Monday, October 23, 2023

TANZANIA YAPONGEZWA KWA KUWEKA MIFUMO SHIRIKISHI KATIKA KUIMARISHA HAKI ZA BINADAMU NA WATU

Mwenyekiti  wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutengeneza mifumo shirikishi yenye lengo la kukuza na kuimarisha haki za binadamu na watu nchini.

 

Mhe. Jaji Mwaimu ametoa pongezi hizo leo tarehe 23 Oktoba 2023 wakati akihutubia wajumbe wa Kikao cha Kawaida cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachoendelea jijini Arusha.

 

Mhe. Jaji Mwaimu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanikiwa kuweka mifumo shirikishi inayowezesha wadau mbalimbali kujadili mambo muhimu ya kitaifa ikiwemo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ikiwa ni jitihada za Serikali za kuensdelea kuimarisha na kuboresha usimamizi wa haki za binadamu na watu.

 

Akizitaja  hatua za Serikali zinazodhihirisha mwenendo mzuri wa kuimarika na kustawi kwa haki za bianadamu na Watu nchini kuwa ni pamoja na  kuwekwa mfumo shirikishi  wa kujadili mambo muhimu ya Kitaifa na kuimarika kwa demokrasia ambapo Mhe. Rais Samia aliunda Kamati Maalum kwa ajili ya kutathmini mwenendo mzima wa masuala ya siasa nchini.

 

“Tunapenda katika mkutano huu kuweka msisitizo katika masuala machache ambayo Tume imeona kwamba yana mwelekeo chanya na yamejipambanua kutokana na umuhimu wake. Kwanza ni hatua ya Serikali ya Tanzania ya kuweka mfumo shirikishi wa kujadili mambo muhimu ya kitaifa. Mfano hivi karibuni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na vyama vya siasa nchini walikaa pamoja jijini Dar es Salaam kujadili taarifa ya kamati Maalum iliyoundwa ba Mhe. Rais Dkt. Samia  kwa ajili ya kukuza mwenendo mzima wa masuala ya siasa ikiwemo demokrasia ya vyama vingi.

 

Pia amepongeza hatua ya kuzinduliwa kwa Kampeni ya miaka mitatu ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria ambayo mpaka sasa imetekelezwa kwenye mikoa mitano na kuwafikia zaidi ya wananchi 2,870 waliopo kwenye maeneo 39 ya vizuizi  na zaidi ya wananchi 361,740 waliopo uraiani wamehudumiwa kwa ukamilifu na kufaidika.

 

Amesema, miongoni mwa waliofaidika na Kampeni hii ni wahamiaji raia wa Ethiopia zaidi ya 80 ambao walirejeshwa nchini kwao baada ya kuwa vizuizini kwa changamoto za uhamiaji.

 

Mhe. Jaji Mstaafu Mwaimu pia aliutaja mchakato ulioanzishw ana Mhe. Rais Dkt. Samia wa kupitia upya mfumo wa Taasisi zinazoshughulikia masuala ya Haki Jinai kuwa ni wenye tija kubwa  na wa kupigiw amfano kwenye kuimarisha  Nyanja za haki za binadamu na watu nchini.

 

“Tume imeona suala la Mhe. Rais Dkt. Samia la kuanzisha mchakato wa kupitia upya mfumo wa taasisi zinazoshughulikia masuala ya haki jinai kuwa ni jambo kubwa na lenye tija. Mchakato huu ambao unalenga kufanya mapitio ya mnyororo mzima wa haki jinai kwa kushughulikia dosari za upatikanaji wa haki za binadamu utaleta tija na kuimarisha haki za binadamu hapa nchini pale utakapokamilika,” alisisitiza Mhe. Jaji Mwaimu.

 

Pia Tume hiyo imepongeza utayari wa Serikali wa kuanza kuandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Biashara na Haki za Binadamu ambao ukikamilika utawezesha kuingiza katika mfumo Kanuni za Umoja wa Mataifa za masuala ya Haki za Binadamu na Biashara na kuwahakikishi a Watanzania kufanya shughuli za biashara kwa namna inayozingatia na kuhifadhi haki za binadamu.

