Saturday, March 23, 2024

BILA YA AMANI, HAKUNA MTANGAMANO NA MAENDELEO

 

Nchi Wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimetakiwa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa nchi zao zinakuwa na amani, Umoja na utulivu na kutafuta ufumbuzi wa migogoro kwa kutumia njia zao wenyewe.


Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Mulambo Haimbe wakati anafungua Mkutano huo uliofanyika jijini Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.

 

Tanzania inatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi hiyo baada ya Zambia na katika Mkutano huo, Tanzania inawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb).

 

Mkutano huo pamoja na mambo mengine unapokea ripoti ya utekelezaji wa vikosi vya kulinda amani katika Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji na mchakato unaoendelea wa kupeleka vikosi vya kulinda amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

 

Nchi Wanachama zimehimizwa kuimarisha zaidi mshikamano na kuchangia rasilimali walizonazo ili kuviangamiza vikundi vya waasi vinavyotishia amani kwenye Kanda ya SADC. Imeelezwa kuwa bila ya amani na Usalama katika Kanda hiyo, wananchi wasitarajie kufikiwa kwa mtangamano na maendeleo ya kweli.

 

Mkutano huo wa Mawaziri ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya SADC utakaofanyika Machi 23, 2024 ambapo Tanzania itawakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb) akisoma makabrasha yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024. Kulia kwake ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) na kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo

Mwenyekiti wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Mulambo Haimbe akisoma hotuba wakati ufunguzi wa Mkutano huo uliofanyika jijini Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.

Wajumbe wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kulia) wakiimba nyimbo za taifa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.