Nchi
wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) zimekumbushwa kuwa
ni jukumu lao kufanya kazi kwa pamoja ili kumaliza changamoto za kiusalama
zinazozikabili Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji na Mashariki mwa Jamhuri
ya Kidiplomasia ya Congo (DRC).
Ukumbusho
huo umetolewa na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye
pia ni Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichelema wakati anafungua Mkutano wa
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya SADC
uliohitimishwa jijini Lusaka, Zambia Machi 23, 2024.
Katika
Mkutano huo ambapo Tanzania iliwakilishwa
na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango pamoja na mambo mengine, ulilenga kutathimini hali
ya usalama katika Kanda ya SADC. Ilielezwa kuwa hali ya
usalama Mashariki mwa DRC bado hairidhishi, hivyo umetolewa wito kwa nchi
wanachama na washirika
wa maendeleo kuchangia rasilimali ili vikosi vya kulinda amani vilivyopo huko na vingine vitakavyopelekwa, viweze
kutimiza majukumu yake ipasavyo.
Ilibainishwa kuwa
suala la kutafuta amani katika Kanda ni suala la kimkataba wa jumuiya hiyo na
Itifaki ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama, hivyo ni wajibu kwa mataifa hayo
kuungana pamoja kukabiliana na changamoto za kiusalama.
Wachambuzi
wa mambo wamesema kuwa mahudhurio mazuri ya viongozi katika ngazi ya Rais, Makamu
wa Rais na Mawaziri Wakuu katika mkutano huo yanadhihirisha kuwa nchi za SADC
zimedhamiria kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto ya usalama nchini
Msumbiji na DRC.
Marais walioshiriki Mkutano huo ni Mhe. Hakainde Hichelema wa Zambia, Mhe. Emmerson Mnangwa wa Zimbabwe: Mhe. Félix Tshisekedi was DRC; Mhe. Lazarus Chakwera wa Malawi; Mhe. Filipe Nyusi wa Msumbiji na Mhe. João Lourenço wa Angola. Nchi za Tanzania na Namibia ziliwakilishwa na Makamu wa Rais, Lesotho, Waziri Mkuu na Afrika Kusini na Botswana ziliwakilishwa na Mawaziri wa Ulinzi
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.