Monday, June 19, 2023

WAZIRI TAX AWAAGA MABALOZI WA EU, UJERUMANI NA NORWAY

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amekutana na kuwaaga mabalozi watatu waliokuwa wanaziwakilisha nchi zao hapa nchini baada ya kumaliza muda wao wa uwakilishi.

Dkt. Tax amewaaga mabalozi hao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Mabalozi walioagwa ni Balozi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya nchini, Mhe. Manfredo Fanti, Balozi wa Ujerumani nchini Mhe. Regine Hess pamoja na Balozi wa Norway Nchini Mhe.  Elisabeth Jacobsen.

Awali Mhe. Tax alimpongeza Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini, Mhe. Fanti kwa ushirikiano alioutoa kwa Serikali ya Tanzania wakati wa uwakilishi wake na kumuahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya wakati wote hususani katika sekta ya biashara na uwekezaji.

“Nakupongeza kwa kazi nzuri na kubwa uliyoifanya wakati wa uwakilishi wako hapa nchini, ambapo umefanikiwa kuimarisha uhusiano mzuri baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya katika sekta ya siasa pamoja na uchumi. Kupitia muda wako wa uwakilishi, wote tumeshuhudia mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya yakiimarika. 

Pia tumekuwa na makongamano kadhaa ya biashara yaliyowakutanisha wafanyabishara wa mataifa yetu na kujadili fursa za biashara baina ya mataifa yetu,” alisema Dkt. Tax

Naye Balozi Fanti ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano iliompatia wakati wote wa uwakilishi na kuahidi kuwa ataendelea kuwa Balozi bora wa Tanzania.

Kadhalika, Dkt. Tax amemuaga Balozi wa Ujerumani nchini hapa nchini Mhe. Regine Hess. Waziri Tax alimshukuru kwa ushirikiano aliouonesha kwa Serikali ya Tanzania wakati wa uwakilishi wake hapa nchini.

“Tanzania tunakushukuru kwa ushirikiano wako wakati wote wa uwakilishi wako hapa nchini, ushirikiano wetu (Tanzania na Ujerumani) umekuwa imara na bora wakati wote na tunaamini utaendelea kuimarika,” alisema Dkt. Tax

Naye Balozi Hess alisema kuwa anaondoka akiwa na faraja ya kuona masuala ya utawala bora, haki za binadamu pamoja na amani na usalama yakiwa yameboreshwa kwa kiasi kikubwa. 

Katika tukio jingine, Dkt. Tax amekutana na kumuaga Balozi wa Norway nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen ambapo ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa ushirikiano wakati wa kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Balozi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya nchini, Mhe. Manfredo Fanti baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini. Dkt. Tax amemuaga Balozi Fanti katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimkabidhi zawadi ya picha na Balozi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya nchini, Mhe. Manfredo Fanti baada ya kumaliza muda wao wa uwakilishi nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimsikiliza Balozi wa Ujerumani nchini Mhe. Regine Hess baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini. Dkt. Tax amemuaga Balozi Hess katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiagana akizungumza na Balozi wa Norway Nchini Mhe.  Elisabeth Jacobsen katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Balozi Elisabeth amemaliza muda wake wa uwakilishi nchini.  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na Balozi wa Norway Nchini Mhe.  Elisabeth Jacobsen katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Idaya ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (mwenye koti jeupe) pamoja na maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ubalozi wa Norway.  





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.