Sunday, January 21, 2024

DIPLOMASIA YA TANZANIA YAZIDI KUNG’ARA KIMATAIFA

Diplomasia ya Tanzania imezidi kung’ara kimataifa kufuatia viongozi wakuu kutoka mataifa mbalimbali kufanya ziara nchini kwa lengo la kuimarisha na kudumisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na mataifa hayo. 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), alipozungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam. 

Akielezea ziara za viongozi hao nchini Waziri Makamba amesema  tarehe 22 Januari 2024 atawasili Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na Mjumbe wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China, Mhe. Liu Guozhong ambaye atakuwa nchini tarehe 22 - 24 Januari , 2024.

“Mara baada ya kuwasili nchini, kiongozi huyo anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mb.), pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko (Mb.),” alisema Waziri Makamba. 

Amesema Kiongozi mwingine mkuu anayetarajiwa kuwasili nchini ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mheshimiwa Salvador Valdes Mesa, ambaye atafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 23 – 25 Januari, 2024. Pamoja na mambo mengine, ziara hiyo imelenga kuendelea kudumisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Cuba. 

Waziri Makamba, amesema Mheshimiwa Mesa anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Husein Ali Mwinyi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Tulia Akson.

Pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Mesa atamtembelea Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere na kushiriki mkutano wa wanachama wa urafiki kati ya Tanzania na Cuba, Watanzania waliosoma Cuba na Taasisi ya Pan African Movement na kutembelea kiwanda kinachozalisha dawa za viuadudu ya Biolarvicide cha Kibaha, Pwani.

Kiongozi mwingine anayetarajiwa kuwasili nchini ni Rais wa Jamhuri ya Poland, Mheshimiwa Andrzej Duda  atakayewasili nchini kwa ziara ya kikazi tarahe 8 – 9 Februari 2024. 

Akiwa nchini, Mheshimiwa Duda atakutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo lengo la ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Poland.

Amesema Tanzania na Poland zinashirikiana katika miradi ya maendeleo ya miundombinu, uhifadhi wa wanyama pori, elimu, maji,  usimamizi wa mazingira, utalii, biashara, uwekezaji na ushirikiano wa mabunge.

Aidha, ziara hiyo inatarajia kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano katika maeneo ya ulinzi na usalama, nishati na gesi, madini, usafiri, ulinzi wa mitandao, utamaduni na uchumi wa buluu.

Mbali na viongozi wakuu wa mataifa tajwa kufanya ziara nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan atafanya ziara ya Kitaifa nchini Indonesia kuanzia tarehe 24 – 26 Januari 2024, kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mheshimiwa Joko Widodo. Ziara hiyo ya Kitaifa inafuatia ziara ya Kitaifa ya Rais Joko Widodo aliyoifanya nchini Tanzania mwezi Agosti 2023. 

“Ziara hii inalenga kukukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Indonesia kupitia sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji, kilimo, nishati, madini, mifugo, uvuvi, uchumi wa buluu, elimu, utalii na ulinzi,” aliongeza Waziri Makamba.

Kadhalika, Waziri Makamba amewaeleza waandishi kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia pia kufanya Ziara ya Kitaifa Vatican tarehe 11 – 12 Februari, 2024 kufuatia mwaliko wa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Papa Francis.

Waziri Makamba ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Vatican, atakuwa na mazungumzo na Baba Mtakatifu Papa Francis pamoja na Katibu wa Vatican, Mhe. Pietro Parolin. Uhusiano kati ya Tanzania na Vatican ulianza miaka ya 1960 wakati ambapo Vatican ilianzisha Ubalozi wake hapa nchini. 

Tangu wakati huo Vatican kupitia Kanisa Katoliki imekuwa mstari wa mbele katika kujishughulisha na masuala ya kiroho, amani, elimu na program za afya. Kwenye ziara hiyo Mhe. Rais Samia ataongozana na wawakilishi watano wa waumini wa Kanisa Katoliki Tanzania kutoka kwenye jumuiya mbalimbali za kanisa hilo. 

Amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan atafanya ziara ya Kitaifa nchini Norway, tarehe 13-14 Februari 2024 kufuatia mwaliko kutoka kwa Mfalme Herald wa Norway na Malkia Sonja. Ameongeza kuwa ziara hiyo inafanyika ikiwa ni miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Norway.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa na mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Norway akiwemo Mfalme Herald. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Rais pia atashiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Norway pamoja na Kongamano la Nishati la Oslo,” alisema Waziri Makamba

Tanzania na Norway zinashirikiana kupitia sekta mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, nishati kama mafuta na gesi, elimu na masuala ya kodi na utawala bora.

Kuanzia mwaka 2010, Serikali ya Norway imekua ikishirikiana na Tanzania kwenye programu mbalimbali za maendeleo zilizo gharimu takribani TZS. 300 bilioni. Programu hizo zimesaidia na kuimarisha sekta muhimu za kiuchumi ikiwa ni pamoja na Sekta ya Nishati; Sekta ya Elimu; Sekta ya Mafuta na Gesi; Mpango wa Usimamizi wa Fedha za Umma; programu za Mabadiliko ya Tabianchi; na programu za Usimamizi wa Misitu.

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anaandika historia kupitia ziara hii nchini humo kwani mara ya mwisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutembelea nchi hiyo kwa Ziara ya Kitaifa ilikua mwaka 1976.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam. Mkutano huo umehudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa na Wakurugenzi wa Idara na Vitengo vya Wizara.



Saturday, January 20, 2024

VITU LAZIMA VITOKEE, WAZIRI MAKAMBA

“Vitu lazima vitokee", ni msemo ambao ameutumia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) alipokutana na Mawaziri wenzake jijini Kampala, Uganda pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) na Mkutano wa Kundi la Nchi 77+China tarehe 15 hadi 22 Januari 2024.

Waziri Makamba ambaye alishiriki kwa siku tatu katika Mikutano hiyo alikutana na Mawaziri 17 kutoka nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na nchi hizo na kuweka mikakati ya kushirikiana kiuchumi kwa manufaa ya pande zote.

Waziri Makamba aliifanya Mikutano hiyo ambayo imekusanya takriban theluthi mbili ya nchi zote duniani kama fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania kidiplomasia na kujadili mikakati na nyenzo za kujiletea maendeleo na kutatua changamoto zinazoikabili dunia.

Mawaziri wa Mambo ya Nje waliokutana na Mhe. Makamba wanatoka nchi za Kenya, Msumbiji, Somalia, Malawi, Misri, Ghana, Morocco, Filipino, Ethiopia, Singapore, Vietnam, Cuba, Iraq, Bahamas, Venezuela, Jamhuri ya Kidemokrsia ya Congo na Azerbaijan.

Masuala muhimu ambayo Waziri Makamba ameyasisitiza kwa mawaziri wenzake ni kutumia nyezo za kawaida za kidiplomasia kukuza ushirikiano baina ya mataifa yao. Nyenzo hizo ni pamoja na Midahalo ya Kisiasa, Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano (JPCs), Mikutano ya Majukwaa ya Kiuchumi, Tume za Pamoja za Mawaziri (JMCs) na ziara za viongozi wa kitaifa.

Mhe. Makamba amesema kuwa endapo vyombo hivyo vitatumika ipasavyo vitatoa fursa kwa pande husika kukuza biashara, uwekezaji, utalii pamoja na kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa masuala ambayo pande husika zimekubaliana.

Wakati wa mazungumzo na Mawaziri wa nchi za Singapore, Vietnam na Filipino, Mhe. Makamba alisema nchi hizo ni mfano wa kuigwa na nchi zinazoendelea duniani kutokana na kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kipindi kifupi.

Alikubaliana na mawaziri wa nchi hizo kushirikiana katika mafunzo, hususan, kueendeleza rasilimali watu, utalii na kilimo.

