Wednesday, July 6, 2022

BALOZI MULAMULA: SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA WEZESHI KWA SEKTA BINAFSI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mazungumzo na Wawakilishi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) katika ofisi ndogo za Wizara leo tarehe 6 Julai 2022 jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo Waziri Mulamula amewahakikishia Wawakilishi hao kuwa Serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kukuza sekta za uzalishaji kwa maslahi mapana ya Taifa.

‘’ Wizara kupitia Balozi zetu nje imeendelea kuhakikisha fursa mbalimbali zinazopatikana nchini zinatangazwa katika maeneo ya uwakilishi ili kuzihakikishia sekta hizo mageuzi makubwa ya  kiuchumi” alisema Balozi Mulamula.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF, Bi. Angelina Ngalula pamoja na wajumbe alioambatana nao wameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mkazo wa kuinua sekta binafsi.

Akifafanua Bi. Ngalula ameeleza juu ya uwepo wa mafanikio katika sekta za biashara, Utalii, uwekezaji, kilimo, madini, huduma, uchukuzi na usafirishaji na ujenzi.

“Sisi sekta binafsi tunaishukuru Serikali yetu kwa kuboresha mazingira ya biashara, sasa tunashuhudia mipaka inafunguka sambamba na ongezeko la watalii kupitia jitihada za makusudi zinazofanyika katika kuitangaza filamu ya “Tanzania the Royal Tour” alisema Bi. Ngalula

Aidha, akafafanua matokeo yaliyopatikana kupitia ziara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwamba kupitia ziara hizo mikutano na makongamano ya biashara yalifanyika katika nchi mbalimbali na yamesaidia kupatikana kwa washirika wa kibiashara kutoka mataifa hayo.

Kupitia mazungumzo hayo Waziri Mulamula na Wawakilishi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi, wamekubaliana kuanzisha timu maalum ya uratibu na ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ya kimkakati kitaifa, kwa lengo la kuimarisha na kukuza diplomasia ya uchumi nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kati) akizungumza na Wawakilishi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) leo tarehe 6 Julai 2022 katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF, Bi. Angelina Ngalula.


Waziri Mulamula akizungumza na Wawakilishi wa Bodi ya TPSF kutoka katika Sekta za Huduma, Sekta Umma, Sekta ya Wenye Viwanda Vidogo,Sekta ya Wafanyabiashara Wanawake, Sekta ya Uhandisi na Ujenzi, na ulioambatana, Uongozi wa TPSF uliokuwa umeambatana na Bi. Ngalula.

Kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga akifafanua jambo katika mazungumzo hayo.


Balozi Mulamula akimkabidhi  Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF, Bi. Ngalula vitabu vya Diplomasia ya Uchumi.

Picha ya Pamoja.



VACANCY ANNOUNCEMENT


 

VACANCY ANNOUNCEMENT









 

NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI ZATAKIWA KUKUZA, KUENZI KISWAHILI

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimetakiwa kuweka mikakati ya muda mrefu ili kukuza, kuendeleza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Bw. Khamis Abdalla Saidi aliyemwakilisha Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe.Tabia Maulid Mwita katika Kongamano la kwanza la Siku ya Kiswahili Duniani lililoanza leo tarehe 6 Julai, 2022 Zanzibar. 

Kongamano hilo linalongozwa na Kauli Mbiu: “Kiswahili kwa Amani, Ustawi na Utangamano wa Kikanda” litahitimishwa kwenye siku ya Kilele cha Siku ya Kiswahili duniani tarehe 7 Julai 2022.

Katika hotuba yake, Bw. Saidi amesema kuenea kwa Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki na Mataifa mengine ni bidhaa ya bishara, hivyo umuhimu wa Kiswahili ni mkubwa katika kupiga hatua ya kimaendeleo. 

“Ni jukumu la kila mmoja wetu kukifuatilia Kiswahili katika kila hatua na kutafuta na kubuni njia na mikakati ya muda mrefu na ya kisasa ya kuikuza lugha hii adhimu ya Kiswahili,” amesema Bw. Saidi.

Bw. Saidi aliongeza Lugha ya Kiswahili inatakiwa itumike kama bidhaa inayouzwa na kupata tija. Kuna haja kubwa ya kuwekeza kuwasomesha wataalamu wa lugha kuwa na stadi na uwezo unaotakiwa katika kutoa huduma ya kufundisha, ukalimani, kutafrisi na kuandaa machapisho mbali mbali kwa Kiswahili.

