Friday, December 8, 2023

NCHI WANACHAMA WA EAC ZAHIMIZWA KUWAUNGA MKONO WAJASIRIAMALI KUPUNGUZA CHANGAMOTO YA AJIRA

Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimehimizwa kuendelea kuunga mkono jitihada za kujikwamua kiuchumi zinazofanywa na wajasiriamali wadogo na wa kati ili kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana na wanawake na kukuza uchumi wa nchi hizo.

 

Rai hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Burundi, Mhe. Prosper Bazombaza leo tarehe 08 Desemba 2023 jijini Bujumbura, Burundi wakati akifungua rasmi Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayoendelea jijini hapa kuanzia tarehe 05 hadi 15 Desemba 2023.

 

Amesema Nchi Wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaweza kujikwamua katika  changamoto ya ajira kwa vijana na wanawake kwa kuandaa mazingira yanawezesha makundi hayo kujiajiri ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarisha na kuboresha  Maonesho ya Wajasiriamali wadogo na wakati maarufu kama Nguvu Kazi/Jua Kali ili kuwa na tija zaidi kwa maslahi mapana ya wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

 Ameongeza kusema kuwa maonesho hayo  ambayo yalianza kufanyika mwaka 1999 pamoja na mambo mengine yanalenga kupunguza umaskini kwa kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake pamoja na kukuza uchumi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wakati kutumia jukwaa hilo kukutana, kubadilishana uzoefu, kuuza bidhaa zao na kukuza ujuzi na teknolojia.

 

Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maoenesho hayo, Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania ambaye pia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha Wajasiriamali 259 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania kushiriki Maonesho hayo ambayo yamewawezesha kutambulika kimataifa na kupata soko kwa bidhaa na huduma mbalimbali walizo nazo.

 

Ameongeza kuwa, Serikali ya Tanzania itaendelea kuwawezesha Wajasiriamali wadogo kuendelea kushiriki katika fursa maonesho ya aina hiyo ili kuwa sehemu ya kuboresha mazingira yao ya biashara na kuongeza ajira.

 

“Nimezungumza na wajasiriamali wengi wa Tanzania waliopo hapa Burundi na wengi wao wamenieleza kuwa wamepata kazi ya kuuza bidhaa zao katika baadhi ya Nchi za Afrika Mashariki ikiwemo kina mama kutoka Kigoma wanaotengeza Chaki wamepata zabuni ya kupeleka Chaki hizo nchini Congo na Uganda. Hivyo kupitia maonesho haya tunawaonesha Watanzania wenzetu kwamba fursa ni nyingi na wazichangamkie amesema Mhandisi Luhemeja.

 

Naye Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Gelasius Byakanwa amewapongeza na kuwashukuru Wajasiriamali walioshiriki maonesho hayo na kutoka wito kwa wajasiriamali wengine kuendelea  kushiriki maonesho hayo kwani ni fursa ya kuyafikia masoko na kupata uzoefu na kujifunza ubunifu kutoka kwa wajasiriamali wengine wanaoshiriki.

 

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Fedha na Biashara, Bi. Annette Mutaawe ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo kwenye ufunguzi wa maonesho hayo amesema kuwa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo itaendelea kuboresha maonesho hayo ambapo wajasiriamali hao wanachangia kupunguza changamoto ya ajira kwa asilimia 65 na pato la kanda kwa asilimia 15.

 

Akizungumza kwa niaba ya Wajasiriamali hao, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati Afrika Mashariki,  Bw. Josephat Rweyemamu amezishukuru Serikali zinazounda Nchi Wanachama kwa kuwewawezesha kushiriki na kusisitiza umuhimu wa nchi  hizo  wanachama kufanyia kazi changamoto chache zilizopo ili kuboresha biashara miongoni mwa watu wake ikiwemo kuwa na sarafu moja ili kurahisisha biashara pamoja na kuendelea kukuza lugha ya Kiswahili kwa kukifanya kuwa lugha ya biashara.

 

Wakati wa ufunguzi huo, washiriki walishuhudia uzinduzi rasmi wa Mfumo wa Kielektroniki  wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Kutoa taarifa na kufuatilia uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Forodha ambao pamoja na mambo mengine unalenga kurahisisha ufanyaji biashara baina ya nchi wanachama hususan kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.

 

Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo yamebeba Kaulimbiu isemayo “Kuunganisha Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki kufanya biashara katika Eneo la Afrika Mashariki” yamehudhuriwa na zaidi ya wajasiriamali 1,000 kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Makamu wa Rais wa Burundi, Mhe. Prosper Bazombaza akitoa hotuba tarehe 08 Desemba 2023 wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Bujumbura tarehe 08 Desemba 2023. Maonesho hayo ambayo yamewashirikisha wajasiriamali zaidi ya 1,000 kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yanafanyika kuanzia tarehe 05 hadi 15 Desemba 2023.

Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali wadodgo na wa kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonesho hayo yanayofanyika jijini Bujumbura, Burundi kuanzia tarehe 05 hadi 15 Desemba 2023
Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Gelasius Byakanwa akishiriki  hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati yanayofanyika jijini Bujumbura
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakishiriki hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati yanayofanyika jijini Bujumbura

Makamu wa Rais wa Burundi, Mhe. Prosper Bazombaza  akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kutembelea banda la Tanzania mara baada ya kufungua rasmi Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayofanyika ijini Bujumbur. Wanaoshuhudia ni Mhandisi Luhemeja (kushoto) na Mhe. Balozi Byakanwa

Makamu wa Rais wa Burundi, Mhe. Prosper Bazombaza akiwa kwenye picha ya pamoja na Mhe. Mhandisi Luhemeja, Mhe. Balozi Byakanwa na wageni wengine walioshiriki ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mhe. Mhandisi Luhemeja akisalimiana na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati Afrika Mashariki,  Bw. Josephat Rweyemamu alipotembelea Banda la Tanzania

Mhe. Balozi Byakanwa akiteta jambo na Mhe. Mhandisi Luhemeja

Mhe. Mhandisi Luhemeja akizungumza na mmoja wa wajasiriamali kutoka Tanzania anayeshiriki Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali wadogo na wa kati maarfu kama Nguvu Kazi/Jua Kali alipotembelea mabanda ya wajasiriamali hao jijini Bujumbura


Mhe. Mhandisi Luhemeja akiwa na Mhe. Balozi Byakanwa wakizungumza na mmoja wa wajasiriamali anayeshiriki Maonesho ya 23 ya ajasiriamali wadogo na wa kati yanayoendelea jijini Bujumbura

Mhe. Balozi Byakanwa akisaini kitabu cha wageni alipotembelea Banda la Maonesho la Mfuko wa Taifa wa Jamii (NSSF). Mfuko huo unashiriki ili kuhamasisha Diaspora wa Tanzania waliopo Burundi kujiunga na huduma mbalimbali zinazotolewa kwao na mfuko huo

Picha ya pamoja











 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.