 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni Idara huru ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2001 ambayo pamoja na mambo mengine husimamia utekelezaji wa haki za binadamu na watu nchini.

 

Kikao cha Kawaida cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kilifunguliwa rasmi tarehe 20 Oktoba 2023 na kinatarajiwa kumalizika tarehe 09 Novemba, 2023


Mwenyekiti  wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akizungumza wakati wa Kikao cha Kawaida cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachoendelea jijini Arusha.  Katika hotuba yake Mhe. Jaji Mwaimu ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuanzisha mifumo shirikishi ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha masuala ya haki za binadamu na watu na demokrasia nchini. Kikao cha 77 kilifunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi tarehe 20 Oktoba 2023 na kitamalizika tarehe 09 Novemba 2023
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na watu, Mhe. Janet Ratatouille Sallah-Njie (wa tatu kushoto) akiendesha kikao cha 77 cha Tume hiyo kinachoendelea jijini Arusha.
Sehemu ya Washiriki wa Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu naWatu wakifuatilia kikao

Sehemu nyingine ya washiriki

Kikao kikiendelea


 

UN KUADHIMISHA MIAKA 78 YA KUANZISHWA KWAKE

Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania unatarajia kuadhimisha miaka 78 tangu ilipoanzishwa mwaka 1945.

Akizungumza na waandishi wa Habari kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda amesema maadhimisho ya miaka 78 ya Umoja wa Mataifa yatafanyika tarehe 24 Oktoba 2023 katika viwanja vya Karemjee Jijini Dar es Salaam.

Balozi Kaganda amesema wakati UN ukiadhimisha miaka 78 tangu kuanziswa kwake, Tanzania inajivunia kuwa mwanachama wa Umoja huo na imekuwa ikifanya vizuri katika baadhi ya maeneno ya malengo ya maendeleo endelevu hususan katika masuala ya chakula, elimu, jinsia, nishati, maji, amani na usalama.

“Tanzania tunajivunia kufanya vizuri katika masuala ya chakula, elimu, jinsia, nishati, maji pamoja na amani na usalama. Lakini kuna changamoto ya umasikini ambayo imekuwa ikikabili ulimwengu na nchi zinazoendelea ambapo tunahitaji kuongeza nguvu ya kukabiliana nayo,” alisema Balozi Kaganda.

Balozi kaganda aliongeza kuwa Tanzania inajisikia fahari kama mwanachama wa UN kwa kusimamia kikamilifu misingi ya Umoja huo na kuendelea kutoa mchango wake katika kutekeleza malengo adhimu.

“Tanzania imekuwa ikishiriki kikamilifu katika operesheni za ulinzi wa amani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa, utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo, kulinda na kuchochea haki za binadamu na utawala wa sheria na kushiriki katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa, yakiwemo maendeleo endelevu yanayotekelezwa wakati huu,” alisema Balozi Kaganda.

Kwa Upande wake Mratibu Mkazi wa UN Tanzania, Bw. Zlatan Milišić alisema Umoja wa Mataifa unafurahia kuadhimisha miaka 78 tangu kuanzishwa kwake na miaka 62 ya ushirikiano kati yake na Tanzania ambapo wakati wote zimekuwa na uhusiano mzuri na imara na Tanzania imekuwa ikichangia kikamilifu katika kuchagiza ajenda ya maendeleo ya kimataifa, katika kuandaa na kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

"Tunapoadhimisha miaka 78 ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, tunatambua ushirikiano mzuri na imara kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Mataifa ambapo umekuwa ukichagiza Malengo ya Maendeleo Endelevu katika jamii," alisema Bw. Milišić.

Maadhimisho ya mwaka huu yataongozwa na kaulimbiu isemayo “Kuwekeza leo kwa ajili ya kesho kwa kuinua vijana wa Kitanzania”. Maadhimisho hayo yataongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki, (Mb.).

Mratibu Mkazi wa UN Tanzania, Bw. Zlatan Milišić akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikianmo wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam

Mratibu Mkazi wa UN Tanzania, Bw. Zlatan Milišić akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikianmo wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda. 

