Monday, June 12, 2023

TANZANIA YAZINDUA UBALOZI WAKE VIENNA, AUSTRIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa Ubalozi na Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa mataifa Vienna, Austria. Pamoja naye ni Naibu Waziri wa Austria aneyeshughulikia masuala ya Ulaya na Uhusiano wa Kimataifa Mhe. Peter Launsky-Tieffenthal ambaye alihudhuria hafla hiyo ya ufunguzi iliyofanyika tarehe 12 Juni, 2023.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa na Naibu Waziri wa Austria anayeshughulikia Masuala ya Ulaya na Uhusiano wa Kimataifa  Mhe. Peter Launsky-Tieffenthal wakipongezana  baada ya ufunguzi rasmi wa Ubalozi wa Tanzania jijini Vienna, Austria.

 


Kaimu Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa Vienna nchini Austria Bi. Elizabeth Rwitunga akizungumza katika hafla ya kuzindua Ubalozi wa Tanzania Vienna terehe 12 Juni, 2013

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa Ubalozi wa Tanzania jijini Vienna Austria.
Mhe. Dkt. Tax akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa Ubalozi wa Tanzania jijini Vienna Austria.




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa na Naibu Waziri wa Austria anayeshughulikia Masuala ya Ulaya na Uhusiano wa Kimataifa  Mhe. Peter Launsky-Tieffenthal wakinyanyua mikono baada ya ufunguzi rasmi wa Ubalozi wa Tanzania jijini Vienna, Austria.


 

Naibu Waziri wa Austria anayeshughulikia Masuala ya Ulaya na Uhusiano wa Kimataifa  Mhe. Peter Launsky-Tieffenthal akizungumza wakati wa hafla ufunguzi wa Ubalozi wa Tanzania jijini Vienna, nchini Austria.

 

Baadhi ya wanadiplomasia waliopo jijini Vienna walioshiriki hafla ya  ufunguzi rasmi wa Ubalozi wa Tanzania jijini Vienna wakifuatilia ufunguzi huo.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa na Naibu Waziri wa Austria anayeshughulikia Masuala ya Ulaya na Uhusiano wa Kimataifa  Mhe. Peter Launsky-Tieffenthal katika picha ya pamoja na Diaspora wa Tanzania nchini Austria walioshiriki hafla ya  ufunguzi rasmi wa Ubalozi wa Tanzania jijini Vienna

 






 



 


 

 

 


 

 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua rasmi Ubalozi na Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa jijini Vienna nchini Austria.

 

Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amesema kufunguliwa kwa Ubalozi huo ni mafanikio yanayoimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Austria na Taasisi za Umoja wa Mataifa zilizopo jijini Vienna na kinaonesha jinsi Tanzania inavyoipa kipaumbele Austria.

 

“Kufunguliwa kwa Ubalozi huu ni mafanikio makubwa ambayo yanaimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Austria na Taasisi za Umoja wa Mataifa zilizopo hapa jijini Vienna na kinaonesha kwa vitendo kuwa Tanzania inaipa kipaumbele Uhusiano wake na Austria,” alisema Dkt. Tax.

 

Ameishukuru Serikali ya Austria na Wizara inayoshughulikia masuala ya Ulaya na uhusiano wa Kimataifa kwa ushirikiano mkubwa ambao imekua ikiupatia Ubalozi wa Tanzania Vienna tangu ulipoanzishwa hadi kufikia siku ya uzinduzi.

 

Akiongelea uhusiano uliopo Dkt. Tax amesema Tanzania na Austria zimeendelea kufaidika na uhusiano mzuri kati yao kupitia maeneo mbalimbali kama elimu, afya, miundombinu na hivyo kuchangia maendeleo ya kiuchumi kwa faida ya wananchi wake.

 

Amesema Serikali ya Tanzania inathamini uhusiano na ushirikiano na wadau wote ambao wanapambania agenda moja za kulinda na kukuza amani na usalama pamoja na kupambana na uhalifu wa kupangwa, rushwa, ugaidi na amewaomba kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta maendeleo endelevu kwa manufaa ya watu wote.

 

“Serikali ya Tanzania inathamini uhusiano na ushirikiano na wadau wote ambao tunapigania agenda moja, ajenda hizi ni kama  kulinda na kukuza amani na usalama, kupambana na uhalifu wa kupangwa, rushwa, ugaidi na mengine mengi , nawaomba tuendelee kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta maendeleo endelevu kwa manufaa ya watu wote,” alisisitiza Dkt. Tax.

 

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Ubalozi huo jijini Vienna Naibu Waziri anayeshughulikia Masuala ya Ulaya na Uhusiano wa Kimataifa wa Austria Mhe. Peter Launsky-Tieffenthal amesema Austria inapongeza uamuzi wa Serikali ya Tanzania wa kufungua Ubalozi wake Austria na kuungana na nchi nyingine 16 za Afrika zenye Ubalozi nchini humo na kuahidi kuusaidia Ubalozi huo kwa kila hali ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.

 

 “Austria inapongeza uamuzi wa Serikali ya Tanzania wa kufungua Ubalozi wake Austria na hivyo kuungana na nchi nyingine 16 za Afrika ambazo zina Balozi zao hapa nchini, niwa ahidi na kuwahakikishia kuwa Serikali ya Austria iko tayari kuusaidia Ubalozi huo kwa kila hali ili ufikie  malengo ya kuanzishwa kwake”, alisisitiza Waziri huyo.

 

Amesema Austria inaangalia uhusiano wake na Tanzania ambao una miaka mingi ukiwa imara na dhabiti na kuongeza kuwa ni imani yao kuwa kufunguliwa kwa Ubalozi huo ni hatua muhimu ya kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo.

 

Alisema Tanzania ina picha nzuri nchini Austria na nchi yao ni mshirika mkubwa anayeamini katika demokrasia imara na kuongeza kuwa Tanzania kujihusisha na harakati za kutafuta amani katika ukanda wa Afrika Mashariki na katika maeneo mengine kunavutia zaidi.


“Tanzania ina picha nzuri hapa Vienna, niseme wazi kuwa Nchi yetu ni mshirika mkubwa anayeamini katika demokrasia imara na kujihusisha kwa Tanzania katika harakati za kutafuta amani katika ukanda wa Afrika Mashariki na kwingineko kunaongeza uzuri wa picha yake,” alisema.


Hafla ya uzinduzi wa Ubalozi huo ulioanzishwa mwaka 2021 ilihudhuriwa na  wanadiplomasia mbalimbali walioko jijini Vienna.

 

 








No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.