Friday, September 17, 2021

NUU YATAKIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUKUZA DILOMASIA YA UCHUMI

 Na Mwandishi Wetu, Dar

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax ameishauri Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) kutumia teknolojia vizuri katika kukuza na kuendeleza diplomasia ya uchumi pamoja na masuala ya ulinzi na usalama

Dk. Stergomena Tax ametoa ushauri huo wakati alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku tano ya Wajumbe wa Kamati ya NUU yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea ujuzi wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hio katika masuala ya diplomasia ya uchumi, maslai ya taifa, mawasiliano ya kidemokrasia, uchumi wa bluu, ushirikiano wa Kimataifa na usalama wa nyaraka za kibalozi.

"Huwezi ukatenganisha diplomasia na ulinzi na usalama hususani katika dunia ya sasa ambayo ni dunia ya teknolojia, inayokuwa kwa kasi, diplomasia inatengemea ulinzi na usalama, diplomasia inaongoza maslahi ya Taifa haya ni mambo ambayo hayawezi kutenganishwa," amesema na kuongeza kuwa;

"Teknolojia hii ni muhimu sana katika kuendeleza uchumi na masuala ya diplomasia, ulinzi na usalama kama ikitumika vyema, ila ni vyema tukazitambua pande zote mbili wakati tunatumia teknolojia hii tunalo jukumu ya kutuletea manufaa lakini pia tunalo jukumu la kuwa walinzi wa rasilimali za Taifa letu,"

Awali akimkaribisha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mwenyekiti wa Kamati ya NUU Bw. Mussa Zungu amewasihi watanzania kubadilika na kujikita kujenga uchumi imara.

“Uchumi imara unahitaji diplomasia katika kusimamia maslahi mapana ya Taifa……………hatuwezi kupigwa kama tutakuwa na  watu imara wanaopigania maslahi ya taifa letu, lazima sisi kama kamati inayo ‘cross-cut’ masuala mengi tusimamie maslahi ya taifa letu” Amesema Mhe. Zungu

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amesema Wizara itaendelea kuboresha mafunzo mbalimbali kwa kamati ya NUU kwa lengo la kuwajengea uwezo na ujuzi katika kutekeleza majukumu yao kadri dunia inavyo kwenda.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Bw. Mussa Zungu (Mb) akitoa hotuba kwa wajumbe wa kamati anayoiongoza Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax akihutubia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) katika hafla ya kufunga mafunzo maalumu kwa kamati hiyo Jijini Dar es Salaam 


Wajumbe wa Kamati ya NUU wakimsikiliza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax (hayupo pichani) alipokuwa akihutubia 


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax akimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine  


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Katai ya NUU mara baada ya kumaliza mafunzo maalumu yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.