Mjasiriamali kutoka Tanzania ameibuka mshindi wa kwanza wa jumla kwenye Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi/Juakali yaliyomalizika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 15 Desemba 2023.
Mshindi wa pili ametokea Kenya huku mshindi wa tatu akitokea Uganda.
Mjasiriamali huyo, Dkt. Herieth Mkangaa maarufu kama Mama batiki ambaye
anamiliki Kampuni ya kutengeneza Batiki ya MoroBatiki ya mkoani Morogoro
ametangazwa mshindi wakati wa ufungaji rasmi wa Maonesho hayo ambayo
yamewashirikisha wajasiriamali 1,500 kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Dkt. Mkangaa ni pia maarufu kwa kutengeneza vazi la batiki lililompatia
umaarufu la “Suti ya Samia” ikiashiria mtindo wa nguo unaopendelewa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Dkt. Mkanga amesema kuwa
amefurahia ushindi huo ambao ni mkubwa kwake na kwa Tanzania na kwamba tuzo
hiyo ni chachu kwake ya kuendelea kujituma zaidi na kutengeneza bidhaa nyingi
na zenye ubora ili kulikamata soko la Afrika Mashariki, Afrika na Duniani kwa
ujumla.
Pia amewahamasisha wajasiriamali kote nchini kujiamini na kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara, masoko na uwekezaji zinazotangazwa na Serikali ndani na nje ya nchi.
Wakati huohuo, Wajasiriamali wawili wenye ulemavu wa macho kutoka Zanzibar, Bw.
Abdul Kadir Amini Ahmed na Bw. Khamis Khamis Haji wanaojishughulisha na
utenegenezaji wa mikeka wamepongezwa na waandaji wa maonesho hayo kwa
kufanikiwa kushiriki maonesho hayo kikamilifu licha ya hali ya ulemavu waliyo
nayo huku jamii ikitakiwa kuiga mfano wao wa kujituma katika kazi badala ya
kutegemea kuomba kusaidiwa.
Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ambayo yamebeba Kaulimbiu isemayo “Kuunganisha Wajasiriamali Wadogo
na wa Kati wa Afrika Mashariki kufanya biashara katika Eneo la Afrika Mashariki”
hufanyika kila mwaka kwa utaratibu wa mzunguko kutoka nchi moja kwenda nchi
nyingine ambapo maonesho ya 24 yanatarajiwa kufanyika nchini Sudan Kusini mwaka
2024.
Sehemu ya wadau mbalimbali walioshiriki hafla ya ufungaji wa maonesho hayo |
Jukwaa kuu |
Bi. Kisa akipokea zawadi ya mkeka mdogo kutoka kwa wajasiriamali wenye ulemavu wa macho kutoka Zanzibar |
Kikundi cha ngoma maarufu ya Burundi wakitumbuiza wakati wa hafla ya kufunga maonesho hayo |
Shamrashamra za ushindi zikiendelea |