Thursday, March 21, 2024

NAIBU WAZIRI WA USHIRIKIANO WA MAENDELEO WA SWEDEN AZURU NCHINI


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisalimiana na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse alipomlaki katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma

Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 21 – 22 Machi, 2023 na kupokelewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa jijini Dodoma.

Lengo la ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi uliopo kati ya Tanzania na Sweden. Pia kupitia ziara hiyo Serikali ya Sweden inatarajiwa kueleza dhamira ya kuongeza muda wa Mpango wa Maendeleo unaotarajiwa kafikia ukomo mwaka huu 2024.

Baada ya kuwasili Mhe. Janse amefanya mazungumzo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.) ambapo katika mazungumzo yao wamejadili juu ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za viwanda, biashara, uwekezaji na ujenzi wa miundombinu hususan uendelezaji wa mradi wa mabasi yaendayo kasi (Bus Rapid Transit Project).

Viongozi wengine aliofanya nao mazungumzo jijini Dododma ni pamoja na, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (Mb.) na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb.)

Vilevile, Mhe. Janse anatarajia kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk tarehe 22 Machi 2022 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Tanzania na Sweden zilianzisha ushirikiano tangu mwaka 1960 ambapo nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za nishati, tafiti, elimu, usimamizi wa mazingira, uchangiaji wa bajeti ya Serikali, biashara, viwanda, uwekezaji na miundombinu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisalimiana na Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mhe. Charlotta Ozaki Macias wakati wa mapokezi ya Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse jijini Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisalimiana na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse alipomlaki katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma. Kando yao ni Balozi Swahiba Mndeme, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na America
Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akijadili jambo na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse alipowasili jijini Dodoma
Picha ya Pamoja
Mazungumzo baina ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.) na  Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana yakiendelea jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana  Janse akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.) yaliyofanyika jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana  Janse yaliyofanyika jijini Dodoma
Picha ya pamoja

Tuesday, March 19, 2024


 


 

TAARIFA KWA UMMA

 

 

SEMINA MAALUM KUHUSU MPANGO WA BIASHARA WA NCHI YA UINGEREZA NA NCHI ZINAZOENDELEA KUFANYIKA TAREHE

 28 MACHI 2024, DAR ES SALAAM.

 

Dodoma, tarehe 19 Machi, 2024.

 

Semina maalum kuhusu Mpango wa Biashara wa nchi ya Uingereza na Nchi Zinazoendelea (UK Developing Countries Trading Scheme – DCTS) inatarajiwa kufanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa jijini Dar es Salaam, tarehe 28 Machi 2024, kuanzia saa 3:00 asubuhi.

 

Semina hiyo ya siku moja itafunguliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na kufungwa na Mhe. Omar Said Shabaan, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Zanzibar.

 

Semina hiyo ina lengo la kufahamisha wadau wa biashara  nchini juu ya fursa ya mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la Uingereza kupitia Mpango wa Serikali ya Uingereza wa Kufanya Biashara na Nchi Zinazoendelea uliozinduliwa mwezi Mei mwaka 2023. Tanzania ni miongoni mwa nchi 65 ambazo Uingereza imezijumuisha katika mpango huo ili kuweza kuuza bidhaa zake bila kulipa ushuru na imeingia pia katika kundi la nchi ambazo asilimia 99 ya bidhaa zake zitanufaika na msamaha wa kodi.

 

Walengwa wa semina hiyo ni wadau wa biashara wenye nia ya kuuza bidhaa za aina mbalimbali katika soko la Uingereza. Wadau wanaweza pia kushiriki katika Semina hiyo kwa njia ya mtandao, kupitia link maalum ya mtandao wa “Teams” itakayotolewa kwa watakaojisajili kupitiahttps://docs.google.com/forms/d/e/1FAIpQLSdjoGDLwkXfu9PWlV7Oc3LOnn5tRyELsimZVUaMaFhCGFB1Mw/viewform

 

Aidha, wananchi wote wanaweza kuifuatilia Semina hiyo kupitia na chaneli ya YouTube ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza ijulikanayo kama Ubalozi London (http://www.youtube.com/@ubaloziLondon).

