Thursday, August 26, 2021

MABALOZI WATEULE WAWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA RAIS SAMIA

Balozi wa Nigeria hapa nchini Mhe. Hamisu Umar Takalmawa akiwasilisha Hati za utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam Agosti 25, 2021 

                      

               

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa Nigeria hapa nchini Mhe. Hamisu Umar Takalmawa mara baada ya kupokea Hati za utambulisho kutoka kwa Balozi huyo Ikulu Jijini Dar es Salaam  Agosti 25,2021


Balozi wa India hapa nchini Mhe. Binaya Srikanta Pradhan akiwasilisha Hati za utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam Agosti 25,2021 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa India hapa nchini Mhe. Binaya Srikanta Pradhan, mara baada ya kupokea Hati ya utambulisho kutoka kwa Balozi huyo Ikulu Jijini Dar es Salaam  Agosti 25,2021




 Balozi wa Uholanzi hapa nchini Mhe. Wiebe Jokob De Boer akizungumza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan mara baada ya kupokea Hati ya utambulisho kutoka kwa Balozi huyo Ikulu Jijini Dar es salaam Agosti 25, 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa Uholanzi hapa nchini Mhe. Wiebe Jokob De Boer m ara baada ya kuwasilisha Hati za utambulisho Ikulu Jijini Dar es Salaam Agosti 25, 2021 

Balozi wa Burkina Faso hapa nchini mwenye makazo yake Nchini Kenya Mhe. Madina Diaby Kassamba Ganou akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es salaam Agosti 25,2021 



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Balozi wa Burkina Faso hapa nchini mwenye makazo yake Nchini Kenya Mhe. Madina Diaby Kassamba Ganou, baada ya kuwasilisha Hati za utambulisho kutoka kwa Balozi huyo Ikulu Jijini Dar es Salaam Agosti 25, 2021



Balozi mteule wa Guinea hapa nchini mwenye makazo yake Nchini Addis Ababa, Ethiopia Mhe. Gaoussou Toure akiwasilisha Hati za utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam Agosti 25, 2021 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Balozi wa Guinea hapa nchini Mhe. Gaoussou Toure mwenye Makazi yake Addis Ababa, Ethiopia, Ikulu Jijini Dar es Salaam Agosti 25, 2021  









Wednesday, August 25, 2021

Mabalozi wa Chile, Colombia, Guinea, Australia, Belarus, Burkina Faso na Czech wawasilisha Nakala za Hati za Utambulisho

Balozi Mteule wa Colombia nchini Mhe. Monica Greiff Lindo mwenye makazi yake nchini Kenya akiwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Anisa Mbega kwenye ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam tarehe 25 Agosti 2021 

Balozi Mteule wa Guinea nchini Mhe. Gaoussou Toure mwenye makazi yake nchini Ethiopia akiwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Anisa Mbega kwenye ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam tarehe 25 Agosti 2021

Balozi Mteule wa Chile nchini Mhe. Maria Alejendra Ferraz de Andrade mwenye makazi yake nchini Kenya akiwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Anisa Mbega kwenye ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam tarehe 25 Agosti 2021

Balozi Mteule wa Burkina Faso nchini Mhe. Madina Diaby Kassamba Ganou mwenye makazi yake nchini Kenya akiwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Anisa Mbega kwenye ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam tarehe 25 Agosti 2021

Balozi Mteule wa  Australia nchini Mhe. Luke Joseph Williams mwenye makazi yake nchini Kenya akiwasilisha nakala za Hati za Utambulisho kwa Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Anisa Mbega kwenye ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam tarehe 25 Agosti 2021

Balozi Mteule wa Czech nchini Mhe. Martin Kleptko mwenye makazi yake nchini Kenya akiwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Anisa Mbega kwenye ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam tarehe 25 Agosti 2021

Balozi Mteule wa  Belarus nchini Mhe. Pavel Vziatkin mwenye makazi yake nchini Kenya akiwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Anisa Mbega kwenye ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam tarehe 25 Agosti 2021

 

WAZIRI MULAMULA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WATANZANIA WAISHIO KENYA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amewahimiza Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora) kwenye maeneo mbalimbali duniani kuwa na utaratibu wa kujitambulisha na kujiandikisha kwenye Balozi za Tanzania zilizo karibu yao ili kuiwezesha Serikali kuwa na taarifa zao na kuwashirikisha kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi.

Waziri Mulamula ametoa rai hiyo alipokutana kwa mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Kenya katika mkutano uliofanyika kwenye Makazi ya Balozi jijini Nairobi hivi karibuni.

