Saturday, October 1, 2022

TANZANIA YAJIVUNIA USHIRIKIANO WAKE NA CHINA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema inaendelea kujivunia ushirikiano wake na Serikali ya Watu wa China kwa vitendo zaidi kwa maslahi ya pande zote mbili. 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, (Mb.) katika hafla ya maadhimisho ya miaka 73 ya uhuru wa China iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

Katika maadhimishio hayo, Balozi Mulamula na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian, walipanda miti katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ikiwa ni ishara ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya mataifa hayo. 

Balozi Mulamula pamoja na mambo mengine, amesema kuwa Tanzania iko tayari kufanya kazi na China ili kuendeleza na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Maendeleo wa Ulimwengu na Mpango wa Usalama wa Ulimwengu katika kuimarisha ushirikiano wa pande zote.

“Tunapoadhimisha miaka 73 ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, tunaadhimisha miaka 61 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi zetu mbili. Tanzania na China ni marafiki wa wakati wote, katika shida na raha,” amesema Balozi Mulamula.

Kwa upande wake, Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Chen Mingjian amesema uhusiano wa China na Tanzania umekuwa ukiendelea kukua kwa kasi na kufikia viwango vya juu kutokana na misingi imara inayosimamiwa na Viongozi wa mataifa haya mawili.

Viongozi wetu, Rais wa China Mhe. Xi Jinping na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wanajali na kuongoza maendeleo ya uhusiano wa mataifa yao kwa maslahi ya pande zote mbili.

“China na Tanzania zimekuwa zikifurahia uhusiano ulioasisiwa na Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa China na Baba wa Taifa hilo Hayati Mao Zedong,” amesema Balozi Mingjean

Balozi Mingjean ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 73 ya uhuru wa China, kumekuwa na ongezeko la miradi ya ushirikiano baina ya China na Tanzania ambapo ongezeko hilo limekuwa chachu ya maendeleo.

Tanzania na China zimekuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali zikiwemo, afya, mawasiliano, elimu, uchumi wa kidijitali, biashara na uwekezaji, miundombinu pamoja na utekelezaji wa miradi midogo ya kujikimu kimaisha inayoweza kuwanufaisha wananchi. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian wakimwagilia maji kwenye mti walioupanda katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian wakipanda mti katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea katika hafla ya upandaji mti katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Picha ya pamoja 


Friday, September 30, 2022

WAZIRI KIJAJI AFUNGUA JUKWAA LA PILI LA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA ITALIA

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya Uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ambapo tayari Mswada kuhusu mapendekezo ya Sheria mpya ya Uwekezaji umesomwa bungeni hivi karibuni.

 

Mhe. Kijaji ametoa kauli hiyo leo tarehe 30 Septemba 2022 wakati akifungua Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na Italia.

 

Mhe. Dkt. Kijaji ambaye alimwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye ufunguzi wa Jukwaa hilo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia inaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya biashara na uwekezaji ili kuwawezesha watanzania na wawekezaji kutoka nje kunufaika na fursa lukuki za biashara na uwekezaji zilizopo nchini.

 

Amesema miongoni mwa maboresho hayo ni mapendekezo ya Sheria Mpya ya Uwekezaji ambayo tayari imesomwa Bungeni  hivi karibuni. Sheria hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kuwekeza kwenye miradi mikubwa ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.

 

Mhe. Dkt. Kijaji alitumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania na wadau mbalimbali wa uwekezaji kutoa maoni yao kuhusu mapendekezo ya sheria hiyo ambayo tayari ipo wazi kwa umma wa watanzania kwa ajili ya kutoa maoni yao.