 

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali

Sunday, March 17, 2024

TANZANIA NA ITALIA KUIMARISHA USHIRIKIANO SEKTA ZA KIMKAKATI

Serikali ya Tanzania na Italia zimeahidi kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati ambazo ni kilimo, nishati, elimu pamoja na uchumi wa buluu kwa maslahi ya pande zote mbili.

Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbaouk (Mb.) alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Balozi Riccardo Guariglia wakati wa Iftari iliyoandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania jana jioni.

Balozi Mbarouk ameipongeza Serikali ya Italia kwa kuipa Serikali ya Tanzania kipaumbele cha kuwa moja kati ya nchi nne za Bara la Afrika zitakazonufaika na mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan). “Tanzania tunaamini kuwa kupitia mpango wa Mattei ushirikiano wa kiuchumi kati yetu na Italia utazidi kuimarika,” alisema Balozi Mbarouk.

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa mpango wa mattei utainua sekta za kimkakati ambazo ni kilimo, nishati, elimu na uchumi wa buluu kwa upande wa Zanzibar, Sekta hizi zimepewa kipaumbele kufuatia umuhimu wake  katika kukuza uchumi.

Pamoja na masuala mengine Tanzania imeihakikishia Italia ushirikiano katika kuunda kamati ya kuratibu mpango wa mattei ambayo itahakikisha sekta za kimkakati zilizoainishwa katika mpango huo zinananufaika kama ilivyopangwa kwa maslahi ya pande zote mbili. 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Balozi Riccardo Guariglia alisema kuwa Italia ni rafiki wa Tanzania wa muda mrefu na mataifa hayo yamekuwa yakishirikiana katika sekta mbalimbali. Hivyo mpango wa Mattei ni moja ya njia za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya Italia na Tanzania na Afrika kwa ujumla.

“Tupo hapa kuonesha na kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika na mpango wa mattei, lakini pia kuiona Afrika ikifanikisha kuweka vipaumbele vya malengo na kutekeleza majukumu yake kupitia mpango wa mattei kwa ufanisi,” alisema Balozi Guariglia

Balozi Guariglia aliongeza kuwa lengo la mpango wa mattei ni kuendelea kuimarisha uchumi wa Bara la Afrika kwa kuzishirikisha sekta za umma na binafsi za Italia katika kufadhili mpango huo kwa maslahi ya pande zote mbili.

Mwezi Januari 2024, baada ya kumalizika kwa mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia, serikali ya nchi hiyo iliahidi kutuma ujumbe wa wataalam kutoka Chemba ya Biashara ya Italia kuja Tanzania kwa ajili ya kukutana na timu ya wataalam ya upande wa Tanzania kwa lengo la kukamilisha hatua za awali za utiaji saini wa ushirikiano za kutekeleza mpango wa mattei.

Aidha, katika kutekeleza hilo, mwezi Machi 15, 2024 Ujumbe wa Italia ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia, Mhe. Stefano Gatti ulikutana na timu ya wataalamu wa Tanzania na kuainisha sekta za kipaumbele zitakazo nufaika na mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan).

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbaouk akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Balozi Riccardo Guariglia wakati wa Iftari iliyoandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania jana jioni Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Balozi Riccardo Guariglia akiteta jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbaouk (kulia) wakati wa Iftari iliyoandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania jana jioni Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbaouk akisalimiana na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Italia wakati wa Iftari iliyoandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania jana jioni Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbaouk akistoa hotuba yake wakati wa Iftari iliyoandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania jana jioni Jijini Dar es Salaam


Friday, March 15, 2024

TANZANIA, ITALIA ZAAINISHA SEKTA ZA KIPAUMBELE MPANGO WA MATTEI

Serikali ya Tanzania na Serikali ya Italia zimekutana na kuainisha sekta za kipaumbele zitakazo nufaika na mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan). 

Sekta zinazotarajiwa kunufaika na Mpango wa Mattei ni kilimo, nishati, elimu afya na uchumi wa buluu. Akizungumza wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo (Mb,) amesema mkutano huo umelenga kujadili utekelezaji wa mpango mpya wa kimkakati wa Mattei kati ya Tanzania na Italia.

Prof. Mkumbo amesema katika mpango huo vipaumbele vikubwa vimetolewa katika sekta za elimu, kilimo, maji na nishati na kuongeza kuwa maeneo waliyobainisha yanaendena na vipaumbele vya Serikali ya Tanzania ambavyo ni elimu, afya, nishati, miundombinu na kilimo.

“Tumekubalina kuanza kutengeneza miradi kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu. Miradi hiyo inatekelezwa katika nchi nne za Afrika ambazo ni Tanzania, Ethiopia, Kenya na Uganda. Tumekubaliana kujikita katika maendeleo ya zao la kahawa,” amesema Prof. Mkumbo

Prof. Mkumbo ameongeza kuwa Tanzania imekuwa ikipambana kuongeza uzalishaji wa mazao hususan kahawa, kuongeza masoko hasa katika bara la Ulaya pamoja na kuongeza thamani katika mazao. “Hivyo kupitia Mpango wa Mattei Tanzania  itasafirisha mazao yenye thamani nje ya nchi na kuliwezesha Taifa kupata fedha za kigeni,” amesema Waziri Mkumbo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia, Mhe. Stefano Gatti amesema Mpango wa Mattei umetoa kipaumbele kwa Tanzania katika sekta ya Kilimo hususan zao la kahawa ambapo nchi hizo mbili zitaendelea kushirikiana kuendeleza zao la Kahawa.

“Sisi kama Serikali tutashirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha zao la Kahawa kutoka Tanzania tunaliongezea thamani pamoja na kuwanufaisha wakulima wa zao hilo licha ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Mhe. Gatti

Mhe. Gatti aliongeza kuwa Mpango wa Mattei utaihusisha sekta ya uchumi wa buluu – Zanzibar pamoja na kutoa elimu katika sekta zitakazo nufaika na Mpango wa Mattei.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Italia katika kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya pande zote mbili.

Mpango wa Mattei umelenga kuimarisha malengo ya maendeleo endelevu yenye lengo la kuboresha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Italia.  

“Kupitia Mpango wa Matei, Italia na bara la Afrika sasa wamekuja na dhana mpya ya ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ambayo yatakuza kiuchumi kwa viwango vya juu zaidi,” alisema Balozi Mussa.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na usshirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Marco Lombardi, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na maafisa mbalimbali waandamizi wa serikali kutoka wizara za kisekta.

Mwezi Januari 2024, Tanzania ilichaguliwa kuwa moja ya nchi za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan) ambapo kiasi cha Euro bilioni 5 za awali kilitengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. Miradi hiyo ya kipaumbele kupitia Mpango mpya wa Kimkakati wa Mattei (Mattei plan) ipo katika sekta ya nishati, elimu na kilimo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na usshirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mwenye Suti ya Kijivu) akizungumza wakati wa Mkutano wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia Jijini Dar es Salaam

Mkutano kati ya ujumbe wa Tanzania na Italia ukiendelea jijini Dar es Salaam. Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo

Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia, Mhe. Stefano Gatti akiongea wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Italia na Tanzania Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo akitioa hotuba ya ufunguzi wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia jijini Dar es Salaam 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida akichangia jambo wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia Jijini Dar es Salaam 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa akichangia jambo wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia Jijini Dar es Salaam 

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akiwasilisha mchango wake kuhusu mradi wa Mattei

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo pamoja na Ujumbe wa Italia ulioongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia, Mhe. Stefano Gatti wakiwa katika pichaa ya pamoja Jijini Dar es Salaam



WAZIRI BYABATO: IMARISHENI UHUSIANO WA TANZANIA NA KENYA, MASHIRIKA YA KIMATAIFA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.)  ametembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya na kuzungumza na watumishi wa ubalozi wa Tanzania jijini Nairobi 

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Byabato amewataka watumishi wa ubalozi huo  kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Kenya pamoja na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo jijini Nairobi. 

