuwa asilimia kubwa ya Ziwa Victoria ipo Tanzania (kwa 51%) hivyo, Serikali ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania inayapa kipaumbele kinachostahili masuala yote ya maendeleo yanayoendelea katika Ziwa hilo sambamba na masuala ya kiusalama. “Serikali inafanya kazi kubwa sana ya kutengeneza meli kubwa za usafirishaji na uvuvi ili kuwezesha maendeleo ya wananchi na kuhakisha usalama wao wakati wote wakiwa wanatekeleza majuku yao” amasema Balozi Ibuge.

Wakati huohuo Balozi Brigedia Jenerali Ibuge amepokea taarifa ya mpango mkakati wa utelezaji wa miradi mbalimbali katika Bonde la Ziwa Victoria, iliyowasilishwa na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde hilo Dkt. Ally Said Matano. Sambamba na uwasilishaji wa taarifa hiyo Dkt. Matano ametoa rai kwa Serikali ya Tanzania kuendelea kutoa ushirikiano kwa LVBC katika kutekeleza majukumu yake ambayo yanalenga kuboresha maisha ya wana Afrika Mashariki. 

LVBC ni Taasisi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye Makao Makuu yake Kisumu, Kenya. Taasisi hii ilianzishwa ili kuratibu maendeleo endelevu na usimamizi wa Bonde la Ziwa Victoria katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo nchi hizo zililitaja Bonde hilo kuwa eneo la “maslahi makubwa ya kiuchumi na eneo la ukuaji wa uchumi wa Kikanda litakaloendelezwa kwa pamoja na Nchi wanachama wa Jumuiya

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akifuatilia uwasilishwaji wa mpango mkakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Bonde la Ziwa Victoria uliokuwa ukifanywa na Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde hilo Dkt. Ally Said Matano.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge (kulia) akimfuatilia Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde la Ziwa Victoria Dkt. Ally Said Matano (kushoto) wakati akiwasilisha mpango mkakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Bonde hilo.
Sehemu ya Wadau kutoka sekta mbalimbali wakifuatilia uwasilishwaji wa mpango mkakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Bonde la Ziwa Victoria uliokuwa ukifanywa na Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde hilo Dkt. Ally Said Matano.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akisisitiza jambo baada ya uwasilishwaji wa mkakati wa utekelezaji wa mpango miradi katika Bonde la Ziwa Victoria

Thursday, April 15, 2021

BALOZI BRIGEDIA JENERALI IBUGE AFANYA ZIARA YA KUKAGUA MIRADI MKOANI MWANZA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge leo ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu Mkoani Mwanza. Ziara hii inalenga kufuatilia maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) katika Ukanda wa Ziwa Victoria. 

Akiwa mkoani Mwanza Balozi Brigedia Jenerali Ibuge ametembelea mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi katika Bonde la Ziwa Victoria uliopo Walayani Magu, Mwanza. Utekelezaji wa mradi huu wa Kikanda unaratibiwa na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria chini ya ufadhili na Adaptation Fund (AF). Mradi huu utatekelezwa kwa muda wa miaka mitatu ambapo pia utahusisha Nchi zingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Burundi, Rwanda, Kenya na Uganda.

Balozi Brigedia Jenerali Ibuge akiwa katika eneo la mradi ameeleza kuridhishwa na ubunifu wa mradi huo na kuwaeleza wananchi waliojitokeza kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inafautilia utekelezaji wa mradi huo wa mazingira unaowanufanisha wakazi wa eneo hilo kwa sababu unatekelezwa chini ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na hivyo Wizara ndio yenye dhamana ya kuratibu masuala yote yanayohusu au kutokana na Jumuiya. “Hatuwezi tukawa tunaenda kwenye vikao na kuzungumzia kuhusu kutumia pesa za walipa kodi katika kutekeleza miradi bila sisi wenyewe kufika kuona na kujiridhisha juu ya ubora na maendeleo ya miradi husika; Niwahakikishie, haya yote yanafungamana na namna serikali mliyoichagua inavyowajali katika kuleta maendeleo yetu sote kwa pamoja” ameeleza Balozi Brigedia Jenerali Ibuge. 

Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde la Ziwa Victoria Dkt. Ally Said Matano kwa upande wake ameeleza kuwa, LVBC itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kubuni na kutekeleza miradi itakayo tatua changamoto katika jamii na kuchagiza maendeleo ya Nchi na watu wake.

Kabla ya kuanza kwa ziara hiyo Balozi Brigedia Jenerali Ibuge alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwaza Mhe. John V.K. Mongela na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde la Ziwa Victoria Dkt. Ally Said Matano ambaye pia aliambatana naye katika ziara ya kutembelea miradi. Balozi Brigedia Jenerali Ibuge ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanaitunza miradi hiyo na kuitumia ipasavyo ili kuboresha maisha yao kama ilivyokusidiwa kwenye malengo ya kuanzishwa kwake. 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge (kushoto) akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John V.K Mongela.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John V.K Mongela wakiwa katika mazungumzo pamoja na watendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria na Wizara.
Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii,Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Eliabi Chodota, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John V.K Mongela, Mtendaji wa Sekretarieti ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) Dkt. Ally Said Matano na Mhandisi Hilda Luoga kutoka LVBC
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akiwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wa Magu.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Salum A. Kalli kwenye ukaguzi wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi katika Bonde la Ziwa Victoria uliopo Walayani humo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akiongea na baadhi ya wananchi wa Magu (hawapo pichani) waliojitokeza kwenye ziara yake ya ukaguzi wa mradi.


 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akielekeza jambo kwa Watendaji alipotembelea eneo la Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi uliopo wilayani Magu, Mwanza.

Thursday, April 8, 2021

MAPOKEZI YA NAIBU KATIBU MKUU KATIKA MAKAO MAKUU YA WIZARA – DODOMA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma M. Rajab leo amewasili katika Ofisi za Makao Makuu ya Wizara zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma na kupolewa na Watumishi na Menejimenti ya Wizara.

Balozi Fatma Rajab baada ya mapokezi hayo alipata wasaha wa kuongea na Wakuu wa Idara na Vitengo ambapo licha yakuwataka kuendelea kufanya kazi kwa weledi na juhudi amewaahidi ushirikiano katika kuteleza majumu yao ya kila siku. 

Balozi Fatma aliapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki tarehe 6 Aprili, 2021.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma M. Rajab akipokelewa Wizarani Mtumba, jijini Dodoma. 
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma M. Rajab akisalimiana na Balozi Anisa Mbega alipowasili Wizarani. 
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma M. Rajab akisalimiana na Balozi Stephen P. Mbundi wakati anapokelewa Wizarani.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma M. Rajab akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi na Menejimenti ya Wizara mara baada ya mapokezi ya kukaribishwa Wizarani.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma M. Rajab akisaini kitabu cha wageni alipowasili Wizarani
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma M. Rajab akiongea na Watumishi na Menejimenti ya Wizara (hawapo pichani) mara baada ya kuwasili Wizarani

Tuesday, April 6, 2021

MAPOKEZI YA KATIBU MKUU, NAIBU KATIBU MKUU KATIKA OFISI NDOGO ZA WIZARA - DAR

 Na Mwandishi wetu, Dar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameendelea kumuamini Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge katika nafasi ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Balozi Ibuge aliteuliwa Februari 06, 2020 kuwa katibu mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki nafasi anayoendelea kuishikilia mpaka sasa.

Kabla ya wadhifa huo, Balozi Ibuge alikuwa Mkuu wa Itifaki (Chief of Protocal) Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amemuapisha Balozi Fatma Mohammed Rajab kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Balozi Fatma aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Qatar Desemba 03, 2016 nafasi aliyokuwa akiishikilia hadi alipoteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (Hayupo Pichani) akimuapisha Balozi Fatma Mohammed Rajab kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo Ikulu Jijini Dar es Salaam



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mhe. Balozi Fatma Mohammed Rajab wakipokelewa na baadhi ya watumishi katika Ofisi Ndogo za Wizara leo Jijini Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiteta jambo na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mhe. Balozi Fatma Mohammed Rajab mara baada ya kuwasili katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Fatma Mohammed Rajab akisalimiana na baadhi ya watumishi wa Wizara wakati wa mapokezi katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam 


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Fatma Mohammed Rajab akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam