Thursday, September 23, 2021

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE MHE. BALOZI MBAROUK ATEMBELEA MAKAO MAKUU YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI JIJINI ARUSHA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ameipongeza Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuendelea kuratibu na kuendesha shughuli mbalimbali za mtangamano kwa manufaa ya Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo.

 

Mhe. Balozi Mbarouk ametoa pongezi hizo leo tarehe 23 Septemba 2021 jijini Arusha wakati wa mazungumzo yaliyofanyika kati yake na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Mhandisi Steven Mlote ikiwa ni ziara yake ya kwanza aliyoifanya kwenye Makao Makuu ya Jumuiya hiyo kwa lengo la kujitambulisha tangu kuteuliwa kwake kwenye wadhifa huo.

 

Wakati wa mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Mbarouk alimweleza Mhandisi Mlote kwamba, amefarijika kutembelea Ofisi hizo na kujionea shughuli mbalimbali za uendeshaji zinazofanyika na kusisitiza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kuwa Jumuiya muhimu kwa nchi zote sita wanachama kwa kuwa ni kiunganishi kikubwa katika kuziletea maendeleo endelevu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii nchi hizo.

 

Aidha alisisitiza kuwa, Tanzania itaendelea kutekeleza majukumu mbalimbali kama yalivyoainishwa kwenye Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa michango yake ya mwaka ajili ya kuwezesha uendeshaji wa Jumuiya hiyo.

 

Kwa upande wake, Mhandisi Mlote ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, alimshukuru Mhe. Mbarouk kwa kutenga muda na kutembelea Ofisi hizo na alitumia fursa hiyo kumweleza mfumo mzima wa uendeshaji wa Jumuiya kupitia Sekretarieti.

 

Mbali na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu, Mhe. Naibu Waziri pia alipata fursa ya kuzungumza na Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Mhe. Ngoga Karoli Martin pamoja na Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Jaji Nestor Kayobera ambapo kwenye mazungumzo yao viongozi hao walijadili masuala mbalimbali yanayohusu mchango wa Bunge na Mahakama hiyo kwenye Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Kadhalika, wakati wa ziara hiyo, Mhe. Balozi Mbarouk alimtembelea Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella ambapo viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Mkoa huo na Wizara hususan yale yanayohusu kuimarisha diplomasia ya uchumi kupitia sekta ya utalii ambayo imeshamiri kwenye mkoa huo.

 

Wakati huohuo, Mhe. Mbarouk amekitembelea Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) ambacho ni moja ya Taasisi iliyo chini ya Wizara na kuitaka Menejimenti ya Kituo hicho kuendelea kuboresha utoaji huduma za kituo hicho lii kuendana ushindani uliopo kwenye sekta ya huduma ya utalii wa mikutano.

 

Aidha, Mhe. Naibu Waziri aliwahimiza AICC kukamilisha mchakato wa kuanza ujenzi wa Kituo kipya cha Mikutano cha Kimataifa cha Mlima Kilimanjaro (MKICC) ambacho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia mikutano mikubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Vilevile alipata fursa ya kutembelea baadhi ya miradi ya uwekezaji inayomilikiwa na AICC ikiwemo Kumbi, Hospitali, Kiwanja kitakapojengwa kituo cha MKICC na nyumba za makazi zaidi ya 600 zilizopo maeneo ya Kijenge, Soweto na Barabara ya Range kwenye Jiji la Arusha.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi za Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote (kushoto) kwa ajili ya kuanza ziara yake kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Jumuiya hiyo zilizopo jijini Arusha. Ziara hiyo ambayo ililenga kujitambulisha na kujionea shughuli za utendaji za Sekretarieti imefanyika tarehe 23 Septemba 2021.

Mhe. Naibu Waziri akizungumza na Mhandisi Mlote ambaye alimpokea kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Jumuiyay wakati wa ziara yake ya kujitambulisha aliyoifanya kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha tarehe 23 Septemba 2021.

Mhandisi Mlote akimkabidhi Mhe. Balozi Mbarouk  zawadi ya machapisho mbalimbali kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mhe. Balozi Mborouk na Mhandisi Mlote wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe walioambatana nao wakati wa mazungumzo yaliyofanyika kati yao

Mhe. Balozi Mbarouk akizungumza na Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Jaji...alipomtembelea ofisini kwake wakati wa ziara yake kwenye Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha tarehe 23 Septemba 2021. Kushoto ni Msajili wa Mahakama hiyo.

Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Jaji Kayobera

Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Mhe. Jaji Kayobera, Mhandisi Mlote (kulia) na Msajili wa Mahakama hiyo (kushoto)

Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja na Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe.Ngoga Karoli Martin (kulia)  mara baada ya kumaliza mazungumzo yao

Mhe. Balozi Mbarouk akisikiliza maelezo kuhusu utendaji kazi wa Kituo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Kuratibu mwenendo wa magari ya  mizigo hususan katika kipindi hiki cha ugonjwa wa UVIKO-19

Mhe. Balozi Mbarouk akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella. Mhe. Mbarouk alimtembelea Mkuu huyo wa Mkoa wakati wa ziara yake ya kikazi kwenye Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mongella

Mhe. Balozi Mbarouk akizungumza na Menejimenti ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) alipokitembelea kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinanatekelezwa na Kituo hicho ambacho ni moja ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Bw. Savo Mung'ong'o.

Kikao kikiendelea na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya AICC

Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja naWajumbe wa Menejimenti ya AICC

Mhe. Balozi Mbarouk akipata maelezo kuhusu Ukumbi wa Simba uliopo AICC. 

Mhe. Balozi Mbarouk akipata maelezo alipotembelea nyumba za kupangisha ikiwa ni baadhi ya miradi ya uwekezaji inayomilikiwa na AICC

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.