Friday, October 29, 2021

UMOJA WA ULAYA WARIDHISHWA NA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI TANZANIA


Mwenyekiti mwenza wa Kikao hicho ambaye pia ni Mkurugenzi Mwendeshaji anayeshughulikia masuala ya Afrika kutoka  Umoja wa Ulaya Balozi Rita Liranjinha akizungumza na waandishi wa habari kuelezea majadiliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika mashariki na Mwenyekiti mwenza wa Kikao cha  majadiliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuelezea umuhimu wa kikao hicho

Mkurugenzi Mwendeshaji anayeshughulikia masuala ya Afrika wa  Umoja wa Ulaya Balozi Rita Liranjinha (kushoto) akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) katika picha ya pamoja baada ya kuzungumza na waandishi wa habari kuelezea majadiliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya yaliyofanyika jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi Mwendeshaji anayeshughulikia masuala ya Afrika wa  Umoja wa Ulaya Mhe. Balozi Rita Liranjinha (kushoto) akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Wizara na mabalozi  walioshiriki majadiliano ya pamoja kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya baada ya kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.


Washiriki wa majadiliano ya pamoja kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya yaliyofanyika jijini Dar es Salaam katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mwendeshaji anayeshughulikia masuala ya Afrika wa  Umoja wa Ulaya Balozi Rita Liranjinha na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula


Viongozi walioshiriki majadiliano ya pamoja kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya yaliyofanyika jijini Dar es Salaam katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mwendeshaji anayeshughulikia masuala ya Afrika wa  Umoja wa Ulaya Balozi Rita Liranjinha na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula



 


Na Waandishi wetu, Dar


Umoja wa Ulaya umeoneshwa kuridhishwa na mazingira ya uwekezaji na ufanyaji wa biashara nchini Tanzania na kuahidi kuhamasisha wawekezaji kutoka katika umoja huo kuja kuwekeza na kufanya biashara zaidi.


Akizungumza katika ufunguzi wa majadiliano kuhusu masuala mtambuka na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti mwenza wa Kikao hicho ambaye pia ni Mkurugenzi Mwendeshaji anayeshughulikia masuala ya Afrika kutoka  Umoja wa Ulaya Balozi Rita Liranjinha amesema Umoja wa Ulaya Umeridhishwa na mazingira ya biashara na uwekezaji hapa Tanzania na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika Sekta ya biashara na uwekezaji.

Balozi Rita pia amepongeza kitendo cha Tanzania kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali katika harakati za kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini na hivyo kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji wengi nchini. 

Kadhalika, Balozi Rita ameipongeza Tanzania kwa kufanya kazi na watanzania wote hasa sekta binafsi kwani huchangia kutoa ajira kwa watu wengi na kuichangia kuinua maendeleo.

“Naipongeza Serikali kwa kusikiliza sauti za wananchi na kuchukua hatua kukabiliana na changammoto zinazowakabili wananchi kwa wakati ambacho amekielezea kuwa ni sawa na kupanda mbegu ya matumaini kwa wanachi,” amesema Balozi Rita.

Ameongeza kuwa Umoja wa Ulaya unaiona Tanzania ni mdau mkubwa wa Tanzania na kwamba umoja huo utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha maendeleo ya kweli yanapatikana kwa maslahi ya pande zote mbili.   

“Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na Tanzania kuboresha mazingira bora ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na  kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kama Uviko 19, mabadiliko ya tabia nchi na kuondoa umasikini,” amesema Balozi Rita.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti mwenza wa majadiliano hayo, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameupongeza Umoja wa Ulaya kwa  utayari wake wa kuisaida Tanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili dunia kwa sasa.

Balozi Mulamula amesema Uhusiano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya umedumu kwa muda mrefu na kwamba Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya katika kukuza na kuendeleza ushirikiano huo kwa maslahi ya pande zote mbili hasa katika kukuza na kuendeleza  biashara, uwekezaji, haki za binadamu na mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO19.  

Balozi Mulamula ameihakikisha Jumuiya hiyo kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya katika harakati zake za kupambana na umasikini nchini hata kwa nchi nyingine zinazoizunguka.

Ameongeza kuwa pamoja na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza kama vile ugonjwa wa Uviko 19, Tanzania itaendelea kuchukua tahadhari na kuimarisha sekta ya afya ili kuendelea kupambana na janga hilo.

Waziri Mulamula ameuhakikishia Umoja wa Ulaya kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha na kuboresha mazingira ya  biashara na uwekezaji nchini ili kukuza uchumi na hivyo kuleta maendeleo.

Majadiliano hayo yamehudhuriwa na mabalozi mbalimbali kutoka Umoja wa Ulaya ambao ni Balozi wa Umoja wa Ulaya, Ubelgiji, Finland, Sweden, Denmark, Italia, Czech, Ufaransa, Ujerumani, Hispania, Canada, Poland, Ireland na Uholanzi.

