Monday, September 13, 2021

KAMATI YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA (NUU) YAPIGWA MSASA

 Na Mwandishi Wetu, Dar

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeipiga msasa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) kwa kuipatia mafunzo maalumu yenye malengo mbalimbali hasa katika kutetea maslahi ya Taifa.

Pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo pia yatajikita  katika masuala ya Itifaki, mawasiliano ya Kidiplomasia, usalama wa Kimtandao na Diplomasia ya Uchumi  ili kuwajengea uwezo wabunge wa kamati hiyo katika kutekeleza majukumu yao ya Kamati na Bunge kikamilifu.

Akifungua mafunzo hayo ya siku tano Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema kuwa kupitia mafunzo hayo kamati itapata ujuzi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu Kamati maslahi ya Taifa, masuala ya Itifaki, mawasiliano ya Kidiplomasia, usalama wa Kimtandao na Diplomasia ya Uchumi  ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yenu ya Kamati na Bunge kikamilifu.

“Ninayo furaha kuwajulisha kuwa mtapata fursa ya kuelimishwa juu ya mambo Uchumi wa Buluu, mada itakayotolewa na Wizara yenye dhamana ya usimamizi wa uchumi wa buluu kutoka Zanzibar ambayo imepiga hatua katika utekelezaji wake,” Amesema Balozi Mulamula.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, Wizara inaamini kuwa wajumbe wa Kamati na washiriki wote wa mafunzo wataendelea kutumia ujuzi watakaoupata kuishauri Wizara na kuwa Mabalozi wazuri ndani na nje ya Bunge katika kulinda taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Niihakikishie Kamati kuwa Wizara itaendelea kushirikiana nanyi kikamilifu hasa katika kipindi hiki tunapoandaa Sera yetu ya Mambo ya Nje. Tunaamini kuwa ushiriki wenu utaiwezesha nchi yetu kuwa wa sera iliyosheheni masuala muhimu yatakayoiwezesha nchi kunufaika,” ameongeza Balozi Mulamula

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Bw. Mussa Zungu amesema kamati anayoiongoza inafanya kazi kuwa kwa maslahi mapana ya nchi na kuahidi kuwa vichocheo vya maslahi ya nchi vinalindwa kwa maslahi mapana ya nchi.

“Kamati inatoa ushauri ‘cross-cutting’ kwa maana inagusa kila eneo kwa taifa letu, jambo lolote lile linalohusiana na masuala ya foreign huwa tunashauri, mambo ya ulinzi na usalama…..kwa hiyo inatoa mambo yak echini kwa chini kwa malengo ya kuisaidia serikali,” Amesema Bw. Zungu

Mafunzo haya muhimu kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) yameandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Chuo cha Diplomasia na yatafanyika kuanzia tarehe 13 – 17 Septemba 2021 jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akijadili jambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Bw. Mussa Zungu (Mb) Jijini Dar es Salaam


Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) hayupo pichani

Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bibi. Agnela Nyoni akitoa hotuba kabla ya kumkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula kuongea na wajumbe wa Kamati ya NUU


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba ya ufunguzi wa mafunzo maalum ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Jijini Dar es Salaam



Sunday, September 12, 2021

Shule ya Kimataifa ya Wakimbizi kujengwa Tanzania

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju (kulia) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Shirika la Elimu, Utamadani na Sayansi la Umoja wa Nchi za Kiarabu, Mhe. Amir Fehri alipotembelea Ofisi ya Ubalozi nchini Uholanzi.

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju akimpa zawadi ya kahawa ya Tanzania Balozi Fehri

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju akipokea barua kwa ajili ya kuwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Shule ya Kimataifa ya Wakimbizi kujngwa Tanzania

 

Balozi wa Shirika la Elimu, Utamaduni na Sayansi la Umoja wa Nchi za Kiarabu (The Arab League Educational, Cultural and Scientific Organization-ALECSO), Mhe. Amir Fehri anakusudia kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ili aombe ridhaa ya kujenga shule ya kimataifa kwa ajili ya wakimbizi-watoto nchini Tanzania.

