Thursday, April 20, 2023
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI YASHIRIKI UFUNGUZI WA MICHEZO YA MAADHIMISHO YA MEI MOSI
TANZANIA KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA NCHI ZA EAC KULINDA RASILIMALI ZA UVUVI ZIWA VICTORIA
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha rasilimali za uvuvi katika Ziwa Victoria zinalindwa ili zinufaishe jamii zinazozunguka ziwa hilo na mataifa husika kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe aliyeongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tano wa Baraza la Mawaziri la Sekta ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 19, Aprili jijini Kampala, Uganda.
Prof. Shemdoe aliuhakikishia mkutano huo kuwa, Tanzania itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kusimamia ziwa hilo kama nchi wanachama wa wa LVFO zilivyokubaliana. Alisisitiza pia kuwa Tanzania inaendelea kudhibiti matumizi ya zana haramu za uvuvi, kupiga marufuku uvuvi wa samaki wachanga, kudhibiti utoroshaji wa mazao ya uvuvi na kuhamasisha ufugaji wa samaki kwa vizimba katika Ziwa Victoria bila kuathiri mazingira.
Amesema pia, Tanzania imeimarisha udhibiti wa uingizaji wa zana za kuvulia samaki ili kuzuia uingizaji wa zana haramu nchini na kuendesha ukaguzi wa kina ili kuhakikisha uvuvi endelevu unafanyika kwa tija.
Pia Profesa Shemdoe alitanabaisha kuwa mchango wa Sekta za Uvuvi katika uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mdogo sana kwakuwa mchango wake unahesabiwa katika maeneo ya uvuvi na ukuzaji bila kujumuisha mapato yanayotokana na shughuli zote zinazofanyika katika minyororo yake ya thamani.
“Mchango wa Sekta za Uvuvi katika uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mdogo sana kwakuwa mchango wake unahesabiwa katika maeneo ya uvuvi na ukuzaji bila kujumuisha mapato yanayotokana na shughuli zote zinazofanyika katika minyororo yake ya thamaniBadala yake thamani hiyo inajumuishwa katika sekta zingine na hivyo kutokutoa picha halisi ya Sekta ya Uvuvi,” alisema.
Katika mkutano huo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima, alimwakilisha Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo.
Kikao hiki kimehudhuriwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilizopo katika Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa
Wednesday, April 19, 2023
WATANZANIA WALIOPO SUDAN WAPO SALAMA: DKT. TAX
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuchukua hatua stahiki kwa kushirikiana na nchi jirani, Jumuiya za Kikanda, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha watanzania na raia wengine waliopo nchini Sudan wanakuwa salama wakati huu ambapo nchi hiyo ipo katika changamoto za kiusalama.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax Bungeni jijini Dodoma, tarehe 19 Aprili 2023 wakati akitoa Taarifa ya Serikali kuhusu Hali ya Amani na Usalama nchini Sudan.
Amesema tangu kuibuka kwa mapigano mjini Khartoum tarehe 15 Aprili 2023 kati ya vikosi vya Serikali (Sudan Armed Forces - SAF) na Vikosi vya Msaada yaani Rapid Support Forces (RSF) na kusambaa katika maeneo mengine ya nchi hiyo, tayari athari mbalimbali zimeanza kujitokeza ikwemo vifo vya watu 185 majeruhi zaidi ya 1,000 na uharibifu wa mali.
Amesema mapigano hayo pia yamechangia kurudisha nyuma jitihada zinazoendelea za kutafuta amani Sudan na kwamba Serikali ya Tanzania inasikitishwa na kuzorota kwa hali ya amani na usalama inayoendelea nchini humo.
Ameongeza kusema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine inao raia wake wapatao 210 nchini Sudan wakiwemo wanafunzi 171, wanadiplomasia na raia wengine ambao hadi sasa wapo salama na hakuna aliyeathiriwa na mapigano hayo.
Mhe. Dkt. Tax amesema kuwa, jitihada za pamoja za Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na nchi na taasisi mbalimbali zimefanikisha kusitishwa kwa mapigano nchini Sudan kwa muda wa saa 24 kuanzia tarehe 18 Aprili 2023 jioni ili kutoa nafasi kwa misaada ya kibinadamu kutolewa kwa raia.
