Shirika la Ndege la Ufaransa yaani Air France limezindua safari yake ya kwanza kutoka Paris Charles de Gaulle hadi jijini Dar es Salaam tarehe 12 Juni 2023.
Uzinduzi wa safari hizi ni mwendelezo wa huduma za Shirika hilo baada ya kuazisha safari zake za moja kwa moja kutoka Paris hadi Zanzibar mwaka 2021.
Kuanzishwa kwa safari hii mpya na Shirika hilo ni matokeo ya jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhamasisha utalii, biashara na uwekezaji nchini . Lakini pia zinatokana na ushirikiano na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania na Ufaransa.
Aidha, inatarajiwa kuwa kuanzishwa kwa safari hizi kutasaidia kuongeza idadi ya watalii, wawekezaji na wafanyabiashara watakaotembelea nchini na hatimaye kukuza uchumi wa nchi.
Huduma za usafiri kupitia Air France zitafanyika mara tatu kwa wiki katika siku za Jumatatu, Jumatano na Jumamosi ambapo Shirika hilo litatumia ndege aina ya Boeing 787-9.
Viongozi wa Serikali wakiongozwa na Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi walishiriki kwenye mapokezi hayo ambayo pia yalimshirikisha Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui huku Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma M. Rajab akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax kwenye mapokezi hayo.
Hafla ikiendelea |
Picha ya pamoja |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.