Balozi huyo kijana (17) na maarufu duniani, raia wa Tunisia alibainisha hayo alipokutana na kufanya mazungumzo hivi karibuni na Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju.

“Naomba kupatiwa nafasi ya kukutana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan ili kumuomba nasaha zake (moral support) katika kampeni yangu ya kusambaza salaam ya Amani na Uvumilivu duniani, lakini zaidi kuomba ridhaa ya Mheshimiwa Rais ili niweze kujenga shule yenye hadhi ya kimataifa kwa ajili ya wakimbizi-watoto nchini Tanzania”, Balozi Fehri alisema.

Akielezea kuhusu matarajio yake hayo, alisema, shule hiyo itakuwa inatoa vyeti vya kimataifa ili kuwasaidia watoto hao ama kupata kazi nchini Tanzania au wakirejea katika nchi zao. Aidha, Mhe. Fehri ameomba apatiwe nafasi ya kukutana na wanafunzi wa shule na vyuo mbalimbali nchini Tanzania ili kuwaelimisha kuhusu unyanyasaji unaofanyika mashuleni (bullying) na madhara yake pamoja na njia za kukabiliana na kadhia hiyo.

Kwa upande wake, Balozi Kasyanju alimpongeza Mheshimiwa Fehri kwa jitihada zake thabiti na kumshukuru kwa mapenzi yake juu ya Tanzania, lakini zaidi kwa dhamira yake ya kujenga shule ya wakimbizi nchini Tanzania.

Alisema ni kweli kwamba, Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi kwa zaidi ya miaka 40 na moja ya changamoto kubwa inayojitokeza ni pale ambapo wakimbizi hao wanaporejea katika nchi zao kwa hiari, wanashindwa kujumuika ipasavyo na jamii zao kutokana na ukosefu wa elimu stahiki itakayowawezesha pamoja na mambo mengine kupata ajira. 

 

Balozi Kasyanju alitumia fursa hiyo pia kumpongeza sana Balozi Fehri kwa umaarufu wake duniani kama vile; kuteuliwa kuwa Balozi wa Francophonie ulimwenguni; kuweza kuchapisha vitabu 4 akiwa na umri wa miaka 12, ambavyo vilimpa tuzo 25 za kimataifa katika fasihi kama Sanaa na Barua za Tuzo ya Kimataifa ya Ufaransa, 2014; na kuzungumza lugha saba (Kikurdi-Kifaransa-Kichina-Kiingereza-Kijerumani-Kiarabu-Kilatini) sifa iliyomuwezesha kuwasiliana na viongozi wakubwa duniani. 

 

Balozi Fehri anashirikiana na Rais wa Tume ya Ulaya, kupitia Mfuko wa Amir Fehri (Amir Fehri Foundation) kufungua shule ya kwanza ya Kimataifa huko Mossoul, Iraq. Shule hiyo itakuwa ishara halisi ya elimu kwani itajengwa ndani ya kambi za wakimbizi na itatoa nafasi mpya kwa watoto wote wakimbizi.

 


 

Friday, September 10, 2021

VACANCY ANNOUNCEMENT AT THE OACPS SECRETARIAT


 

MTOTO BARKA SEIF MWENYE KIPAJI CHA MPIRA WA MIGUU ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UHOLANZI


Mtoto Barka Seif mwenye umri wa miaka 7 ambaye anakipaji cha kucheza mpira wa miguu,akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi Mhe. Erine Kasyanju alipotembelea ubalozini hapo. Barka Seif yuko Nchini Uholanzi katika klabu ya Ajax.
Mtoto Barka Seif mwenye umri wa miaka 7 ambaye anakipaji cha kucheza mpira wa miguu,akiteta jambo na Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi Mhe. Erine Kasyanju alipotembelea ubalozini hapo. Barka Seif yuko Nchini Uholanzi katika klabu ya Ajax.
Mtoto Barka Seif mwenye umri wa miaka 7 ambaye anakipaji cha kucheza mpira wa miguu,akisaini kitabu cha Wageni katika Ubalozi wa Tanzania Nchini Uholanzi. Barka Seif yuko Nchini Uholanzi katika klabu ya Ajax.

Mtoto Barka Seif mwenye umri wa miaka 7 ambaye anakipaji cha kucheza mpira wa miguu,akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania Nchini Uholanzi Mhe. Erine Kasyanju alipotembelea ubalozini hapo. Barka Seif yuko Nchini Uholanzi katika klabu ya Ajax.
 

Thursday, September 9, 2021

UINGEREZA IMEIPONGEZA TANZANIA KWA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA, UWEKEZAJI, HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Uingereza imeipongeza Tanzania kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji, Haki za Binadamu na Utawala Bora, jambo ambalo limeimarisha ushirikiano baina ya Nchi hizo. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameyasema hayo wakati wa mazungumzo kwa njia ya mtandao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Mhe. James Duddridge, ukiwa ni utekelezaji wa mazungumzo ya awali kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri huyo alipofanya ziara hapa nchini

Balozi Mulamula ameongeza kuwa kutokana na mazungumzo hayo Uingereza na Tanzania zimekubaliana kufanya kongamano kubwa litakalojumuisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uingereza ili kuja kuwekeza hapa nchini. 

Pia Balozi Mulamula ameishukuru Uingereza kwa kuiunga mkono Tanzania katika bodi ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) jambo lililoiwezesha Tanzania kupata mkopo wa masharti nafuu wa shilingi Trilioni 1.3 kwa ajili ya kukabiliana na adhari za UVIKO 19.

Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami, ambapo ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kulisaidia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ili kuliwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwemo kuwarejesha wakimbizi makwao kwa hiari.

“Ili shirika hili liendelee kuhudumia vyema wakimbizi ni muhimu Jumuiya ya Kimataifa ikaendelea kutoa mchango wake, hasa kwa kuwaongezea bajeti UNHCR ambayo itawawezesha kutimiza majukumu yao kwa wakati na kwa ufanisi zaidi” alisema Mheshimiwa Balozi Mulamula 

Kwa upande wake Mkurugenzi huyo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami kwa niaba ya Shirika hilo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania kwa kuendelea kutoa mchango wa muda mrefu katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakimbizi. 

Ofisi ya Kikanda ya UNHCR iliyopo Kasulu, Kigoma inahudumia nchi Kumi na Moja (11) ambazo ni; Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, South Sudan, Tanzania and Uganda.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo kwa njia ya mtandao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Mhe. James Duddridge. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami yaliyofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akijadili jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Bw. Gerald Mbwafu baada ya kumaliza mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Mhe. James Duddridge. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami (kushoto) wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mazungumzo yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara na Watendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi.

Monday, September 6, 2021

SERIKALI YAAINISHA VIPAUMBELE SEKTA YA AFYA

Na Mwandishi Wetu, Dar

Serikali imeainisha vipaumbele vitakavyonufaika na mradi wa sekta ya afya kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ufadhili wa Serikali ya Italia.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee Prof. Abel Makubi amevitaja hivyo alipokutana na madaktari kutoka Italia leo Jijini Dar es Salaam ambavyo ni mafunzo kwa wataalamu wa afya katika hospitali za mkoa, kanda na Taifa kwa ujumla, kununua vifaa vya matibabu vya kisasa, kujenga na kukarabati hospitali za kanda na taifa.

“Vipaumbele vingine ni kuanzisha na kuendeleza ushirikiano katika sekta ya afya kati ya Tanzania na Italia, kuimarisha mifumo ya maabara katika hospitali na kuendelea kupambana na ugonjwa wa Uviko 19 ikiwa ni pamoja na kuelimisha umuhimu wa chanjo” amesema Prof. Makubi.