Pia Mhe. Dkt. Tax amempongeza Balozi wa Tanzania nchini Sudan, Mhe. Silima Haji Kombo kwa kuendelea kuhakikisha usalama wa watanzania waliopo Sudan na kwamba Serikali inaendelea kufuatilia hali nchini humo pamoja na kuandaa mpango wa kuwaondoa raia wa Tanzania kadri itakavyohitajika.
Amesema Tanzania ambayo ni Mjumbe wa Baraza la Amani la Afrika inaendelea kuunga mkono tamko lililotolewa na Baraza hilo katika mkutano wake uliofanyika tarehe 16 Aprili 2023 la kulaani mapigano yanayoendelea na kutoa wito kwa pande zote mbili katika mgogoro huo kusitisha mapigano hayo.
Pia Tanzania inaendelea kuzitaka pande hizo mbili hasimu kutatua mgogoro huo kwa njia za amani na usalama huku zikihakikisha mahitaji ya kibinadamu, usalama na ustawi wa raia wa Sudana na raia kutoka nchi nyingine.
TUSAMBAZE ELIMU YA UKUZAJI VIUMBE MAJI NCHI NZIMA - BALOZI MLIMA
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda Mhe. Dkt. Aziz Mlima ameisihi sekta ya uvuvi nchini kuangalia namna ya kufanya ili juhudi za ukuzaji viumbe maji zisambae nchi nzima.
Mhe. Balozi Mlima ametoa rai hiyo jijini Kampala alipozungumza na washiriki wa Mkutano wa Tano Baraza la Mawaziri la kisekta la Uvuvi Ukuzaji Viumbe Maji la Jumuiya ya Afrika Mashariki waliofika Ubalozini kumpa taarifa kuhusu mkutano huo unaoendelea jijini Kamapala.
Akizungumza na wataalamu hao Mhe. Balozi Dkt. Mlima amesema sekta ya Uvuvi kupitia eneo la ukuzaji viumbe maji lazima ihakikishe programu za ufugaji samaki zinaenea katika maeneo mengine yenye maziwa na isiishie maeneo ya Ziwa Victoria pekee ili nchi itumie fursa hiyo vizuri na kunufaika nayo.
“Tanzania tuna eneo kubwa la maji lakini ufugaji wa samaki kwetu sio mzuri Inabidi tuoneshe njia, suala hili linatoa ajira na lina soko kubwa niwaambie tu kuwa bidhaa zitakazozalishwa soko liko DRC,” alisema na kuongeza kuwa Tanzania lazima kufanya ufugaji samaki kuwa suala la kimkakati.
Amesema kinachotakiwa kufanywa au kuangaliwa ni suala la kuzalisha chakula cha samaki ili kuwa na uhakika wa malisho yao na hapo mambo yataenda vizuri kwani suala la kutengeneza chakula ni kubwa na ana hakika chuo cha uvuvi na Taasisi ya Utafiti ya uvuvi wanaweza kusimamia eneo hilo.
Amesema sekta inabidi ioneshe njia na kutilia mkazo suala la ufugaji wa samaki nchini kwani ajira nyingi zitatengenezwa katika eneo hilo na kwa kuzingatia kuwa kuna soko kubwa kwa nchi jirani ya DRC na hivyo nchi itanufaika na fursa hii kuwa na mashine za uhakika za uzalishaji wa chakula cha Samaki
“Tuangalie na tufanye suala hili kimkakati hasa katika eneo la kutengeneza chakula cha samaki ni suala kubwa na la msingi, nina hakika chuo cha uvuvi na taasisi ya utafiti wakilisimamia hili tutapata mitambo ya kuzalisha chakula cha samaki.
Amesema anaona ufugaji Samaki ukizingatia masharti na vigezo vyake ni kitu rahisi kwa mwananchi kufanya kwakua changamoto pekee inayoweza kumsumbua mfugaji husika ni wizi wa mazao yake tu na kwamba akijipanga kudhibiti hilo hakuna shida nyingine kama ana uhakika wa chakula bora.
