Tanzania na Marekani zimeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano zaidi katika sekta za biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi baina ya mataifa hayo.
Ahadi hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo alipomwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) katika maadhimisho ya miaka 247 ya uhuru wa Marekani na Miaka 62 ya Ushirikiano wa Marekani na Tanzania yaliyofanyika tarehe 04 Julai 2023 jioni nyumbani kwa Balozi wa Marekani nchini Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Shelukindo alisema Tanzania na Marekani zimekuwa zikifanya kazi pamoja katika kukuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, ambapo Tanzania imeendelea kuvutia wawekezaji na wauzaji bidhaa kutoka Marekani na Tanzania imekuwa ikisafirisha bidhaa za nguo kwenda Marekani chini ya Mpango wa Ukuzaji fursa za kiuchumi Afrika (AGOA).
“Takwimu zinaonesha kuwa uagizaji wa bidhaa kutoka Marekani umeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 201.8 mwaka kwa 2017 hadi Dola za Marekani milioni 215 mwaka 2022. Pia, katika miaka ya hivi karibuni, mauzo ya nje kutoka Tanzania kwenda Marekani yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 9.7 mwaka 2017 kufikia Dola za Marekani milioni 49.5 mwaka 2022,” alisema Dkt. Shelukindo.
Balozi Shelukindo aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuwavutia zaidi wafanyabiashara na wawekezaji nchini na kuwawezesha Watanzania kufanya biashara katika mazingira mazuri na rafiki.
“Kuanzia mwaka 1997 hadi 2023, Marekani imefanya uwekezaji nchini Tanzania wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 4.8 katika sekta za Kilimo, Nishati, Taasisi za Fedha, Rasilimali Watu, Uzalishaji Asili, Maliasili, Madini, Mawasiliano, Utalii na Uchukuzi, uwekezaji huo umezalisha ajira zaidi ya 54,900 nchini,” alisema Balozi Shelukindo.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Shelukindo aliwakaribisha wawekezaji zaidi kutoka Marekani kuwekeza katika sekta mbalimbali zikiwemo nishati mbadala, viwanda vya magari, viwanda vya dawa, mafuta ya kula, viwanda vya pamba na nguo, kilimo, utalii, mifugo, uvuvi, Samaki, madini na miundombinu.
Kwa upande wake Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle alisema ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Tanzania ni wa muda mrefu na umekuwa imara tangu ulipoanzishwa.
Mhe. Balozi Battle aliongeza kuwa wakati Marekani inasherekea maadhimisho ya miaka 247 na miaka 62 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati yake na Tanzania ni vyema kuendeleza ushirikiano baina ya mataifa hayo na kuhakikisha wananchi wanapata mambo ya msingi hususan elimu, kazi, afya, ulinzi, usalama, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na diplomasia inayounganisha kwa manufaa ya baadae ya wananchi wote.
“Marekani tumedhamiria kufanya biashara na uwekezaji na Tanzania kwa maslahi mapana ya nchi zetu. Uwekezaji katika sekta hiyo bila shaka utachangia kuboresha zaidi uchumi wa Tanzania,” alisema Mhe. Balozi Battle
“Uhusiano wetu na Tanzania umedumu kwa takribani miaka 62…..tulisimama na Tanzania, tumesimama na Tanzania na tutaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyakati zote,” aliongeza Mhe. Balozi Battle.
Tanzania na Marekani zimekuwa zikishirikiana katika sekta za Afya, Kilimo, Nishati, Taasisi za Fedha, Rasilimali Watu, Uzalishaji Asili, Maliasili, Madini, Mawasiliano, Utalii na Uchukuzi.
|
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akihutubia katika maadhimisho ya miaka 247 ya uhuru wa Marekani na Miaka 62 ya Ushirikiano wa Marekani na Tanzania yaliyofanyika tarehe 04 Julai 2023 jioni nyumbani kwa Balozi wa Marekani nchini Jijini Dar es Salaam |
|
Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle akizungumza katika maadhimisho ya miaka 247 ya uhuru wa Marekani na Miaka 62 ya Ushirikiano wa Marekani na Tanzania yaliyofanyika tarehe 04 Julai 2023 jioni Jijini Dar es Salaam |
|
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisalimiana na Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle baada ya kuwasili nyumbani kwa Balozi huyo Jijini Dar es Salaam |
|
sehemu ya Mabalozi, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na wananchi mbalimbali wakifuatilia maadhimisho ya miaka 247 ya uhuru wa Marekani na Miaka 62 ya Ushirikiano wa Marekani na Tanzania Jijini Dar es Salaam |
|
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo katika picha ya pamoja na Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle
|