Monday, October 3, 2022

TANZANIA, CZECH KUIMARISHA UTALII, BIASHARA NA UWEKEZAJI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Jamhuri ya Czech zimekubaliana kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano hususan utalii, biashara na uwekezaji ili kukuza na kuimarisha misingi ya diplomasia iliyopo baina ya mataifa hayo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.), amebainisha hayo alipozungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Balozi Mbarouk amesema Tanzania ilisaini mkataba wa ushirikiano na Jamhuri ya Czech mwaka 2006 hivyo ni wakati muafaka wa kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano.

“Ni muda tangu tuliposaini mkataba wa makubaliano hivyo kwa sasa ni wakati muafaka baina yetu kuingia mkataba wa makubaliano katika maeneo mapya ya ushirikiano hususan katika sekta biashara na uwekezaji, Utalii,” amesema Balozi Mbarouk

Balozi Mbarouk ameongeza kuwa katika sekta ya utalii, miaka ya nyuma Tanzania ilikuwa inapokea watalii 6,000 kutoka Jamhuri ya Czech, na kwa kuwa maambuzi ya uviko 19 yamepungua duniani, Tanzania imeboresha mazingira ya utalii, biashara na uwekezaji.

Amewasihi watalii na wawekezaji kutoka Czech kuja kutalii na kuwekeza Tanzania.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa amesema Czech inajivunia ushirikiano wake imara na wa muda mrefu na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuwa Czech itaendelea kudumisha ushirikiano huo.

“Nakuahidi kuwa tutaendelea kuwahamasisha watalii, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Czech kuja kutalii na kuwekeza Tanzania…..ni jukumu letu kuhakikisha kuwa sekta ya biashara na uwekezaji inakuwa na kunufaisha mataifa yote mawili,” amesema Mhe. Tlapa

Mhe. Tlapa ameahidi kuwa Czech itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mengine ya ushirikiano kama vile elimu, afya, kilimo, utamaduni na michezo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Tlapa yupo nchini kwa ziara ya kikazi kuanzia tarehe 2 – 4, Oktoba 2022.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akimkaribisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk  katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Kikao baina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa kikiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa  katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na ujumbe wa Jamhuri ya Czech unaoongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa  

DKT. TAX AWASILI WIZARANI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amewasili katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam na kupokelewa na Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.), Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine pamoja na baadhi ya watumishi wa Wizara.

Dkt. Tax ameteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 02 Oktoba 2022 na kuapishwa tarehe 03 Oktoba 2022 Ikulu Jijini Dar es Salaam. 

Dkt. Tax amechukua nafasi ya Balozi Liberata Mulamula baada ya Mhe. Rais kufanya mabadiliko madogo kwenye Baraza la Mawaziri. 

Akizungumza baada ya kuwasili katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, Mhe  Dkt. Tax amesema atashirikiana na watumishi wote wa Wizara katika kila ngazi ili kuhakikisha malengo ya Wizara yanatekelezwa kikamilifu.

“Nipo tayari kufanya kazi na nyinyi, na kujifunza kutoka kwenu ili kutekeleza majukumu yangu….. Taasisi yoyote ili iweze kufanikiwa lazima ifanye kazi kwa pamoja na kuwa na ushirikiano,” amesema Dkt. Tax

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokelewa na  Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk alipowasili katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na mmoja wa watumishi wa Wizara alipowasili katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk  na Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk  wakimsikilza Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine alipokuwa akimkaribisha Dkt. Tax katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akimkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, naibu Waziri Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine katika picha ya pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, naibu Waziri Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine, Wakurugenzi wa Idara mbalimbali katika Wizara na baadhi ya watumishi katika picha ya pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika 
Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Sunday, October 2, 2022

NAIBU WAZIRI MAMBO YA NJE CZECH AWASILI NCHINI KWA ZIARA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa amewasili nchi leo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 2 hadi 4 Oktoba 2022.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, Mhe. Tlapa amepokelewa na Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya, katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na Balozi wa Tanzania nchi Ujerumani ambaye pia anawakilisha Jamhuri ya Czech, Mhe. Dkt. Abdallah Possi.

Akiwa nchini, Mhe. Tlapa kwa nyakati tofauti, atakutana kwa mazungumzo na Waziri wa Nchi-Tamisemi,  Waziri wa Afya,  Waziri wa Viwanda na Biashara, pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) pamoja na Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa Hospitali ya Jeshi la Wananchi (JWTZ).  

