Thursday, March 14, 2024

AINA TATU MPYA ZA KAHAWA ZA TANZANIA YAZINDULIWA NCHINI JAPAN


Kampuni ya ITO EN LTD, ambayo ni kampuni tanzu ya Tully’s Co. Ltd., inayomiliki migahawa maarufu ya Tully’s Coffee, imezindua aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania, nchini Japan katika hafla iliyofayika jijini Tokyo tarehe 14 Machi, 2024. 

Aina za kinywaji hicho pendwa nchini humo kinachotokana na kahawa kutoka Tanzania ni TULLY’s COFFEE BARISTA BLACK KILIMANJARO; TULLY’S COFFEE MY HOME BLACK KILIMANJARO; na TULLY’S COFFEE BARISTA ROAST COLD BREW – KILIMANJARO BLEND. Kahawa hizo ni kutoka mkoa wa Arusha, Tarime mkoani mara na mashamba ya GDM yaliyoko Mbozi mkoani Mbeya. 

Zoezi hilo la uzinduzi lililofanyika katika Ubalozi wa Tanzania jijini Tokyo na liliongozwa na Mhe. Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan, lilimshirikisha pia Bw. Osamu Aizawa, Meneja Mkuu wa Kampuni ya ITO ENaliyeambatana na wawakilishi wa kampuni hiyo na Kampuni ya Tully’s Coffee.

Kampuni ya ITO EN Ltd. ambayo, ni kampuni tanzu ya Tully’s Coffee ni kampuni inayoongoza kwa biashara ya vinywaji nchini Japan, inamiliki migahawa ya kahawa takriban 700 nchini humo huku ikiwa imejipatia umaarufu mkubwa katika biashara ya uuzaji wa kahawa aina mbalimbali duniani. 

Hii ni mara ya pili, kwa Kampuni ya Tully’s kuzindua kahawa ya Tanzania katika migahawa yake, uzinduzi kama huu uliwahi kufanyika mwezi Juni na Agosti 2023 ukihusisha kahawa aina ya GDM full washed, GDM natural na Tarime Coffee.

Kuzinduliwa kwa aina nyingine tatu mpya za kahawa nchini Japan, kunaendelea kuleta uhakika na kuongezeka kwa soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo imejizolea umaarufu mkubwa kwa ubora na ladha ya aina yake na kupelekea kupewa jina maarufu la kibiashara la Kilimanjaro Coffee.

Kilimanjrao Coffee ni miongoni mwa bidhaa tatu za kahawa zinazopendwa zaidi Japan; na jina hilo hutumika nchini humo kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania. 

Tanzania inasifika Japan kwa kuzalisha kahawa bora aina ya Arabica (Arabica laini - full washed na Arabica ngumu - natural) inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera. 



Akizungumza katika uzinduzi huo, Balozi Baraka Luvanda alizihakikishia kampuni za Japan, uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji wanapoamua kuwekeza katika kilimo au sekta nyinginezo hapa nchini. 

Balozi Luvanda amelitaja zao la kahawa kuwa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati yanayongoza kwa kulipatia Taifa pato na kuingiza fedha za kigeni. Akitolea mfano wa Japan, alieleza kuwa kwa mwaka, Tanzania inauza kahawa yake Japan kwa wastani wa asilimia 33 ya kahawa inayolimwa nchini, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu million 15 (tani 15,000) ya kahawa yote ya Tanzania inayouzwa nchini humo. Takwimu zinazoifanya Japan kuwa mnunuzi namba moja (1) wa kahawa inayolimwa nchini.

Aidha, Balozi Luvanda alielezea juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuwekeza katika miradi ya muda mrefu na mfupi ikiwemo kutatua changamoto za kilimo kuanzia shambani hadi sokoni ili kujihakikishia uhakika wa chakula na biashara. 

Vilevile Balozi ametoa wito kwa wadau wa kahawa nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa ya Mwaka 2024 (World Specialty Coffee Conference and Exhibition 2024) yanayotarajiwa kufanyika jijini Tokyo mwezi Oktoba 2024, ambayo yanaratibiwa na Ubalozi kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania. 
Balozi Baraka Luvanda, Bw. Osamu Aizawa, Meneja Mkuu wa Kampuni ya ITO EN  na wawakilishi wa Kampuni ya Tully’s Coffee, wakiwa katika picha ya pamoja kwenye hafla ya uzinduzi wa kahawa ya Tanzania  iliyofanyika jijini Tokyo, Japan.
Mtaalam wa Kahawa (barista) wa Kampuni ya Tully’s Coffee akielezea utayarishaji wa kahawa kwenye hafla ya uzinduzi wa aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania kwa Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee za nchini Japan
Mtaalam wa Kahawa (barista) wa Kampuni ya Tully’s Coffee akielezea utayarishaji wa kahawa  katika hafla ya uzinduzi wa aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania za Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee, nchini Japan 
Balozi Baraka Luvanda kwenye picha ya pamoja na wawakilishi wa Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee kwenye hafla ya uzinduzi wa kahawa tatu mpya kutoka Tanzania zitakazouzwa na Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee, nchini Japan

Mheshimiwa Baraka Luvanda akitoa salamu za ukaribisho katika hafla ya uzinduzi wa aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania zilizozinduliwa na Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee nchini Japan

Mtaalam wa Kahawa (barista) wa Kampuni ya Tully’s Coffee akielezea maeneo inapolimwa kahawa ya Tanzania iliyozinduliwa nchini Japan na Kampuni ya ITO EN na Tully’s Coffee 

Bw. Osamu Aizawa, Meneja Mkuu wa Kampuni ya ITO EN, akitambulisha aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania  katika hafla ya uzinduzi wa kahawa hizo, nchini Japan

Balozi Baraka Luvanda kwenye picha ya pamoja na Bw. Osamu Aizawa, Meneja Mkuu wa Kampuni ya ITO EN, wakitambulisha kahawa za Tanzania  katika hafla ya uzinduzi wa kahawa hizo, nchini Japan

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.