 

“Watanzania wenzangu, tunapokutana kwenye jukwaa hili la uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, Serikali yetu ipo kwenye mchakato wa kuandaa Sheria mpya ya Uwekezaji na tayari tumeileta kwa wananchi. Sheria hiyo inakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania, ambapo pamoja na mambo mengine inapendekeza kushushwa kwa kiwango cha mwekezaji mzawa kutoka mtaji wa Dola za Marekani 100,000 hadi 50,000.  Hivyo niwaombe watanzania wa kada zote, wawekezaji, sekta binafsi ni wakati wetu sasa wa kutoa maoni yetu kuhusu sheria hiyo” alisema Dkt. Kijaji.

 

Mhe. Kijaji ametaja maboresho mengine yanayofanywa na Serikali kwenye Sekta ya Biashara na uwekezaji kuwa ni pamoja na kuanzishwa mifumo ya kiteknolojia inayomrahisishia mwekezaji namna ya kuanza biashara, kupata namba ya mlipa kodi, leseni, viza na vibali vya kazi na ukaazi. Kadhalika serikali inakamilisha kuandaa mfumo wa Kielektroniki kwa ajili ya kurahisisha utoaji mizigo bandarini.

 

Akizungumzia ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, amesema unaendelea vizuri ambapo hadi sasa Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimesajili miradi 111 kutoka Italia yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 274.7 na kuifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa wa uwekezaji kutoka nje hapa nchini.

 

Pia amezitaka taasisi za Serikali na Binafsi zinazosimamia masuala ya biashara na uwekezaji hapa nchini kukutana na kuandaa taarifa ya pamoja ikijumuisha changamoto na mafanikio yaliyoainishwa wakati wa Jukwaa hili na kuzifanyia kazi changamoto hizo.

 

Akifunga Jukwaa hilo ambalo limefanyika Zanzibar na Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amewapongeza waandaji wa Jukwaa hilo wakiwemo Mabalozi wa Tanzania na Italia kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa kupitia jukwaa hilo na kuahidi kuendeleza jukwaa hilo ili kufikia malengo kusudiwa katika  utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

 

“Nawapongeza waandaji wa Jukwaa hili muhimu wakiwemo Mabalozi wetu  na sitalifunga bali nitaliahirisha ili wakati mwingine tuendelee pale tulipoishia” alisema Balozi Mulamula.

 

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo ameendelea kutoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za masoko kama matunda, maua nchini Italia ili kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia katika kukuza uchumi wa nchi.

 

Naye Balozi wa Italia hapa nchini amesisitiza kuendelea kutoa ushirikiano wowote unaohitajika ili kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kupitia majukwaa mbalimbali ya ushirikiano.

 

Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limefanyika Zanzibar na Dar es Salaam kuanzia tarehe 27 hadi 30 Septemba 2022. Jukwaa hili limewakutanisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na Italia.   

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kikaji akifungua kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba 2022.

Sehemu ya wageni waalikwa wakiwemo wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na Italia wakifuatilia hotuba ya ufunguzi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akihutubia wakati wa Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombp akizungumza wakati wa Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia

Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi nae akizungumza wakati wa Jukwaa hilo

Sehemu nyingine  ya washiriki wakiwa kwenye mkutano

Sehemu nyingine ya Washiriki wakati wa mkutano wa Jukwaa hilo
Mhe. Dkt. Kijaji akiwa katika picha ya pamoja na washiriki

Mhe. Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki

Mhe. Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Kombo (kulia), Balozi wa Italia nchini, Mhe. Lombardi (kushoto) na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania jijini Milan, Italia, Bw. Cecil

Mhe. Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania, Italia na Balozi wa Italia nchini pamoja na Mabalozi wastaafu, Balozi Modest Mero (kulia aliyesimama) na Balozi James Msekela (kushoto)

 

TANZANIA, INDIA KUONGEZA USHIRIKIANO SEKTA YA FILAMU

Serikali ya Tanzania pamoja na Serikali ya India zimekubaliana kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo sekta ya filamu. 

Akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India leo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.), amesema ushirikiano wa Tanzania na India ni wa kihistoria na umekuwa imara nyakati zote, na kwa sasa mataifa hayo yamekusudia kuongeza maeneo ya ushirikiano hususan katika sekta ya filamu.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, maeneno mengine ambayo Tanzania na India zimekusudia kuongeza ushirikiano ni katika sekta ya filamu hasa katika kuwaendeleza wasanii wa Tanzania katika kujifunza zaidi masuala ya uzalishaji wa filamu bora kama wanavyofanya wenzetu wa India.

“Tumekubaliana na Balozi kuwa tufufue ushirikiano katika eneo hili muhimu ili kuwawezesha wasanii wetu hapa nchini kuwa na uwezo wa kutengeneza filamu zenye viwango kama wenzetu wa India,” amesema Balozi Mulamula

Awali Balozi Mulamula amesema ushirikiano wa Tanzania na India umekuwa imara wakati wote kutokana na misingi ya kihistoria iliyowekwa na waasisi wa mataifa hayo mawili, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julias Nyerere wa Tanzania na Baba wa Taifa la India, Mahatma Gandhi. 

Waziri Mulamula ameongeza kuwa misingi hiyo imesaidia kukuza ushirikiano wa Tanzania na India katika sekta za elimu, afya, maji, ulinzi, utalii, tehama, kilimo, mabadiliko ya tabia nchi, nishati na uchumi wa buluu pamoja na biashara na uwekezaji. Alama ya ushirikiano katika nyanja hizo iliachwa na waasisi wa mataifa haya mawili (Mwl. Nyerere na Mahatma Gandhi) imekuwa chachu ya kuimarisha uhusiano wa Tanzania na India nyakati zote kwa maslahi ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Srikanta Pradhan ameongeza kuwa India imekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania, ambapo uhusiano huo umesaidia kuimarisha maendeleo baina ya mataifa hayo katika nyanja za elimu, afya, biashara na uwekezaji, kilimo na utamaduni.

“Ushirikiano uliopo baina ya India na Tanzania umekuwa chachu ya maendeleo kwa mataifa yetu na tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika sekta za biashara na uwekezaji ambayo yamekuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wetu,” amesema Balozi Pradhan 

Mwezi Agosti, 2022, Tanzania na India ziliahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano ikiwemo kuhakikisha sekta za afya na nyingine zinaimarika ikiwemo kilimo.

Aidha, India kupitia hospitali ya Apollo zilisaini mkataba wa makubaliano (MoU) na Kampuni ya Eclipse Group Afrika ya Jijini Dar es Salaam wa kujenga kituo cha kisasa cha kutoa huduma za uchunguzi za magonjwa ya saratani kinachotarajiwa kuanza kujengwa nchini kuanzia mwezi Novemba 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India Jijini Dar es Salaam

Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Pradhan akiwasilisha hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India Jijini Dar es Salaam

Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India ukiendelea katika Ofizi za Ubalozi wa India Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka ubalozi wa India nchini, ukiongozwa na Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Pradhan

Mkurugenzi wa Taasisi ya Masomo ya Kijamii na Utamaduni ya India, Bw. Arindam Mukherjee akiwasilisha hotuba yake wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India



Wednesday, September 28, 2022

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR AFUNGUA KONGAMANO LA PILI LA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA ITALIA

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman amesema Serikali ya Zanzibar inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuwawezesha Wawekezaji wenye tija  kuwekeza katika sekta  mbalimbali  ikiwemo sekta ya Uchumi wa Bluu.



Mhe. Othman ametoa kauli hiyo wakati akifungua rasmi Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Zanzibar tarehe 28 Septemba, 2022 na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na Italia.



Mhe. Othman ambaye alimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwenye kongamano hilo amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefungua milango kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali na kwamba inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuzifanyia maboresho sheria na kanuni mbalimbali za uwekezaji.