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikianmo wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam




Sunday, October 22, 2023

TANZANIA KUENDELEA KULINDA NA KUKUZA HAKI ZA WANAWAKE


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kukuza na kulinda haki za wanawake na kuhakikisha wananufaika na haki za binadamu na watu kwa kuzingatia matakwa ya Itifaki ya Maputo ya mwaka 2003.

 

Kauli hiyo imetolewa tarehe 22 Oktoba 2023 na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Richard Kilanga wakati akitoa maelezo ya nchi kuhusu hali ya haki za wanawake nchini ikiwa ni mwendelezo wa vikao vya Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu vinavyofanyika jijini Arusha.

 

Bw. Kilanga ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Biandamu katika Wizara hiyo, Bi. Nkasori Sarakikya amesema Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria mbalimbali zinazopinga unyanyasaji dhidi  ya wanawake ikiwemo sheria ya kupinga mila potofu ya ukeketaji wanawake.

 

Amesema katika kukabiloana na  vitendo vya ukeketaji, Serikali imeandaa na inatekeleza  Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji wa mwaka 2020/21-2024/2025 na Kanuni ya Adhabu  Sura ya 16 ambayo  imetaja ukeketaji kama kosa la jinai.

 

“Tunapongeza taarifa ya Mtaalam wa Haki za Wanawake kutoka Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na tunaunga mkono maoni na ushauri wake kwamba ukeketaji ni kati  ya mila ambazo zinamnyima mwanamke haki zake. Katika hili, Tanzania imechukua hatua mbalimbali za maksudi ili kutokomeza kabisa vitendo vya ukeketaji ikiwemo kutekeleza mpango wa taifa wa kutokomeza ukeketaji,” amesema Bw. Kilanga.

 

Pia ameongeza kusema kuwa, katika kulinda na kutetea haki za wanawake hapa nchini, Jukwaa la Kitaifa la Haki za Mwanamke lilizinduliwa tarehe 06 Juni 2023 likiwa na lengo la kurahisisha upatikanaji wa haki za mwanamke kwa wakati  kwa wanawake wa mijini na vijijini.

 

Pia amesema katika kukabiliana na na ukatili kwa wanawake na watoto Serikali imekuwa ikitekeleza  Mpango kazi wa Kitaifa wa Kuzuia Ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017/18-2021/2022. Amesema katika utekeelzaji wa mpango huu sheria mbalimbali zimetungwa ikiwemo Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21 ambapo suala hili limepata sura ya kitaifa na linatekelezwa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia.

 

Kwa upande wa Zanzibar, Serikali inatekeleza Mpango Mkakati wa Kupinga ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kwa kuanzisha Mahakama Maalum zinazoshughulikia masuala ya udhalilishaji.

 

Awali akiwasilisha Ripoti Maalum ya Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kuhusu Haki za Wanawake, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo ambaye pia ni Mtaalam wa Haki za Wanawake, Mhe. Janet Ratatouille Sallah-Njie ameipongeza Tanzania kwa jitihada mbalimbali inazochukua katika kusimamia haki za wanawake na watoto na kuitaja kuwa miongoni mwa nchi chache za Afrika zilizofanikiwa na za mfano wa kuigwa.

Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Richard Kilanga kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu wa Wizara hiyo, Bi. Nkasori Sarakikya akitoa maelezo ya nchi kuhusu hali ya haki za wanawake  wakati wa vikao vya Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu vinavyofanyika jijini Arusha. Kikao hicho kilichofanyika tarehe 22 Oktoba 2023 pamoja na mambo mengine kilipokea Taarifa ya Hali ya Haki za Wanawake barani Afrika iliyowasilishwa na Mtaalam kutoka Tume hiyo Mhe.  Mhe. Janet Ratatouille Sallah-Nji.

Saturday, October 21, 2023

RAIS DKT. SAMIA ATUNUKIWA TUZO YA HESHIMA NA TUME YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU

Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imemtunukia Tuzo ya Heshima Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wake katika kutetea, kulinda na kuimarisha haki za binadamu katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

 

Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana kwa niaba ya Mhe. Rais Samia wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu Afrika na maadhimisho ya miaka 20 ya Itifaki ya Maputo kuhusu Haki za Wanawake yaliyofanyika jijini ARusha tarehe 21 Oktoba 2023.