Kwa upande wake Balozi wa Italia hapa nchini, Mhe. Marco Lombardi amelipongeza Shirika la Maendeleo la Italia kwa kutenga Euro 1,250,000 za msaada wenye manufaa kwa sekta ya afya nchini.

“Ushirikiano baina ya Tanzania na Italia ni wa muda mrefu na imara, naomba nikuhakikishie kuwa Italia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta ya afya pamoja na sekta nyingine kwa maslahi ya pande zote mbili na kwetu sisi kama Italia huu ni mwanzo na tunaamini kuwa kupitia mradi huu uhusiano wetu utaendelea kuimarika zaidi,” amesema Balozi Lombardi.

Nae Dkt. Davide Bonechi, Daktari kutoka Kituo cha Taifa la Italia cha Afya Duniani amesema kuwa kupitia mpango wao wa kuboresha na kuimarisha sekta ya afya katika ukanda wa Afrika, mbali na Tanzania nchi nyingine zitakazo nufaika na mpango huo ni Kenya na Uganda.

 

“Lengo letu ni kuboresha sekta ya afya kwa ujumla pamoja na kuwaongezea uwezo wataalamu wa afya ili waweze kukabiliana na magonjwa mbalimbali yanayowapata binadamu,” amesema Dkt. Bonechi

Tarehe 3 September ujumbe wa wataalam wa afya kutoka nchini Italia uliwasili Tanzania kwa ziara maalum ya kutathmini na kufahamu mahitaji na vipaumbele vya Tanzania katika ya afya kwa hospitali zilizopo nchini.

Ujumbe wa wataalam wa afya kutoka nchini Italia unaongozwa na Dkt. Davide Bonechi, Dkt. Giulia Dagliana, pamoja na Dkt. Beatrice Borchi, wote wakitoka katika Kituo cha Taifa la Italia cha Afya Duniani.

Tanzania imekuwa ikishirikiana na Italia katika miradi mbalimbali ya afya hapa nchini ambapo ushirikiano rasmi katika sekta ya afya ulianza mwaka 1968 kupitia Shirika la Madaktari wa Italia-CUAMM-Doctors with Africa. Kuanzia wakati huo, Serikali ya Italia imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya afya hapa nchini kama vile miradi ya kupambana na utapiamlo, afya ya watoto wachanga, afya ya uzazi na kupunguza maambizi ya virusi vya ukimwi.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikipokea madaktari wa binadamu na wataalamu wa dawa za binadamu kutoka Italia ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa kutoa huduma za matibabu. 

Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi (kushoto) akielezea jambo katika kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi (kulia) akiwaelezea vipaumbele vya Serikali sekta ya afya madaktari kutoka Italia. Madaktari hao wameambatana na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi.   


Mmoja kati ya madaktari kutoka Italia akieleza jambo wakati wa kikao


Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi (kushoto) akifafanua jambo wakati wa kikao


Kikao kikiendelea 



Friday, September 3, 2021

TANZANIA, UFARANSA NI UJUMBE WA UTULIVU NA AMANI DUNIANI

  Na Mwandishi wetu, Dar

Tanzania na Ufaransa zimetajwa kuwa ni ujumbe wa utulivu, amani na maendeleo duniani na kwamba tukio la hivi karibuni katika ubalozi huo halikuathiri kwa namna yeyote mahusiano baina ya Nchi hizo.

Balozi wa Ufaransa hapa nchini mhe. Frederic Clavier ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam alipokutana kwa mazungumzo pamoja na kumuaga Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini na kuongeza kuwa katika kipindi chote cha utumishi wake ameiona Tanzania kuwa ni ujumbe wa utulivu,amani na maendeleo kwa Bara la Afrika na duniani kwa ujumla.

