Mhe. Dkt. Tax ametoa pongezi hizo hivi karibuni wakati akipokea Hati za
Utambulisho za Konseli Mkuu wa UAE, Zanzibar Mhe. Balozi Saleh Ahmed
Alhemeiri katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi za Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Zanzibar.
Amesema hatua hiyo ni muhimu sana katika kuimarisha ushirikiano wa
kihistoria uliopo kati ya Tanzania na UAE kwani sasa fursa nyingi
zilizopo Zanzibar ikiwemo utalii, uchumi wa buluu na biashara vitashamiri zaidi
na kukua.
Ameongeza kusema Serikali ya Awamu ya Sita chini
ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar chini ya uongozi wa Mhe. Dkt.
Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi zimeendelea kuimarisha ushirikiano na nchi
mbalimbali pamoja na kutafuta fursa za biashara, utalii, uwekezaji na
masoko kwa bidhaa za Tanzania ili kuiwainua kiuchumi watanzania wote.
Ameongeza kwamba kufunguliwa kwa Konseli Kuu hiyo ni matokeo ya
ziara mbalimbali za viongozi hao nchini humo ikiwemo ile ya Mhe. Rais Samia
aliyoifanya nchini UAE mwezi Februari 2022 wakati wa Maonesho ya Biashara ya
Kimataifa ya Dubai Expo 2020.
Pia amesema wakati wa ziara hiyo, pamoja na mambo mengine,
Mikataba na Hati za Makubaliano mbalimbali zilisainiwa kwa ajili ya
kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
"Napongeza kwa dhati uamuzi wa Serikali ya UAE wa kufungua Konseli
Kuu au Ubalozi mdogo hapa Zanzibar. Ni imani yangu kuwa, uwepo wa Konseli Kuu
hii utasaidia kuharakisha utekelezaji wa masuala mbalimbali ya
ushirikiano ambayo tayari yamekubalika kwa manufaa ya pande hizi mbili"
alisema Dkt. Tax.
Akitaja maeneo ya kipaumbele ya ushirikiano kwa upande wa Zanzibar, Mhe.
Waziri Tax amesema ni pamoja na Uchumi wa Buluu hususan katika uvuvi wa bahari
kuu, utalii, biashara na uwekezaji kwa ujumla.
Pia Mhe. Dkt Tax amemhakikishia ushirikiano Balozi
huyo na kwamba ana imani kuwa kupitia yeye masuala mengi yatakamilika.
" Tutashirikiana na wewe kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa kati
ya nchi hizi mbili hususan kwa upande wa Zanzibar yanatekelezwa na kama
ulivyosema awali kwa kiasi fulani Zanzibar inafanana na Dubai, basi tujielekeze
kuigeuza Zanzibar kuwa Dubai ya Afrika" alisema Dkt. Tax.
Kwa upande wake, Mhe. Alhemeiri amesema amefarijika kuwepo
Zanzibar na kwamba yupo tayari kushirikiana na Serikali hiyo katika kukuza
biashara, kilimo, elimu, na uchumi wa buluu kwani zipo fursa lukuki katika
Kisiwa hiki zinazohitaji kuendelezwa.
"Nia yetu ni kushirikiana na Serikali kukiendeleza Kisiwa kizuri
cha Zanzibar. Nimeona zipo fursa nyingi
za kufanyia kazi. Nitajikita zaidi kwenye masuala ya utalii, biashara, elimu,
uchumi wa buluu na usafirishaji kwa kuzishawishi mamlaka za UAE kuongeza safari
za moja kwa moja za Mashirika ya Ndege ya UAE kuja Zanzibar ili kukuza utalii,
alisema Mhe. Alhemeiri.
Mhe. Dkt. Tax yupo mjini Zanzibar kwa ajili ya
kushiriki Mkutano wa Sita wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan na Mabalozi wa Tanzania unaofanyika Kisiwanio humo kuanzia
tarehe 14 hadi 21 Novemba 2022.
Mhe. Dkt. Tax akiagana na Mhe. Alhemeiri mara baada ya kumaliza mazungumzo. |