Alipowasili nchini Kenya, Mhe. Byabato amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini huko, Mhe. Dkt. Bernard Kibesse.

Katika hatua nyingine, Waziri Byabato amekutana na kupata chakula cha jioni na Wabunge wa Tanzania wanaoiwakilisha nchi katika Bunge la Afrika Mashariki. 

Aidha, Mhe. Byabato alitumia fursa hiyo kuwaasa na kuwakumbusha Wabunge kuendelea kuiwakililisha vyema Tanzania na kusimamia maslahi na misimamo ya nchi yetu. 

Waziri Byabato yupo Jijini Nairobi kushiriki Mkutano wa Tano Kikao cha Tatu cha Bunge la Afrika Mashariki linalofanyika Jijini Nairobi Kenya.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Bernard Kibesse alipowasili katika Ofisi za Ubalozi, Jijini Nairobi, Kenya


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato akizungumza na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Bernard Kibesse

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Bernard Kibesse pamoja na watumishi wa ubalozi


Thursday, March 14, 2024

AINA TATU MPYA ZA KAHAWA ZA TANZANIA YAZINDULIWA NCHINI JAPAN


Kampuni ya ITO EN LTD, ambayo ni kampuni tanzu ya Tully’s Co. Ltd., inayomiliki migahawa maarufu ya Tully’s Coffee, imezindua aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania, nchini Japan katika hafla iliyofayika jijini Tokyo tarehe 14 Machi, 2024. 

Aina za kinywaji hicho pendwa nchini humo kinachotokana na kahawa kutoka Tanzania ni TULLY’s COFFEE BARISTA BLACK KILIMANJARO; TULLY’S COFFEE MY HOME BLACK KILIMANJARO; na TULLY’S COFFEE BARISTA ROAST COLD BREW – KILIMANJARO BLEND. Kahawa hizo ni kutoka mkoa wa Arusha, Tarime mkoani mara na mashamba ya GDM yaliyoko Mbozi mkoani Mbeya. 

Zoezi hilo la uzinduzi lililofanyika katika Ubalozi wa Tanzania jijini Tokyo na liliongozwa na Mhe. Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan, lilimshirikisha pia Bw. Osamu Aizawa, Meneja Mkuu wa Kampuni ya ITO ENaliyeambatana na wawakilishi wa kampuni hiyo na Kampuni ya Tully’s Coffee.

Kampuni ya ITO EN Ltd. ambayo, ni kampuni tanzu ya Tully’s Coffee ni kampuni inayoongoza kwa biashara ya vinywaji nchini Japan, inamiliki migahawa ya kahawa takriban 700 nchini humo huku ikiwa imejipatia umaarufu mkubwa katika biashara ya uuzaji wa kahawa aina mbalimbali duniani. 

Hii ni mara ya pili, kwa Kampuni ya Tully’s kuzindua kahawa ya Tanzania katika migahawa yake, uzinduzi kama huu uliwahi kufanyika mwezi Juni na Agosti 2023 ukihusisha kahawa aina ya GDM full washed, GDM natural na Tarime Coffee.

Kuzinduliwa kwa aina nyingine tatu mpya za kahawa nchini Japan, kunaendelea kuleta uhakika na kuongezeka kwa soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo imejizolea umaarufu mkubwa kwa ubora na ladha ya aina yake na kupelekea kupewa jina maarufu la kibiashara la Kilimanjaro Coffee.

