Mjasiriamali kutoka
Tanzania ameibuka mshindi wa kwanza wa jumla kwenye Maonesho ya 23 ya
Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu
Kazi/Juakali yaliyomalizika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 15 Desemba 2023.
Mshindi
wa pili ametokea Kenya huku mshindi wa tatu akitokea Uganda.
Mjasiriamali huyo, Dkt. Herieth Mkangaa maarufu kama Mama batiki ambaye
anamiliki Kampuni ya kutengeneza Batiki ya MoroBatiki ya mkoani Morogoro
ametangazwa mshindi wakati wa ufungaji rasmi wa Maonesho hayo ambayo
yamewashirikisha wajasiriamali 1,500 kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Dkt. Mkangaa ni pia maarufu kwa kutengeneza vazi la batiki lililompatia
umaarufu la “Suti ya Samia” ikiashiria mtindo wa nguo unaopendelewa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Dkt. Mkanga amesema kuwa
amefurahia ushindi huo ambao ni mkubwa kwake na kwa Tanzania na kwamba tuzo
hiyo ni chachu kwake ya kuendelea kujituma zaidi na kutengeneza bidhaa nyingi
na zenye ubora ili kulikamata soko la Afrika Mashariki, Afrika na Duniani kwa
ujumla.
Pia amewahamasisha wajasiriamali kote nchini kujiamini na kuchangamkia fursa
mbalimbali za biashara, masoko na uwekezaji zinazotangazwa na Serikali
ndani na nje ya nchi.
Wakati huohuo, Wajasiriamali wawili wenye ulemavu wa macho kutoka Zanzibar, Bw.
Abdul Kadir Amini Ahmed na Bw. Khamis Khamis Haji wanaojishughulisha na
utenegenezaji wa mikeka wamepongezwa na waandaji wa maonesho hayo kwa
kufanikiwa kushiriki maonesho hayo kikamilifu licha ya hali ya ulemavu waliyo
nayo huku jamii ikitakiwa kuiga mfano wao wa kujituma katika kazi badala ya
kutegemea kuomba kusaidiwa.
Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ambayo yamebeba Kaulimbiu isemayo “Kuunganisha Wajasiriamali Wadogo
na wa Kati wa Afrika Mashariki kufanya biashara katika Eneo la Afrika Mashariki”
hufanyika kila mwaka kwa utaratibu wa mzunguko kutoka nchi moja kwenda nchi
nyingine ambapo maonesho ya 24 yanatarajiwa kufanyika nchini Sudan Kusini mwaka
2024.
|
Waziri wa Viwanda, Biashara, Uchukuzi na Utalii wa Burundi, Mhe. Nijimbere Marie Chantal akimakibidhi tuzo Mshindi wa kwanza wa jumla wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali wadogo na wa kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Dkt. Herieth Mkangaa baada ya kuibuka mshindi kutokana na kuonesha bidhaa zenye ubora aina ya Batiki. Mshindi wa pili ametoka Kenya na mshindi wa tatu ametokea Uganda. Maonesho hayo ambayo yamefanyika jijini Bujumbura, Burundi kuanzia tarehe 05 hadi 15 Desemba 2023 yamewashirikisha Wajasiriamali 1,500 kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo.
|
|
Mgeni Rasmi ambaye pia ni Waziri wa Viwanda, Biashara, Uchukuzi na Utalii wa Burundi, Mhe. Nijimbere Marie Chantal akizungumza wakati wa hafla ya ufungaji wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofanyika jijini Bujumbura kuanzia tarehe 05 hadi 15 Desemba 2023
|
|
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Bi. Kisa akizungumza kwa niaba ya ujumbe wa Tanzania kwenye hafala ya ufungaji wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofanyika jijini Bujumbura kuanzia tarehe 05 hadi 15 Desemba 2023
|
|
Mgeni Rasmi ambaye pia ni Waziri wa Viwanda, Biashara, Uchukuzi na Utalii wa Burundi, Mhe. Nijimbere Marie Chantal akiwa katika picha ya pamoja na Wajasiriamali wenye ulemavu wa macho kutoka Zanzibar. Wajasiriamali hao Bw. Khamis Khamis Haji (katikati) na Bw. AbdulKadir Amini Ahmed wamepongezwa na waandaaji wa maonesho hayo kwa kushiriki kikamilifu.
|
|
Mshindi wa Kwanza wa jumla na wa kwanza katika kundi la Tanzania wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Herieth Mkangaa (katikati) akiwa na washindi wengine kutoka kundi la Tanzania ambao ni mshindi wa pili Bi. Aisha Rutta (kulia) kutoka Kampuni ya Komati ya Mkoani Pwani inayojishughulisha na utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na Nazi na mshindi wa tatu Bi. Mwanahamisi Rashidi anayejishughulisha na utengenezaji wa majiko kutoka Umoja wa Wajasiriamali wa Tabora
|
|
Sehemu ya wadau mbalimbali walioshiriki hafla ya ufungaji wa maonesho hayo |
|
Jukwaa kuu
|
|
Bi. Kisa akipokea zawadi ya mkeka mdogo kutoka kwa wajasiriamali wenye ulemavu wa macho kutoka Zanzibar
|
|
Naibu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Fedha na
Biashara, Bi. Annette Mutaawe akimkabidhi Mjumbe wa Sudan Kusini bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kama ishara ya kuikabidhi rasmi nchi hiyo jukumu la kuandaa Maonesho ya 24 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya hiyo yatakayofanyika nchini humo mwaka 2024
|
|
Kikundi cha ngoma maarufu ya Burundi wakitumbuiza wakati wa hafla ya kufunga maonesho hayo
|
|
Wadau kutoka Tanzania wakishangilia baada ya kutangazwa kwa Mshindi wa kwanza wa jumla wa maonesho ya 23 ya wajasiriamali wadogo na wa kati wa Jumuiaya ya Afrika Mashariki, Dkt. Herieth Mkangaa kutoka Tanzania
|
|
Shamrashamra za ushindi zikiendelea
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.