Mhe. Balozi Mulamula ambaye alifuatana na Mawaziri kadhaa kwenye mkutano huo, alisema kwamba kwa sasa Wizara ya Mambo ya Nje ina mpango mahsusi wa kuwatambua Diaspora wote kwa kukusanya taarifa zao na kuzihifadhi katika Kanzidata (Database) kwa lengo la kuiwezesha Serikali kuwa na taarifa muhimu za Watanzania hao hususan elimu, kazi, ujuzi na mitaji ili iwe rahisi kuwashirikisha kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ya taifa.

Kadhalika aliongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango wa Diaspora kwenye maendeleo ya Taifa na imejipanga kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuwawezesha kuchangia kikamilifu maendeleo ya nchi. “Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua mchango wa Diaspora kwenye maendeleo ya Taifa. Na haya si maneno yangu kwani tayari yameainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 184, sura ya 7 kipengele D pamoja na Sera mpya ya Mambo ya Nje ambayo imejumuisha masuala ya Diaspora” alisisitiza Balozi Mulamula.

Pia Mhe Balozi Mulamula alitumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania Kote ulimwenguni kuheshimu sheria za nchi walizopo na kupeperusha bendera ya Tanzania ya maadili mema ambayo inajulikana duniani kote. “Wapo Watanzania wachache wamefungwa magerezani kwenye nchi mbalimbali kwa makosa ya uvunjifu wa sheria. Tafadhali nawaomba mfuate sheria kwenye nchi mlizopo na mbebe bendera ya Tanzania ya tabia njema ambayo inajulikana duaniani” alisema Balozi Mulamula.

Kuhusu Lugha ya Kiswahili, Mhe Waziri Mulamula alitumia nafasi hiyo kuwahamasisha Diaspora hao kuchangamkia fursa ya kuanzisha vituo vya Kiswahili kwenye nchi walizopo ili kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa inayouzika. Pia aliwaomba kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutangaza biashara, uwekezaji, utalii na bidhaa za Tanzania ili kuchangia maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi ambaye amefuatana na Mhe. Waziri Mulamula nchini Kenya aliwahimiza Diaspora wanaohitaji ardhi kuja nchini na kufika Wizarani kwake ili kupata ufafanuzi wa kina wa masuala ya ardhi badala ya kutafuta taarifa nje ya utaratibu na kujikuta wanatapeliwa fedha zao.

Awali akimkaribisha Mhe. Waziri Mulamula, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. John Simbachawene alisema kuwa hali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ni nzuri na kwamba Watanzania wanaoishi nchini hapo wakiwemo wafanyabiashara, wafanyakazi na wanafunzi wanaendelea vizuri na shughuli zao bila kubughudhiwa. Aliongeza kuwa, hali hii ya utulivu imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ziara ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyika nchini Kenya mwezi Mei 2021.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania waishio Kenya, Padri Cleophas Tesha alimshukuru Mhe. Balozi Mulamula kwa kutenga muda wa kuzungumza na Jumuiya hiyo na kumwomba kuendelea kuwashirikisha Diaspora kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Diaspora hao.

Mhe. Waziri Mulamula alikuwa nchini Kenya kwa ajili ya ziara ya kikazi pamoja na kushiriki Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ambao ulifanyika nchini humo kuanzia tarehe 19 hadi 24 Agosti, 2021. Wakati wa Mkutano huo Mhe. Balozi Mulamula alifuatana na Mhe. Lukuvi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Khamis Chilo na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe.

Waziri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisalimiana na baadhi ya Wanafunzi wanaosoma Vyuo mbalimbali nchini Kenya wakati alipokutana na Watanzania waishio nchini humo.

Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Simbachawene akitoa hutuba ya kuwakaribisha wageni mbalimbali waliohudhuria hafla iliyowakutanisha baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri wa Tanzania na Watanzania wanaoishi nchini humo iliyofanyika jijini Nairobi.

 Kutoka kushoto; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi (Mb), Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Simbachawene, Waziri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (Mb) na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) wakiwa wamesimama wakati Wimbo wa Taifa ukiimbwa walipokuna kwa mazungumzo na Watanzania waishio nchini Kenya.

Waziri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb), Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Simbachawene na Prof. Prof. Patrick Loch Otieno Lumumba wakifurahia jambo walipokutana kwenye hafla iliyowakutanisha viongozi hao na Watanzania waishio nchini Kenya.
Mawaziri, Balozi wa Tanzania nchini Kenya na Watumishi wa Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini humo wakiwa katika picha ya pamoja.


Mawaziri, Balozi wa Tanzania nchini Kenya na baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wakiwa katika picha ya pamoja

Tuesday, August 24, 2021

HATI TATU ZA MAKUBALIANO ZASAINIWA KUHITIMISHA MKUTANO WA NNE WA TUME YA PAMOJA KATI YA TANZANIA NA KENYA


Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya umehitimishwa leo tarehe 24 Agosti 2021 kwa kusainiwa Hati tatu za Makubaliano ya ushirikiano kwenye masuala ya Diplomasia na Siasa, Elimu na Uhakiki wa Mpaka.

Mkutano huo ambao umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Raychelle Omamo umefanyika katika Hoteli ya Movenpick jijini Nairobi na kuwashirikisha Mawaziri, Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi kutoka Tanzania na Kenya.

Akizungumza wakati wa Mkutano huo, Mhe. Balozi Mulamula amesema kuwa, amefarijika sana kwa Mkutano huo kufanyika kwa mafanikio na kueleza kuwa hiyo ni hatua muhimu kwenye mahusiano kati ya nchi na nchi na kwamba ana imani kubwa yale yote yaliyokubalika yatatekelezwa kwa ufanisi ili kufikia malengo tarajiwa ya nchi hizi mbili na Serikali kwa ujumla.

Alieleza kuwa, miongoni mwa mafanikio ya mkutano huo ni kusainiwa kwa hati tatu muhimu za makubaliano ambazo zitawezesha utekelezaji wa makubaliano kufanyika kwa ufanisi na kwa wakati kama ilivyokubalika. Hati zilizosainiwa ni ile ya Makubaliano ya Mashauriano ya Kisiasa na Kidiplomasia; Uhakiki wa Mpaka kati ya Tanzania na Kenya na Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.

Akielezea umuhimu wa kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano kuhusu Uhakiki wa Mpaka Mhe. Balozi Mulamula alisema pamoja na mambo mengine kutazipa Nchi zote mbili msingi wa kisheria wa kuhakiki mpaka uliowekwa na wakoloni kwa kuuimarisha na kuweka alama zinazoonekana ili kuondoa mwingiliano wa jamii za mpakani na hivyo kupunguza migogoro ya mara kwa mara. 

Kadhalika alifafanua kuwa, Hati ya ushirikiano kwenye masuala ya elimu inalenga kuanzisha ushirikiano kati ya taasisi za pande zote katika maeneo ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ili kuleta manufaa kwa nchi zote katika kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo wa masuala ya elimu ya juu, Sayansi na teknolojia kwa pande zote.

Kuhusu Hati ya Mashauriano ya Kisiasa na Kidiplomasia, Balozi Mulamula alisema ina umuhimu katikakuendeleza na kuimarisha mahusiano mazuri ya kisiasa na kidiplomasia yaliyopo kati ya Tanzania na Kenya na katika ngazi za kikanda na kimataifa. 

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Omamo aliipongeza na kuishukuru Tanzania kwa kushiriki kikamilifu na kwa kuupa uzito wa hali ya juu Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ambapo alisema kuwa hiyo ni dalili njema inayoonesha nia iliyopo ya kukuza ushirikiano wa kihistoria na kindugu uliopo kati ya Kenya na Tanzania.

Aliongeza kuwa, mbali na kusainiwa kwa Hati za makubaliano, Mkutano huo umepokea taarifa njema kuhusu utatuzi wa changamoto 30 kati ya 64 zilizokuwa zinaikabili sekta ya biashara baada ya kufanyika kwa Mkutano wa Mawaziri mwezi Julai 2021. Alisema, Mkutano wa Nne umeelekeza vikwazo 34 vya biashara visivyo vya kiforodha vilivyosalia kuondolewa kabla ya mwisho wa mwezi Desemba 2021 ili kuwezesha ufanyaji biashara kati ya nchi hizi mbili kuendelea kwa ufanisi.

Kadhalika alieleza kuwa, Mkutano huo pia umepokea taarifa kuhusu makubaliano ya ushirikiano katika Sekta ya Afya yaliyofikiwa wakati wa mkutano wa pamoja wa Mawaziri wa Afya uliofanyika jijini Nairobi hivi karibuni. Pamoja na mambo mengine ilikubalika nchi hizi mbili kuandaa utaratibu wa kushirikiana kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 ikiwa ni pamoja na kushirikiana kwenye masuala ya upimaji na chanjo pamoja na kubadilishana Wataalam wa Afya.

Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ilianzishwa rasmi mwezi Septemba 2009 jijini Arusha, Tanzania na kufuatiwa na Mkutano wa Kwanza wa Tume hiyo uliofanyika jijini hapo mwaka 2009. Mkutano wa Pili wa Tume hiyo ulifanyika jijini Nairobi, Kenya mwezi Septemba 2012 na Mkutano wa Tatu ulifanyika jijini Dar es Salaam mwezi Desemba 2016.

Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya umefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya walipokutana wakati wa ziara ya Mhe. Rais Samia iliyofanyika nchini Kenya mwezi Mei 2021.

Mbali na Mhe. Balozi Mulamula, Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Keya umehudhuriwa na Mawaziri kadhaa kutoka Tanzania akiwemo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Madini, Mhe. Dotto Biteko, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe. Khalid Salum Mohammed na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki. Wengine ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Khamis Chilo na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe.
Waziri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.

 

Waziri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisaini Hati ya Makubaliano kati ya Tanzania na Kenya katika Siasa na Diplomasia kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.
Waziri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Balozi Raychelle Omamo wakifuatilia Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (Mb) akisaini Hati ya Makubaliano kati ya Tanzania na Kenya katika Elimu, Sayansi na Teknolojia kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.
Sehemu ya Ujumbe kutoka Tanzania ukifuatilia Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Nairobi, Kenya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Balozi Raychelle Omamo akisaini Hati ya Makubaliano kati ya Tanzania na Kenya katika Siasa na Diplomasia kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.
Waziri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Balozi Raychelle Omamo wakionesha Hati ya Makubaliano mara baada ya kukamilisha zoezi la kusaini Hati hizo kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Nairobi, Kenya
Mkutano wa Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano Ngazi ya Mawaziri ukiendelea jijini Nairobi, Kenya
Mawaziri, Manaibu Waziri, na Makatibu Wakuu wanaosimamia Sekta mbalimbali kutoka Tanzania na Kenya walioshiriki Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Nairobi, wakiwa katika picha ya pamoja. 

Monday, August 23, 2021

BALOZI SOKOINE AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KWENYE MKUTANO WA NNE WA TUME YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA KENYA ULIOFANYIKA JIJINI NAIROBI KWA NGAZI YA MAKATIBU WAKUU.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine leo tarehe 23 Agosti 2021 ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya kwa Ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Nairobi

Pamoja na mambo mengine Mkutano wa Makatibu Wakuu umepitia na kuthibitisha agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwao na Wataalam kabla ya agenda hizo kuwasilishwa na kupitishwa kwenye Mkutano wa Mawaziri unaotarajiwa kufanyika jijinii humo tarehe 24 Agosti 2021.

Kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano huo, Balozi Sokoine amewapongeza Wataalam kutoka Tanzania na Kenya kwa kukamilisha taarifa kwa wakati na kuwezesha mkutano wa makatibu wakuu kufanyika.

Alisema kuwa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ni nyenzo muhimu katika kukuza ushirikiano kati ya nchi na nchi kwani hutoa fursa ya kuangalia maeneo ya ushirikiano kwa upana wake pamoja na kutoa nafasi ya kukubaliana maeneo ambayo ni ya kipaumbele na kuainisha mpango wa utekelezaji kwa ufanisi zaidi.

Pia aliongeza kuwa, Mkutano huo wa Nne utatoa nafasi kwa nchi hizi kutathmini namna makubaliano ya awali yalivyotekelezwa, kuainisha changamoto zilizojitokeza kwenye utekelezaji na kutoa suluhu ya namna ya kuzitatua ili kuimarisha ushirikiano uliopo kwa manufaa ya nchi hizi mbili na wananchi kwa ujumla. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, Balozi Macharia Kamau aliwakaribisha wajumbe kutoka Tanzania nchini Kenya na kuwataka wajumbe wote wa mkutano huo kupitia na kujadili taarifa zilizowasilishwa kwao kwa ufasaha ili kukamilisha jukumu hilo kwa ufanisi.

Mkutano wa Makatibu Wakuu ni mwendelezo wa maandalizi ya Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano unaotarajiwa kuhitimishwa na Mkutano wa Mawaziri hapo tarehe 24 Agosti 2021.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya katika ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Nairobi.

Meza Kuu wakifuatilia Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya katika ngazi ya Makatibu Wakuu uliokuwa ukiendelea jijini Nairobi.


Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia Mkutano wa wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya katika ngazi ya Makatibu Wakuu uliokuwa ukiendelea, jijini Nairobi. 

Mkutano wa wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya katika ngazi ya Makatibu Wakuu ukiendelea, jijini Nairobi.