Tanzania na Czech zimekuwa zikishirikiana katika sekta za elimu,utamaduni, afya, biashara na uwekezaji.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa amewasili nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Tanzania nchi Ujerumani ambaye pia anawakilisha Jamhuri ya Czech, Mhe. Dkt. Abdallah Possi (wa kwanza kushoto) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa walipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya, katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa walipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Martin Tlapa akiteta jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya, katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme



TANZANIA, KOREA KUIMARISHA MISINGI YA USHIRIKIANO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Korea ili kuimarisha zaidi misingi ya uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi hizo.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) katika maadhimisho ya siku ya kuanzishwa kwa Taifa hill iliyofanyika  Jijini Dar es Salaam tarehe 1 Oktoba, 2022.

Mhe. Waziri Mulamula aliongeza kuwa Tanzania imekusudia kuendelea kuimarisha misingi ya uhusiano wake wa kidiplomasia uliopo kati yake na Jamhuri ya Korea kwa kuongeza maeneo ya ushirikiano katika sekta za maji, teknolojia, afya, elimu, nishati, usafirishaji na uchukuzi, pamoja na biashara na uwekezaji. 

“Mwaka huu tunatimiza miaka 30 ya uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati yetu, kudumu kwa ushirikiano huu muda wote ni ishara ya uhusiano mzuri uliopo baina yetu, tutaendelea kuulinda na kuuthamini ushirikiano huu nyakati zote kwa maslahi mapana ya nchi zetu mbili,” amesema Mhe. Balozi Mulamula

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri Mulamula ameongeza kuwa Jamhuri ya Korea imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwa Tanzania kwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Ameongeza kuwa, Wakala wa Kukuza Biashara na Uwekezaji wa Korea (KOTRA), Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Korea (KOICA) pamoja na Benki ya EXIM ya Korea ni Taasisi ambazo zinashiriki katika harakati za kuchangia maendeleo ya Taifa la Tanzania.

Naye Balozi wa Jamhuri ya Korea hapa nchini, Mhe. Kim Sun-Pyo amesema Tanzania imekuwa mdau mkubwa wa Jamhuri ya Korea kwa nyakati zote na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya mataifa yote mawili.

“Tumekuwa tukishirikiana katika nyanja mbalimbali kama vile nishati, elimu, afya, maji na miundombinu hivyo ni matarajio yetu kuwa tutaendelea kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano hususan katika nyanja za biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi wa mataifa yetu,” amesema Mhe. Balozi Sun-Pyo.

Mhe. Balozi Sun-Pyo amesema takwimu za biashara zinaonesha kuwa ujazo wa biashara kati ya Korea na Tanzania umeongezeka lakini bado tumekusudia kuongeza maeneo ya ushirikiano ili kuwawezesha wafanyabiashara na wawekezaji wa mataifa yote mawili kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana katika mataifa haya.

Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha misingi ya uhusiano wa muda mrefu uliopo kati yake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akitoa hotuba yake ya ufunguzi wakati wa maadhimisho ya siku ya kuanzishwa kwa Taifa hill iliyofanyika  Jijini Dar es Salaam tarehe 1 Oktoba, 2022

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akitoa hotuba yake ya ufunguzi wakati wa maadhimisho ya siku ya kuanzishwa kwa Taifa hill iliyofanyika  Jijini Dar es Salaam tarehe 1 Oktoba, 2022








BIASHARA TANZANIA, NIGERIA YAONGEZEKA

Biashara kati ya Tanzania na Nigeria imeongezeka kutoka shilingi bilioni 23 mwaka 2020 hadi shilingi bilioni 24 mwaka 2021. 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.) alipokuwa akishiriki katika hafla ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Nigeria yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam

Balozi Mulamula ameongeza kuwa takwimu za biashara na uwekezaji zinatia moyo kuona kiwango cha biashara kati ya nchi zetu mbili kimeendelea kuongezeka, kutoka shilingi bilioni 23 mwaka 2020 hadi shilingi bilioni 24 mwaka 2021. Kuhusu uwekezaji, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili Kampuni 23 za Nigeria ambazo zimewekeza Tanzania kwa uwekezaji wa jumla ya Dola za Kimarekani milioni 466.50 na kutoa takriban ajira 1,734.

