Thursday, June 1, 2023

DKT. MPANGO AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUTOKA BURUNDI KUJA KUWEKEZA NCHINI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Mpango amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Burundi kuja kuwekeza nchini na kuitaja Tanzania kama sehemu salama ya kuwekeza mitaji yao.

Mhe. Dkt. Mpango ametoa wito huo alipokutana kwa mazungumzo na timu ya wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa 17 wa Burundi ambao wameonesha nia ya kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo za madini, ufugaji, kilimo na  viwanda vya mbolea na saruji.

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara ikiwa ni pamoja na kuzifanyia kazi changamoto za kisera na kisheria.

Ameongeza kusema  uchumi wa Tanzania upo imara,huku mazingira na miundombinu kwa ujumla kama maji, umeme, barabara na reli vikiboreshwa ili  kukidhi mahitaji ya wawekezaji.

Amesema uwekezaji ni gharama na kwamba Serikali inaboresha mazingira ili mwekezaji yeyote apate faida lakini pia na nchi ifaidike na uwekezaji huo.  Hivyo katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa Serikali iliandaa Mpango wa maboresho ya biashara ambao umejumuishaa maoni na mapendekezo mbalimbali kutoka kwa wadau  wa biasharana  uwekezaji.

Pia amesema kupitia mpango huo Serikali imefanikiwa kubadilisha mifumo mbalimbali na kuondoa kero mbalimbali kama upatikanaji wa leseni, ulipaji kodi ili ieandane na wakati uliopo ikiwemo banadari, kituo cha uwekezaji Tanzania na sekta nyingine.

“Nimefurahi sana Kampuni 17 kuja kuwekeza Tanzania ni jambo zuri na pia ninafarijika na kampuni za Tanzania pia zilizowekeza hapa Burundi. Naendelea kusisitiza badala ya kufanya biashara na nchi za mbali huko tufanye biashara wenyewe kwa wenyewe  kwani tuna mengi ya kubadilisha katika biashara ili pia tuwaunge mkono Wakuu wa Nchi za Afrika waliofanya uamuzi wa makusudi wa kuanzisha Ukanda Huru wa Biashara Barani Afrika. Kuna bidhaa zinapatikana Tanzania, Burundi hazipo lakini pia kuna bidhaa zinapatikana Burundi, Tanzania hazipo hivyo tufanye biashara,  alisisitiza Mhe. Dkt. Mpango.

Amesema mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Afrika kuhusu  ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Uvinza-Msongati hadi Gitega yanaendelea vizuri na kwamba kukamilika kwa reli hiyo kutarahisha biashara na nchi jirani. Pia ameeleza kuwa, ujenzi wa Barabara ya lami kutoka Uvinza hadi Malagarasi unaendelea huku zikiwa zimebakia kilomita 52 pekee kukamilika.

Pia alitoa rai kwa Wawekezaji hao kuendelea kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania  uliopo nchini humo kwa kuwasilisha changamoto zao ili ubalozi nao uziwasilishe kwa wahusika kila inapohitajika.

Kwa upande wake, Kiongozi wa wawekezaji hao ambaye pia ni Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Bujumbura, Bw. Fredrick Siwale amemshukuru Makamu wa Rais kwa kutenga muda na kuzungumza nao. Pia alieleza kuwa Benki hiyo imewekeza mtaji wa Dola za Marekani Milioni 210 kwa ajili ya kuwawezesha wawekezaji hao kuwekeza nchini.

Ameongeza kusema katika kutekeleza suala zima la uwekezaji nchini Tanzania kwa wawekezaji kutoka Burundi, wamekuwa wakiwapatia mikopo baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa nchi hiyo  ili kutumia mikopo hiyo kuwekeza Tanzania ambapo hadi sasa wafanyabiashara hao wamewekeza kwa kujenga kiwanda cha Mbolea cha Intracom jijini Dodoma, kiwanda cha kutengeneza saruji mjini Kigoma na ujenzi wa hoteli  ya kitalii mjini Tanga.

Wawekezaji hao pia wamempongeza Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko na wafanyakazi wa Ubalozi kwa ushirikiano wanaopata kila wakati wanapohitaji msaada.

Mhe. Dkt. Mpango alikuwa nchini Burundi kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano Maalum wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Phillip Mpango akizungumza na Wawekezaji na Wafanyabiashara wa Burundi alipokutana nao jijini Bujumbura, Burundi pembezoni mwa Mkutano Maalum wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo alishiriki kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wawekezaji hao wameonesha ya kuja nchini kuwekeza kwenye sekta za kilimo, madini, ufagaji, ujenzi wa viwanda vya saruji na mbolea na ujenzi wa hoteli.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza wakati wa mkutano huo
Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko akitoa taarifa kwa Mhe. Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mpango kuhusu wawekezaji hao kutoka Burundi
Kiongozi wa Wawekezaji hao ambaye pia ni Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Bujumbura, Bw. Fredrick Siwale akizungumza wakati wa kikao kati yao na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mpango
Kikao kikiendelea. huku viongozi mbalimbali kutoka Tanzania akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi (wa tatu kushoto) na Mhe. Balozi Maleko (kushoto) wakifuatilia
Sehemu ya wawekezaji hao wakifuatilia kikao
Sehemu nyingine ya wawekezaji
Picha ya pamoja kati ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mpango (wa pili kushoto), Dkt. Mnyepe (wa pili kulia), Mhe. Balozi Maleko (kushoto) na Bw. Siwale (kulia)
Picha ya pamoja kati ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mpango (katikati), Dkt. Mnyepe (wa pili kulia), Mhe. Balozi Maleko (wa pili kkushoto) na wawekezaji (kushoto na kulia) kutoka Burundi ambao wamewekeza kwenye Kiwanda cha kutengeneza mbolea cha Intracom kilichopo jijini Dodoma
Picha ya pamoja
Picha ya pamoja
Picha ya pamoja

Picha ya pamoja kati ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mpango, Dkt. Mnyepe, Mhe. Balozi Maleko na baadhi ya wawekezaji kutoka Burundi wenye nia ya kuwekeza Tanzania

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.