Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) amemuaga Balozi wa Australia nchini mwenye makazi yake nchini Kenya, Mhe. Luke Williams baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi.
Akizungumza na Mhe. Balozi Williams walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, Waziri Mbarouk amesema Tanzania na Australia zimekuwa na uhusiano mzuri uliowezesha mataifa hayo kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta za elimu, utalii, madini, nishati, mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na biashara na uwekezaji.
Waziri Mbarouk ameongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Australia ni jambo lililochochewa na kazi nzuri iliyofanywa na Balozi Williams wakati akitekeleza majukumu yake ya kibalozi.
“Katika kipindi chako umeiwakilisha vyema Australia na kuonesha mafanikio makubwa ambayo yamefikiwa kati ya Tanzania na Australia.
Kazi yako imechochea uboreshaji wa sekta za elimu, utalii, madini, nishati, uchumi wa buluu na kuchangia ukuaji wa sekta ya biashara uwekezaji katika nchi zetu, ni matumaini yangu kuwa utaendelea kuwa Balozi mwema kwa Tanzania nchini Australia na kokote uendako Duniani,” amesema Balozi Mbarouk.
Balozi Mbarouk ameongeza kuwa Australia imekuwa ikitoa fursa za ufadhili wa masomo katika sekta mbalimbali, ila kwa sasa Tanzania inaomba fursa hizo zijikite zaidi katika sekta ya nishati.
Pamoja na mambo mengine, Balozi Mbarouk amemueleza Balozi Williams kuwa kwa sasa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kiasi kikubwa na kuwaalika wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Australia kuja kuwekeza kwa wingi nchini.