Saturday, December 9, 2023

BALOZI MWAMWETA AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Mheshimiwa Hassan Iddi Mwamweta amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Mheshimiwa Frank Walter Steinmeier katika Ikulu ya Nchi hiyo Jijini Berlin.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya Hati hizo Mheshimiwa Rais Frank Walter Steinmeier alifafanua kuwa Serikali yake inaunga mkono jitihada za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais was Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tanzania na Ujerumani zinashirikiana kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya afya; elimu; utunzaji wa mazingira; utamaduni; uhifadhi wa mazingira; utalii; biashara; uwekezaji pamoja na kubidhaisha kiswahili.

Itakumbukwa pia katika jitihada za kuimarisha ushirikiano Mheshimiwa Steinmeier alifanya ziara ya siku tatu nchini Tanzania kuanzia tarehe 30 Oktoba mpaka tarehe 1 Novemba 2023 akiwa ameambatana na ujumbe wa Makampuni mbalimbali kwa ajili ya kuangalia fursa ili kuwekeza nchini.

Pamoja na ratiba nyingine, akiwa nchini alifanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuendeleza na kukuza ushirikiano wa kijamii na kiuchumi kwa maslahi ya pande zote mbili.



Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Mheshimiwa Hassan Iddi Mwamweta (kushoto) akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Mheshimiwa Frank Walter Steinmeier katika Ikulu ya Nchi hiyo jijini Berlin

Picha ya Pamoja  Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Mheshimiwa Frank Walter Steinmeier na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Mheshimiwa Hassan Iddi Mwamweta katika Ikulu ya Ujerumani jijini Berlin.

Mheshimiwa Balozi Mwamweta (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Waandamizi wa Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kutoka katika Ofisi ya Rais na Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi hiyo.

Mhe. Balozi Mwamweta akikaribishwa katika Ikulu ya Ujerumani jinini Berlin wakati wa hafla ya kuwasilisha Hati za Utambulisho Utambulisho.

Mheshimiwa Balozi Mwamweta akisaini Kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya Ujerumani jijini Berlin.

Bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikipandishwa katika Ikulu ya Ujerumani jijini Berlini kwa heshima ya Serikali ya Tanzania wakati wa hafla ya kuwasilisha Hati za Utambulisho. 

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Mheshimiwa Hassan Iddi Mwamweta (kushoto) akijitambulisha na kuwasilisha ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Mheshimiwa Frank Walter Steinmeier katika Ikulu ya Nchi hiyo jijini Berlin.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.