Kilimanjrao Coffee ni miongoni mwa bidhaa tatu za kahawa zinazopendwa zaidi Japan; na jina hilo hutumika nchini humo kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania. 

Tanzania inasifika Japan kwa kuzalisha kahawa bora aina ya Arabica (Arabica laini - full washed na Arabica ngumu - natural) inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera. 



Akizungumza katika uzinduzi huo, Balozi Baraka Luvanda alizihakikishia kampuni za Japan, uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji wanapoamua kuwekeza katika kilimo au sekta nyinginezo hapa nchini. 

Balozi Luvanda amelitaja zao la kahawa kuwa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati yanayongoza kwa kulipatia Taifa pato na kuingiza fedha za kigeni. Akitolea mfano wa Japan, alieleza kuwa kwa mwaka, Tanzania inauza kahawa yake Japan kwa wastani wa asilimia 33 ya kahawa inayolimwa nchini, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu million 15 (tani 15,000) ya kahawa yote ya Tanzania inayouzwa nchini humo. Takwimu zinazoifanya Japan kuwa mnunuzi namba moja (1) wa kahawa inayolimwa nchini.

Aidha, Balozi Luvanda alielezea juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuwekeza katika miradi ya muda mrefu na mfupi ikiwemo kutatua changamoto za kilimo kuanzia shambani hadi sokoni ili kujihakikishia uhakika wa chakula na biashara. 

Vilevile Balozi ametoa wito kwa wadau wa kahawa nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa ya Mwaka 2024 (World Specialty Coffee Conference and Exhibition 2024) yanayotarajiwa kufanyika jijini Tokyo mwezi Oktoba 2024, ambayo yanaratibiwa na Ubalozi kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania. 
Balozi Baraka Luvanda, Bw. Osamu Aizawa, Meneja Mkuu wa Kampuni ya ITO EN  na wawakilishi wa Kampuni ya Tully’s Coffee, wakiwa katika picha ya pamoja kwenye hafla ya uzinduzi wa kahawa ya Tanzania  iliyofanyika jijini Tokyo, Japan.
Mtaalam wa Kahawa (barista) wa Kampuni ya Tully’s Coffee akielezea utayarishaji wa kahawa kwenye hafla ya uzinduzi wa aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania kwa Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee za nchini Japan
Mtaalam wa Kahawa (barista) wa Kampuni ya Tully’s Coffee akielezea utayarishaji wa kahawa  katika hafla ya uzinduzi wa aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania za Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee, nchini Japan 
Balozi Baraka Luvanda kwenye picha ya pamoja na wawakilishi wa Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee kwenye hafla ya uzinduzi wa kahawa tatu mpya kutoka Tanzania zitakazouzwa na Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee, nchini Japan

Mheshimiwa Baraka Luvanda akitoa salamu za ukaribisho katika hafla ya uzinduzi wa aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania zilizozinduliwa na Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee nchini Japan

Mtaalam wa Kahawa (barista) wa Kampuni ya Tully’s Coffee akielezea maeneo inapolimwa kahawa ya Tanzania iliyozinduliwa nchini Japan na Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee 

Bw. Osamu Aizawa, Meneja Mkuu wa Kampuni ya ITO EN, akitambulisha aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania  katika hafla ya uzinduzi wa kahawa hizo, nchini Japan

Balozi Baraka Luvanda kwenye picha ya pamoja na Bw. Osamu Aizawa, Meneja Mkuu wa Kampuni ya ITO EN, wakitambulisha kahawa za Tanzania  katika hafla ya uzinduzi wa kahawa hizo, nchini Japan

Tuesday, March 12, 2024

TANZANIA, PAKISTAN KUSHIRIKIANA SEKTA ZA BIASHARA NA UWEKEZAJI

Tanzania na Pakistan zimeahidi kuendelea kushirikiana kuimarisha zaidi sekta za biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote mbili. 