“Nangependa kutumia fursa hii kuhimiza jumuiya zetu za wafanyabiashara kuangalia fursa za biashara zinazopatikana katika nchi hizi mbili (Tanzania na Nigeria). Serikali ya Tanzania imefungua milango yake kwa mtu yeyote karibuni kuwekeza,” amesema Balozi Mulamula

Tanzania na Nigeria zinashirikiana kwa karibu kukuza Ajenda ya mwaka 2030 ya Umoja wa Afrika. Hii inalazimu, miongoni mwa mambo mengine, kukuzwa kwa jamii zenye amani, usawa, na ajenda ya maendeleo ya bara la Afrika na watu wake.

Kwa Upande wake Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takalmawa amesema kuwa Nigeria inajivunia kuwa rafiki wa Tanzania kwani mataifa haya yamekuwa yakishirikiana kijamii katika masuala ya utamaduni, muziki, nyimbo na tamthilia....n.k

“Ushirikiano na umoja baina ya Nigeria na Tanzania umekuwa na misingi imara ya kukuza na kuimarisha diplomasia baina ya mataifa yetu mawili,” amesema Balozi Takalmawa

Balozi Takalmawa ameongeza kuwa biashara kati ya Nigeria na Tanzania imeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita, kadhalika uwekezaji nao umeongezaka jambo ambalo linaashiria mazingira bora ya biashara na uwekezaji. Mbali na kuadhimisha siku ya Uhuru wa Nigeria, pia Waziri Mulamula alizindua maktaba katika ofisi za Ubalozi wa Nigeria hapa nchini. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takalmawa katika Ofisi za Ubalozi wa Nigeria Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake wakati wa maadhimisho ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Nigeria yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takalmawa wakikata utepe wa kufungua maktaba ya ubalozi wa Nigeria katika Ofisi za ubalozi huo Jijini Dar es Salaam



Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takalmawa akikabidhi nakala ya kitabu kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula baada ya kufungua maktaba ya ubalozi huo Jijini Dar es Salaam

Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na baadhi ya mabalozi walioshiriki katika maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Nigeria yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam 





Saturday, October 1, 2022

TANZANIA YAJIVUNIA USHIRIKIANO WAKE NA CHINA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema inaendelea kujivunia ushirikiano wake na Serikali ya Watu wa China kwa vitendo zaidi kwa maslahi ya pande zote mbili. 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, (Mb.) katika hafla ya maadhimisho ya miaka 73 ya uhuru wa China iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

Katika maadhimishio hayo, Balozi Mulamula na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian, walipanda miti katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ikiwa ni ishara ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya mataifa hayo. 

Balozi Mulamula pamoja na mambo mengine, amesema kuwa Tanzania iko tayari kufanya kazi na China ili kuendeleza na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Maendeleo wa Ulimwengu na Mpango wa Usalama wa Ulimwengu katika kuimarisha ushirikiano wa pande zote.

“Tunapoadhimisha miaka 73 ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, tunaadhimisha miaka 61 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi zetu mbili. Tanzania na China ni marafiki wa wakati wote, katika shida na raha,” amesema Balozi Mulamula.

Kwa upande wake, Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Chen Mingjian amesema uhusiano wa China na Tanzania umekuwa ukiendelea kukua kwa kasi na kufikia viwango vya juu kutokana na misingi imara inayosimamiwa na Viongozi wa mataifa haya mawili.

Viongozi wetu, Rais wa China Mhe. Xi Jinping na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wanajali na kuongoza maendeleo ya uhusiano wa mataifa yao kwa maslahi ya pande zote mbili.

“China na Tanzania zimekuwa zikifurahia uhusiano ulioasisiwa na Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa China na Baba wa Taifa hilo Hayati Mao Zedong,” amesema Balozi Mingjean

Balozi Mingjean ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 73 ya uhuru wa China, kumekuwa na ongezeko la miradi ya ushirikiano baina ya China na Tanzania ambapo ongezeko hilo limekuwa chachu ya maendeleo.

