Tanzania na India
zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye maeneo ya kimkakati ambayo yana
manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili
ikiwemo maji, kilimo, nishati, teknolojia, afya, ulinzi na usalama, utamaduni
na michezo, uchukuzi na biashara na
uwekezaji.
Hayo yamebainishwa wakati
wa mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari mara baada ya mazungumzo ya faragha kati ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa
India, Mhe. Narendra Modi yaliyofanyika katika jengo la kupokelea wageni wa
kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi tarehe 09 Oktoba 2023.
Akizungumza kwenye mkutano
huo, Mhe. Rais Dkt. Samia ameipongeza Serikali ya India kwa kuendelea kuwa
mshirika muhimu na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya Tanzania
hususan kwenye maeneo ya kimkakati kama maji, afya, kilimo, teknolojia, ulinzi
na usalama, na baiashara na uwekezaji.
Pia amesema Tanzania
inapongeza uamuzi wa Serikali ya India wa kuanziasha kampasi ya kwanza la
Taasisi ya Teknolojia ya India nje ya nchi hiyo ambayo itaanzishwa hivi
karibuni Zanzibar na kuutaja uamuzi huo kama heshima na upendeleo kwa Tanzania kwani
utawanufaisha watanzania, Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumzia biashara
baina ya nchini hizi, Mhe. Rais Samia amesema, thamani ya ufanyaji biashara
kati ya Tanzania na India imeendelea kuongezeka ambapo kwa takwimu zilizopo
nchini biashara kati ya nchi hizi mbili imeongezeka hadi kufikia Dola za
Marekani Bilioni 3.1 mwaka 2022 kutoka
Dola za Marekani Bilioni 2.6 mwaka 2017.
Kwenye medani za
ushirikiano wa kimataifa, Mhe. Rais Samia amempongeza Waziri Mkuu Modi kwa
kuandaa kwa mafanikio Mkutano wa Wakuu wa Nchi za G20 uliofanyika nchini hapa
mwezi Septemba 2023 ambapo Afrika kupitia Umoja wa Afrika imefanikiwa kuwa mwanachama
wa kudumu wa Umoja huo.
“Siwezi kusita kuipongeza
India kwa kufanikiwa kuandaa Mkutano wa G20 ambao ulishuhudia Afrika inakuwa
mwanachama kamili wa G20, nampongeza Waziri Modi kwa kutetea mpango wa
kupunguza madeni kwa mataifa madogo na kutangaza mpango wa dharura wa
kuhamasisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya nchi zinazoendelea ili kuwezesha
upatikanaji wa teknolojia ya nishati safi ifikapo mwaka 2050” amesema Mhe. Rais
Samia.
Kwa upande wake, Waziri
Mkuu Modi ameitaja Tanzania kama mshirika wake wa karibu na mkubwa katika
maendeleo barani Afrika na kwamba nchi hizo zimekubaliana kuupeleka
ushirikiano uliopo katika viwango vya juu kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania
na India.
Amesema India itaendelea
kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ya kukuza ujuzi,
usambazaji maji, teknolojia ya habari na mawasiliano na uhusiano wa watu wa
India na Tanzania, nishati safi na ulinzi na usalama.
Pia ameongeza kusema nchi
hizo zimekubaliana kuwa na mpango wa miaka mitano wa ushirikiano katika masuala
ya ulinzi na usalama hususan katika maeneo ya kujenga uwezo, mafunzo na ulinzi baharini.
Akizungumzia ushirikiano
katika biashara, Mhe. Modi amesema nchi
hizo zimekubaliana kuangalia uwezekano wa kuongeza biashara kwa kutumia sarafu
za nchi zao kwa lengo la kupunguza gharama na matumizi ya Dola za Marekani.
Wakati wa Mkutano huo,
Mhe. Rais Samia na Mhe. Modi walishuhudia ubadilishanaji wa Hati Sita za
Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Hati 14 na Mkataba mmoja zilizosainiwa kati
ya Tanzania na India wakati wa ziara hii. Hati hizo zinagusa sekta za Uchukuzi,
Utamaduni, Michezo, Uwekezaji, TEHAMA na Elimu.
Mhe. Dkt. Rais Samia yupo
nchini India kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 8 hadi 11 Oktoba,
2023.
|
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri Mkuu
wa India, Mhe. Narendra Modi wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mara
baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya faragha kati yao yaliyofanyika katika jengo la kupokelea
wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi, India tarehe 09
Oktoba 2023
|
|
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya faragha kati yake na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi yaliyofanyika katika jengo la kupokelea wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi, India tarehe 09 Oktoba 2023
|
|
Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mara
baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya faragha kati yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
wa India, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yaliyofanyika katika jengo la kupokelea
wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi, India tarehe 09
Oktoba 2023 |
|
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa pamoja na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi, wakiwashuhudia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar wakibadilishana moja ya Hati za Makubaliano ya Ushirikiano zilizosainiwa wakati wa ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia nchini India
|
|
Uadilishanaji wa Hati za Makubaliano ukiendelea
|
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (kulia) akiwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (kushoto) na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega wakifuatilia Mkutano wa Mhe. Rais Dkt. Samia na Mhe.Modi na waandishi wa habari uliofanyika jijini New Delhi wakati wa ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia nchini India |
|
|
Mhe. Rais Samia akiwa na Mhe. Modi mara baada ya kuwasili katika jengo la kupokelea
wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi, India tarehe 09
Oktoba 2023 |
|
Mhe. Rais Samia akiwa na Mhe. Modi mara baada ya kuwasili katika jengo la kupokelea
wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi, India tarehe 09
Oktoba 2023
|