“Katika kipindi chote cha uwakilishi wangu hapa Tanzania, nimeiona Tanzania kuwa ni ujumbe wa utulivu, amani na maendeleo kwa Bara la Afrika na duniani kwa ujumla,” Amesema Balozi Clavier.

Balozi Clavier ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Ufaransa na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya, miundombinu biashara na uwekezaji umeendelea kukua kwa kiwango kikubwa na kwamba Ufaransa itaendela kukuza mahusiano hayo ya kihistoria baina ya nchi hizo mbili.

Ameongeza kuwa Ufaransa itaendelea kutoa kipaumbele katika kuendeleza uchumi wa buluu ambao kwa sasa umewekewa mikakati mahususi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kama chanzo kipya cha kuongeza mapato ya serikali lakini pia kupunguza umasikini kwa Watanzania wote na kwamba anaporejea Ufaransa atahamasisha makampuni, wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali kutoka Ufaransa kuja kuwekeza Tanzania.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amemshukuru Balozi Frederic Clavier kwa kuimarisha na kuendeleza mahusiano baina ya Tanzania na Ufaransa.

Balozi Mulamula amempa pole Balozi huyo kwa tukio la kihalifu lililotokea hivi karibuni katika Ubalozi wa Ufaransa na kumhakikishia kuwa licha ya tukio hilo ambalo lilidhibitiwa na vyombo vya dola,Tanzania ni salama.

Balozi wa Ufaransa aliyemaliza muda wa uwakilishi hapa nchini, Mhe. Frederic Clavier akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Maongezi baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Ufaransa aliyemaliza muda wa uwakilishi hapa nchini, Mhe. Frederic Clavier yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam  


Maongezi baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Ufaransa aliyemaliza muda wa uwakilishi hapa nchini, Mhe. Frederic Clavier yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Libarata Mulamula (Mb) akitoa zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro kwa Balozi wa Ufaransa aliyemaliza muda wa uwakilishi hapa nchini, Mhe. Frederic Clavier  



Wednesday, September 1, 2021

BALOZI SOKOINE AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CANADA NCHINI


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine, leo terehe 1 Septemba 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Pamela O’Donnell Balozi wa Canada nchini Tanzania, yaliyofanyika jijini Dodoma. 

Katika mazungumzo hayo Balozi Sokoine na Balozi Pamela O’Donnell wamejadili masuala mbalimbali muhimu katika kudumisha na kuboresha mahusiano ya kidiplomasia na ushirikiano katika masuala ya uchumi baina ya Tanzania na Canada. Kwa kipindi cha takribani miongo sita mahusiano ya Tanzania na Canada yamejikita katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii kama vile maendeleo ya viwanda, afya, kuendeleza rasilimali watu, ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa mazingira. 

Tanzania ilianzisha mahusiano ya kidiplomasia na Canada mwaka 1961 mara baada ya uhuru. 
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Canada nchini Tanzania Mhe. Pamela O’Donnell yaliyofanyika katika Ofisi ya Wizara jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine na Balozi wa Canada nchini Tanzania Mhe. Pamela O’Donnell wakijadili jambo walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma.
Balozi wa Canada nchini Tanzania Mhe. Pamela O’Donnell akielezea jambo kwenye mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine. 

Mazungumzo yakiendelea




Umoja wa Mataifa umetangaza nafasi ya kazi ya Katibu Mkuu Msaidizi atakayeshughulikia masuala ya Amani (Assistant Secretary General for Peacebuilding Support). Fursa hii iko wazi kwa nchi wanachama wote wa Umoja wa Mataifa. 


Maelezo zaidi ya nafasi hiyo na jinsi ya kuwasilisha maombi yanapatikana kupitia  ukurasa wa Tovuti ya Umoja wa Mataifa wa https://www.un.org/peacebuilding/supportoffice.
 
Mwisho wa kupokea maombi hayo ni tarehe 20 Septemba 2021.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawahimiza Watanzania wenye sifa kuomba nafasi hiyo.