Friday, June 2, 2023

SERIKALI YAKABIDHI ENEO LA UJENZI WA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imekabidhi eneo la ujezi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kwa Mkandarasi ambaye ni CRJE (East Africa) Ltd na Mshauri Elekezi Aru Built Environment Consulting Company Ltd (ABECC) katika eneo la Lakilaki, Jijini Arusha.

Hafla ya makabidhiano ya eneo hilo la ujenzi imeongozwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo ambaye amekabidhi eneo hilo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baada ya makabidhiano hayo Dkt. Shelukindo amesema kuwa Serikali imetoa eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 26 hivyo Wizara itaendelea kutoa usaidizi wa karibu katika usimamizi wa ujenzi wa mradi huu ambao katika hatua ya awali unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilllingi billioni nane (8) na utakamilika baada ya miaka miwili kulingana na mkataba wa mradi huo. 

“Ujenzi wa majengo ya mahakama hiyo utakuwa wa kisasa kwa kuwa umezingatia taratibu na vigezo vya ujenzi wa majengo ya ofisi za kimataifa ambapo pamoja na jengo kuu, kutakuwa pia na jengo la mahakama, hospitali, shule na mengine yanayoendana na huduma za mahakama hiyo,” alisema Dkt. Shelukindo

Naye Rais wa Mahakama wa Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Jaji Imani Aboud alieleza kuwa amefurahishwa na hatua hiyo iliyofikiwa na Serikali ya kukabidhi eneo la ujenzi wa mradi huo lililosubiriwa kwa muda mrefu.

‘’ Tunaishukuru na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa hatua hii itaiwezesha Mahakama kuwa na majengo ya kisasa na ofisi za kudumu kwa ajili ya kutoa huduma zake na tunatarajia ujenzi wa maradi huu utakamilika kwa wakati na salama” alisema Mhe. Jaji Aboud.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella ameishukuru pia Serikali kwa kuitimza ndoto yake ya miaka mingi ya kujenga mahakama hiyo nchini ambayo italiletea fursa nyingi Jiji la Arusha ikiwemo ajira za mafundi, walinzi pamoja na kuongeza taswira nzuri ya jiji hilo la kitalii.

“Jiji la Arusha limebahatika kuwa mwenyeji wa taasisi za kimataifa zinazojengwa katika eneo hili la Lakilaki hivyo Mkoa utatoa usaidizi wakati wa ujenzi wa mradi huu ili ukamilike kwa ubora na wakati na kuyafikia malengo yaliyowekwa na Serikali” alisema Mhe. Mongella. 

Hafla hiyo ya makabidhiano ilihudhuriwa pia na Meneja wa Mradi kutoka CRJE (East Africa) Ltd, Bw. Zhang Cuishan, Mshauri elekezi kutoka chuo cha Ardhi, QS. Dkt. Godwin Maro, viongozi na Maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja watumishi kutoka Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.

Mwaka 2005 Umoja wa Afrika uliridhia kuwepo na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ambapo Tanzania ilijitolea kuwa mwenyeji wa Mahakama hiyo na kuanzia wakati huo Serikali imekuwa ikikamilisha taratibu mbalimbali za nyaraka za eneo la mradi ambao utajengwa katika eneo la Lakilaki nje kidogo ya jiji la Arusha.

Viongozi wakiwasili katika eneo la Lakilaki Jijini Arusha tayari kwa ajili ya kumkabidhi Mkandarasi CRJE (East Africa) Ltd na Mshauri Elekezi Aru Built Environment Consulting Company Ltd (ABECC) eneo la ujenzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akimkabidhi nakala za mitakaba ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Meneja wa Mradi kutoka CRJE (East Africa) Ltd, Bw. Zhang Cuishan. Ujenzi wa mahakama hiyo utakuwa katika eneo la Lakilaki Jijini Arusha. Wanaoshuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella pamoja na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Jaji Imani Aboud, viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na maafisa waandamizi kutoka Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akimkabidhi nakala za mitakaba ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Rais wa Mahakama hiyo, Mhe. Jaji Imani Aboud


Viongozi na watumishi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja






No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.