Makamu
wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullah
amezitaka taasisi na wadau mbalimbali wanaoshughulikia maendeleo ya Lugha ya
Kiswahili nchini kuchambua kwa kina na kutoa mapendekezo ya namna ambavyo Tanzania
inaweza kunufaika na Lugha ya Kiswahili kupitia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC).
Mhe.
Abdullah ametoa agizo hilo leo tarehe 26 Mei 2021 wakati akifungua rasmi
Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC lililofanyika kwenye Chuo Kikuu
cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na kuwashirikisha wanafunzi na wadau kutoka sekta
mbalimbali.
Mhe.
Abdullah amesema kuwa, Lugha ya Kiswahili ambayo ilipitishwa kuwa miongoni mwa
Lugha nne rasmi zinazotumika SADC ni rasilimali
mojawapo inayoweza kuchangia uchumi wa nchi endapo Serikali, Taasisi, Mashirika
na Wadau mbalimbali watashirikiana kikamilifu ili kuifanya lugha hiyo kuwa bidhaa
inayouzika katika nchi za SADC.
“Kwa
kuwa lugha ya Kiswahili ndio lugha mama, lugha ya taifa na rasmi kwenye Taifa
letu ni vizuri Kongamano hili likachambua kwa kina jinsi ambavyo Zanzibar na
Tanzania kwa ujumla inaweza kunufaika na Lugha hii kupitia Jumuiya. Pia
tuchekeche kwa undani na kupendekeza kile ambacho Serikali inaweza kufanya kwa
kushirikiana na wadau husika ili kuona Kiswahili kinakuwa ni bidhaa inayouzika
kwa nchi za SADC” alisema Mhe. Abdullah
Aliongeza
kusema kuwa kwa sasa wapo vijana wengi wahitimu wa ngazi mbalimbali wa mafunzo
ya ualimu wa Kiswahili na hawana ajira, hivyo alisema vijana hao wanaweza kutumia
fursa hiyo na kwenda kufundisha Kiswahili kama lugha ya pili katika nchi za
SADC.
Kadhalika
Mhe. Abdulah alitumia fursa hiyo kulikumbusha Baraza la Kiswahili la Zanzibar
kuzingatia maelekezo yaliyotolewa kwao wakati wa Kongamano la Kiswahili
lililofanyika mwaka 2020 ya kujiimarisha ili kuona Kiswahili kinastawi na
kuuzika nje ya nchi kwa faida ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.
Mbali
na Lugha ya Kiswahili, Mhe. Abdullah aliwataka washiriki wa Kongamano hilo pia
kujadili na kutoa mapendekezo ya namna ya kunufaika na Sekta ya Uchumi wa Bluu
ambayo ni miongoni mwa sekta za kipaumbele za Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar.
“Napenda
kuwakumbusha kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeipa kipaumbele sekta ya
uchumi wa bluu inayoelekeza matumizi mazuri na endelevu ya rasilimali Bahari
ili kuwawezesha wananchi kuondokana na umaskini. Hivyo basi ni muhimu kuonesha
namna ambavyo Zanzibar inaweza kutekeleza kipaumbele hicho na kuimarisha sekta
ya uchumi wa bluu kupitia SADC” alisisitiza Mhe. Abdullah.
Pia
alisisiza umuhimu wa kutumia maadhimisho hayo kuuelewesha umma wa Watanzania
kuhusu Jumuiya hiyo katika ustawi na maendeleo ya kiuchumi na kutoa wito kwa
watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo kwenye SADC.
Awali
akizungumza wakati wa Kongamano hilo ambalo liliandaliwa kwa ushirikiano kati
ya Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na SUZA, Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Simai Mohammed Said alisema kuwa kuwa
upo umuhimu wa kuendelea kujenga ushirikiano katika sekta ya elimu na nchi za
SADC ili wananchi wa Tanzania wanufaike na fursa za elimu ikiwemo vyuo vya
elimu ya juu vinavyopatikana kwenye nchi hizo.
Kwa
upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha SUZA, Dkt. Zakia Mohammed Abubakar alisema
kuwa Jumuiya ya SADC inazo fursa nyingi za kitaaluma na kitaalam ambazo
zitasaidia Chuo hicho kujenga mashirikiano na vyuo ambavyo vipo katika nchi
wanachama kwa manufaa ya watanzania.
Naye
Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye
ni Balozi Mteule na Kaimu Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Zanzibar, Bw. Masoud Abdallah Balozi aliwashukuru wadau
mbalimbali walioshiriki Kongamano hilo na kuwaomba kuendelea kushirikiana na
Wizara ili kwa pamoja waweze kunufaika na Jumuiya ya SADC.
Wakati wa Kongamano hilo, mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa ikiwemo “Historia ya SADC” iliyowasilishwa na Waziri Wa Fedha Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa mada isemayo “Fursa zilizopo SADC kwa Zanzibar” ambayo iliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga na mada kuhusu “Mafanikio na Changamoto katika SADC iliyowasilishwa na Mhadhiri Mwandamizi wa SUZA, Dkt. Abdallah Rashid Mkumbukwa.
Mhe. Abdullah akihutubia Kongamano |
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Zanzibar, Mhe. Simai Mohammed Said akizungumza wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC |
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dkt. Zakia Mohammed Abubakar naye akizungumza wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC |
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe. Idrisa Kitwana Mustafa akizungumza wakati wa Kongamano hilo |
Mabalozi Wadogo na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa waliopo Zanzibar wakiwa kwenye Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC |
Wadau mbalimbali walioshiriki Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC |
Sehemu ya Wanafunzi wakifuatilia matukio |
Wadau wengine walioshiriki Kongamano |
Kongamano likiendelea |
Waziri wa Fedha Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa akiwasilisha mada kuhusu Historia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakati wa Kongamano hilo |
Balozi Mtaafu, Mhe. Mohammed Haji Hamza akiongoza majadiliano wakati wa Kongamano hilo |
Mhadhiri Mwandamizi kutoka SUZA, Dkt. Abdallah Rashid Mkumbukwa akiwasilisha mada kuhusu " Mafanikio na Changamoto miongoni mwa Nchi Wanachama wa SADC" |
Mhadhiri Mwandamizi wa SUZA naye akiwasilisha mada |
Picha ya pamoja |
Wadau mbalimbali wakichangia wakati wa majadiliano |
Mmoja wa washiriki akichangia jambo |
Mwanafunzi wa SUZA akichangia jambo |
Mdau akichangia |