Ahadi hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvastory Mbilinyi alipokutana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, Bw. Shehryar Akbar Khan katika majadiliano ya Kidiplomasia kati ya Tanzania na Pakistan kwa lengo la kuimarisha, kukuza na kudumisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kipaumbele.

Bw. Mbilinyi amesema Pakistan ni miongoni mwa nchi za Asia ambazo zina majadiliano ya kidiplomasia na Tanzania. Amesema chimbuko la majadaliano hayo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Pakistan.

Akizungumza katika mkutano uliokutanisha pande hizo mbili katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, Bw. Mbilinyi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita zaidi katika kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji nchini hivyo wafanyabiashara kutoka Pakistan wasisite kuwekeza Tanzania kwani ni salama.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, Bw. Shehryar Akbar Khan amesema Pakistan na Tanzania zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali wakati wote.

“Nchi zetu zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali, ila kwa sasa tunaona ni vyema zaidi tukaimarisha zaidi sekta ya biashara na uwekezaji kwani kila nchi inahitaji biashara na uwekezaji,” alisema Bw. Khan na kuongeza kuwa Pakistan imekusudia kushirikiana na Tanzania katika sekta ya uchumi wa buluu.  

Katika mazungumzo hayo pande zote mbili zimeahidi kuimarisha ushirikiano katia sekta za elimu, afya, ulinzi, kilimo, nishati  uchumi wa buluu na usafirishaji.


Kaimu Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvastory Mbilinyi (kushoto) akizungumza na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, Bw. Shehryar Akbar Khan wakati wa Majadiliano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Pakistan.  majadiliano hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Majadiliano ya Kidiplomasia kati ya Tanzania na Pakistan yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, Bw. Shehryar Akbar Khan akieleza jambo wakati wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Pakistan.  Majadiliano hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.


AFRIKA KUSINI YAENZI MCHANGO WA HAYATI MWL. JULIUS KAMBARAGE NYERERE


Serikali ya Afrika Kusini imeendelea kutambua na kuuenzi mchango wa Baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo na bara la Afrika kwa ujumla.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Candith Mashego-Dlamini wakati akichangia hoja katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC uliomalizika tarehe 11 Machi 2024 jioni jijini Luanda, Angola.

Akizungumza kwenye agenda ya Sanamu ya Hayati Mwl. Julius Nyerere iliyozinduliwa rasmi tarehe 18 Februari 2024 kwa uratibu wa SADC katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa, Ethiopia, Mhe. Dlamini alieleza kuwa uzinduzi wa sanamu hiyo ni ishara muhimu ya kuenzi jitihada na mawazo yake ambayo yataendelea kukumbukwa daima.

Aidha, alieleza kuwa Tanzania kupitia Mwl. Nyerere iliweka bayana nia ya dhati na ya wazi ya kuzikomboa Nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo Afrika Kusini ambapo katika mapambano hayo ilitoa usaidizi wa kisiasa, mawazo, vifaa, hifadhi kwa viongozi na wapiganaji wake ikiwemo African National Congress (ANC) na Pan-African National Congress hadi pale walipofanikisha upatikanaji wa Uhuru wa Afrika Kusini mwaka 1994.

Tanzania ndio ilikuwa kimbilio la kwanza kwa Afrika Kusini baada ya kutokea kwa mauaji maarufu ya “Sharpeville massacre” yaliyotokea tarehe 21 Machi, 1960. Hatua hii ikaongeza chachu ya Mwl. Nyerere kuendeleza juhudi za kupinga ubaguzi wa rangi na ukoloni kwa ujumla wake na hivyo kujidhatiti kufanikisha kupatikana kwa uhuru kamili wa Afrika nzima.

