Friday, June 9, 2023

WAZIRI TAX: WATUMISHI TEKELEZENI DIPLOMASIA YA UCHUMI KWA BIDII


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisaini kitabu cha wageni aliposili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Italia

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Dkt. Stergomena Tax amewataka watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa bidii ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Akizungumza na watumishi hao katika Ofisi za Ubalozi huo Jijini Roma, Mhe. Dkt. Tax amesema Serikali inawategemea wao kama wadau wa kubwa katika kutekeleza diplomasia ya uchumi ili kuinufaisha nchi.

“Wizara inategemea Balozi katika kutekeleza diplomasia ya uchumi, kwa hiyo mna wajibu wa kuhakikisha mnafanya kazi hii kwa ukamilifu” alisema Dkt.Tax.

Aidha, Dkt. Tax ameupongeza Ubalozi huo kwa kuandaa mkakati wa kutekeleza diplomasia ya uchumi katika eneo lake la uwakilishi na kuzitaka Balozi nyingine za Tanzania kuiga mfano huo.

“Nimesikia hapa mmeandaa mpango mkakati wa kutekeleza Diplomasia ya Uchumi katika eneo lenu, hili ni jambo zuri niwapongeze kwa hilo na balozi zetu nyingine hazina budi kuiga mfano huu,” alisema Dkt. Tax

Aliongeza kuwa Wizara inatengeneza mkakati wa kitaifa wa utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, tutawaletea muuone na mtoe maoni yenu ili kuuboresha zaidi.

Amesema anaamini kuwa kupitia mkakati huo Wizara itajifunza kitu na hivyo kuja na mkakati bora wa utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

Mhe.Waziri amewasihi watendaji wa ubalozi kuhakikisha wana shirikisha sekta binafsi katika kutekeleza kazi zao kwani kufanya hivyo kutasaidia kuondoa uwiano mdogo wa kibiashara uliopo kati ya Tanzania na Italia.

Awali akizungumza katika kikao hicho Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo alisema ubalozi unaendelea kusimamia na kutekeleza diplomasia ya uchumi kupitia utalii,kilimo,uwekezaji, biashara na masoko ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na nchini inazowakilisha.

Alisema ubalozi pia unashirikisha Diaspora katika shughuli za maendeleo ya nchi na kupongeza mpango wa kusajili Diaspora wa Tanzania kwa njia ya Kidigitalia

Mhe. Dkt. Tax yuko nchini Italia kwa ziara ya kikazi ambapo anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akifuatilia taarifa iliyokuwa ikiwasilishwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia Mhe. Mahmoud Kombo wakati wa kikao kazi watumishi wa Ubalozi huo. Kushoto ni Mkurugezi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Swahiba Mndeme na kulia ni Mkuu wa Utawala Ubalozi wa Utalia Bi. Jubilata Shao
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Balozi wa Tanzania nchini Italia Mhe. Mahmoud Kombo wakiwa picha ya pamoja
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Balozi wa Tanzania nchini Italia Mhe. Mahmoud Kombo wakiwa picha ya pamoja na Watumishi wa Ubalozi 

Balozi wa Tanzania nchini Italia Mhe. Mahmoud T. Kombo akielezea jambo kwa Waziri Tax alipokuwa akitembelea maeno ya Ubalozi

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.