“Ni jukumu la vyuo vikuu vya Afrika Mashariki kutilia mkazo mikakati ya muda mrefu ya uwekezaji wa kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa kufanya tafiti mbalimbali za lugha,” ameongeza Bw. Saidi. 

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote amesema kuwa jumuiya ya Afrika Mashariki inapaswa kushirikiana kwa pamoja na wadau wa Lugha ya Kiswahili ili kuweza kupata uzoefu wa matumizi ya Kiswahili pamoja na kujadili changamoto za lugha hiyo ili kuimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili yataimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa lugha hii ni lugha ya biashara hivyo tunapaswa kujivunia lugha hii adhimu kwa maslahi mapana ya jumuiya yetu,” amesema Mhandisi Mlote.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (MS TCDC), Bi. Yusta Mganga amesema licha ya kuimarika kwa matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukanda huo unapaswa kuchukua hatua madhubuti zaidi kwa ajili ya kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakuzwa na kuendelezwa miongoni mwa nchi ambazo bado hazijaimarika katika matumizi ya Kiswahili. 

“Kuna njia mbalimbali za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kama vile kufanya tafiti, uandaaji wa makongamano na semina mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya Kiswahili…….katika kuandhimisha siku hii muhimu ni vyema tukatafakari mafanikio ya Kiswahili katika ukanda wa Jumuiya yetu ili kuimarisha amani na utangamano wa kikanda,” amesema Bb. Mganga

Novemba 23, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) lilitangazwa rasmi kuwa tarehe 7 Julai ya kila mwaka ni siku maalumu ya kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani. 

Februari 2022, Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika katika mkutano wake wa kawaida wa 35 walipitisha Kiswahili kama Lugha ya Kazi na mawasiliano mapana Barani Afrika.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, Bw. Khamis Abdalla Saidi akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani linalofanyika Zanzibar kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote akitoa hotuba yake katika Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar

Kaimu Katibu Mtendaji Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. James Jowi akizungumza na washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar 

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Dkt. Mwanahija Ali Juma akielezea mchango wa BAKIZA katika Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar 

Meza Kuu wakifuatilia kikundi cha ngoma za asili kutoka Zanzibar wakati wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar 

Washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani wakifuatilia kikundi cha ngoma za asili kutoka Zanzibar  

Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota akitoa mchango wake katika Kongamano la Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar

Washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani wakiimba wimbo wa Taifa  

Washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani wakifuatilia Kongamano hilo lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar 

Meza Kuu katika picha ya pamoja na wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar 



WATANZANIA WAASWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MASOKO YA KIMATAIFA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amewasihi Watanzania kuchangamkia fursa za masoko ya bidhaa mbalimbali nje ya nchi.

Balozi Fatma ametoa rai hiyo leo alipotembelea Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam.

Balozi Fatma ameeleza Wizara ya Mambo ya Nje kupitia Balozi zake nje imekuwa ikitatafuta fursa za uwekezaji, masoko ya bidhaa na kutangaza vivutio vya utalii kupitia majukwaa na mikutano mbalimbali inayofanyika katika vituo vya uwakilishi nje ya nchi.

“Fursa za masoko zinazopatikana kwa sasa ni pamoja na; Soko la zao la ufuta, mihogo na soya nchini China; Soko la nyama na wanyama kama mbuzi na kondoo nchini Saud Arabia; Soko la nafaka kama maharage na mbaazi nchini Oman na Umoja wa Falme za kiarabu (U.A.E);  Soko la parachichi nchini Ufaransa, India na Uholanzi; na Soko la asali katika nchi za Scandnavia na Mashariki ya Kati.

Balozi Fatma pia ameeleza uwepo wa soko la uyoga katika masoko ya kimataifa kufuatia umuhimu wa zao hilo na kutoa rai kwa watanzania kuchangamkia kilimo kwa ajili ya biashara badala ya kuzalisha kwa chakula pekee.

Aidha, aliongeza kusema jitihada hizi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zinafanywa kwa kushirikiana na Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Mamlaka ya Usimamizi wa Biashara Tanzania (TANTRADE) pamoja na Wizara ya Kilimo kwa lengo la kuhamasisha wakulima na wafanyabiashara kuchangamkia fursa mbalimbali za masoko ili kujitangaza kimataifa na kukuza mitaji ya biashara zao.

Wakati huo huo Balozi Fatma amezungumzia jitihada zinazofanywa na Balozi zetu katika kutangaza filamu ya “Tanzania the Roya Tour” kwa lengo la kuongeza watalii sambamba na kuitangaza Tanzania Nje ya mipaka kupitia mandhari na mazingira ya asili yanayo onekana katika filamu hiyo.

Kadhalika, ameeleza fursa zinazopatikana kutokana na jitihada za wizara kupitia Balozi zake katika kukuza lugha ya Kiswahili duniani hususan wakati huu tunapoelekea tarehe 7 Julai 2022 kwenye maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayoadhimishwa kitaifa Jijini Dar es Salaam.

Balozi Fatma akiwa katika viwanja vya Maonesho ya Sabasaba pia ametembelea banda la Kituo cha Mikutano cha Kitamataifa cha Arusha (AICC), Kenya, Zanzibar, pamoja na Shirika la Madini (Stamico).

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akipokea maelezo kutoka kwa maafisa wa Wizara hiyo wakati wa maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba tarehe 5 Julai 2022 jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akipokea maelezo kutoka kwa maafisa wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha wakati wa maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba tarehe 5 Julai 2022 jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akipokea maelezo kutoka kwa mjasiliamali anayeshiriki maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba  tarehe 5 Julai 2022 jijini Dar es Salaam.


BALOZI MUSHY AITAFUTIA MSHIRIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA

Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy akiwa katika kikao na uongozi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna ambapo wamekubaliana kuandaa Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuanzisha ushirikino na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma.

Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy
akiwa na baadhi ya viongozi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna baada ya kikao chao walichokubaliana kuandaa Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuanzisha ushirikino na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma.

Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy akiwa na baadhi ya madaktari wa
Hospitali na Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna. Hospitali hiyo imekubali kuanzisha ushirikino na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma.

Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy akiwa katika picha ya pamoja na Watanzania wanaoishi nchini Ausrtia baada ya kufanya nao mkutano wa kujadili mustakabali wao. katika mkutano huo Watanzania hao walianzisha umoja wao na kuchagua viongozi wa umoja huo  utakaoitwa Tanzania Diaspora in Austria (TADA)

Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy (tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Umoja wa Watanzania wanaoishi Austria mara baada ya kuanzisha umoja huo na kuchagua viongozi wake.





 

TANZANIA NA AFRIKA KUSINI KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA ELIMU

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini, Mhe. Matsie Angelina Motshekga ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi.

Wakati wa kikao chao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam leo tarehe 5 Julai 2022, Mawaziri hao walijadili pamoja na mambo mengine, namna nchi zao zitakavyoweza kushirikiana katika sekta ya elimu.

Mhe. Motshekga anayetarajiwa kusaini Hati ya Makubaliano na Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda kuhusu Tanzania kushirikiana na Afrika Kusini kufundisha Kiswahili katika nchi hiyo, alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuainisha maeneo ya kipaumbele ya aina ya elimu tunayoihitaji ili tuweze kubadilishana uzoefu katika maeneo hayo.

Maeneo mengine ambayo viongozi hao waliyadili ni pamoja na programu za kubadilishana wanafunzi na walimu na changamoto zinazoikabili sekta za elimu za nchi hizo ambazo ni pamoja na uhaba wa miundombinu, mimba za mapema, kuacha shule na uhaba wa vitabu.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberrata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angelina jijini Dar Es Salaam.

Ujumbe ulioambatana na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angelina ukifuatilia kwa makini mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberrata Mulamula na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angelina jijini Dar Es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberrata Mulamula na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angelina wakiendelea kujadili masuala ya elimu kuhusu nchi zao huku ujumbe wa Tanzania ukifuatilia kwa makini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberrata Mulamula akiwa na mgeni wake, Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angelina baada ya mazungumzo yao.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberrata Mulamula  na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini, Mhe. Matsie Angelina wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe walioambatana nao kwenye mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam.


 

TANZANIA YASIFIWA INAFANYA VIZURI KATIKA CHANJO ZA UVIKO-19.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeratibu msauala ya UVIKO-19, Dkt. Ted Chaibans jijini Dar Es Salaam tarehe 5 Julai 2022.

Katika kikao hicho, Balozi Mulamula alielezea hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania za kudhibiti ugonjwa wa UVIKO-19 na kusisitiza umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kushirikiana na Tanzania kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Balozi Mulamula alisema licha ya changamoto za uhaba wa miundombinu na ukubwa wa nchi, Serikali imejitahidi kupambana na ugonjwa huo, hususan kwa kuhamasisha wananchi wajitokeze kupata chanjo za UVIKO-19.

Balozi Mulamula alihitimisha mazungumzo hayo kwa kukumbushia wito wa Serikali kuhusu kupata msaada wa Jumuiya ya Kimataifa ili Serikali ya Tanzania iweze kutimiza azma yake ya kujenga kiwanda cha kutengeneza chanjo za Uviko-19 na magonjwa mengine.

Kwa upande wake, Dkt. Chaibans alikiri kuwa licha ya Tanzania kuchelewa kuanza matumizi ya chanjo za UVIKO-19 lakini imepiga hatua kubwa kuliko baadhi ya nchi zilizoanza mapema kampeni za kuhamasisha chanjo. Alisisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kuhamasisha watu kwa kubuni mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwatumia viongozi wa dini. Aliendelea kwa kutoa wito kwa Serikali ya Tanzania, ihakikishe kuwa makundi ya kipaumbele kama Wazee, wenye maradhi ya kudumu, watumishi wa sekta za afya, elimu na utalii wanahamasishwa ili wapate chanjo za UVIKO-19.

Wakati huo huo, Balozi Mulamula amekutana na wajumbe wa Kamati ya Afrika ya Hydrogen inayojihusisha na uwekezaji katika nishati jadidifu (renewable energy).  Wajumbe wa Kamati hiyo walimweleza Mhe. Waziri Mulamula utajiri wa vyanzo mbalimbali vya nishati ilivyonavyo Tanzania ambavyo vina fursa nyingi za kibiashara, endapo vitatumiwa vizuri. Kamati hiyo imeelezea utayari wa kufanya kazi na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa rasimali hizo zinatumika vizuri ili ziweze kuleta maendeleo endelevu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimkaribisha Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeratibu masuala ya UVIKO-19, Dkt. Ted Chaiban ili waweze kujadili masuala ya UVIKO-19.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeratibu masuala ya UVIKO-19, Dkt. Ted Chaiban ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi.

Ujumbe ulioambatana na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeratibu masuala ya UVIKO-19, Dkt. Ted Chaiban ukifuatilia kwa makini mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeratibu masuala ya UVIKO-19, Dkt. Ted Chaiban.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeratibu masuala ya UVIKO-19, Dkt. Ted Chaiban wakiendelea na mazungumzo yao huku ujumbe wa Tanzania ukifuatilia kwa makini mazungumzo hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeratibu masuala ya UVIKO-19, Dkt. Ted Chaiban wakisikiliza ufafanuzi wa jambo kutoka kwa mtaalamu wa UN kuhusu UVIKO-19.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiteta jambo na mmoja wa mjumbe  aliyeambatana na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeratibu masuala ya UVIKO-19, Dkt. Ted Chaiban.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeratibu masuala ya UVIKO-19, Dkt. Ted Chaiban wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe walioambatana nao wakati wa mazungumzo kuhusu UVIKO-19.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Kamati ya Afrika ya Hydrogen ambayo inajishughulisha na masuala ya kutoa ushauri na uwekezaji katika Nishati jadidifu (renewable energy).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha y pamoja na wajumbe wa kamati ya Afrika ya Hydrogen.

Tuesday, July 5, 2022

Balozi Mulamula Apokea Nakala za Hati za Utambulisho

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa Serikali haiwezi kutekeleza majukumu yake ipasavyo bila ya kuwa na sekta binafsi iliyoimarika.

Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 5 Julai 2022 jijini Dar Es Salaam wakati akipokea nakala za Hati za Utambulisho za Balozi Mteule wa Uganda hapa nchini, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye.

Balozi Mulamula amesema kuwa Tanzania na Uganda zina uhusiano mzuri wa kihistoria na umekuwa ukiimarika siku hadi siku kutokana na masuala mbalimbali ya ushirikiano yanayoendelea, yakiwemo ziara za viongozi wa kitaifa.

Alisema kuwa hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alifanya ziara nchini Uganda ambapo makubaliano na ahadi mbalimbali zilitolewa katika ziara hiyo. Makubaliano hayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa sekta binafsi za nchi hizi mbili zinawekewa mazingira mazuri ya kufanya uwekezaji na biashara kwa faida ya wananchi wake.

Alielezea matumaini yake kuwa Balozi Mteule atahakikisha kuwa ahadi na makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande mbili hizo yanatekelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga unatekelezwa kama ulivyopangwa.

Mhe. Waziri alimalizia kwa kumuhakikishia Balozi huyo kuwa Wizara na Serikali kwa ujumla itampa ushirikiano wa kutosha ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Balozi Mwesigye aliahidi kuwa atatumia ujuzi na maarifa aliyopewa kwa kushirikiana na wenzake balozini kuhakikisha kuwa makubaliano na maelekezo yaliyotolewa wakati wa ziara za viongozi wa kitaifa na majukwaa mengine yanatekelezwa ipasavyo.

Balozi Mteule wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye akiwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula jijini Dar Es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiendelea na mazungumzo na Balozi Mteule wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Balozi Mteule wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye baada ya kuwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi Mteule wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wao 
baada ya kuwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho.

 



Monday, July 4, 2022

BALOZI MULAMULA: WIZARA KUENDELEA KUHAMASISHA WAWEKEZAJI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema Wizara itaendelea kuhakikisha kuwa sekta za uwekezaji, biashara na utalii zinazidi kuimarika.

Balozi Mulamula alitoa kauli hiyo wakati alipotembelea banda la Wizara katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam.

Akiwa katika banda la Wizara, Waziri Mulamula amewapongeza watumishi wanaoiwakilisha Wizara katika maonesho hayo na kuongeza kwamba Wizara imekuwa ikijivunia kuwa sehemu ya kutafuta wawekezaji na wafanyabiashara ili kuja kuwekeza nchini kama ambavyo kauli mbiu ya maonesho hayo inavyosema ‘Tanzania: Mahali sahihi pa Biashara na Uwekezaji’

“Wizara kupitia Balozi zake Nje ya nchi inaendelea kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali katika kuhakikisha kuwa tunapata wawekezaji wa kutosha kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imejitahidi kuboresha mazingira ya biashara na uwekeza” alisema Balozi Mulamula

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri aliwasihi watumishi wa Wizara kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, juhudi na bidii na kuendelea kuzitangaza fursa za biashara, uwekezaji pamoja na vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini.

Katika tukio jingine Balozi Mulamula alishiriki katika hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 46 ya Biashara ya Sabasaba yaliyofunguliwa na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) Mhe. Wamkele Mene tarehe 03 Juni, 2022 Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda na Wizara inayoiongoza katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na watumishi wa Wizara katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na watumishi wa Wizara alipotembelea banda la wizara katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Watumishi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AlCC) katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam

Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) Mhe. Wamkele Mene akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati wa hafla ya ufunguzi wa maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam





Friday, July 1, 2022

TANZANIA YASHIRIKI KONGANANO LA MIJI DUNIANI

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshiriki Kongamano la Kumi na Moja la Miji Duniani, lililofanyika jijini Katowice, Poland tarehe 26 hadi 30 Juni 2022.

Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya na Mwakilishi katika Shirika la UN Habitat Mhe. John Simbachawene

Katika kongamano hilo, Balozi Simbachawene alieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuleta maendeleo endelevu ya miji kwa kutengeneza sera ya maendeleo ya miji, kuwekeza kwenye miundombinu, kuwezesha sekta binafsi na kuhamasisha utunzaji wa mazingira katika miji. 

Kupitia konganabo hilo, Balozi Simbachawene alipata nafasi ya kuzungumza na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo UN Habitat, AfDB, UNECA, UNDP, Islamic Fund, Saudi Fund, European Commission ambao aliwaelezea kuhusu mipango ya Serikali ya kuendeleza miji na kuwaomba kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa mipango hiyo ili kutimiza lengo Namba 11 la Umoja wa Mataifa  la Maendeleo Endelevu  linalohusu maendeleo  makazi na miji na (SDG 11).

Mbali na Balozi Simbachawene, Balozi wa Ujerumani anayewakilisha pia nchini Poland Mhe. Dkt. Abdalah Possi pia alishiriki kongamano hilo.  

Taasisi nyingine zilizoshiriki ni pamoja na Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Manispaa ya Jiji la Dodoma, TARURA na DART.