 

Kadhalika alisema maboresho hayo yanakwenda sambamba na yale ya sekta ya utoaji huduma kama vile za viza, vibali vya kazi na ukaazi pamoja na  kuboresha mawasiliano kupitia mifumo ya kidigitali ambapo Serikali hiyo inatarajia hivi karibuni kuzindua  mfumo wa uombaji viza kwa njia ya mtandao.



"Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili  
kuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa maeneo bora ya uwekezaji duniani. Uwekezaji una manufaa makubwa ya kiuchumi kwa nchi ikiwa ni pamoja na kukuza pato la taifa pamoja na  kutenegeneza ajira kwa vijana na wanawake " alisema Mhe. Othman.



Mhe. Othman ameeleza kuwa, katika kipindi cha miaka miwili kuanzia mwezi Novemba 2020 hadi wakati wa kongamano hilo Zanzibar imesajili miradi ya uwekezaji 196 yenye thamani ya dola za marekani bilioni 1. 4 ambapo miradi hiyo inatarajiwa  kutengeneza ajira zipatazo 9,000. Hivyo alihimiza washiriki kutumia  Kongamano hilo kama  chachu ya kuhamasisha wawekezaji wengi zaidi kuja nchini.  

 

“Kongamano hili liwe chachu ya kuvutia na kuhamasisha wawekezaji zaidi kuja Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Naendelea kutoa wito kwa wawekezaji kutoka Italia na duniani kote kuchangamkia fursa lukuki za uwekezaji tulizonazo. Namaliza kwa kusema Wekeza Zanzibar, Wekeza sasa” alisisitiza Mhe. Othman



Awali akizungumza wakati wa kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Soraga amepongeza jitihada zinazofanywa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo na Balozi mwenzake wa Italia hapa nchini, Mhe. Marco Lombardi za kuandaa kongamano hilo kwa mara ya pili ikiwa ni mchango wao wa  kuhakikisha nchi hizi mbili zinanufaika kupitia ushirikiano mzuri uliopo.

 

Pia aliwataka washiriki wote kutumia kongamano hilo kama fursa ya kubadilishana  mawazo na uzoefu miongoni mwao ili kuendelea kuboresha sekta ya biashara na uwekezaji  nchini. 

 

 Mhe. Soraga  pia alitumia fursa hiyo kuainisha fursa za kipaumbele za uwekezaji Zanzibar kuwa ni pamoja na Sekta ya Uchumi wa  Bluu, Kilimo, Usindikaji wa mazao ya kilimo, Utalii, ufugaji wa samaki, utalii unaozingatia utunzaji wa mazingira , miundombinu, nishati na uwekezaji katika mali zisizohamishika kama majengo.


Wakati wa Kongamano hilo mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa ikiwemo Maendeleo ya Miundombinu, Uchumi wa Bluu na Kilimobiashara na Kilimo cha Kisasa cha kutumia mashine na mitambo. Kongamano hilo ambalo limewashrikisha wadau kutoka sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji wa hapa nchini na kutoka Italia litahitimishwa rasmi tarehe 30 Septemba 2022 jijini Dar es Salaam.

 


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman akifungua rasmi Kongamano la Pili la Uwekezajikati ya Tanzania na Italia lililofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar tarehe 28 Septemba, 2022. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Othman ametoa wito kwa wawekezaji kutoka Italia na duniani kote kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali za manufaa
Sehemu ya Washiriki wa Kongamano wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Soraga nae akizungumza wakati wa Kongamano hilo

Sehemu ya Mabalozi na wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya Mhe Soraga

Mkurugezni Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) akifafanunua fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Zanzibar

Mhe. Makamu wa Kwanza wa Rais akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (kushoto) na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi (katikati)

Sehemu ya washiriki wa kongamano

Sehemu nyingine ya washiriki

Mhe. Balozi Lombardi akizungumza na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar, Bi.  Leluu Abdallah (kushoto) na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Salma Baraka  


 


VACANCY ANNOUNCEMENT