Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula leo tarehe 23 Agosti 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Raychelle Omamo ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili nchini humo yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya.
Katika mazungumzo hayo ambayo yamefanyika kwenye Hoteli ya Movenpick jijini Nairobi, Mhe. Balozi Mulamula amemshukuru Mwenyeji wake kwa mwaliko na kumweleza kwamba mwaliko huo umekuja wakati muafaka ili kuwawezesha kuweka mikakati ya pamoja ya kutekeleza maagizo ya Viongozi Wakuu wa Nchi hizi mbili waliyoyatoa wakati wa ziara ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyika nchini Kenya mwezi Mei 2021.
Aliongeza kuwa, hadi sasa yapo masuala mbalimbali ambayo yameendelea kutekelezwa na nchi hizi mbili kufuatia maagizo hayo ikiwa ni pamoja kufanyika kwa mkutano wa Mawaziri wa Biashara wa nchi hizi mbili mwezi Julai 2021 ambapo kwa pamoja waliweza kujadili na kutatua changamoto kadhaa za ufanyaji biashara ikiwemo kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kiforodha 30 kati ya 60 vilivyokuwa vinazikabili nchini hizi mbili. Masuala mengine yanayotekelezwa yanagusa sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, miundombinu, utalii, kilimo, mifugo na uvuvi.
Kadhalika, alisema kuwa nchi hizi mbili zina mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa kila mmoja hivyo uangaliwe utaratibu mzuri wa kuwezesha ubadilishanaji wa program mbalimbali za elimu na mafunzo zitakazowahusisha vijana ili kuwajengea uwezo kwenye maeneo mbalimbali ya utaalam ikiwemo nyanja za diplomasia.
Kuhusu ufanyaji biashara, Mhe. Balozi Mulamula alishukuru kwamba urari wa biashara kati ya Tanzania na Kenya sasa unakwenda vizuri na alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya Kenya kuendelea kuweka mazingira ambayo yatawawezesha watanzania wengi zaidi kuwekeza nchini humo kama ilivyo kwa kampuni nyingi za Kenya ambazo zimewekeza Tanzania.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Balozi Omamo alimshukuru Mhe. Balozi Mulamula kwa kukubali mwaliko wake na kwamba kitendo hicho ni heshima kubwa kwao na kusisitiza kuwa ushirikiano huo wa kihistoria uendelee kwa kuanzisha mikutano ya mara kwa mara kwa ajili ya kujadili masuala muhimu yenye manufaa kwa nchi hizi mbili.
Pia alipongeza ukuaji wa biashara unaoendelea kati ya nchi hizi mbili na kueleza kuwa Tanzania na Kenya zina fursa nyingi za kushirikiana na kinachotakiwa ni kuendelea kutekeleza kikamilifu masuala yote ambayo tayari yamekubalika kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizi mbili.
Wakati huohuo, Mhe. Balozi Mulamula amezungumza na Maafisa Mambo ya Nje Wanawake Vijana wa Kenya kupitia Mpango wa Azizi ambapo amewataka Maafisa hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu kazi na mamlaka, kuwa wavumilivu na kufuata misingi ya kazi ili kufikia malengo ya juu ya kazi zao kwa manufaa yao ya baadaye na nchi kwa ujumla.
“Ili kufikia malengo ya juu ya kazi yako kuna mambo mengi ya kutekeleza. Uvumilivu, heshima, kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano na wengine na umaridadi ni miongoni mwa mambo muhimu ya kuzingatia ili kufikia malengo hayo” alisisitiza Waziri Mulamula.
Waziri Mulamula alitumia nafasi hiyo kuwaeleza Maafisa hao hatua mbalimbali alizopitia hadi kufikia nafasi hiyo ikiwemo kuajiriwa kama Afisa Mambo ya Nje Daraja la Tatu, kuwa Katibu Mtendaji wa Kwanza wa Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu, kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki hadi kuteuliwa katika wadhifa wa Waziri mwaka 2021.
Katika hatua nyingine, Mhe. Balozi Mulamula amekitembelea Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Kenya na kutoa mhadhara wenye mada isemayo “Mtazamo wa Tanzania kwenye Agenda ya Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama” kwa Washiriki 62 kutoka Nchi 15 za Afrika, Ulaya na Asia waliohudhuria mhadhara huo.
Katika maelezo yake, Mhe. Balozi Mulamula ambaye amewahi kukitembelea Chuo hicho miaka 10 iliyopita alisema wanawake wana nafasi na umuhimu mkubwa wa kushirikishwa katika masuala ya amani na usalama tangu ngazi ya familia hadi kimataifa kwani wao ndio walezi wakuu wa familia hususan pale amani inapotoweka.
Alieleza kuwa, pamoja na kuwepo kwa mikataba ya kitaifa, kikanda na kimataifa inayotambua umuhimu wa ushirikishwaji wanawake kwenye masuala ya kulinda amani na utatuzi wa migogoro bado ushirikishwaji huo haujapewa kipaumbele ukilinganisha na ule wa wanaume.
Akizungumzia nafasi ya Tanzania, alisema kuwa, kwa kiasi fulani Tanzania imepiga hatua kwenye masuala kadhaa ya kuwainua wanawake hususan kwenye agenda ya amani na usalama ambapo tayari mikataba kadhaa inayotambua ushirikishaji wanawake imesainiwa ukiwemo Mkataba wa Beijing.
Pia alisema kwamba, Tanzania imeendelea kuchangia vikosi vya ulinzi wa amani kwenye nchini mbalimbali duniani ambapo hadi sasa Tanzania ina takribani wanajeshi 1,759 waliopelekwa kwenye maeneo mbalimbali ya kulinda amani ambapo kati ya hao 149 ni wanawake.
Mhe. Waziri Mulamula ambaye yupo nchini Kenya kwa ziara ya kikazi ya siku mbili pia anaongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya utakaofanyika kwa ngazi ya Mawaziri tarehe 24 Agosti 2021. Ujumbe wa Tanzania pia unawahusisha Mawaziri kadhaa pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka sekta mbalimbali.
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Balozi Raychelle Omamo yaliyofanyika jijini Nairobi.
|
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea baina yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Balozi Raychelle Omamo jijini Nairobi. |
|
Mazunguzo yakiendelea |
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Balozi Raychelle Omamo wakiwa katika picha ya pamoja |
|
Kutoka kushoto; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb), Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko (Mb) na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (Mb) wakifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendea |
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa ameambatana na Waziri wa Ulinzi wa Kenya Mhe. Dkt. Monika Juma (kushoto) walipowasili katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha nchini Kenya |
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akielezea jambo wakati akitoa Mhadhara kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Kenya |
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akitoa mhadhara katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Kenya
|
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na wenyeji wake alipotembelea Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Kenya |
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akitoa mhadhara kwa Maafisa Mambo ya Nje Wanawake Vijana wa Kenya, jijini Nairobi. |
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Balozi Raychelle Omamo jijini Nairobi wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Mambo ya Nje Wanawake Vijana wa Kenya. |