TANZANIA NA UMOJA WA ULAYA WAKUTANA KWA MAJADILIANOO DAR ES SALAAM

Waziri  wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza kufungua mkutano wa majadiliano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya uliofanyika jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Joseph Sokoine akizungumza kumkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufungua mkutano wa majadiliano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya uliofanyika jijini Dar es Salaam

Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Manfredo Fanti akizungumza wakati wa Mkutano wa majadiliano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya uliofanyika jijini Dar es Salaam

Mwenyekiti mwenza wa Kikao cha Majadiliano ya pamoja kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya ambaye pia ni Mkurugenzi Mwendeshaji anayeshughulikia masuala ya Afrika kutoka  Umoja wa Ulaya Mhe. Balozi Rita Liranjinha akizungumza wakati wa ufunguzi wa  mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam

Mabalozi kutoka nchi za Umoja wanaoziwakilisha nchi zao nchini wakishiriki katika Mkutano wa majadiliano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya uliofanyika jijini Dar es Salaam

Washiriki wa wa Mkutano wa majadiliano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya uliofanyika jijini Dar es Salaam wakifuatilia kikao hicho

Washiriki wa wa Mkutano wa majadiliano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya uliofanyika jijini Dar es Salaam wakifuatilia kikao hicho

 

TANZANIA NA RWANDA ZASAINI HATI YA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA ULINZI

Tanzania na Rwanda zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Ulinzi (Memorandum of Understanding between United Republic of Tanzania and Republic of Rwanda on Defence Cooperation). Hati hiyo imesainiwa tarehe 28 Oktoba, 2021 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda Mhe. Dkt. Vincent Biruta kwenye Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ya Kudumu uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza kwenye Mkutano huo, Waziri Mulamula ameeleza kuwa miongoni mwa faida za mkutano huo ni kusainiwa kwa Hati hiyo ya Makubaliano ambayo itasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa watu,mali na mipaka baina ya Mataifa haya mawili.

“kusainiwa kwa Hati hii ni hatua muhimu kwenye mahusiano kati ya nchi zetu hizi mbili, vilevile nina imani kubwa yale yote yaliyokubalika yatatekelezwa kwa ufanisi ili kufikia malengo tarajiwa ya nchi hizi mbili na Serikali kwa ujumla” amesema Balozi Mulamula.

Sambamba na kusaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Ulinzi, Tanzania na Rwanda zilijadili na kukubaliana kuhusu maeneo mengine mapya ya ushirikiano ikiwemo Manunuzi ya Umeme kutoka Mradi wa Rusumo, Ushirikiano katika Uchimbaji wa Petroli na Gesi na kubadilishana wanafunzi kati ya Chuo cha Diplomasia cha Tanzania na Chuo cha Diplomasia cha Rwanda kinachorajiwa kuanzishwa mwaka 2022.

Kwa upande wake, Dkt. Birtua aliipongeza na kuishukuru Tanzania kwa kuandaa, kushiriki kikamilifu na kuupa uzito wa hali ya juu Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda ambapo alisema kuwa hiyo ni dalili njema inayoonesha nia iliyopo ya kudumisha na kukuza ushirikiano wa kihistoria na kindugu uliopo kati ya kati Nchi hizi mbili.

Vilevile Balozi Mulamula alitoa wito kwa Sekta zinazohusika na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano huo, kuhakikisha zinatekeleza kikamilifu maagizo yaliyotolewa na kuwasilisha ripoti zake katika Mkutano wa Kamati ya Pamoja ya Utekelezaji uliopangwa kufanyika mwezi Machi, 2022 nchini Rwanda. 

Mkutano huu wa Kumi na Tano (15) wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ya Kudumu ulitanguliwa na Kikao cha Wataalamu wa Tanzania na Rwanda kilichofanyika tarehe 25 na 26 Oktoba, 2021 na kufuatiwa na Kikao cha Makatibu Wakuu wa nchi hizi mbili kilichofanyika tarehe 27 Oktoba, 2021.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiongoza Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda katika ngazi ya Mawaziri uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda katika ngazi ya Mawaziri uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Meza kuu wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Taifa wa Tanzania na Rwanda unaimbwa kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika ngazi ya Mawaziri
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda Mhe. Dkt. Vincent Biruta akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwandakatika ngazi ya Mawaziri uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa Mkutano kutoka Tanzania na Rwanda wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Mataifa hayo mawili unaimbwa kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika ngazi ya Mawaziri
Mkutano ukiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda Mhe. Dkt. Vincent Biruta wakisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Ulinzi.
Picha ya pamoja ya Viongozi walioshiriki Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda
Picha ya pamoja ya washiriki wa Mkutano wa 15 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda