Waziri wa Norway anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic Mhe. Anne Beathe Tvinnereim akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chihembe-Mvumi jijini Dodoma. |
Wednesday, September 7, 2022
NORWAY KUONGEZA BAJETI YA KUTEKELEZA MIRADI MBALIMBALI NCHINI
WAZIRI MULAMULA AKUTANA NA MABALOZI WA UTURUKI, ETHIOPIA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) kwa nyakati tofauti amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Uturuki nchini, Mhe. Dkt. Mehment Gulluoglu na Balozi wa Ethiopia nchini, Mhe. Shibru Mamo Kedida tarehe 7 Septemba 2022 katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Akiongea na Dkt. Gulluoglu Waziri Mulamula amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Uturuki katika masuala ya biashara, masoko, kilimo, uwekezaji, utalii, madini na uchumi wa bluu.
Naye Balozi wa Uturuki nchini, Mhe. Dkt. Mehment Gulluoglu ameeleza kuwa katika kipindi chake cha uwakilishi anafanya jitihada za makusudi kuhakikisha Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki unafanyika ili kuongeza nguvu ya utekelezaji katika maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa.
Katika tukio jingine, Waziri Mulamula amemhakikishia Balozi wa Ethiopia nchini, Mhe. Kedida kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano wa muda mrefu na wa kihistoria ulioasisiwa na waasisi wa mataifa yao ili kufikia malengo ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.
Ameongeza kuwa Tanzania itaendelea kuzingatia utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yanayofikiwa katika Umoja wa Afrika hususan umuhimu wa mto Nile na manufaa yake katika sekta za kilimo na huduma nyingine za kijamii.
Naye Mhe. Kedida amemueleza Waziri Mulamula kuwa Ethiopia itaendeleza jitihada za kukuza ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo kusimamia makubaliano yaliyoanzishwa kati ya Tanzania na Ethiopia hususan ushirikiano kati ya Shirika la Utangazaji la Tanzania na Shirika la Utangazaji la Ethiopia pamoja na ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Ethiopia.
=======================================
Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na maafisa kutoka Wizara hiyo wakifuatilia mazungumzo. |
Picha ya pamoja ================================== Wakati huohuo Waziri Mulamula alikutana kwa mazungumzo na Balozi wa Ethiopia nchini, Mhe. Shibru Mamo Kedida. |
Watumishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mazungumzo. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiteta jambo na Mhe. Kedida katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam. |
BALOZI SOKOINE AKUTANA NA MKUU WA IDARA YA UHAMIAJI WA SAUDI ARABIA
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine amekutana kwa mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Uhamiaji wa Ufalme wa Saudi Arabia Luteni Generali Suliman Al-Yahya katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na Mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya kukuza ushirikiano baina ya pande hizo mbili ambapo Saudi Arabia imeonyesha utayari wa kujadiliana na Serikali ya Tanzania kuhusu masuala ya upatikanaji wa viza za kuingia nchini Saudi Arabia.
Kwa upande wake, Balozi Sokoine ameishukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa ushirikiano wake kwa Tanzania katika nyanja mbalimbali.
Balozi Sokoine ametumia mazungumzo hayo kuelezea utayari wa Tanzania kuingia makubaliano ya kuanzishwa Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) kati ya nchi hizi mbili katika kusimamia utekelezaji wa masuala mbalimbali ya ushirikiano.
Ujumbe wa Tanzania ukiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Saudi Arabia |
BAKITA YATOA VITABU 1,650 VYA KISWAHILI KWA UBALOZI WA TANZANIA UJERUMANI
Katika jitihada za kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili Duniani Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) limetoa vitabu 1,650 vya Kiswahili vitakavyotumiwa na vyuo, vituo na taasisi zinazojishughulisha na ufundishaji wa lugha ya Kiswahili nchini Ujerumani.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vitabu hivyo, iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine ameipongeza BAKITA kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya katika kubidhaisha lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Kimataifa.
“Naamini kuwa BAKITA itaendelea kufungua mlango kwa ajili ya maombi ya vitabu vya kufundishia lugha ya Kiswahili katika nchi rafiki na nchi nyingine zote duniani ambazo zitaonesha nia ya kufundisha raia wake lugha adhimu ya Kiswahili, alisema Balozi Sokoine
Alisema kuwa juhudi hizo ni muhimu sana wakati huu kwa kuwa Shirika la UNESCO liliipitisha tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani, huku SADC, EAC na AU pia zilipitisha lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi zinazotumika katika utendaji kazi wa mitangamano hii na kuongeza kuwa kwa sasa ni dhahiri kuwa lugha ya kiswahili itakuwa kwa kasi na mahitaji ya vitabu na zana nyingine za kufundishia yataongezeka pia
"Kitendo hiki ni muhimu sana hasa ikizingatiwa kuwa UNESCO iliipitisha tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani, SADC, EAC na AU nazo zilipitisha lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi za kazi, ni dhahiri kuwa lugha hii sasa itakuwa kwa kasi na hivyo, mahitaji ya vitabu na zana nyingine za kufundishia yataongezeka,” amesema Balozi Sokoine.
Naye Naibu katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema uchapishwaji wa vitabu hivyo utasaidia kukuza lugha ya kiswahili nchini Ujeremani pamoja na mataifa mengine ya jirani.
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mtendaji wa BAKITA Bi. Consolata Mushi ameahidi kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuendelea kubidhaisha lugha ya Kiswahili kimataifa zaidi.
“BAKITA katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria na mkakati wa taifa wa kubidhaisha Kiswahili itaendelea kusambaza vitabu katika balozi mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zikiwemo Urusi, Uholanzi, Afrika Kusini, Burundi, Namibia, Korea Kusini, Nigeria na Mauritius,” amesema Bi. Mushi
Ameongeza kuwa BAKITA imetoa vitabu hivyo ikishirikiana na wachapishaji wa vitabu kutoka kampuni mbalimbali kwa lengo la kubidhaisha lugha ya Kiswahili na kutangaza soko jipya la vitabu katika nchi za Ulaya ikilenga kuwasaidia walimu wanaofundisha Kiswahili ambao ni Wadachi wenye nasaba na Waswahili pamoja na Diaspora wa Tanzania ambao wameanza kufundisha Kiswahili.
Meza Kuu katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa BAKITA |
TANZANIA, NORWAY KUSHIRIKIANA KUIMARISHA UCHUMI
Serikali za Tanzania na Norway zimesisitiza kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo ili kukuza uchumi.
Msisitizo huo umetolewa wakati wa mazungumzo ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) na Waziri wa Norway anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim walipokutana tarehe 06 Septemba 2022 katika ofisi ndogo za wizara Jijini Dar es Salaam.
Nchi hizo zinashirikiana katika masuala ya elimu, afya, kilimo, uwekezaji, miundombinu, nishati, madini, tehama, utafiti, maboresho kwenye mifumo ya ukusanyaji wa kodi, uchangiaji wa bajeti kuu ya Serikali, misitu, demokrasia, haki za binadamu, usawa wa jinsia, utunzaji wa mazingira na ukuzaji wa sekta ya biashara.
Balozi Mulamula alieleza kuwa Tanzania inathamini ushirikiano uliopo baina yake na Norway kwa kusimamia miradi ya maendeleo iliyo kwenye makubaliano na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano kwa lengo la kujenga uchumi wa Wananchi.
“Norway ni mshirika wa maendeleo wa Tanzania wa muda mrefu na imesaidia kujenga uwezo katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji ikiwemo uboreshaji wa mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara, usimamizi wa mfumo wa ulipaji kodi,” alisema Balozi Mulamuala.
Kadhalika, Serikali ya Norway imeongeza muda wa miaka mitano ya utekelezaji wa makubaliano ya majadiliano ya kisiasa yaliyoingiwa kati yake na Tanzania yanaendelea ili kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kipaumbele ya Serikali ya awamu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Doroth Gwajima alieleza kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Norway katika utekelezaji wa pendekezo la mpango wa miaka mitano wa kujenga usawa na uwezo kwa wanawake, vijana na makundi maalum unaotegemewa kuinua uchumi na kuwawezesha kuajiriwa na kujiajiri katika kazi rasmi.
Mpango huo pia umezingatia umuhimu wa afya ya uzazi kuwa agenda muhimu ili kuyafikia Malengo ya Mpango wa Maendeleo Endelevu.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Antony Mavunde alieleza kuwa kupitia sekta ya kilimo Tanzania inayo nia ya kushirikiana na Norway katika masuala ya kujenga uwezo katika vyuo vya kilimo na taasisi zake ili kuwezesha tafiti za sekta hiyo kwa lengo la kuinua uwezo binafsi wa kuzalisha mbegu za mazao, kusimamia usalama wa chakula nchini, kujenga mabwawa na kuimarisha miradi ya umwagiliaji.
Maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na upatikanaji wa mbolea kwa gharama nafuu, uimarishaji na ujenzi wa miundominu ya kilimo ili kujenga uwezo wa kuzalisha kwa mwaka mzima badala ya kusubiri msimu wa mvua kama ilivyosasa.
Vilevile Wizara ya Kilimo imeandaa mpango wa miradi ya kilimo kwa Wanawake na Vijana itakayotekelezwa katika mikoa ya Mbeya na Dodoma ambapo mradi huo utatumia jumla ya ekari 69 hivyo, kupitia ushirikiano uliopo Tanzania ina dhamira ya dhati ya kushirikiana na Norway ili kuyafikia malengo ya uzalishaji yaliyowekwa katika kufanya kilimo cha biashara na kulifikia soko la kimataifa.
Naye Mhe. Tvinnereim ameeleza kuwa Norway imejenga uwezo mkubwa katika masuala ya uzalishaji wa mbegu hivyo itaendelea kushirikiana na Tazania katika eneo hilo na maeneo mengine yaliyoelezwa na mawaziri walioshiriki mazungumzo hayo kwa lengo la kuondoa umasikini, kuongeza nafasi za ajira na kujenga uwezo wa kiuchumi kwa wananchi.
Ujumbe wa Tanzania ukiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Norway |
Tuesday, September 6, 2022
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NORWAY AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA SIKU TATU
Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim amewasili nchini leo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 6 - 8 Septemba 2022 na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula.
Akiwa nchini Mhe. Tvinnereim kwa nyakati tofauti, atakutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jaffo na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde.
Aidha, Mhe. Tvinereim pia anataraji kutembelea miradi ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) pamoja na Mji wa Serikali (Mtumba) Jijini Dodoma ili kujionea maendeleo ya miradi sambamba na mikakati ya Serikali katika kufanikisha miradi hiyo.
Tanzania na Norway zinashirikiana katika sekta za elimu, afya, kilimo, uwekezaji, miundombinu, nishati, madini, tehama, utafiti, maboresho kwenye mifumo ya ukusanyaji wa kodi, uchangiaji wa bajeti kuu ya Serikali, misitu, demokrasia, haki za binadamu, usawa wa jinsia, utunzaji wa mazingira na ukuzaji wa sekta ya biashara.
Maeneo mengine mtambuka ya ushirikiano ni pamoja na masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, utawala bora, usimamizi wa migogoro, amani na ulinzi.
TANZANIA, NORWAY KUSHIRIKIANA KUIMARISHA UCHUMI
Monday, September 5, 2022
TANZANIA, VENEZUELA ZASAINI HATI ZA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Venezuella zimesaini Hati za Makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kisiasa na mkataba wa ushirikiano katika nyanja mbalimbali baina ya nchi hizo.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.), pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Yuri Pimentel Moura katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
“Tumesaini mikataba miwili ambapo mmoja unalenga kuendeleza majadiliano ya kisiasa (political consultation) lakini pia makubaliano ya kuwa na ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo kichumi, nishati, afya, elimu na kilimo,” amesema Balozi Mulamula.
Kusainiwa kwa mikataba hiyo ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano kati ya Tanzania na Venezuela katika sekta za nishati, afya, elimu na kilimo kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Yuri Pimentel Moura amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo miwili ni hatua muhimu ya kudumisha na kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali baina ya Venezuela na Tanzania.
Mhe. Moura amewasili nchini leo akitokea Venezuela na atakuwepo nchini kwa siku mbili kwa ziara ya kikazi.
Katika tukio jingine, Balozi Mulamula amekutana na kupokea barua za utambulisho kutoka kwa Konseli Mkuu wa Kenya mwenye makazi yake Arusha, Bw. Dennis Mburu katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Baada ya kupokea barua za utambulisho kutoka kwa Bw. Mburu Balozi Mulamula amemuahidi ushirikiano kutoka Serikalini wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala ya biashara na uwekezaji pamoja na utalii.