 

Akieleza sababu za kumtunuku Mhe. Rais Dkt Samia tuzo hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Janet Ratatouille Sallah-Njie amesema Mhe. Rais Dkt. Samia amekuwa kiongozi wa mfano barani Afrika katika kusimamia na kuimarisha haki za binadamu kuanzia ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

 

Amesema Mhe. Rais Samia amefanikiwa kusimamia haki za binadamu kwa kuimarisha usawa wa kijinsia nchini, kuimarishaupatikanaji wa huduma za afya na elimu kwa wasichana, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kupambana na ukatili wa kijinsia, kuimarisha demokrasia na maridhiano, uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa vyombo vya habari.

 

Ameongeza kusema ni bahati ya pekee kwa Afrika kuadhimisha miaka 20 ya Itifaki ya Maputo ya Haki za Wanawake kwenye ardhi ambayo Rais wake ndiye mwanamke pekee mwenye wadhifa huo wa juu barani humo.

“Hakuna namna bora ya kusherehekea miaka 20 ya Itifaki ya Maputo ya Haki za Wanawake zaidi ya kusherehekea hapa Tanzania ambapo Kiongozi  wa nchi ndiye Rais pekee mwanamke barani Afrika. Tuna kila sababu ya kumtunuku tuzo hii siyo tu kwa sababu ni mwanamke bali pia ni kutokana na hatua kubwa za maendeleo alizopiga na mchango wake kwenye masuala ya haki za binadamu nchini kwake na kwenye medani za kimataifa,” amesisitiza Mhe. Sallah-Njie

 

Amesema nafasi ya Rais Samia ambaye anasismama kama balozi wa usawa wa kijinsia duniani ni chachu na mfano wa kuigwa kwa wanawake na wasichana wa Afrika katika kuwahamasisha na kuwatia moyo katika kufanyia kazi ndoto zao kwa kushinda vikwazo mbalimbali na kwamba wana uwezo wa kushika nafasi kubwa na za juu za uongozi.

 

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo,  Mhe. Balozi Dkt. Chana ameishukuru Tume hiyo kwa kumtunuku tuzo Mhe. Rais Dkt. Samia na kumuelezea Mhe. Rais kama mwanamke kiongozi shujaa, mtetezi wa haki za binadamu na watu, mchapakazi na mtoto wa Afrika ambaye ni mwelewa na ameleta maendeleo nchini.

 

Amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia kumekuwa na kasi kubwa katika kuleta maendeleo na kuwezesha mifumo ya upatikanaji haki kwenye Nyanja mbalimbali ikiwemo utoaji wa haki huru, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kuabudu, uhakika wa chakula, kuwawezesha vijana kujiajiri, uwezeshaji wanawake na kuanzishwa kwa mpango wa msaada wa kisheria wa Dkt. Samia.

 

Pia amesema katika kipindi hiki cha awamu ya sita ya Mhe. Dkt. Samia idadi ya wanawake katika vyombo vya utoaji maamuzi ikiwemo Mahakama, Bunge na Serikalini kwa ujumla imeongezeka.

 

“Mhe. Dkt. Samia mara baada ya kuingia madarakani alianzisha falsafa ya R4 kwa maana ya maridhiano na upatanishi, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi mpya. Huu ni utaratibu wenye lengo la kustawisha na kudumisha amani, umoja, undugu na maridhiano kwa wananchi ili kuchocea maendeleo,” amesema Mhe. Balozi Chana.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akipokea Tuzo ya Heshima kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Afrika ya Haki za Biandamu na Watu, Mhe. Janet Ratatouille Sallah-Njie (kulia). Tume hiyo imemtunukia tuzo hiyo Mhe. Dkt. Samia kwa kutambua mchango wake kwenye masuala ya haki za binadamu na watu hususan katika kuimarisha usawa wa kijinsia  na demokrasia. Tuzo hiyo imetolewa jijini Arusha wakati wa Kikao cha 77 cha tume hiyo kinachoendelea jijini hapa.
Mhe. Balozi Chana akizungumza mara baada ya kupokea Tuzo kwa niaba ya Mhe. Rais Dkt. Samia

Mhe. Dkt Chana akizungumza