Tanzania na China zimekuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali zikiwemo, afya, mawasiliano, elimu, uchumi wa kidijitali, biashara na uwekezaji, miundombinu pamoja na utekelezaji wa miradi midogo ya kujikimu kimaisha inayoweza kuwanufaisha wananchi. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian wakimwagilia maji kwenye mti walioupanda katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian wakipanda mti katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea katika hafla ya upandaji mti katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Picha ya pamoja 


Friday, September 30, 2022

WAZIRI KIJAJI AFUNGUA JUKWAA LA PILI LA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA ITALIA

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya Uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ambapo tayari Mswada kuhusu mapendekezo ya Sheria mpya ya Uwekezaji umesomwa bungeni hivi karibuni.

 

Mhe. Kijaji ametoa kauli hiyo leo tarehe 30 Septemba 2022 wakati akifungua Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na Italia.

 

Mhe. Dkt. Kijaji ambaye alimwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye ufunguzi wa Jukwaa hilo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia inaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya biashara na uwekezaji ili kuwawezesha watanzania na wawekezaji kutoka nje kunufaika na fursa lukuki za biashara na uwekezaji zilizopo nchini.

 

Amesema miongoni mwa maboresho hayo ni mapendekezo ya Sheria Mpya ya Uwekezaji ambayo tayari imesomwa Bungeni  hivi karibuni. Sheria hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kuwekeza kwenye miradi mikubwa ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.

 

Mhe. Dkt. Kijaji alitumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania na wadau mbalimbali wa uwekezaji kutoa maoni yao kuhusu mapendekezo ya sheria hiyo ambayo tayari ipo wazi kwa umma wa watanzania kwa ajili ya kutoa maoni yao.

 

“Watanzania wenzangu, tunapokutana kwenye jukwaa hili la uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, Serikali yetu ipo kwenye mchakato wa kuandaa Sheria mpya ya Uwekezaji na tayari tumeileta kwa wananchi. Sheria hiyo inakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania, ambapo pamoja na mambo mengine inapendekeza kushushwa kwa kiwango cha mwekezaji mzawa kutoka mtaji wa Dola za Marekani 100,000 hadi 50,000.  Hivyo niwaombe watanzania wa kada zote, wawekezaji, sekta binafsi ni wakati wetu sasa wa kutoa maoni yetu kuhusu sheria hiyo” alisema Dkt. Kijaji.

 

Mhe. Kijaji ametaja maboresho mengine yanayofanywa na Serikali kwenye Sekta ya Biashara na uwekezaji kuwa ni pamoja na kuanzishwa mifumo ya kiteknolojia inayomrahisishia mwekezaji namna ya kuanza biashara, kupata namba ya mlipa kodi, leseni, viza na vibali vya kazi na ukaazi. Kadhalika serikali inakamilisha kuandaa mfumo wa Kielektroniki kwa ajili ya kurahisisha utoaji mizigo bandarini.

 

Akizungumzia ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, amesema unaendelea vizuri ambapo hadi sasa Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimesajili miradi 111 kutoka Italia yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 274.7 na kuifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa wa uwekezaji kutoka nje hapa nchini.

 

Pia amezitaka taasisi za Serikali na Binafsi zinazosimamia masuala ya biashara na uwekezaji hapa nchini kukutana na kuandaa taarifa ya pamoja ikijumuisha changamoto na mafanikio yaliyoainishwa wakati wa Jukwaa hili na kuzifanyia kazi changamoto hizo.

 

Akifunga Jukwaa hilo ambalo limefanyika Zanzibar na Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amewapongeza waandaji wa Jukwaa hilo wakiwemo Mabalozi wa Tanzania na Italia kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa kupitia jukwaa hilo na kuahidi kuendeleza jukwaa hilo ili kufikia malengo kusudiwa katika  utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

 

“Nawapongeza waandaji wa Jukwaa hili muhimu wakiwemo Mabalozi wetu  na sitalifunga bali nitaliahirisha ili wakati mwingine tuendelee pale tulipoishia” alisema Balozi Mulamula.

 

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo ameendelea kutoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za masoko kama matunda, maua nchini Italia ili kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia katika kukuza uchumi wa nchi.

 

Naye Balozi wa Italia hapa nchini amesisitiza kuendelea kutoa ushirikiano wowote unaohitajika ili kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kupitia majukwaa mbalimbali ya ushirikiano.

 

Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limefanyika Zanzibar na Dar es Salaam kuanzia tarehe 27 hadi 30 Septemba 2022. Jukwaa hili limewakutanisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na Italia.   

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kikaji akifungua kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba 2022.

