Sunday, September 12, 2021

Shule ya Kimataifa ya Wakimbizi kujengwa Tanzania

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju (kulia) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Shirika la Elimu, Utamadani na Sayansi la Umoja wa Nchi za Kiarabu, Mhe. Amir Fehri alipotembelea Ofisi ya Ubalozi nchini Uholanzi.

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju akimpa zawadi ya kahawa ya Tanzania Balozi Fehri

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju akipokea barua kwa ajili ya kuwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Shule ya Kimataifa ya Wakimbizi kujngwa Tanzania

 

Balozi wa Shirika la Elimu, Utamaduni na Sayansi la Umoja wa Nchi za Kiarabu (The Arab League Educational, Cultural and Scientific Organization-ALECSO), Mhe. Amir Fehri anakusudia kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ili aombe ridhaa ya kujenga shule ya kimataifa kwa ajili ya wakimbizi-watoto nchini Tanzania.

Balozi huyo kijana (17) na maarufu duniani, raia wa Tunisia alibainisha hayo alipokutana na kufanya mazungumzo hivi karibuni na Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju.

“Naomba kupatiwa nafasi ya kukutana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan ili kumuomba nasaha zake (moral support) katika kampeni yangu ya kusambaza salaam ya Amani na Uvumilivu duniani, lakini zaidi kuomba ridhaa ya Mheshimiwa Rais ili niweze kujenga shule yenye hadhi ya kimataifa kwa ajili ya wakimbizi-watoto nchini Tanzania”, Balozi Fehri alisema.

Akielezea kuhusu matarajio yake hayo, alisema, shule hiyo itakuwa inatoa vyeti vya kimataifa ili kuwasaidia watoto hao ama kupata kazi nchini Tanzania au wakirejea katika nchi zao. Aidha, Mhe. Fehri ameomba apatiwe nafasi ya kukutana na wanafunzi wa shule na vyuo mbalimbali nchini Tanzania ili kuwaelimisha kuhusu unyanyasaji unaofanyika mashuleni (bullying) na madhara yake pamoja na njia za kukabiliana na kadhia hiyo.

Kwa upande wake, Balozi Kasyanju alimpongeza Mheshimiwa Fehri kwa jitihada zake thabiti na kumshukuru kwa mapenzi yake juu ya Tanzania, lakini zaidi kwa dhamira yake ya kujenga shule ya wakimbizi nchini Tanzania.

Alisema ni kweli kwamba, Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi kwa zaidi ya miaka 40 na moja ya changamoto kubwa inayojitokeza ni pale ambapo wakimbizi hao wanaporejea katika nchi zao kwa hiari, wanashindwa kujumuika ipasavyo na jamii zao kutokana na ukosefu wa elimu stahiki itakayowawezesha pamoja na mambo mengine kupata ajira. 

 

Balozi Kasyanju alitumia fursa hiyo pia kumpongeza sana Balozi Fehri kwa umaarufu wake duniani kama vile; kuteuliwa kuwa Balozi wa Francophonie ulimwenguni; kuweza kuchapisha vitabu 4 akiwa na umri wa miaka 12, ambavyo vilimpa tuzo 25 za kimataifa katika fasihi kama Sanaa na Barua za Tuzo ya Kimataifa ya Ufaransa, 2014; na kuzungumza lugha saba (Kikurdi-Kifaransa-Kichina-Kiingereza-Kijerumani-Kiarabu-Kilatini) sifa iliyomuwezesha kuwasiliana na viongozi wakubwa duniani. 

 

Balozi Fehri anashirikiana na Rais wa Tume ya Ulaya, kupitia Mfuko wa Amir Fehri (Amir Fehri Foundation) kufungua shule ya kwanza ya Kimataifa huko Mossoul, Iraq. Shule hiyo itakuwa ishara halisi ya elimu kwani itajengwa ndani ya kambi za wakimbizi na itatoa nafasi mpya kwa watoto wote wakimbizi.

 


 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.