Mhe.Balozi Dkt. Mlima atashiriki katika Mkutano huo utakaofanyika tarehe 19 Aprili akimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo utaongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo Prof. Riziki Shemdoe kwa ngazi ya Makatibu Wakuu.
Tuesday, April 18, 2023
KAMATI KUTATHMINI UTEKELEZJI WA DIPLOMASIA YA UCHUMI YAANZA KAZI RASMI
Kikao na Kamati kikiendelea |
Mjumbe wa Kamati, Mhe. Balozi Mwanaidi Maajar akiwa kwenye Kikao kati ya Kamati hiyo na Mhe. Dkt. Tax. Kushoto ni Mjumbe wa Sekretarieti ya Kamati hiyo |
Wajumbe wengine wa Kamati ambao ni Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kulia) na Balozi Peter Kalaghe wakati wa kikao kati ya kamati hiyo na Mhe. Dkt. Tax |
Mjumbe wa Kamati, Mhe. Balozi Jack Mugendi Zoka (kulia) akiwa na Mjumbe wa Sekretarieti ya Kamati (kushoto) |
Wajumbe wengine wa Kamati ambao ni Balozi Tuvako Manongi (kushoto) na Mhe. Balozi George Madafa wakati wa kikao kati ya Kamati na Mhe. Waziri Tax |
Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati wakifuatilia kikao |
Kikao kikiendelea |
Monday, April 17, 2023
TANZANIA - WADAU WAMAENDELEO KUENDELEA KUSHIRIKIANA
MKUTANO WA TANO WA BARAZA LA MAWAZIRI LA SEKTA YA UVUVI NA UKUZAJI VIUMBE MAJI WA EAC WAANZA KAMPALA, UGANDA
Mkutano wa Tano wa Baraza la Mawaziri la Sekta ya Uvuvi na ukuzaji Viumbe Maji wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanyika jijini Kampala, Uganda kuanzia tarehe 17-21 Aprili 2023.
Mkutano huo umeanza kwa kuwakutanisha Maafisa Waandamizi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki za Burundi, Kenya, Tanzania na Uganda unafanyika tarehe 17 - 18 Aprili 2023.
Mkutano huo utafuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 19 Aprili 2023 na Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika tarehe 20 - 21 Aprili 2023.
Ujumbe wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania katika kikao cha Maafisa Waandamizi unaongozwa
na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na
Uvuvi Dkt. Nazael Madalla. Aidha, ujumbe wa Tanzania unajumuisha
ushiriki wa maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania
Katika kikao hicho, maafisa waandamizi wanajadili na kuandaa nyaraka zitakazojadiliwa katika kikao cha Makatibu Wakuu kinachotarajiwa kufanyika tarehe 19 Aprili 2023 kitakachojadili taarifa nyingine na kupitia utekelezaji wa maamuzi/maagizo ya mikutano iliyopita na Utekelezaji wa Program na Miradi ya Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe maji katika Ziwa Victoria.
Ujumbe wa Tanzania katika Kikao cha Makatibu Wakuu unatarajiwa kuongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe na kujumuisha ushiriki wa Balozi wa Tanzania nchini Uganda Mhe. Dkt. Aziz Mlima ambaye atamuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo.
Tarehe 20 - 21 Aprili 2023 kitafanyika kikao cha Baraza la Mawaziri ambacho pamoja na mambo mengine kitakamilisha Mkutano wa Nne ulioishia ngazi ya Makatibu Wakuu, kupitia, kujadili na kuridhia taarifa ya kikao cha Makatibu Wakuu itakayowasilishwa katika kikao hicho.
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Kikao cha Mawaziri unatarajiwa kuongozwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa David Silinde.