Sehemu ya wageni waalikwa wakiwemo wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na Italia wakifuatilia hotuba ya ufunguzi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akihutubia wakati wa Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombp akizungumza wakati wa Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia

Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi nae akizungumza wakati wa Jukwaa hilo

Sehemu nyingine  ya washiriki wakiwa kwenye mkutano

Sehemu nyingine ya Washiriki wakati wa mkutano wa Jukwaa hilo
Mhe. Dkt. Kijaji akiwa katika picha ya pamoja na washiriki

Mhe. Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki

Mhe. Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Kombo (kulia), Balozi wa Italia nchini, Mhe. Lombardi (kushoto) na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania jijini Milan, Italia, Bw. Cecil

Mhe. Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania, Italia na Balozi wa Italia nchini pamoja na Mabalozi wastaafu, Balozi Modest Mero (kulia aliyesimama) na Balozi James Msekela (kushoto)

 

TANZANIA, INDIA KUONGEZA USHIRIKIANO SEKTA YA FILAMU

Serikali ya Tanzania pamoja na Serikali ya India zimekubaliana kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo sekta ya filamu. 

Akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India leo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.), amesema ushirikiano wa Tanzania na India ni wa kihistoria na umekuwa imara nyakati zote, na kwa sasa mataifa hayo yamekusudia kuongeza maeneo ya ushirikiano hususan katika sekta ya filamu.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, maeneno mengine ambayo Tanzania na India zimekusudia kuongeza ushirikiano ni katika sekta ya filamu hasa katika kuwaendeleza wasanii wa Tanzania katika kujifunza zaidi masuala ya uzalishaji wa filamu bora kama wanavyofanya wenzetu wa India.

“Tumekubaliana na Balozi kuwa tufufue ushirikiano katika eneo hili muhimu ili kuwawezesha wasanii wetu hapa nchini kuwa na uwezo wa kutengeneza filamu zenye viwango kama wenzetu wa India,” amesema Balozi Mulamula

Awali Balozi Mulamula amesema ushirikiano wa Tanzania na India umekuwa imara wakati wote kutokana na misingi ya kihistoria iliyowekwa na waasisi wa mataifa hayo mawili, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julias Nyerere wa Tanzania na Baba wa Taifa la India, Mahatma Gandhi. 

Waziri Mulamula ameongeza kuwa misingi hiyo imesaidia kukuza ushirikiano wa Tanzania na India katika sekta za elimu, afya, maji, ulinzi, utalii, tehama, kilimo, mabadiliko ya tabia nchi, nishati na uchumi wa buluu pamoja na biashara na uwekezaji. Alama ya ushirikiano katika nyanja hizo iliachwa na waasisi wa mataifa haya mawili (Mwl. Nyerere na Mahatma Gandhi) imekuwa chachu ya kuimarisha uhusiano wa Tanzania na India nyakati zote kwa maslahi ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Srikanta Pradhan ameongeza kuwa India imekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania, ambapo uhusiano huo umesaidia kuimarisha maendeleo baina ya mataifa hayo katika nyanja za elimu, afya, biashara na uwekezaji, kilimo na utamaduni.

“Ushirikiano uliopo baina ya India na Tanzania umekuwa chachu ya maendeleo kwa mataifa yetu na tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika sekta za biashara na uwekezaji ambayo yamekuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wetu,” amesema Balozi Pradhan 

Mwezi Agosti, 2022, Tanzania na India ziliahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano ikiwemo kuhakikisha sekta za afya na nyingine zinaimarika ikiwemo kilimo.

Aidha, India kupitia hospitali ya Apollo zilisaini mkataba wa makubaliano (MoU) na Kampuni ya Eclipse Group Afrika ya Jijini Dar es Salaam wa kujenga kituo cha kisasa cha kutoa huduma za uchunguzi za magonjwa ya saratani kinachotarajiwa kuanza kujengwa nchini kuanzia mwezi Novemba 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India Jijini Dar es Salaam

Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Pradhan akiwasilisha hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India Jijini Dar es Salaam

Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India ukiendelea katika Ofizi za Ubalozi wa India Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka ubalozi wa India nchini, ukiongozwa na Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Pradhan

Mkurugenzi wa Taasisi ya Masomo ya Kijamii na Utamaduni ya India, Bw. Arindam Mukherjee akiwasilisha hotuba yake wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India