Thursday, December 7, 2023

BALOZI KIBESSE AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA RAIS RUTO

Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Bernard Kibesse amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto, katika hafla iliyofanyika Ikulu, Nairobi tarehe 7 Disemba 2023. 

Wakati akiwasilisha Hati zake za Utambulisho, Mhe. Balozi Kibesse alimshukuru Mhe. Rais Ruto kwa kuridhia uteuzi wake kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya na kuahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na Kenya.

Kwa upande wa Mhe. Rais Ruto alimkaribisha Mhe. Balozi Kibesse na kueleza kwamba amekuwa na ushirikiano mzuri na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika masuala ya kitaifa na kimataifa. Amemtakia heri Balozi Kibesse na kueleza kwamba yupo tayari kushirikiana naye katika kufanikisha majukumu yake ya kuiwakilisha Tanzania nchini Kenya

Aidha, katika mazungumzo yao, viongozi hao wamekubaliana kuongeza juhudi katika kuboresha biashara kati ya Tanzania na Kenya zikiwa ni nchi majirani na rafiki zenye ushirikiano mkubwa wa kibiashara katika muktadha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Bernard Kibesse akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto baada ya kuwasili Ikulu Jijini Nairobi, kuwasilisha Hati za Utambulisho


Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Bernard Kibesse akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto Ikulu Jijini Nairobi

Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Bernard Kibesse pamoja na Mabalozi mbalimbali baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho Ikulu Jijini Nairobi



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.