Monday, September 13, 2021

BALOZI SOKOINE AFUNGUA KIKAO KAZI CHA WADAU WA IORA

 

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) kinachofanyika mjini Zanzibar

 

Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Aboud S. Jumbe (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine katika kikao kazi cha wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) 

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Agness Kayola akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA)kinachofanyika mjini Zanzibar

Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar Balozi Masoud A Balozi (kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Agness Kayola wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) kinachofanyika mjini Zanzibar


Wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakimsikiliza Mratibu wa masuala ya IORA Tanzania Balozi Agness  Kayola kinachofanyika mjini Zanzibar
Wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika picha ya Pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine baada ya ufunguzi wa kikao kazi chao kinachofanyika mjini Zanzibar


 Na mwandishi wetu, Zanzibar

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amefungua kikao kazi cha wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) na kuwataka washiriki wa kikao hicho kutoa msukumo na kipaumbele kwa shughuli zinazoratibiwa na Jumuiya hiyo.

Balozi Sokoine amesema hayo mjini Zanzibar alipokuwa akifungua kikao kazi hicho na kuongeza kuwa kufanya hivyo watakuwa wanalinda kwa vitendo maslahi ya Taifa na kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania, Nchi Wanachama na Washirika wa Mazungumzo na hivyo kuleta tija kwa Tanzania.

Amesema uanachama wa Tanzania kwenye Jumuiya hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya diplomasia, ushirikiano wa kikanda na kimataifa hasa ikizingatiwa kuwa inakutanisha nchi mbalimbali kubwa zilizoendeleana kwamba  Tanzania inaweza kutumia fursa ya Jukwaa la IORA kuimarisha ushirikiano wa nchi na nchi na Washirika wa Mazungumzo ambao wana nguvu kiuchumi na wameendelea kisayani na kiteknolojia.

Amewataka wadau hao kuandaa Mapendekezo ya Miradi yenye sifa na vigezo vya kupatiwa ufadhili kwenye Mfuko Maalum wa Jumuiya ya IORA ili kusaidia kuwezesha, kuhudumia wananchi na kuwezesha  jamii inayozunguka maeneo ya ukanda wa bahari,  uhifadhi wa mazingira ya bahari, uvunaji endelevu wa rasilimali za bahari, uwezeshaji wananchi kiuchumi na maeneo mengine mtambuka yenye tija na maslahi kwa wananchi.

Awali akizungumza katika kikao kazi hicho Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Balozi Agness Kayola alisema Kikao Kazi hiko kina lengo la kuimarisha ushiriki wa Nchi kwenye Jumuiya ya IORA; kuimarisha ushirikiano wa kisekta kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuimarisha vikundi kazi ili kuweza kunufaika na uanachama wa Tanzania katika IORA.

Alisema kwa sasa, IORA ina vikundi kazi vinane (8) ambavyo vinafanya kazi chini ya Uratibu wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda - Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Amevitaja vikundi hivyo kuwa ni Ulinzi na Usalama; Biashara na Uwekezaji; Kazi cha Utalii na Utamaduni; Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi; Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu; Uvuvi; Maafa na Uchumi wa Bluu  

Kikao kazi hicho kinajadili mada zinazohusiana na upatikanaji wa fursa za uwekezaji zilizopo kwenye uchumi wa bluu; sheria, kanuni na taratibu za kuvuna na kuhifadhi rasilimali zilizopo kwenye bahari hususan kwenye ukanda wa bahari kuu; sera na mwongozo wa kufanikisha utekelezaji wa masuala ya uchumi wa bluu pamoja na umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya bahari kwa maendeleo endelevu na usalama wa eneo la bahari.

Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye Mwambao wa Bahari ya Hindi inaundwa na nchi 23 ambazo ni Australia,  Afrika Kusini, Bangladesh, Comoro, India, Indonesia, Iran, Kenya, Madagascar, Malaysia, Maldieves, Msumbiji, Mauritius, Oman, Seychelles, Singapore, Somalia, Sri Lanka, Tanzania na Thailand, Umoja wa Falme za Kiarabu, Yemen na Ufaransa kupitia Visiwa vya Reunion ambavyo inavimiliki.

 

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.