Ujumbe wa Jamhuri ya Burundi katika Mkutano wa Tano wa Baraza la Mawaziri la Sekta ya Uvuvi na ukuzaji Viumbe Maji wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika jijini Kampala, Uganda kuanzia tarehe 17-21 Aprili 2023
Ujumbe wa Jamhuri ya Uganda katika Mkutano wa Tano wa Baraza la Mawaziri la Sekta ya Uvuvi na ukuzaji
Viumbe Maji wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki unaofanyika jijini Kampala, Uganda kuanzia tarehe 17-21 Aprili 2023
Friday, April 14, 2023
MFUMO WA KIELEKRTONIKI WA KUSAJILI DIASPORA KUKAMILIKA MWEZI JUNI 2023 - BALOZI MBAROUK
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inakamilisha mfumo wa Kidigitali wa uandikishaji wa Diaspora unaotarajiwa kukamilika mwezi June 2023 ili kuwezesha ukusanyaji endelevu wa takwimu za Diaspora.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni jijini Dodoma tarehe 14 Aprili 2023 na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk alipojibu swali la Mhe. Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi aliyetaka kujua idadi ya Diaspora wa Tanzania na mchango wao katika uchumi wa nchi.
Mhe. Balozi Mbarouk amesema Diaspora kama walivyo raia wengine wa Tanzania wana mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi na maendeleo kwa ujumla kupitia shughuli mbalimbali wanazozifanya ikiwemo utumaji wa fedha za kigeni nchini (remittances), uwekezaji, kuleta mitaji, utaalam na teknolojia ambayo huchangia katika kukuza uzalishaji wa mazao, bidhaa na huduma mbalimbali zenye tija kiuchumi.
Ameongeza kuwa, Diaspora pia wanachangia uchumi wa nchi kwa kutangaza fursa za kiuchumi, biashara, utalii na uwekezaji zinazopatikana nchini na kwamba kwa mujibu wa taarifa kutoka Balozi za Tanzania na maeneo yake ya Uwakilishi, hadi sasa idadi ya Diaspora wa Tanzania ni Milioni 1.5.
Amesema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la utumaji wa fedha za kigeni nchini kutoka kwa Diaspora hadi kufikia Shilingi Trilioni 2.6 mwezi Desemba 2022.
“Diaspora huchangia katika maendeleo ya nchi kwa kutuma fedha za kigeni nchini (Remittances); kuwekeza, kuleta mitaji, utaalamu na Teknolojia inayoweza kuchangia kukuza uzalishaji wa mazao, bidhaa na huduma mbalimbali zenye tija kiuchumi. Mathalan katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Desemba 2022, Diaspora walituma nchini kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 1.1 sawa na Shilingi Trilioni 2.6. Vilevile, katika kipindi hicho Diaspora wamewekeza kupitia ununuzi wa nyumba na viwanja wenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.4 na ununuzi wa Hisa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.5” amesema Balozi Mbarouk.
DKT. TAX AKUTANA NA RAIS MSTAAFU WA MSUMBIJI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimsikiliza Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Joaquim Chisano walipokutana jijini Dar es Salam kwa mazungumzo. Mhe Chisano yuko nchini kwa mwaliko wa kushiriki utoaji wa Tuzo za Taifa za Uandishi Bunifu za Mwl. Nyerere uliyofanyika tarehe 13 Aprili, 2023. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimsikiliza Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Joaquim Chisano walipokutana jijini Dar es Salam kwa mazungumzo. Mhe Chisano yuko nchini kwa mwaliko wa kushiriki utoaji wa Tuzo za Taifa za Uandishi Bunifu za Mwl. Nyerere uliyofanyika tarehe 13 Aprili, 2023. |
mazungumzo yakiendelea |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt.
Stergomena Tax katika picha na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe.
Joaquim Chisano walipokutana jijini Dar es Salam kwa mazungumzo. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax amekutana na kuzungumza na Rais Mstaafu wa Msumbiji Mhe. Joaquim Chisano jijini Dar es Salam.
Mhe.Dkt. amemshukuru Mhe. Chisano kwa kukubali mwaliko wa kuja kushiriki utoaji wa Tuzo za Taifa za Uandishi Bunifu za Mwl. Nyerere zilizofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 13 Aprili, 2023.
“Mhe. Chisano naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kitendo cha kukubali kuja nchini na kuwa mgeni rasmi katika utoaji wa tuzo uliofanyika jana, tunakushukuru sana na karibu tena Tanzania,” alisema Dkt Tax.
Amesema kitendo hicho kinaonesha uhusiano wa kidugu na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji na pia kunaongeza jitihada za kuitangaza lugha ya Kiswahili katika bara la Afrika na Duniani kwa ujumla