Jambo lingine lililojitokeza ni ushirikiano katika ujenzi wa miundombinu na usafiri wa anga wa moja kwa moja baina ya mataifa. Waheshimiwa Mawaziri walijiridhisha bila shaka kuwa ukosefu wa miundombinu unakwamisha ufanyaji wa biashara na kuongeza gharama katika uzalishaji, hivyo wamesisitiza kutumia rasilimali za nchi zao kujiletea maendeleo.   

Aidha, Mhe. Waziri alisisitiza umuhimu wa kutafuta suluhu kwa njia za kidiplomasia panapotokea migogoro ya kisiasa na aliwahakikishia viongozi wenzake kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi nyingine katika utatuzi wa migogoro na ujenzi wa amani duniani.

Waziri Makamba katika kusimamia msemo wake wa “Vitu lazima vitokee" alikubaliana na viongozi wenzake kufufua makubaliano ya ushirikiano waliyojiwekea ili kuongeza kasi ya utekelezaji na kunzisha ushirikiano rasmi na nchi ambazo Tanzania haina mikataba rasmi ya ushirikiano.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf. Mazungumzo hayo yalifanyika pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Mchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) uliofanyika Kampala, Uganda tarehe 15 hadi 20 Januari 2024.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Mhe. Shirley Ayorkor Botchwey
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Mhe. Veronica Macamo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore, Mhe. . Dkt. Mohamad Maliki Bin Osman
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Eduardo Rodriguez Parrilla

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Vietnam, Mhe. Do Hung Viet

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Sameh Shoukry
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. Musalia Mudavadi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mhe. Christophe Lutundula
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Simalia, Mhe.  Ali Mohammed Omar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Uhamiaji na Bima ya Taifa wa Bahamas, Mhe. Alfred Sears.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Aberzaijan, Mhe.  Jeyhun Bayra.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Mhe. Mesganu Moach.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco, Mhe. Nasser Bourita
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Philipino, Mhe. Enrique A. Manalo,

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb), akibadilishana mawasiliano na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Mhe. Omer Ahmed Berzinji.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Nancy Tembo



Thursday, January 18, 2024

BALOZI NAIMI AZIZI AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO UNIDO


Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Austria, Mheshimiwa Naimi Aziz amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), Mhe. Gerd Müller, tarehe 18 Januari, 2024. Katika mazungumzo yao, wamekubaliana kuimarisha na kudumisha ushirikiano kati ya Tanzania na UNIDO hususan katika maendeleo ya viwanda.


Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania  Austria, Mhe. Naimi Aziz akiwa kwenye picha ya pamoja na  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Mhe. Gerd Müller.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania  Austria, Mhe. Naimi Aziz akiwa kwenye picha ya pamoja na  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Mhe. Gerd Müller.


Tuesday, January 16, 2024

TANZANIA, ANGOLA ZASAINI HATI ZA MAKUBALIANO KUONGEZA USHIRIKIANO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Angola zimesaini Hati tatu za Makubaliano ya Ushirikiano (MoUs) katika sekta ya mafuta na gesi, kuondoleana visa kwa wenye hati/pasi za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi pamoja na ushirikiano katika sekta ya afya.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakati wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Angola uliomalizika leo Zanzibar.

Waziri Makamba amesaini hati mbili za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi na kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi. Aidha, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu amesaini hati ya ushirikiano katika sekta ya afya

Mara baada ya kusaini kwa Hati hizo, Waziri Makamba alisema Tanzania na Angola zina uhusiano wa kihistoria ulioanzishwa na viongozi wakuu wa Kitaifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Agostinho Neto walianzisha uhusiano huo kwa matarajio yao kuwa uhusiano huo utoe manufaa kwa nchi zote mbili.

“Leo kupitia mkutano wetu tumesaini Hati za makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Angola. Hati hizo ni pamoja na hati ya makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi, Hati ya makubaliano ya kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi pamoja na hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya afya,” alisema Waziri Makamba.

Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya uhusiano wa kisiasa, ulinzi, elimu, afya, mafuta na gesi, uchumi wa buluu, usafiri wa anga, kubadilishana visa, kusafiri bila visa kati ya nchi zetu mbili na hatimaye tumeingia makubaliano ya ushirikiano.

Kuadhalika, viongozi hao pia wamekubaliana kuyafanyia kazi masuala mbalimbali husasan uwepo wa ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Luanda pamoja na kufanya Kongamano la bishara na uwekezaji na kuziwezesha sekta binafsi kufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano zaidi.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi António amesema Angola imefurahishwa na uamuzi wa Serikali ya Tanzania kukubali kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) na kuelezea utayari wake wa kushirikiana katika nyanja walizokubaliana kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Tanzania na Angola ni marafiki wa siku nyingi, kupitia makubaliano tuliyosaini leo tumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya mataifa yetu, tuahidi kuyatekeleza yale yote tuliyokubaliana katika mkutano wetu ili kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu,” alisema Balozi António. 

Aidha, kuhusu kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Luanda pamoja na kufanya kongamano la biashara na uwekezaji ili kuwawezesha wananchi wetu kubadilisha uzoefu na kuendelea kukuza sekta binafsi kwa mataifa yote mawili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi na kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi leo Zanzibar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakionesha Hati za Makubaliano ya Ushirikiano baada ya kuzisaini leo Zanzibar

Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Afya

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakifuatilia mkutano

Meza Kuu katika Picha ya pamoja, katikati ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António. Wengine pichani ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (wa pili kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Zambia, anayewakilisha pia Tanzania nchini Angola, Mhe. Lt Gen Mathew Edward Mkingule (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje - Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias (mwenye Kamba ya njano shingoni) na Balozi wa Angola nchini Tanzania, Mhe. Mhe. Sandro de Oliveira.





Sunday, January 14, 2024

MKUTANO WA TUME YA PAMOJA YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA ANGOLA WAANZA ZANZIBAR

Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola umeanza tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar.

Mkutano huo unafanyika katika ngazi mbili za maafisa waandamizi unaofanyika tarehe 14 — 15 Januari 2024 na ngazi ya mawaziri utafanyika tarehe 16 Januari 2024.

Mkutano huo unalenga kujadili mambo mbalimbali muhimu ya ushirikiano ya siasa, diplomasia, ulinzi, usalama, Sheria, kilimo, uchumi wa buluu, biashara na uwekezaji.

Maeneo mengine ni pamoja na maendeleo ya miundombinu, ujenzi, uchukuzi, nishati, madini, tehama na huduma za kijamii za afya, elimu, sayansi, na teknolojia ya Habari na mawasiliano. Mkutano huo pia unalenga kuibua maeneo mapya ya ushikiano ili  kuchagiza maendeleo kati ya Tanzania na Angola.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa ngazi ya Maafisa Waandamizi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa amebainisha kuwa mkutano huo utatoa fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo uchumi hususan biashara na uwekezaji, uchumi wa buluu, miundombinu na fedha. 

“Katika mkutano wetu tunategemea kujadili masuala ya uchumi hususan msingi wa diplomasia ya uchumi. Mkutano huu utatoa mipango na mikakati ya pamoja itakayoimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili,” Alisema Balozi Mussa.

Balozi Said aliongeza kuwa mkutano huo unajenga na kuendeleza misingi madhubuti ya mashirikiano katika nyanja mbalimbali na kuhakikisha kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Angola unaendelea kuimarika zaidi kwa maslahi ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias amesema mikutano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano imekuwa ikitoa fursa mbalimbali za kujadili masuala ya kisekta katika maeneo mahususi ya kipaumbele kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Mikutano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano itaendelea kujadili masuala ya kisekta katika maeneo mahususi ya ushirikiano katika nyanja za diplomasia, usalama, ulinzi na uboreshaji wa huduma za kijamii,” alisema Balozi Sardinha Dias.  

Mkutano huu umejumuisha Mabalozi, Watendaji Wakuu na Maafisa mbalimbali wa Serikali kutoka Tanzania na Angola.

Mkutano wa kwanza ulifanyika mwezi Oktoba, 1988 Jijini Dar es Salaam. Kufanyika kwa mkutano huu wa Pili kunafuatia kusainiwa kwa Hati mbili za Makubaliano (MoUs) za kuhuisha/kufufua Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) na Hati ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola mwezi Februari 2023 Addis Ababa.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa akitoa hotuba ya ufunguzi katika Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar

Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda kutoka Wizara ya Mambo ya Nje - Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias akizungumza katika Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar

Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar

Viongozi wa Meza kuu katika picha ya pamoja wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa (mwenye tai nyekundu), Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje - Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias (mwenye kamba ya njano shingoni) , Balozi wa Tanzania nchini Zambia, anayewakilisha pia Tanzania nchini Angola, Mhe. Lt Gen Mathew Edward Mkingule (wa kwanza kushoto) pamoja na Balozi wa Angola nchini Tanzania, Mhe. Sandro de Oliveira (wa kwanza kulia).

Viongozi wa Meza kuu katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar



Saturday, January 13, 2024

TANZANIA, RWANDA ZASAINI HATI YA MAKUBALIANO UENDELEZAJI WA SEKTA YA MAZIWA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini Hati ya Makubaliano ya ushirikiano katika uendelezaji wa Sekta ya Maziwa na Jamhuri ya Rwanda.

Hati hiyo imesainiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi - Tanzania, Mhe. Abdallah Ulega, (Mb.) na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda wa Rwanda, Mhe. Jen. (Rtd.) James Kabarebe tarehe 12 Januari 2024, Visiwani Zanzibar. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Ulega alisema Tanzania kwa kushirikiana na Rwanda wakifanya jitihada za pamoja za kuzalisha maziwa ya kutosha na kuyasindika wananchi watapata ajira za kutosha, kuwapatia wananchi lishe pamoja na kupunguza maradhi.

“Tukifanikiwa kuwa na uzalishaji mzuri wa maziwa tutaweza kuongeza uchumi wetu, na kuifanya biashara ya maziwa kuwa kubwa zaidi,” alisema Waziri Ulega.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda wa Rwanda, Mhe. Jen. (Rtd.) James Kabarebe alisema amefarijika na hatua hiyo iliyofikiwa kwani waliisubiri muda mrefu na ni imani yake kuwa tija kubwa itapatikana katika sekta ya maziwa kupitia ushirikiano huo.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.), Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe. 

Viongozi wengine ni Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mhe. Maj. Gen. Ramson Godwin Mwaisaka, Balozi wa Rwanda nchini, Mhe. Hererimana Fatou pamoja na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Bodi ya Maziwa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi - Tanzania, Mhe. Abdallah Ulega, (Mb.) akizungumza wakati wa hafla ya kusaini Hati ya Makubaliano ya ushirikiano katika uendelezaji wa Sekta ya Maziwa na Jamhuri ya Rwanda. Kushoto ni Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda wa Rwanda, Mhe. Jen. (Rtd.) James Kabarebe tarehe 12 Januari 2024, Visiwani Zanzibar. Wengine pichani ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.). 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi - Tanzania, Mhe. Abdallah Ulega, (Mb.) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda wa Rwanda, Mhe. Jen. (Rtd.) James Kabarebe wakisaini Hati ya Makubaliano ya ushirikiano katika uendelezaji wa Sekta ya Maziwa kati ya Tanzania na Rwanda tarehe 12 Januari 2024, Visiwani Zanzibar

Waziri wa Mifugo na Uvuvi - Tanzania, Mhe. Abdallah Ulega, (Mb.) akimpongeza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda wa Rwanda, Mhe. Jen. (Rtd.) James Kabarebe baada ya kusaini Hati ya Makubaliano ya ushirikiano katika uendelezaji wa Sekta ya Maziwa kati ya Tanzania na Rwanda tarehe 12 Januari 2024, Visiwani Zanzibar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza wakati wa Hafla ya utiaji saini Hati ya Makubaliano ya ushirikiano katika uendelezaji wa Sekta ya Maziwa kati ya Tanzania na Rwanda tarehe 12 Januari 2024, Visiwani Zanzibar

