Tuesday, September 28, 2021

WATAALAMU WAKUTANA KUJADILI MRADI WA KUFUA UMEME MURONGO/KIKAGATI

 Na Mwandishi Wetu, Bukoba

Timu ya wataalamu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekutana na kujadiLi utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa Murongo/Kikagati uliopo katika mto Kagera mpakani mwa Tanzania na Uganda.

Mkutano wa Kitaifa wa Makatibu Wakuu ngazi ya Wataalamu kuhusu mradi wa kufua umeme wa Murongo/Kikagati umefanyika Mjini Bukoba kuanzia tarehe 28 – 30 Septemba, 2021 ambapo pamoja na mambo mengine, wataalamu wamepata fursa ya kujadili mambo mbalimbali kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

Inategemewa kuwa mara baada ya kukamilika kwa mradi huo, utazalisha megawatts 14, na kila nchi itapata megawatts saba. Aidha, Mkutano wa Kitaifa wa Mkatibu Wakuu kwa ngazi ya Wataalamu, utafuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 01 Oktoba 2021.  

Akiongelea kuhusu Mkutano wa Kitaifa wa Mkatibu Wakuu Ngazi ya Wataalamu, Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Kijamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota amesema lengo la Mkutano huo ni kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni mafanikio na changamoto zinazo ukabili mradi kwa sasa. Aidha, Mkutano wa ngazi ya Wataalamu ni utekelezaji wa maagizo ya Mkutano wa 13 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mwezi Novemba 2018.

Ujenzi wa Mradi huo ni makubaliano ya nchi mbili za Tanzania na Uganda ya matumizi bora ya maji ya mto Kagera ambao upo mpakani mwa nchi hizo. Mradi huo unatekelezwa/kujengwa na Kampuni binafsi ya Kikagati Power Company Limited (KPCL).

Awali ujenzi wa mradi huo wenye gharama ya dola milioni 95 ulianza Mei 2018 na sasa unatarajiwa kukamilika Oktoba 2021.

Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Kijamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota akiwasilisha mada katika mkutano wa Kitaifa wa Makatibu Wakuu, ngazi ya Wataalamu kuhusu Mradi wa kufua Umeme wa Murongo/Kikagati leo Mjini Bukoba


Kamishna Msaidizi wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Edward Ishengoma akieleza jambo kwa Wataalamu wakati wa mkutano wa Kitaifa wa Makatibu Wakuu ngazi ya Wataalamu kuhusu Mradi wa kufua Umeme wa Murongo/Kikagati leo Mjini Bukoba


Mhandisi Neema Rushema kutoka Wizara ya Nishati akiongea na Wataalamu katika Mkutano wa Kitaifa wa Makatibu Wakuu ngazi ya Wataalamu kuhusu Mradi wa kufua Umeme wa Murongo/Kikagati


Mhandisi Mgeta Sabe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifafanua jambo katika Mkutano wa Kitaifa wa Makatibu Wakuu ngazi ya Wataalamu kuhusu Mradi wa kufua Umeme wa Murongo/Kikagati

Sehemu ya Wajumbe wakifuatilia Mkutano wa Kitaifa wa Makatibu Wakuu ngazi ya Wataalamu kuhusu Mradi wa kufua Umeme wa Murongo/Kikagati ukiendelea 


Mkutano wa Kitaifa wa Makatibu Wakuu ngazi ya Wataalamu kuhusu Mradi wa kufua Umeme wa Murongo/Kikagati ukiendelea 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.