Na Mwandishi wetu,
Dar
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imekiri uwepo
wa ongezeko la biashara kati ya Tanzania na nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki na Ushoroba wa kusini zikiwemo nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC) tangu Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF)
Bi. Angelina Ngalula amesema kuwa ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na nchi
jirani zikiwemo Kenya, Burundi na Uganda umeongezeka na kwamba ushirikiano kati
ya Tanzania na Mataifa hayo umezidi kuimarika ukiashiria kukua kwa diplomasia
ya uchumi.
“Sasa hivi ukiangali ukuaji wa biashara chini ya
uongozi wa Serikali ya awamu ya sita, Serikali inaishirikisha ipasavyo Sekta
binafsi katika kukuza na kuendeleza biashara na uwekezaji nchini,” amesema Bi.
Ngalua
Ameongeza kuwa ushirikiano ambao Serikali imekuwa
ikiutoa kwa sekta binafsi umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa kiwango
cha biashara kati ya Tanzania na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na
ushoroba wa kusini ikihusisha nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC).
Bi. Ngalula amepongeza hatua ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuamua kuambatana na
wawekezaji na wafanyabiashara kutoka katika Taasisi ya Sekta Binafsi kwa kuwa
hatua hiyo imesaidia kuwakutanisha na kuwaunganisha na wenzao wa Mataifa
mengine tofauti na nyakati zilizopita ambapo kila mfanyabiashara alijitafutia
fursa peke yake.
Kwa uapnde wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameihakikishia Taasisi ya
Sekta Binafsi ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini kwa kuwa Serikali inaamini
uwepo wa sekta binafsi imara ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi imara wa
Nchi.
Balozi Mulamula ameitaka TPSF kuhakikisha kuwa inakuwa
na kanzi data ili kurahisisha azma ya Serikali ya kuiunganisha sekta hiyo na
wafanyabiashara pamoja na wawekezaji kutoka katika mataifa mengine ulimwenguni.
Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa
mazungumzo na Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya uchumi Dkt.
Stefan Oswald aliyefuatana na Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya Afrika
katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Ujerumani kwa lengo la kuzungumzia masuala
mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa kidiplomasia na maendeleo ya Uchumi.
Dkt. Oswald amemuambia Balozi Mulamula kuwa Tanzania
imekuwa ni Nchi ya kwanza kwa viongozi hao wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ujerumani
kuifanya na hiyo imetokana na ishara ya mabadiliko ya kidiplomasia na ushirikiano wa
Maendeleo na Mataifa mengine duniani iliyooneshwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Ameongeza kuwa mazungumzo kati ya Mhe. Samia Suluhu
Hassan na Kansela wa Ujerumani Mhe Angela Merkel ambayo yalilenga kutoa
kipaumbele cha uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji yamekuwa
kichocheo cha Viongozi hao kufanya ziara hapa nchini.
Dkt.Stefan amesema Ujerumani iko tayari kushirikiana
na Tanzania pamoja na Nchi za Afrika kuzisaidia kuimarisha uchumi kutokana na
kuathiriwa na UVIKO 19.
Pamoja na mambo mengine, mazungumzo ya viongozi hao yaligusia
masuala la ulinzi na usalama katika ukanda wa maziwa makuu na kutafuta
suluhisho la kudumu kwa wakimbizi wa Burundi.
|
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata akiwa katika mazungumzo na Mwenyekiti wa
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bi. Angelina Ngalula katika Ofisi Ndogo
za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Mazungumzo
baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi
Liberata akiwa katika mazungumzo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta
Binafsi Tanzania (TPSF) Bi. Angelina Ngalula yakiendelea
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akizungumza
na Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya uchumi Dkt. Stefan
Oswald aliyefuatana na Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya Afrika katika
Wizara ya Mambo ya Nje wa Ujerumani
Mazungumzo baina ya Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya uchumi Dkt. Stefan
Oswald yakiendelea