Jitihada hizo zilipelekea kuanzishwa kwa  Muungano wa nchi za Afrika (OAU) mwaka 1963 na baadae kuitwa Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2002 pamoja na uanzishwaji wa Kamati ya Ukombozi ya OAU jijini Dar es Salaam iliyotoa misaada ya kifedha na vifaa katika kuchagiza harakati za ukombozi wa nchi za bara la Afrika zilizokuwa chini ya utawala wa kikoloni wakati huo Mwl. Nyerere akiwa miongoni mwa walezi wake.

Kwa upande wa SADC, Mhe. Dlamini amemwelezea Mwl. Nyerere kuwa ni miongoni mwa  viongozi waanzilishi wa SADCC mnamo mwaka 1980 na baadae SADC ambayo chimbuko lake lilianzia kwenye nchi zilizokuwa Mstari wa Mbele katika kupinga ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiendelea Afrikal Kusini na nchi nyingine za kusini mwa Afrika.

Pamoja na hayo, ameongeza kuwa Serikali ya Afrika Kusini na wananchi wake itaendelea kuenzi mchango thabiti wa Mwl. Nyerere ambaye wakati wote hakusita kupaza sauti kupinga vitendo vya kikatili na ubaguzi dhidi ya wananchi barani Afrika na dunia nzima.

Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mabarouk  (wa tatu kushoto), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (wa tatu kulia), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa (wa pili kushoto), Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Manejimenti ya Utumishi na Utawala Bora,Xavier Daudi (kulia), Kamishna Idara ya Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Bi. Talha Waziri katika picha ya pamoja  baada ya kumalizika kwa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) jijini Luanda, Angola tarehe 11 Machi, 2024.

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika picha ya pamoja.

Wajumbe wa Baraza la Mawaziri la SADC wakiimba wimbo wa jumuiya baada ya kumalizika kwa baraza hilo.

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sunday, March 10, 2024

MAWAZIRI WA SADC WAWASILISHA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamewasilisha salamu za rambirambi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati  Ali Hassan Mwinyi katika  Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo lililoanza leo tarehe 10 Machi 2024  jijini Luanda, Angola  

Wakati wa ufunguzi wa Baraza hilo, Waziri wa Mambo Nje wa Angola na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Mhe. Balozi Tete António pamoja na Mawaziri wengine wa nchi za SADC walitoa salamu hizo na kusifu uongozi mahiri na mchango wa Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi katika kuchangia maendeleo ya Tanzania na Kanda ya SADC hususan pindi alipokuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Jukwaa la Uratibu wa masuala ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADCC) mwaka 1989 - 1990 na pia aliongoza mchakato wa kubadili Jukwaa hilo kuwa SADC. 

Kwa muda wa siku mbili  Baraza hili litajikita kupitia, kujadili na kuridhia Bajeti ya SADC kwa mwaka wa fedha wa 2024/25. Vile vile, Baraza litajadili hatua iliyofikiwa katika kugharamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC wa 2020–2030, Taarifa ya Kamati ya Rasilimali Watu na Utawala na hatua iliyofikiwa katika kutafsiri nyaraka muhimu za SADC kwa lugha ya Kiswahili.

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Baraza la Mawaziri la SADC umeongozwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.)   ambaye ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (Mb.) na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) linaloendelea jijini Luanda, Angola tarehe 10 – 11 Machi, 2024.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrka Mashariki, Bi. Talha Waziri akiteta jambo na Balozi Mbarouk wakati wa  Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) linaloendelea  jijini Luanda, Angola tarehe 10 – 11 Machi, 2024.
Waziri wa Mambo Nje wa Angola na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Mhe. Balozi Tete António akifungua Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) linaloendelea  jijini Luanda, Angola tarehe 10 – 11 Machi, 2024

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Bw. Elias Magosi akihutubia wakati wa ufunguzi wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) linaloendelea jijini Luanda, Angola tarehe 10 – 11 Machi, 2024

Meza kuu ikiongoza  Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) linaloendele jijini Luanda, Angola tarehe 10 – 11 Machi, 2024

Picha ya pamoja ya wakati wa hafla ya ufunguzi wa Baraza la Mawaziri wa SADC