Viongozi wakiwa katika picha ya pamoja ya kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya ushirikiano katika uendelezaji wa Sekta ya Maziwa kati ya Tanzania na Rwanda tarehe 12 Januari 2024, Visiwani Zanzibar

Viongozi na badhi ya watumishi wakiwa katika picha ya pamoja ya kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya ushirikiano katika uendelezaji wa Sekta ya Maziwa kati ya Tanzania na Rwanda tarehe 12 Januari 2024, Visiwani Zanzibar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda wa Rwanda, Mhe. Jen. (Rtd.) James Kabarebe tarehe 12 Januari 2024, Visiwani Zanzibar


Friday, January 12, 2024

DKT. MWINYI AONGOZA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA MAPINDUZI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameongoza sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Maadhimisho hayo yamefanyika katika Uwanja wa New Amani Complex, Mkoa wa Mjini- Magharibi Unguja, ambapo pia imehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Sherehe za mapinduzi zimehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa mataifa jirani ambao ni Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Museveni, Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Rigathi Gachagua pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Doto Biteko.

Viongozi wengine ni pamoja na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Akson pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali zote mbili.

Akitoa salamu katika sherehe hizo, Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Museveni ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuadhimisha miaka 60 ya mapinduzi matukufu.

“Nawashukuru na kuwapongeza wazanzibar na watanzania kwa ujumla kwa kuulinda Muungano, nawasihi tuendelee kushikamana na kuwa wamoja kwani tumebaini kuwa Bara la Afrika haliwezi kuendelea bila kushikamana,” Alisema Mhe. Museveni

Naye Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa mapinduzi, na kusema kuwa kufanyika kwa Mapinduzi kumedhihirisha ushirikiano na umoja wa Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla. 

Kadhalika, Naibu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe.Rigathi Gachagua ameipongeza Zanzibar na kuwasihi kuendelea kushikamana kama kaka na dada na kuhakikisha umoja wetu hautenganishwi na jambo lolote. “Nawapongeza Wazanzibar kwa kuadhimisha miaka 60 ya mapinduzi,” alisema.

Viongozi wengine walioshiriki sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ni Waziri Mkuu wa Burundi Mhe. Gervais Ndirakobuca na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Marais wastaafu walioshiriki ni pamoja na Rais Mustaafu wa awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete, Rais wa awamu ya sita wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mhe. Aman Abeid Karume. Wengine ni Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mhe. Fredrick Sumaye, Mhe. Peter Pinda pamoja na Mawaziri mbalimbali.

Mapinduzi ya Zanzibar yalifanyika Januari 12 mwaka 1964 ambapo chama cha Afro Shirazi kwa kushirikiana na wanachama wa Chama cha Umma waliiondoa madarakani serikali ya mseto wa vyama vya Wazalendo wa Zanzibar, ZNP, na Chama cha Watu wa Zanzibar na Pemba, ZPPP na kutangaza Jamhuri ya Watu wa Zanzibar badala ya serikali ya Kisultani.

Tukio hilo lilichochea/waafrika wengi, kutanzua tatizo hilo, vyama viwili vya waafrika, Afro Shirazi Party (ASP) viliungana na Umma Party kuongeza nguvu, tarehe 12 Januari 1964, ASP ikiongozwa na John Okello, ilihamasisha wanamapinduzi wapatao 600 kuingia mji wa Zanzibar (Unguja) na kupindua Serikali ya Sultani.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwasalimia wananchi waliojitokeza kushiriki sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi akikagua gwaride katika sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi (mgeni rasmi) pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakifuatilia sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akifuatilia sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar

Rais wa Uganda Mheshimiwa Yoweri Museveni akiongea katika sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar

Rais wa Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame akiongea katika sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) pamoja na viongozi mbalimbali wakifuatilia sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar