Tuesday, October 10, 2023

RAIS DKT. SAMIA AKARIBISHA WAWEKEZAJI KUTOKA INDIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan amefungua rasmi Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na India lililofanyika jijini New Delhi tarehe 10 Oktoba 2023.



Akifungua Kongamano hilo lenye kaulimbiu isemayo “Strong, Togerher ," Mhe. Rais Dkt. Samia amewakaribisha wawekezaji wa India kuja nchini  kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, afya, Tehama,  Utalii na Miundombinu na kuwahakikishia mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara.



Amesema Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kurekebisha  baadhi ya sheria za usimamizi wa biashara, kuboresha huduma na miundombinu,  teknolojia pamoja na kuishirikisha kikamilifu  sekta binafsi.

 

Ameongeza kuwa kutokana na jitihada hizo,  viwango vya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na India  vimeongezeka mwaka ha ambapo kwa takwimu za  Tanzania za mwaka 2021/2022 India  ni miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kwa uwekezaji nchini kwa kuwekeza miradi 630 yenye thamani ya Dola za Marekani 3.7 ambayo imetengeneza ajira kwa watanzania 60,000.



Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara wa India Mhe.  Shri Piyush Goyal amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali  ya Tanzania katika kuboresha mazingira yabuwekezaji na kwamba ziara ya Mhe. Dkt. Samia inafungua ukurasa mpya wa ushirikiano kwenye sekta muhimu ikiwemo biashara na uwekezaji.



Awali akizungumza kwenye kongamano hilo Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, Bi. Angelina Ngalula amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali hizi mbili katika kuboresha mazingira ya uwekezaji  na biashara.



Amesema kutokana na jitihada hizo jukwaa hilo limehudhuriwa na zaidi ya  wafanyabiashara na wawekezaji 250 kutoka  Tanzania na India ambapo kati yao 80 wanatoka Tanzania katika sekta za   Benki, Uchukuzi, Uzalishaji viwandani, TEHAMA,   Burudani na Ubunifu wa mitindo.



Kongamano hilo ambalo limebeba mada isemayo " Nafasi ya Sekta Binafsi katika kuimarisha Biashara kati ya Tanzanaia na India litahitimishwa kwa kupitisha Azimio na Mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha sekta ya biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan akifungua rasmi Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na India lililofanyika jijini New Delhi tarehe 10 Oktoba 2023.Mhe. Rais yupo nchini India kwa zara ya kitaifa ya siku tatu

Mhe. Rais Dkt. Smia akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akimweleza jambo wakati wa Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na India lililofanyika India hivi karibuni
Sehemu ya wawekezaji kutoka Inida pamoja  jumbe wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na India
Mkutano wa Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na India ukiendelea

Mhe. Rais Dkt. Samia akishuhudia ubadlishanaji wa Hati za Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Tanzania na India kwenye sekta ya uwekezaji

Mhe. Rais Dkt. Samia akishuhudia ubadlishanaji wa Hati za Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Tanzania na India kwenye sekta ya biashara
















RAIS DKT. SAMIA ATUNIKIWA SHAHADA YA HESHIMA YA UDAKTARI INDIA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mwanamke wa kwanza kutunikiwa  Shahada ya  Heshima ya Udaktari wa Falsafa na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India na kuitoa shahada hiyo kwa Watoto  wa  kike wanaoishi  katika  mazingira magumu nchini.


Akiipokea Shahada hiyo, ambayo ni ya kwanza kwake kutoka ugenini,  Rais  Samia amesema anakishukuru Chuo  hicho kwa heshima hiyo ambayo ni kubwa na kwamba anaitoa kwa watoto wa kike wa Tanzania  wanaoishi katika mazingira magumu na pembezoni  mwa nchi ambapo amewaka  kutokukata tamaa kutokana na mazingira waliyopo na kuitaka jamii kushirikiana kuwawezesha watoto hao kufikia ndoto zao.



"Mimi ni matokeo ya jozi nyingi za macho na mikono ya watu walioona uwezo ndani yangu wakanilea na kunishika mkono," amesisitiza Rais  Dkt. Samia.



Ameeleza kuwa ameitoa tuzo hiyo kwa watoto hao kutokana na mazingira halisi aliyopitia tangu akiwa shule ya msingi hadi kufikia nafasi aliyonayo nayo sasa.

 

Pia amesema anawashukuru watu mbalimbali wakiwemo wazazi wake, familia, Chama cha Mapinduzi na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwa mchango wao uliomwezesha kufikia hatua hiyo muhimu katika maisha.

 

“Shahada hii inanikumbusha mbali nikiwa mtoto mdogo nikienda shule katika kijiji nilichozaliwa cha Kizimkazi huko Unguja, Zanzibar, huku mama yangu akiwa ni mama wa nyumbani  na baba mwalimu. Nawashukuru kwa kunipatia muda ulioniwezesha kufikia ndoto zangu za elimu, siasa na hatimaye kufikia nafasi niliyo nayo sasa" amesema Rais Dkt. Samia.



Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Santishree Dhulipudi Pandit amesema Chuo hicho kimetunuku Mhe. Rais Samia  Shahada hiyo kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na India, Diplomasia ya Uchumi, mchango wake katika maisha ya kila siku ya wananchi wa Tanzania na mafanikio yake kikanda na kimataifa.

 

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa India Mhe.  Dkt. Subrahmanyam Jaishankar ameielezea Shahada hiyo kama alama ya kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na India.

 

Taarifa kutoka chuoni hapo zinasema kuwa, Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1969, ni viongozi wawili tu ambao wamewahi kutunukiwa shahada hiyo, Rais wa Russia Vladmir Putin pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Hayati Shinzo Abe. 


 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan akitunikiwa Shahada ya  Heshima ya Udaktari wa Falsafa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India, Prof. Santishree Dhulipudi Pandit. Mhe. Rais Dkt. Samia ameitoa Shahada hiyo kwa watoto wa kike nchini ili kuwapa moyo wa kuendelea na jitihada mbalimbali kwa ajili ya mafanikio yao ya baadaye. Mhe. Rais Dkt. Samia anakuwa  mwanamke wa kwanza kupata shahada hiyo kutoka Chuo hicho.

Mhe. Rais Dkt. Samia akizungumza mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari
Viongozi mbalimbali walioshiriki hafla ya Mhe. Rais Dkt. Samia ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari
Sehemu nyingine ya viongozi
Sehemu ya ujumbe wa India


Sehemu nyingine ya ujumbe wa India